Karibu Tanzania, Nchi ya Madalali

Kwa mwananchi wa kawaida, ni ngumu kupata huduma yoyote Tanzania bila kupitia kwa dalali.

subscribe to our newsletter!

Sidhani kama huko nyuma hali ilikuwa kama hivi, lakini hivi sasa inaonekana kila kona ya nchi hii kuna udalali takriban kwenye kila kitu. Iwe unatafuta nyumba ya kupanga au basi la kusafiria, nguo au bodaboda ya kukuwahisha kwenye safari yako, ni ngumu kukwepa kumuona dalali hapa nchini, hususan hapa jijini Dar es Salaam.

Udalali jijini hapa umetapakaa kila mahali kiasi ya kwamba sasa imekuwa ni kero. Ukienda stendi za mabasi ya mikoani, kwa mfano, ile unatokea tu tayari umevamiwa na watu kama ishirini hivi, kila mmoja akikuvuta upande wake, haijalishi kwamba ofisi za mabasi husika ziko pale, kila mtu anaziona.

Ukienda Soko la Karume kujitafutia shati lako la mtumba, yale yale, yaani ukitoa macho tu tayari mtu ameshakutupia nguo ingawa hujaomba. Daladala nazo ni kama bodaboda tu, ukichomoza pua tayari umefuatwa hata kama hujaonesha ishara yoyote ya kuhitaji huduma hiyo.

Hii hali kusema kweli inakera sana na inadhihirisha ni kwa kiwango gani neno ustaarabu halipo katika kamusi ya Watanzania walio wengi. Mtu anaweza kutetea tabia hii kwa kudai kwamba vijana hawa wanatafuta riziki na kwamba kuwahukumu inaweza kuwa siyo jambo sahihi.

Lakini jamani lazima tuambizane ukweli kwamba ustaarabu haupaswi kuwa anasa ya wenye nacho tu, kwamba kwa sababu wewe ni masikini, unatafuta, basi unaweza kujifanyia tu mambo hovyo hovyo katika namna inayowakera wengine.

Pia, kuna watu wengi wanaotafuta riziki na hawafanyi vitu hivi na sidhani kama wamewahi kulalamika kwamba kwa kutokufanya hivyo utafutaji wao umeathirika kwa namna moja ama nyingine.

Kuna ule ustaarabu wa waendesha bajaji, pikipiki au daladala ambapo wanakubaliana kwamba moja kwanza ipakie na kuondoka ndiyo nyingine iweze kufanya hivyo badala ya kugombania abiria.

Kwa hiyo, usiniambie hiki kitu hakiwezekani. Umasikini, au kutafuta kipato, kama nilivyosema, isiwe kigezo cha kutokuwa wastaarabu. Huu ni utaratibu mzuri ambao wengine wanapaswa kuuiga.

Utaratibu wa ajabu

Tukizungumzia madalali, hata hivyo, tatizo kubwa lipo kwenye madalali wa nyumba au vyumba.

Hivi ni utaratibu gani wa ajabu zaidi kushinda ule hawa jamaa wamejiwekea kwamba mtafuta nyumba alipe kodi ya mwezi mmoja kwa dalali aliyemsaidia kupata hiyo nyumba?

Mimi ninavyofahamu mantiki inataka mwenye nyumba ndiye anayepaswa kumlipa dalali maana si ndiyo amemletea mteja, au ni vipi?

Sasa huu utaratibu wa kwamba nikishapata nyumba mbali na kumlipa mwenye nyumba kodi ya miezi sita au 12 natakiwa pia nimlipe na dalali kodi ya mwezi mmoja umetoka wapi?

Hiki kitu hakiingii akilini kabisa na haikushangaza kuona, mnamo Novemba 16, 2021, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipiga marufuku kitendo cha madalali wa nyumba kutoza fedha sawa na kodi ya mwezi mmoja kwa wapangaji wanapo watafutia makazi au maeneo ya biashara.

Licha ya marufuku hiyo, ambayo kwa kweli sijuwi kama ilikuwa na msingi wowote wa kisheria au kikanuni, utaratibu huu unaendelea kama kawaida, hali inayomuongezea mzigo mkubwa mwananchi wa kawaida.

Fikiria machungu ya kubebeshwa mzigo ambao kimsingi anapaswa aubebe mwenye nyumba wako!

Serikali yetu, kwa bahati mbaya, imeonekana kabisa haina uwezo na kushughulika na utamaduni huu wa udalali.

Hata kwenye hili la Lukuvi, kukosekana kwa usimamizi wake kunaonesha kwamba lengo halikuwa kukomesha hilo jambo bali kupiga siasa tu ili kuonesha wananchi kwamba Serikali inajali masuala yao.

Tunaoteseka ni walalohoi 

Lakini lazima tuseme ukweli jamani kwamba ni ngumu kwa Serikali kufanyia kazi malalamiko haya kwani ni kiongozi gani mkubwa wa Serikali, yule anayekaa kabisa katika nafasi za maamuzi, anahitaji msaada wa dalali kutafuta nyumba ya kupanga?

Ni kiongozi gani wa Serikali anakwenda Stendi ya Magufuli kupigana vikumbo na walalahoi kugombea mabasi ya kwenda mikoani au kukurupushana na wanyonge wengine pale Karume kutafuta vinguo vya mtumba vya mtoto wake?

Hakuna hata mmoja!

Hili linatuhusu sisi tusiyokuwa na uwezo wa kupanda ndege kwa ajili ya usafiri; tusio mudu gharama za kununulia watoto wetu nguo kwenye ‘Shopping Malls’; tusiyokuwa na uwezo wa kununua mahitaji yetu ya nyumbani kwenye ‘Supermarkets’; na tusiyokuwa na uwezo wa kumudu gharama za kuishi kwenye ‘Apartments’.

Ikitaka kuwa na msaada kwetu, Serikali ingeweza kutengeneza tovuti inayoendeshwa na Serikali yenyewe ambayo ingemlazimu kila mwenye nyumba anayehitaji wapangaji ajiandikishe humo ili wapangaji tukitaka kupanga tuingie humo na kuwakwepa madalali na ujambazi na ukatili wao.

Mwenye nyumba kama hawezi pilikapilika za kushughulikia maombi ya wapangaji, kama vile kuwazungusha wapangaji, anaweza kuajiri vijana wa kumsaidia.

Pengine hilo litakuwa limejibu hofu ya wale wanaoweza kujiuliza madalali sasa watakwenda wapi. Watakwenda kuajiriwa na wenye nyumba, walipwe huko!

Serikali pia inaweza ikawa kali zaidi kwenye marufuku iliyotangazwa na huyo huyo Lukuvi, mnamo Oktoba 27, 2018, alipolitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuacha kutumia madalali kupangisha nyumba zake na kuwadai kodi ya zaidi ya miezi sita.

Sisi walalahoi hatulipwi mishahara ya miezi sita na muda mwingine unataka kuhama lakini hiyo hela ya miezi sita unaikosa kabisa, kwa hiyo unabaki unataabika.

Lakini, kwa kumalizia, cha muhimu zaidi ni kuhakikisha kwamba tunakuwa wastaarabu kwenye kazi zetu jamani. Iwe ni mabasi ya mikoani, muuza mitumba Karume, mwendesha bajaj au bodaboda.

Ni muhimu sana kuhakikisha tunakuwa na utaratibu unaoeleweka kwenye kutoa hiyo huduma, hali itakayosaidia huduma husika kutolewa katika mazingira ya kistaarabu, na hivyo kumpunguzia usumbufu mteja.

Mkonganyi Makunganya amejitambulisha kama mwananchi wa kawaida anayeipenda nchi yake. Kwa maoni, anapatikana kupitia rickyblair668@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

2 Responses

  1. Kwa maoni yangu naomba Serikali ifuatilie hili la madalali wa vituo vya daladala Vijana wengi Wenye nguvu na afya nzuri kugombea dala dala kama wao ni abiria kumbe wanawahi siti ili apawe tsh 500,kuna kuumizana pia kuibiwa hii Siyo sawa.wasisubiri mpaka achomwe moto mtu ndo waibuke kusema wananchi wasijichukukie sheria mkonon.ni mtazamo wangu.

  2. Hii makala imegusa kile ambacho nilikishuhudia baada ya pasaka mwaka huu 2023.Nilipanda basi ya ‘2 by 3 kuja Majimoto Katavi tokea Kolandoto -Shinyanga nikalipishwa sh 35 000.00 na mawakala huku wakizozana mmoja alikuwa kang’ang’snia shs 40,000.00.Cha ajabu nimetoa kwa wakala shs 35,000.00 nilipoingia ndani ya basi nikapewa tiketi ya sh 20,000.00 nilijiuliza maswali mengi sana.Kwamba huu si ni wizi wa macho macho?Naomba Serikali iliangalie hili suala la madalali Kwa umakini ni kundi la kupandisha gharama za maisha kwa wananchi walio wengi.Na Wala halizalishi chochote kuinua ichumi wa nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts