The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Elizabeth Maruma Mrema: Mfahamu Mtanzania Aliyetajwa Miongoni Mwa Watu 100 Mashuhuri na Jarida la TIME

Mzaliwa wa Moshi, Kilimanjaro, mchango wa mwanamama huyo kwenye utunzaji wa mazingira umemfanya ajizolee tuzo mbalimbali ulimwenguni.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mtanzania Elizabeth Maruma Mrema amekuwa mmoja kati ya watu 100 waliotajwa na jarida la TIME, la nchini Marekani, kama watu wenye ushawishi mkubwa duniani, likimtambua kwa mchango wake katika uhifadhi wa mazingira.

Akiwa kama Katibu Mkuu wa Mkataba wa Anuwai ya Kibiolojia, mkataba wa kimataifa wa ulinzi wa anuwai ya kibiolojia, Mrema alifanikisha kuyashawishi mataifa ya kidunia kukubali kuunga mkono juhudi za kuhifadhi mazingira kwenye asilimia 30 ya ardhi na maji ulimwenguni kote mpaka kufikia 2030.

Jarida la TIME limeitaja hatua hiyo kama “moja kati ya ushindi mkubwa wa kimazingira” uliojitokeza kwenye kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Mrema anatajwa kusukuma makubaliano hayo, akifanikiwa kuwaunganisha wahawilishi kutoka nchi takriban 195, kitu ambacho TIME kinaona siyo cha kawaida, hususan ukizingatia namna mjadala wa mazingira unavyowagawa watu.

Makubaliano hayo, ingawaje hayana nguvu ya kisheria, yanategemewa, kinadharia, kuzisaidia nchi zinazoendelea kama Tanzania kupata fedha za uhifadhi wa mazingira, yataondosha ruzuku zinazoharibu mazingira, pamoja na kulinda haki za jamii za wenyeji.

Kwa sasa akifanya kazi kama Naibu Katibu Mkuu wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP), Mruma ni mwendeshaji mwenza wa kikosi kazi kinacholenga kuweka viwango vya namna makampuni yanavyoweza kuweka kwenye mahesabu namna shughuli zao zinavyoathiri mazingira.

Mkazi wa Montreal, nchini Canada, Mrema alizaliwa mnamo Januari 5, 1957, huko Moshi, mkoani Kilimanjaro. Alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Katibu Mkuu wa Mkataba wa Anuwai ya Kibiolojia, ingawaje kabla ya hapo alishahudumu nyadhifa kadhaa ndani ya UNEP.

Mrema alipata shahada yake ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kabla ya kwenda kufanya shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Dalhousie, kilichopo nchini Canada.

Mrema pia alisomea diploma ya uzamili (postgraduate diploma) kutoka Chuo cha Diplomasia, Kurasini, jijini Dar es Salaam.

Mbali na majukumu yake ya kiuongozi, Mrema pia alishawahi kufanya kazi kama mhadhiri katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya, pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Sheria (IDLO), lililopo Rome, Itali.

Mnamo mwaka 2007, Mrema alikuwa mtu wa kwanza kupokea tuzo ya UNEP Baobab Staff Award kwa “utendaji wake kazi wa kipekee na kujitoa kwenye kufanikisha malengo ya UNEP.”

Mwaka 2021, alitunikiwa tuzo ya Nicholas Robinson Award for Excellence in Environmental Law kwa mchango wake kwenye sheria za kimazingira.

Mnamo mwaka 2022, Mrema, 66, alitunukiwa tuzo ya Kew International Medal na Royal Botanic Gardens, Kew, kwa mchango wake kwenye “kupigania umuhimu wa uhifadhi wa bioanuwai.”

Kwa kuwekwa kwenye orodha hiyo na jarida la TIME, Mrema ametambuliwa pamoja na watu mashuhuri wengine kama mwanamuziki Beyoncé, mwanasoka Lionel Messi, na mwigizaji Michael B. Jordan, pamoja wa watu wengine kadhaa ambao mchango wao katika kuifanya dunia iwe bora zaidi umetambuliwa.

Kila mwaka, jarida la TIME hutoa orodha ya watu 100 ambao wamekuwa na ushawishi mkubwa kwenye kuifanya dunia iwe sehemu bora zaidi. Watu hawa hupatikana kwa njia ya wazi kwa wananchi ulimwenguni kote kupiga kura.

Kuwekwa kwenye orodha hiyo kunatafsiriwa na wengi ulimwenguni kama ishara ya heshima kwa mhusika, hususan kutokana na msisitizo wa jarida lenyewe la TIME kwamba ni watu ambao matendo yao yameibadilisha dunia tu ndiyo wanaoweza kuwekwa kwenye orodha hiyo.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *