Mfumuko wa Bei Unavyohatarisha Biashara za Wanawake Masokoni

Baadhi wanafikiria kuachana na biashara zao na kutafuta vitu vingine vya kufanya

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogondogo kwenye masoko mbalimbali nchini wameelezea namna kuendelea kupanda kwa bei za bidhaa na huduma muhimu kunavyotishia biashara zao hizo, huku wengine wakifikiria kuachana nazo kabisa na kutafuta vitu vingine vya kufanya.

Hilo lilibainika wakati wa tathmini fupi iliyofanywa na The Chanzo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Mtwara na Zanzibar iliyolenga kufahamu namna wanawake hao wa masokoni wanavyokabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, hali inayoendelea kuzua taharuki Tanzania na kwengineko.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kwamba mfumuko wa bei kwa mwezi Disemba 2022 ulikuwa ni asilimia 4.8, huku mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji visivyo na kilevi uliongezeka hadi asilimia 9.7 kutoka asilimia 9.5 iliyorekodiwa mwezi Novemba 2022.

Kwenye tathmini yake hiyo iliyoifanya kwenye mikoa mbalimbali nchini, The Chanzo ilibaini kwamba hofu kubwa inayowakabili akina mama wanaofanya biashara masokoni ni kushindwa kurejesha mikopo waliyoichukua kwa ajili ya biashara kwani bei za bidhaa za sasa si sawa na vile zilivyokuwa wakati wakiomba mikopo hiyo.

Hofu hii imewakumba akina mama wengi wanaofanya shughuli zao kwenye Soko la Sabasaba jijini Dodoma ambao waliieleza The Chanzo kwamba kama hali haitabadilika basi watalazimika kuachana na biashara hiyo kwani si biashara ambayo inawalipa kwa sasa.

Vitu bei juu

“Kipindi cha nyuma vyakula vilikuwa vingi na bei haikuwa kubwa,” anasema Flora Mushi, mfanyabiashara sokoni hapo. “Kwa unga wa ugali sasa hivi kilo ni Sh2,000. Ukinunua kilo 25 ni Sh43,000 au Sh44,000. Hebu ona, mpaka unga wa ugali umefika sehemu kama hiyo!”

“Tunanunua nyanya kwa Sh120,000 kwa tenga halafu sisi tunakuja kuuza sado kwa Sh4,000,” analalama mfanyabiashara mwengine Sophia Simoni. “Wafanyabiashara wadogo magengeni hawana uwezo wa kusema watakwenda kununua sado kwa Sh7,000 kama tukiwapandishia bei.”

Mkoani Mtwara nako, sauti hizi hizi za malalamiko zinasikika kutoka kwa wanawake kadhaa wanaofanya biashara masokoni, wengi wao wakielezea mtanziko wanaokabiliana nao kati ya kutengeneza faida na kutunza wateja wao.

“Mchele madukani tunanunua kilo moja kwa Sh3,500,” anasema Asminia Muhaji sokoni hapo. “Wateja wanataka wauziwe sahani moja kwa Sh1,000 kama walivyozoea mwanzo. Unga wa sembe dukani tunanunua Sh2,200 lakini wateja wanataka sahani moja tuwazuie kwa Sh1,000. Sasa sisi tutapata nini?”

SOMA ZAIDI: Nini Kinaweza Kupandisha, Kushusha Bei za Bidhaa 2023?

Hii si changamoto inayowakabili wafanyabiashara wa Mtwara tu bali hata wale wa Dar es Salaam, jiji kuu la biashara nchini Tanzania.

Farida Saidi Juma, kwa mfano, ni mjasiriamali wa biashara ya kuuza chakula katika Soko la Makumbusho jijini Dar es Salaam ambaye aliiambia The Chanzo kwamba kulingana na bei za bidhaa za vyakula kupanda, wao kama wafanyabiashara hawapati faida kwani inawabidi kuuza bei ya siku zote, ili kuepuka kupoteza wateja wao.

“Imetuathiri kwa sababu tunauza chakula kwa Sh2,000 kwa sasa hivi,” Farida, 36, anasema. “Vitu vimepanda juu lakini huwezi kumuuzia mteja chakula kwa Sh2,500 kwani hawezi kununua. Kwa hiyo, na sisi faida tunayopata ni ndogo sana.”

Gradiselia Sunday, 51, mfanyabiashara wa bidhaa za vyakula mbalimbali katika Soko la Makumbusho, ametaja bidhaa ya nyanya kama ndiyo bidhaa iliyopanda bei kwa kiasi kikubwa, huku akitaja bei za bidhaa mbalimbali kama vile viazi mviringo kuonekana kupanda bei kwa kasi hivi karibuni.

“Tulikuwa tunanunua nyanya kwa Sh25,000 au Sh30,000 kwa tenga,” anasema. “Sasa hivi tunanunua kwa Sh65,000 hadi zinafika Sh68,000 au Sh70,000. Viazi [mviringo] tulikuwa tunanunua kwa Sh50,000 hadi Sh60,000 sasa hivi ni Sh80,000 hadi Sh90,000 kulingana na vinavyoingia.”

Josephine Juma anauza nyanya, hoho, vitunguu, na karoti katika Soko la Msuka na Mirogo, Mwanza, anashangazwa na kasi ambayo bidhaa na huduma zinapanda bei.

“Kuna muda hata hatuelewi mambo yanakuwa yanabadilikaje kwa haraka hivyo,” analalama mfanyabiashara huyo. “Tofauti na zamani bei ya mzigo ilikuwa inachukuwa muda mrefu kupanda, siku hizi ndani ya siku tatu kunakuwa na mabadiliko ya bei.”

Wachumi, Serikali wafunguka

Wachumi, hata hivyo, hawashangazwi na malalamiko haya ya wafanyabiashara wadogo kwani wanaamini kwamba athari za mfumuko wa bei huwa ni mtambuka, kwamba humgusa kila mtu na kila sekta ya maisha ya kila siku.

Salum Awadh ni mchambuzi wa masuala ya fedha, uwekezaji na uchumi aliyeiambia The Chanzo kwamba hashangai kusikia mfumuko wa bei umewafanya wafanyabiashara wadogo kushindwa kumudu kuendelea na biashara zao.

“Inaweza ikaleta athari pale ambapo faida yake inatakiwa kuwa asilimia 10 ila ikashuka mpaka asilimia tano au mbili, hii sasa inaweza kutengenza hasara badala ya faida na hali hii inaweza kusababisha biashara hiyo kutokuendelea,” Awadh aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum hivi karibuni.

SOMA ZAIDI: Infographic: Mwenendo wa Kupanda kwa Bei za Bidhaa na Huduma Tanzania

Mtaalamu huyo anapendekeza kwamba Serikali iweke mifumo ya mitaji na fedha ambayo itaweza kuwasaidia wananawake wajasiriamali kipindi kama hiki kama nchi nyengine za Afrika zilivyoweza kufanya.

“Serikali ikiweka mfumo maalum wa kuwakopesha wanawake mikopo isiyo na riba kwenye kipindi kama hiki inaweza kuwasaidia kuendelea na biashara,” anashauri Awadh. “Pia, elimu ya fedha itolewe kwao [wanawake] ili waweze kujua masuala ya faida, hasara na gharama za uzalishaji.”

Mnamo Januari 30, 2023, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aligusia suala la kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu nchini, hali aliyoihusisha na athari zitokanazo na janga la UVIKO-19 pamoja na vita inayoendelea hivi sasa kati ya Urusi na Ukraine.

Bashe, aliyekuwa akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Zuhura Yunus, Ikulu, Dar es Salaam, alibainisha hatua kadhaa ambazo Serikali inazichukua kukabiliana na hali hiyo.

“La kwanza, Rais Samia [Suluhu Hassan] aliamua kutoa ruzuku ya mafuta,” alisema Bashe. “Serikali ya awamu ya sita imeamua kutoa ruzuku ya mbolea, Serikali ya awamu ya sita imeamua kutoa ruzuku kwenye mbegu.”

“La pili, Serikali imeamua kuwekeza kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye uzalishaji wa mbegu,” aliongeza Bashe. “Nchi yetu toka wakati tunapata uhuru tuna mashamba ya mbegu wanaita Seed Farm toka wakati wa Mwalimu [Julius] Nyerere yapo kama 17 Serikali ya mama Samia kwa mara ya kwanza tunaweka miundombinu ya umwagiliaji.”

Wanatokaje?

Hata hivyo, wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogondogo masokoni hawasubiri Serikali iingilie kati na kuwanusuru na athari za mfumuko wa bei. Tayari baadhi yao wameanza kuchukua hatua zinazolenga kukabiliana na hali hiyo.

Khadija Salum Said ni mfanyabiashara wa ndimu katika Soko la Kwerekwe, Unguja, aliyechukua hatua ya kupunguza wingi wa ndimu kutoka 35 hadi hadi 25 kwenye ujazo wa sahani na kuuza kwa Sh1,000, hali iliyotokana na kupanda kwa bei ya kiroba cha ndimu kutoka Sh17,000 hadi Sh21,000.

SOMA ZAIDI: Mbivu Mbichi ya Hoja za Wabunge Kuhusu Mafuta na Kwa nini Bei Inaweza Kupaa Zaidi

“Ukiuza kwa Sh1,000 wateja wanalalamika, hapo ukumbuke una watoto na kodi ya meza na upate faida, sasa inaleta ugumu kwenye biashara kwa sasa,” alisema Khadija akizungumza na The Chanzo.

Lakini je, wanawake hawa wanaweza kwenda mbali zaidi ya hapa?

Jane Magigita, ambaye kupitia shirika lake lisilo la kiserikali la Equality for Growth, amekuwa akifanya kazi na wanawake wa masokoni kuwasaidia kupambana na changamoto mbalimbali, anasema ndiyo.

“Ni kuangalia jinsi ya kuwa na biashara ambazo zinaweza kuwa kwenye mzunguko wa kimaisha ambazo biashara hizo zinahitajika kwenye maisha ya kila siku ili kuendelea kuhimili athari za mfumuko wa bei,” alishauri Magigita.

“Suala la pili ni vizuri pia ikiwa [akina mama hawa] wataangalia mbadala wa biashara ambazo zinaendana na maisha ya watu waliopo kwenye eneo husika ili kuendelea na biashara hizo,” aliongeza Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Equality for Growth.

Habari hii imeandikwa na Najjat Omar (Zanzibar), Hadija Said (Dar es Salaam) Rahma Salumu (Mwanza), Jackline Kuwanda (Dodoma), Asifiwe Mbembela (Mbeya) na Omari Mikoma (Mtwara). Kwa maoni, tuandikie: editor@thechanzo.com 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts