The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Haya Ndiyo Yaliyofanya Dira ya Taifa ya 2025 Isifanikiwe Kikamilifu. Mchakato wa Dira ya 2050 Waanza

Dhamira ya Serikali katika maandalizi ya Dira ya 2050 ni kushirikisha Watanzania kutoka pembe zote za nchi

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Umasikini ni miongoni mwa mwa sababu zilizopelekea malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 kutofikiwa kwa ukamilifu .

Haya yameelezwa leo na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango akizindua Mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 leo jijini Dodoma.

“Pamoja na hatua kubwa iliyofikiwa nchi yetu bado imeendelea kukabiliwa na changamoto, tunakabiliwa na changamoto ya umaskini wa kipato na lishe duni,” amesema Dkt. Mpango kwenye uzinduzi huo.

Dira ya Taifa ya 2025 inayotegemewa kumalizika mwaka 2025, ilianza kuandaliwa  mwaka 1995 na kuzinduliwa mwaka 1999. Lengo kuu la dira hiyo lilikuwa kuweka kwa pamoja malengo na ndoto ya taifa baada ya miongo mingi toka Azimio la Arusha ambalo halikua na kipindi maalum.

Baada ya mabadiliko ya kiuchumi yaliyopelekea Azimio la Arusha kutokunakisi hali halisi, Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamini William Mkapa aliamua kuja na mchakato utakaoweka matamanio, ndoto na matumaini ya taifa pamoja.

Malengo makuu ya dira ya taifa 2025 ilikua ni kufikia uchumi wa kati na kuwa na taifa lenye hali bora ya maisha kwa watu; amani, umoja na utulivu; uongozi bora; jamii iliyoelimika na uchumi wenye ushindani.

Akitoa tathmini ya utekelezaji wa Dira ya 2025, Dk Mpango alisema pamoja na kipato cha Watanzania kuongezeka bado asilimia 26.4 ya watanzania wanaishi chini ya kiwango cha umaskini. Huku mikoa kama ya Kagera, Kigoma, Singida, Tabora na Dodoma inaonesha kiwango chake cha umaskini kuwa kikubwa zaidi kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kihistoria na mindombinu duni.

Kuhusu utawala bora Dkt Mpango amesema mbali na nchi kupiga hatua katika kujenga na kuimarisha utawala wa sheria, haki na demokrasia bado zipo changamoto za rushwa.

Akieleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika Dira ya Taifa ya Mwaka 2025 Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema moja ya mafanikio makubwa ni katika elimu.

“Hakuna kijiji kimoja kinachotokea wanafunzi wanamaliza darasa la saba wote na hakuna aliyechaguliwa, imeshafutika kabisa.”amesema Dk Nchemba. “Kwa hiyo tumetoka upande mwingine na tukaenda upande mwingine kabisa. Na hata hivyo akitokea mwanafunzi mmoja ama wawili ama watatu hajaendelea kwenda kidato cha kwanza sasa ni jambo la ajabu.”

Kwa upande wa pili Dk Mpango alisema licha ya kupata jamii iliyoelimika vyema na inayojifunza, bado vijana wengi wanaomaliza masomo hawapati fursa za ajira. Lakini pia elimu iliyopo haikidhi mahitaji ya soko la ajira wala kuwezesha wahitimu kujiajiri.

Akielezea kwa upande wa uchumi imara na shindani, Dk. Mpango amesema licha ya kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi iliyofikiwa katika karne mbili zilizopita, bado uwezo wa ushindani ni mdogo.

“Inahitajika kuongeza imani ya wawekezaji katika azma yetu ya kujenga mazingira mazuri kwa biashara na uwekezaji.Vilevile, bado, bajeti ya Serikalini tegemezi kwa asilimia 13 kwenye misaada.”amesema.

“Hali kadhalika, uwezo wa Taifa letu wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi nao ni mdogo, hali ambayo imeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za uzalishaji hususan kilimo na ufugaji na huduma muhimu kama upatikanaji wa maji na nishati ya umeme. Tunashuhudia pia uharibifu mkubwa wa miundombinu na kuenea kwa magonjwa yanapotokea mafuriko.”

Kwa kuzingatia baadhi ya changamoto alizozitaja na mabadiliko ya haraka yanayoendelea duniani, hususan ya kiteknolojia, kiuchumi, na mazingira Dkt. Mpango amesema maandalizi ya Dira 2050 yanapaswa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha uwezo wa uchumi uliojengwa hadi sasa na kutumia fursa za kimkakati.

“Tanzania ina fursa kubwa ya kuwa ghala la chakula katika Bara la Afrika au hata Mashariki ya Kati, tukilenga uzalishaji mkubwa wa mahindi, ngano, shayiri, soya, sukari, mafuta ya kupikia, korosho, matunda, mbogamboga, na viungo.”

“Uzoefu unaonesha nchi nyingi zinaganda kwa muda mrefu katika Uchumi wa Kipato cha Kati au kurudi nyuma. Tuangalie nini kiini cha hali hiyo na namna gani Dira ya 2050 itasaidia kutuvusha kwa kishindo kutoka katika hatua hii tuliyofikia sasa.” Alisisitiza zaidi Dk.Mpango

Mpango amesema dhamira ya Serikali katika maandalizi ya Dira hii ni kushirikisha Watanzania kutoka pembe zote za nchi, kutoka matabaka mbalimbali watapata nafasi ya kuchangia mawazo yao. Hivyo kuwataka wadau wote kutoa ushirikiano kwa Timu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackiline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *