The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fahamu Kuhusu Ugonjwa wa Homa ya Virusi vya Marburg

Inashauriwa wataalamu wa afya kutoka katika sekta zote kama za binadamu, wanyama na mazingira kushikirikiana katika kugundua vihatarishi vya magonjwa kama haya.

subscribe to our newsletter!

Kati ya Februari na Machi 2023, nchi mbili za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Equatorial Guinea na Tanzania, ziliripoti kisa cha kwanza cha ugonjwa wa virusi vya Marburg, na kiwango cha vifo vya zaidi ya asilimia 60.

Kwa sababu hizi ni nchi ambazo hazijawahi kuwa na kesi za awali licha ya kuwa katika maeneo yanayosadikika kuwa yana wanyama wanaosababisha ugonjwa huu, visa hivi vinaweza kuwa wito wa kuamka na nia mpya katika  kupambana na magonjwa haya.

Hii ikiwa ni pamoja na kutafuta chanjo na tiba za kupambana na milipiko, hususan ya magonjwa yasiyo na tiba au chanjo.

Andiko hili fupi linalenga kuangazia hatari inayoendelea ambayo ugonjwa wa virusi vya Marburg unaweza kusababisha kwenye  jamii.

Epidemiolojia

Ugonjwa wa Virusi vya Marburg (MVD) ni ugonjwa wa nadra lakini unaoambukiza kwa haraka sana unaosababishwa na virusi vya Marburg, ambavyo ni mwanachama wa familia ya Filoviridae.

Virusi hivyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1967 wakati wa mlipuko huko Marburg, Ujerumani, na tangu wakati huo vimehusishwa na milipuko ya mara kwa mara katika baadhi ya nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. 

Jedwali linaloolesha nchi zilozowahi kuripori kesi za virusi vya Marburg

 Homa inayosababishwa na virusi vya Marburg ina sifa ya milipuko ya hapa na pale, huku visa vingi vikitokea Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mlipuko wa ugonjwa mara nyingi huhusishwa na utunzaji, ugusaji, au utumiaji wa wanyama walioambukizwa, kama vile popo na nyani, au kwa kugusa majimaji ya mwili ya binadamu aliyeambukizwa.

SOMA ZAIDI: Afya Moja Ni Nini Na Kwa Nini Ujali Kuhusu Ufanisi Wake?

Kipindi cha maambukizi mpaka kuonyesha dalili za ugonjwa wa virusi vya Marburg ni kati ya siku tano na kumi, na dalili huonekana ghafla na kuendelea haraka.

Ugonjwa huu ni wa kuambukiza kwa haraka na unaweza kuambukizwa kwa kuwagusa au kuwahudumia kwa karibu watu walioambukizwa au majimaji yao ya mwili, kama vile damu, mate, na matapishi.

Kiwango cha vifo vya ugonjwa wa virusi vya Marburg ni kikubwa, kuanzia asilimia 24 hadi 88 ya watu wanaopata maambukizi, kutegemeana na kinga ya mtu aliyeambukizwa, au huduma ya haraka atakayopatiwa mgonjwa aliyepata maambukizi.

Kwa sasa hakuna tiba maalum ya ugonjwa huo, na huduma ya dalili anazopata mgonjwa ndiyo msingi mkuu wa matibabu.

Kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Marburg ni pamoja na utambuzi wa haraka wa mgonjwa, kutengwa kwa watu walioambukizwa, na utekelezaji wa hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi.

Hatua hizi ni pamoja na matumizi ya vifaa vya kujikinga, kama vile glavu, barakoa na gauni maalum, na utekelezaji wa hatua kali za usafi, kama vile unawaji mikono na kufunika nyuso.

Hatari ya ueneaji

Maambukizi ya  ugonjwa wa virusi vya Marburg ni hatari inayoweza kutokea kwa watu binafsi na vikundi vinavyosafiri kwenda au kutoka kwenye maeneo ya mlipuko. Kiwango cha hatari hutofautiana kulingana na eneo/maeneo yaliyotembelewa na muda wa kukaa.

Kama nilivyosema awali, ugonjwa wa virusi vya Marburg (MVD) huambukizwa kwa kugusana na majimaji ya mwili ya watu walioambukizwa au wanyama, kama vile damu, mate, matapishi, mkojo, kinyesi, au maziwa ya mama.

SOMA ZAIDI: Kutibu Wanyama Wetu Ni Kulinda Afya, Ustawi Wetu Kama Binadamu

Kwa hiyo, mtu yeyote anayekutana, au kumgusa mtu aliyeambukizwa, au mnyama, yuko katika hatari ya kupata ugonjwa huo. Kwa ufafanuzi zaidi, hizi hapa ndiyo namna kuu ugonjwa huu unaweza kusambazwa:

Kugusana na wanyama walioambukizwa: Virusi vya Marburg hupatikana, kwa kawaida, katika popo wa matunda na wanyama wengine wa porini, na watu wanaweza kuambukizwa kwa kugusana na wanyama hawa au majimaji yao ya mwili.

Kugusana moja kwa moja na umajimaji wa mwili: Virusi vinaweza kusambazwa kwa kugusana moja kwa moja na umajimaji wa mwili wa watu walioambukizwa, kama vile damu, matapishi, na mate.

Wahudumu wa afya na wanafamilia wa watu walioambukizwa wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa.

Kugusana na miili  au vitu vilivyochafuliwa na virusi: Virusi vinaweza kuishi kwa siku kadhaa kwenye mwili  au vitu vilivyo na majimaji ya mwili, na watu wanaweza kuambukizwa kwa kugusa nyuso hizi au vitu na kisha kugusa macho, pua, au mdomo wao.

Usambazaji kwa njia ya hewa: Ingawa ni nadra, kuna ushahidi kwamba virusi vya Marburg vinaweza kuambukizwa kupitia hewa katika hali fulani, kama vile wakati wa taratibu za matibabu zinazozalisha erosoli, chembe ambazo zimesimamishwa hewani.

Maambukizi kwa njia ya kujamiiana: Kumekuwa na ripoti za maambukizi ya virusi vya Marburg kwa njia kujamiiana, ingawa hii inaonekana kutokea kwa nadra.

Ni muhimu kutambua kwamba siyo kila mtu anayegusana na virusi atapata dalili za ugonjwa huo, na watu wengine wanaweza kubeba na kusambaza virusi bila kuonyesha dalili zozote.

Ili kuzuia uambukizaji wa ugonjwa wa virusi vya Marburg, ni muhimu kujizoesha na usafi, kuvaa vifaa vya kujikinga unapowatunza watu walioambukizwa, na kuepuka kugusa wanyama walioambukizwa au majimaji yao ya mwili.

Pia, ni muhimu kutambua mara moja na kutoa taarifa za matukio ya ugonjwa huo ili kuzuia kuenea zaidi kwa virusi.

Vipimo na matibabu

Utambuzi wa ugonjwa wa virusi vya Marburg (MVD) unaweza kuwa changamoto kwani dalili za awali zinaweza kuwa sawa na maambukizo mengine kama vile malaria, homa ya thyphoid au ugonjwa wa virusi vya Ebola.

Utambuzi wa magonjwa ya virusi vya Marburg kikawaida huthibitishwa na uchunguzi wa maabara wa damu, mkojo, au maji mengine ya mwili ili kugundua uwepo wa virusi.

Kwa sasa hakuna matibabu, au dawa maalum, za ugonjwa wa virusi vya Mabrurg, isipokua  kutibu dalili zinazojitokeza kutokana na maambukizi, kama vile homa, upungufu wa maji mwilini, na kuzuia kutokwa na damu, na kuongeza kinga ya mwili kwa kutumia majimaji, elektroliti, na utiaji-damu mishipani.

Mbali na huduma hizo, kuna matibabu kadhaa ya majaribio ambayo yanachunguzwa na yamejaribiwa kwa wagojwa wa virusi vya Marburg kama vile kingamwili za monoclonal, dawa za kuzuia virusi, na plasma ya kupona.

Matibabu haya, hata hivyo, bado hayajaidhinishwa kutumika kwa idadi ya watu kwa ujumla na yanapatikana tu katika muktadha wa majaribio ya kimatibabu, au chini ya itifaki za utumiaji panapotokea milipuko.

Matibabu mengine ni pamoja na kuzuia maambukizi na hatua za udhibiti ili kuzuia kuenea kwa virusi.

Hii ni pamoja na kuwatenga watu walioambukizwa, kutumia vifaa vya kinga binafsi, kama vile glavu, barakoa, na gauni, na kutekeleza hatua kali za usafi, kama vile kunawa mikono na kufunika mwili na nyuso, hususan unapohudumia au kushika mgonjwa mwenye maambukizi.

Ni muhimu kutambua kwamba utambuzi wa mapema na matibabu ya haraka ya ugonjwa wa virusi vya Marburg unaweza kuboresha nafasi za kuishi.

Kwa hiyo, mtu yeyote anayeshukiwa kuwa ameambukizwa virusi anapaswa kutafuta matibabu mara moja.

Tafiti nyingi zinependekeza kwamba kutokana na milipuko hii inayotokea kwa binadamu kutoka kwa wanyama ni vyema mbinu ya ‘Afya Moja’ ikatumika katika kukabiliana na maambukizi haya.

‘Afya Moja’ ni mbinu inayoruhusu ushirikiano baina ya wataalamu wa afya kutoka katika sekta zote kama za binadamu, wanyama na mazingira kufanya kazi pamoja katika kugundua vihatarishi, kupambana na kutokomeza magonjwa haya pamoja na yale yote yanayohusisha binadamu, wanyama, mimea na mazingira.

Dk Sima Rugarabamu ni mtaalam wa microbiolojia anayefanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Kwa mrejesho, anapatikana kupitia sima.rugarabamu@sacids.org. Ungepanda kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts