‘Hakuna Biashara’: Machinga Old Airport Mbeya Waeleza Masaibu Yao

Wanasema kukosekana kwa biashara kunachangiwa na miundombinu isiyo rafiki.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Baadhi ya wafanyabiashara wadogo, maarufu kama Machinga, wanaofanya shughuli zao katika Soko la Wafanyabiashara Wadogo Old Airport wamelalamikia kupungua kwa vipato vyao ikiwa ni miaka takriban miwili sasa tangu wahamishiwe hapo kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Mbeya.

Machinga hao ni sehemu ya wafanyabiashara takriban 2,600 waliohamishwa kutoka maeneo ya Kabwe, Mwanjelwa, Sido na Mafyati mnamo mwaka 2021 ikiwa ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kitaifa kuwapanga wafanyabiashara hao wadogo katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Wakizungumza na The Chanzo, Machinga hao katika eneo la Old Airport, lililopo katika stendi ya mabasi ya kwenda wilaya mbalimbali zinazounda mikoa wa Mbeya na Songwe, walisema kwamba tangu wahamishiwe sokoni hapo maisha yao hayajawahi kuwa yale waliyokuwa wameyazoea.

Jackson Swai anauza urembo sokoni hapa ambaye akiwa amevalia sweta nyeusi na kofia nyekundu, akiwa amekaa katika kibanda chake, ameiambia The Chanzo kuwa mauzo tangu kuhamia sokoni hapa yameshuka sana.

Kwa mujibu wa maelezo ya Swai, muda mwingine amekuwa akirudi nyumbani na Sh2,000 au Sh3,000. Hii ni tofauti na alipokuwa Sido, eneo alilohamishwa, ambapo alikuwa na uwezo wa kuuza mpaka Sh20,000 kwa siku.

“Biashara hapa siyo nzuri sana, yaani tunafanya kama biashara za uvumilivu,” Swai alilalama. “Sasa nalazimika kufunga ofisi na kwenda kutembeza urembo majumbani mwa watu kuhakikisha kwamba naongeza kipato changu ili niweze kuhudumia familia yangu.”

Kilio cha Swai ni kilio cha Machinga wengi sokoni hapa ambao wengi wao wanautafsiri uamuzi wa Serikali kuwahamisha kutoka kwenye maeneo yao ya awali kama uamuzi wa kuwarudisha nyuma kimaendeleo.

Malalamiko haya yanafanana na malalamiko ya Machinga wengine wengi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ambao wamekuwa wakikosoa zoezi hilo la “kuwapanga” kwa kukosa ushirikishwaji na muda mwengine kutekelezwa kwa nguvu na mabavu.

SOMA ZAIDI: Kuna Ugumu Gani Kwa Serikali Kuwasikiliza Wamachinga?

Miundombinu mibovu

Hapa Old Airport, malalamiko ya ukosefu wa biashara yanaenda sambamba na malalamiko ya miundombinu mibovu na isiyo rafiki ambayo Machinga wengi wanadhani inachangia biashara katika eneo hilo kuwa ndogo.

Grace Mwang’onda, muuzaji wa maji na juisi sokoni hapa ambaye ameiambia The Chanzo hali chakula kama mzigo wake haujamaliza, anasema barabara kutokupitika imekuwa kero kubwa kwa wafanyabiashara na wateja wao.

“Wateja hawaji huku,” anasema Mwang’onda. “Watakuja vipi wakati barabara hazipitiki? Kama [watu wa Serikali] wanatujali basi angalau wangeboresha hizo barabara, angalau ziwe zinapitika.”

Job Minga ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya ya Mbeya aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum kwamba anashangaa kuona hali ya miundombinu inabaki kuwa siyo rafiki licha ya Serikali kuahidi kurekebisha hali hiyo miaka miwili iliyopita.

“Huku [Old Airport] ni kwamba hakuna wateja, kwani wateja wanashindwa kutufikia kwa sababu mteja hawezi kufika huku kwa sababu hakuna miundombinu mizuri,” Minga alisema. “Ni mwaka wa pili sasa toka wamepelekwa maeneo hayo, lakini mazingira yako vilevile.”

Barabara zote zinazoelekea katika soko hilo ni za vumbi na zenye mashimo. Hali hii imezifanya gari zinazoenda huko kutokuwa nyingi kama ambavyo awali ilitegemewa na mamlaka za jiji.

The Chanzo ilipofika katika soko hilo iliona maji yakiwa yametuwama kutokana na mvua iliyonyesha usiku na kufanya barabara kutokupitika. Hata hivyo, wafanyabiashara sokoni hapa hawajui kipi bora kati ya jua na mvua kwani wakati wa jua kunakuwa na vumbi kubwa linalowakera wao wenyewe na wateja wao.

Kufuatia malalamiko haya, The Chanzo ilimuuliza Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Triphonia Kisiga ni mikakati gani jiji inayo kutatua malalamiko hayo ambapo alisema kwamba wao kama Serikali wameendelea kufanya maboresho kadri fedha inavyopatikana.

Kisiga alisema kwamba Serikali imekuwa ikiboresha miundombinu sokoni hapo, ikiwemo kufanya maboresho kwenye vyoo, kitu ambacho alisema kilikuwa kilio cha siku nyingi cha wafanyabiashara sokoni hapo.

Maboresho mengine yaliyofanyika ni kama vile kuweka taa za usiku na kumwaga vifusi kwenye baadhi ya maeneo korofi.

“Wafanyabiashara wale hatujawasahau, hatujawaacha,” alisema Kisiga kwenye mahojiano hayo. “Wanatakiwa kuwa wavumilivu kwani uboreshaji wa miundombinu unazingatia bajeti ya Serikali. Tunawaasa waendelee kufanya shughuli zao kwani Serikali inaendelea kuboresha miundombinu hiyo.”

Asifiwe Mbembela ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Anapatika kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts