Nadhani kati ya imani potofu kubwa zilizowahi kuibuka Tanzania, na kwengineko ulimwenguni kusema ukweli, ni kuwa wanawake wa zamani, wengi wao wakiwa ni wamama wa nyumbani, walikuwa ‘magolikipa kwa sababu tu hawakuwa na kazi za ofisini au biashara.
Lakini ukweli ni kwamba, wanawake wengi hawakuwa hivyo, na hawako hivyo hata leo hii. Mama zetu na bibi zetu wamefanya, na wanaendelea kufanya, kazi mashambani, na kazi za nyumbani zisizokuwa na malipo yoyote lakini ambazo ziliwezesha familia kula na kuishi.
Binafsi nilikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa wakiamini kwenye imani hii potofu. Mtazamo wangu huo ulibadilika pale tu nilipojifunza, na kukubali, kwamba kazi za ofisini, au biashara, au ujasiriamali, ni sawa sawa tu na kazi za kilimo, ufugaji, au za nyumbani.
Tofauti ni kwamba hizi kazi za nyumbani, kilimo na ufugaji, ambazo mama zetu na bibi zetu wamekuwa wakifanya hazina ujira. Lakini ni kazi zinazolisha familia na ni kazi walizofanya wanawake kwa miaka nenda rudi tangu mwanzo wa dunia.
Kwa hiyo, kama mwanamke hafanyi chochote kabisa, amekaa tu, labda huyo ni ndiyo anaweza kuwa ‘golikipa.’
Lakini kama mwanamke anapika, anafua, anafanya usafi, na kuhakikisha wanafamilia wengine wanaishi vizuri, wanakula, wanavaa safi, na kwenda kazini kila siku, huyu, kwa viwango vyoyote vile, siyo mwanamke ‘golikipa.’
Mwanamke huyu ana mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi na kazi anazofanya ni kubwa kuliko wengi tunavyozichukulia. Ndiyo maana baadhi ya sehemu duniani wanawake wanalipwa kufanya kazi hizi za nyumbani.
Ndiyo, mke analipwa ujira wa kupika, kufua nakadhalika!
Mnamo mwaka 2007, kwa mfano, taifa la Amerika Kusini la Venezuela lilikuwa taifa la kwanza duniani kuanzisha utaratibu wa kulipa wamama wa nyumbani, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wao kwenye kujenga uchumi wa nchi.
SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni
Kama kwa kufanya kazi hizi hizi tunaajiri wasaidizi na kuwalipa kuzifanya, kwa nini zinapofanywa na wake, mama, bibi, au dada zetu zionekane ni ‘ugolikipa’? Mchango wa akina mama wa nyumbani ni mkubwa mno kuliko tunavyoutambua kama jamii.
Nafahamu katika harakati za ukombozi wa wanawake kwamba tumepigania uhuru wa kufanya kazi na sasa tunapigania malipo sawa na bado nchi nyingine haziruhusu baadhi ya kazi kufanywa na wanawake.
Lakini harakati hizi hazimaanishi kuwa akina mama wa nyumbani hawana mchango kwa taifa.
Ukitazama wanawake wa TANU waliopigania uhuru na kufanya kazi za mashinani, akina Bibi Titi, Tatu Mzee, Mashavu Binti Kibonge na wengineo wengi, wengi wao hawakuwa na kazi za ofisini au biashara.
Bibi Titi, tunasoma, alikuwa muimbaji wa ngoma. Na wanawake wengi aliowashawishi walikuwa wakitumia hela walizoachiwa na waume zao kuchangia chama cha TANU, chama kilichoongoza harakati za kupigania uhuru.
Wanawake wengine wasio na biashara ndogo ndogo walichangia mikufu, hereni, na vito vyao vya thamani kusukuma shughuli za kupigania uhuru. Ni mchango wa hawa ‘magolikipa,’ kwa asilimia kubwa, ndiyo umetufikisha hapa kama taifa.
‘Magolikipa’ hawa ndiyo walinunua kadi za chama na kuwachukulia waume zao kadi kwani wafanyakazi wa kampuni na Serikali enzi hizo hawakuruhusiwa kujihusisha na shughuli za chama.
SOMA ZAIDI: Mfumuko wa Bei Unavyohatarisha Biashara za Wanawake Masokoni
Na wamama wa nyumbani wana nguvu sana ambayo inaweza kufanya shughuli za nchi zikasimama.
Historia imejaa mifano ya namna uamuzi wa wamama wa nyumbani kufanya mgomo kulichangia kwenye mabadiliko kadhaa ya kijamii katika sehemu mbalimbali duniani.
Kama tunataka kujua kama mama wa nyumbani ni ‘golikipa’ au la, hebu wajaribu wamama hawa kugoma kabisa kufanya kitu chochote kwa takriban siku tatu mfululizo.
Nchi hii itasimama, nakwambia!
Kwa hiyo, tukiwa tupo kwenye wiki ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ni matumaini yangu kwamba, kama taifa, tutachukua nafasi hiyo kuuona mchango wa akina mama wa nyumbani katika maendeleo ya nchi.
Heri ya Siku ya Wanawake kwa akina mama wote wa nyumbani nchini Tanzania!
Kuduishe Kisowile ni daktari na mchambuzi wa masuala ya afya ya umma. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia kuduzekudu@gmail.com au kupitia Twitter kama @Kudu_ze_Kudu. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
Very very good talk, we really should appreciate what woman’s do in our family and society.. Thanks for the good words DAKTARI MWANDISHI