The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ida Hadjivayanis Aichambua ‘Peponi’ Ya Abdulrazak Gurnah

Asifu hatua ya Serikali kufadhili kazi za uandishi bunifu; asema haoni uamuzi huo ukikinzana na dhana ya uhuru wa mwandishi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mnapo Aprili 16, 2023, mwandishi wa The Chanzo, Khalifa Said, alifanya mahojiano maalum na Ida Hadjivayanis, Mtanzania anayeishi nchini Uingereza ambaye ameitafsiri riwaya ya Paradise ya mshindi wa tuzo ya Nobel Abdulrazak Gurnah kwenda Kiswahili na kuiita Peponi.

Hatua hiyo ilitokana na kuwepo kwa uhitaji kutoka kwa wasomaji wa Kiswahili kusoma kazi za fasihi za Gurnah, Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo hiyo. Peponi ni kazi ya kwanza iliyotokana na ushirikiano kati ya Hadjivayanis na wachapishaji Mkuki na Nyota.

Kwenye mahojiano hayo, Hadjivayanis alikichambua kitabu hicho pamoja na kutueleza anavyomfahamu Gurnah. Hadjivayanis pia alizungumzia kuhusu Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, ikiwa ni kati ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kukuza uandishi, usomaji, na uchapishaji nchini.

Hapa Hadjivayanis anaanza mahojiano yetu kwa kutueleza Ida Hadjivayanis ni nani haswa?:

Ida Hadjivayanis: Mimi ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha SOAS, University of London. SOAS maana yake ni School of Oriental and African Studies. Kwa hiyo, hiki ni Chuo Kikuu ambacho kwa zaidi ya miaka 100 kimekuwa kinafundisha masomo ya Kiafrika na masomo ya Asia na Mashariki ya Kati.

Kwa hivyo, niko hapo na ninafundisha Kiswahili na tafsiri. Pia, ninafundisha masomo yote ya Bahari ya Hindi, magharibi ya Bahari ya Hindi. Kwa hivyo, hii pwani ya mwambao [wa Afrika Mashariki] ndiyo masomo yangu.

Nimefanya PhD yangu hapo hapo SOAS ambapo ndiyo ninafundisha na nilisoma Kidato cha Tano na Sita hapa Dar es Salaam, Zanaki [Sekondari] masomo ya KLF, [yaani] Kiswahili, Kiingereza, na Kifaransa.

Kwa hiyo, Kiswahili ni lugha ambayo nimesoma kwa miaka mingi na naipenda sana. Nafikiri labda mimi ndiyo huyo.

The Chanzo: Sawasawa. Pengine utuambie mchakato wa kutafsiri hiki kitabu ulianza vipi, yaani ni nini kilikusukuma wewe, au nyinyi, kuamua kwamba hiki kitabu inabidi tukitafsiri kwenye lugha ya Kiswahili?

Ida Hadjivayanis: Sasa jibu langu kwa kweli litakuwa si jibu la kitaaluma. Kwa sababu ukweli ni kwamba mimi nimekuwa nikimsoma Abdulrazak Gurnah kwa miaka mingi, tangu mwaka 2003, na ni mwandishi ambaye nampenda sana.

Kama kuna chake kinatoka, huwa ninaagiza kabla [ya kuchapishwa] kwamba nataka nikisome, kikitoka tu nikipate.

Lakini unakumbuka kulikuwa kuna ugonjwa wa UVIKO-19 ambao ulitokea miaka miwili [au] mitatu iliyopita na mimi niliumwa sana. Niliumwa sana UVIKO-19. Niliumwa nikawa hospitali kwenye koma.

The Chanzo: Pole sana.

Ida Hadjivayanis: Asante! Nilipoamka, unajua unakuwa huwezi kufanya vitu vingi, kama kuzungumza. Mwili unakuwa kama umepooza na nilipata miezi sita ya kupumzika nyumbani.

Katika muda ule, nilikuwa na daktari akaniambia lazima utumie akili yako kwa sababu bila hivyo, wewe ni mtu wa kufundisha utasahau mengi. Nikasema, kwa hiyo? Akasema labda tafsiri au andika.

Nikasema hebu nitafsiri Paradise. Kwa hivyo, nikaanza kutafsiri Machi mwaka 2021, yeye akashinda mwaka 2021 Oktoba. Kwa hivyo, alivyoshinda tuzo mimi nilikuwa nimeshatafsiri kama theluthi mbili ya kitabu tayari. Na nilitafsiri kweli ni kama, wanasemaje, ilikuwa ni kama dawa kwangu mimi na ndiyo maana.

The Chanzo: Kwa hiyo, mimi pengine nilidhani kwamba uamuzi wa kutafsiri ulitokana na hatua ya yeye kushinda tuzo ya Nobel?

Ida Hadjivayanis: Hapana. Mimi nilishaanza kumtafsiri tangu mwanzo. Na pia nikuambie. Mimi nimekuwa nikifundisha kazi zake kwa sababu mimi hapa nafundisha pia masomo ya Bahari ya Hindi. Kwa hivyo, Gurnah ni mtu ambaye anaandika hasa kuhusu mwambao wa Afrika Mashariki, hasa Zanzibar, ndiyo mandhari ya maandiko yake na pia Tanzania, Kenya [na] maeneo hayo.

Kwa hivyo, hata nilipoamua kwamba ningependa kutafsiri yaani hakukuwa na muda wa kutafakari kwa muda mrefu. Nilijua palepale kwamba ni Gurnah. Kwa sababu nilishafahamu kwamba watu wengi hawajamsoma hapa.

Ni kitu ambacho kwangu mimi ni kwamba kinasikitisha. Kwa sababu unajua kabla ya kushinda tuzo Gurnah, ambaye ni mhamiaji kule, siyo mtu ambaye anasomwa na watu wengi wa Uingereza au Ulaya.

Watu wanaomsoma ni wachache. Lakini hata kwao pia hasomwi, alikuwa. Kumbe nikafikiri labda nimtafsiri Gurnah. Kwa hivyo, itakuwa kama dawa kwangu na pia ndipo atapata kuja kujulikana.

The Chanzo: Sawasawa. Wewe umekisoma hiki kitabu na umekitafsiri. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba unaweza ukawa unakifahamu zaidi kuliko msomaji mwingine wa kawaida. Unadhani kwa nini msomaji asome hiki kitabu?

Ida Hadjivayanis: Hiki kitabu kinatuonesha sisi historia yetu.

The Chanzo: Sisi watu wa mwambao?

Ida Hadjivayanis: Sisi watu wa mwambao na watu wa Tanzania Bara na watu wa Kenya pia, haswa. 

Kwa sababu, watu wengi wanazungumzia kuhusu masuala ya Afrika, wanazungumza kwamba kabla ya ukoloni hapa Afrika nzima watu walikuwa na maisha ya raha, walikuwa wana amani nyingi, ilikuwa hakuna matatizo, alipokuja mkoloni ndiyo likaja balaa, matatizo yakataokea.

Lakini Gurnah anaonesha kwamba hiyo si kweli. Ukweli ni kwamba kabla ya kuja kwa mkoloni tayari hapa kulikuwa na makabila tofauti: kulikuwa na Wahindi, kulikuwa na Waarabu, Wasomali, Waswahili wenyewe, Waswahili wale wa mwambao na watu wengine, Waafrika wengine, wa sehemu zingine za Afrika.

Na hawa watu walikuwa na lugha zao. Walikuwa na mila zao na njia zao za kuishi na waliweza kuwa pamoja. Hakukuwa na migongano mikali kiasi hicho.

Kwa hiyo, anatuonesha kwamba historia ambayo tunaifahamu labda si kweli kama tunavyofikiri ilivyokuwa. Kwa hiyo, hiyo ni muhimu kwangu mimi hapa kwamba tunaona ukweli wa maisha kabla ya kuja kwa mkoloni.

Halafu pia kitu ambacho amefanya Abdulrazak Gurnah ni kwamba amejumuisha maandiko ambayo yaliandikwa na Waswahili zamani kwenye kitabu hiki. Kwa hivyo, kwa mfano, kulikuwa na mtu mmoja ambaye anapenda kusafiri anaitwa Suleiman bin Mwinyichande.

The Chanzo: Muhusika?

Ida Hadjivayanis: Siyo mhusika wa kitabu hiki, ni kitabu tofauti.

The Chanzo: Sawa.

Ida Hadjivayanis: Huyo Suleiman bin Mwinyichande yeye alitoka Comoro, yaani Ngazija, akaja Zanzibar, akafanya kazi na Wajerumani wakamchukua kwenye safari akaenda Urusi na Ujerumani. Hapo ni mwaka 1896.

Alipokwenda kule, akaandika kitabu, akaandika kuhusu safari zake kwamba amekwenda huku ameona watu wanafanya hivi, watu weupe wako hivi. Na zile simulizi zake Abdulrazak Gurnah amezijumlisha kwenye hadithi hii. Kwa hivyo, huku kuna hadithi zetu sisi ambazo watu wengi hawakuzifahamu.

Watu wengi wanafikiri kwamba kuandika kumeanza baada ya kuja kwa mkoloni, hapana. Hawa watu walikuwa wanaandika simulizi kabla kabisa. Kwa hivyo, Gurnah amezijumlisha humo ndani. Kuna mpaka simulizi ya Tipu Tipu kwenye kitabu hiki.

Kwa hivyo, kuna simulizi nyingi ambazo nazifahamu zimo humu. Pia zimo za Alfu Lela U Lela. Kwa hiyo, kwangu mimi ni kwamba kuna simulizi, kuna hadithi ambazo ni zetu zimejumlishwa humo ndani.

Halafu kwanza ukisoma hiki kitabu, hiki kitabu kinahusu muhusika mkuu anaitwa Yusuf. Na Yusuf amefinyangwa tofauti kiasi lakini ni Yusuf yule tunayemfahamu kwenye Quran na kwenye Biblia kama Joseph.

Kwa hivyo, amechukua ile hadithi ya Yusuf ameibadilisha na kumfanya kijana wa Kiswahili. Kwa hiyo, Yusuf ni kijana mzuri sana. Kila mtu anayemuona anampenda. Wanawake wakimuona mpaka wanajikata vidole kwa uzuri wake.

Halafu Yusuf anasafiri, baba yake anakuwa anamuweka rehani. Baba yake anakuwa anadaiwa pesa, hawezi kulipa, anamuweka rehani. Yusuf anakuwa mtumwa. Na katika ule utumwa, anasafiri sasa kutoka mwambao anakwenda mpaka Umanyema, Kigoma kule.

Katika hizi safari, anaona watu wengi, makabila mengi, na ndiyo hizi hadithi ambazo unaona humo ndani.

The Chanzo: Kwa hiyo, peponi inasadiki kitu gani?

Ida Hadjivayanis: Labda naweza nikakuambia kuna ukurasa mmoja nitakuambia baadaye. Ni kwamba peponi ni hapa [tulipo, duniani] ndiyo peponi. Labda itabidi usome mwenyewe uone lakini jinsi Abdulrazak Gurnah anavyoongelea ni kwamba hii nchi, wakati ule, ilikuwa ni nzuri sana. Ilikuwa imesheheni. Ina watu tofauti na ndiyo ikawa pepo yenyewe ndiyo.

The Chanzo: Mrejesho kutoka kwa mwandishi wa Paradise ambayo wewe umetafsiri kuwa ni Peponi, bwana Abdulrazak Gurnah, amekipokeaje hiki kitabu?

Ida Hadjivayanis: Amefurahi, amefurahi sana. Unajua bwana Abdulrazak Gurnah ni mtu mstaarabu sana. Kwa hivyo, nilipokuwa natafsiri nikamuambia Abdulrazak. Kwanza, nirudi nyuma kidogo.

Mimi baada ya kumsoma mwaka 2003, nilifurahi mno. Nikamuandikia barua pepe. Nikamuambia mimi naitwa Ida – wakati huo ndiyo kwanza nimeanza kufanya PhD yangu – naitwa Ida nimesoma kitabu chako, nimependa sana, maana yake yaani naona kabisa ni vitu yaani ni vitu ambavyo vinahusu mimi na historia yangu.

Akanijibu, akaniambia nimefurahi kama umependa kazi yangu. Ikawa mara kwa mara nikisoma kitabu chake, namuandikia na ananijibu.

Ni mtu ambaye watu wengi ambao wanampenda, yaani wanasoma kazi zake, watakuambia nilimuandikia, akanijibu. Hata leo ukimuandikia atakujibu. Yaani ni mtu wa aina hiyo.

Kwa hivyo, nikamuambia kwamba Abdulrazak mimi natafsiri, akaniambia hiari yako. Nikamuambia sawa na sasa hivi amefurahi sana. Ananambia kwamba watu watapata kusoma kitabu katika lugha yao.

Na pia nimejaribu kutumia lugha ambayo yeye angeitumia kama angekuwa anakiandika. Kwa sababu yeye ni mtu wa Zanzibar, na anaongea Kiswahili kwa lafudhi ya Kiunguja. Kwa hivyo, nilijaribu kufanya hivyo.

The Chanzo: Kazi ya utafsiri bila shaka si kutoa maneno kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine, si ndiyo? Ni zaidi ya hapo. Unaweza kutuelezea labda pengine ilikuwa ngumu kiasi gani, au rahisi kiasi gani, kwenye mchakato huu mzima?

Nakuambia hivyo kwa sababu mimi nimebahatika kusoma vitabu vya Kiingereza ambavyo vimetafsiriwa kutoka Kifaransa. Na nachelea kusema kwamba nahisi kama nakosa ladha, yaani kuna kitu fulani hivi nakosa.

Yaani hiyo, kama mtafsiri, unachukua jitihada gani kuhakikisha kwamba ndiyo nabadilisha haya maneno kutoka lugha hii kwenda lugha hii, lakini unadumishaje yaani ile ladha ya kile kitabu?

Ida Hadjivayanis: Sasa subiri nikuambie. Bahati iliyopo ni kwamba hiki kitabu kimeandikwa kwa Kiingereza lakini mimi katika mawazo yangu ninavyokisoma, ninahisi kwamba Abdulrazak alikuwa anafikiri kwa Kiswahili pia alipokuwa anaandika.

Na ndiyo maana ninasema kwamba hii tafsiri ni kwamba imerudisha nyumbani kazi ya Kiingereza. Kwa hivyo, kwa kitabu hiki yaani hasa ni kwamba sikuwa na tatizo lile la kwamba ni kujaribu kufikiria sasa kwenye utamaduni huu tunasemaje.

Nilitafsiri kitabu cha Alice in WonderLand kama Alice Ndani ya Nchi ya Ajabu mwaka 2015 na hapo ilikuwa ngumu. Kwa sababu ni kitabu ni cha Kiingereza, kinatokea Uingereza, yule mtoto ni Mwingereza na vitu vingi ambavyo sasa nitasemaje unakuta vitu kama tart ni viite vileja, maana yake sijui vileja sijui niseme nini.

Lakini kwa kazi ya Abdulrazak hiyo haikuwa tatizo kabisa. Lakini sasa nikuambie kwa mtu ambaye anataka kutafsiri, mimi nafikiri kwamba kitu muhimu cha kwanza lazima ufahamu unamtafsiria nani? Kama unapoandika unafikiri unamuandikia nani.

Ukishafahamu hadhira yako – kama itakuwa watoto, watu wazima, watu wa kawaida wa umri fulani – utafahamu ni lugha gani unataka kutumia. Halafu cha pili, nafikiri, ni kwamba lazima ukubali ni kwamba unapotafsiri kuna kitu ambacho kwa Kiingereza kinaitwa loss. Lazima utapoteza vitu. Lakini pia kuna vitu utavipata, lazima utapata raha zaidi.

Kama nilivyokuwa natafsiri kitabu hiki, tuseme, kuna sehemu anasema, kuna huyu mhusika mmoja anaitwa Ami Aziz, tunamuita Ami, kwa sababu ni kama ndugu upande wa baba.

Ami Aziz ni mtu ambaye anapenda magendo. Kwa hivyo, ameweka vipusa kwenye mashamba ilikuwa ni kama maeneo ya Moshi. Basi sasa Mjerumani anakuwa anawakamata wale wanaofanya biashara za vipusa, kwa hiyo vimefichwa kule.

Sasa kwenye Kiingereza imeandikwa kwamba alikuwa ameweka magendo, big money. Yaani ni magendo. [Mwandishi] ameweka neno magendo kwa Kiswahili. Kwa sababu anaweka sana Kiswahili kwenye kazi zake, [ameweka] big money.

Lakini kwa Mswahili anavyosoma anajua kwamba magendo siyo tafsiri ya big money. Ni kwamba utapata ndiyo pesa nyingi lakini kuna zaidi ya hapo. Kwa hivyo, kwa Mswahili, sijui kama umenielewa, kwa mtu ambaye ni Mswahili anapata zaidi kuliko yule Muingereza ambaye labda atafikiri magendo maana yake ni pesa nyingi.

The Chanzo: Na mchakato lazima uwe shirikishi?

Ida Hadjivayanis: Una maana gani?

The Chanzo: Namaanisha kwamba kati yako wewe mtafsiri na mwandishi? Kwa sababu, kwa mfano, kuna hiyo loss ambayo umesema. Mwandishi hatapenda, kwa mfano, akiona kwamba kuna upotevu pengine mkubwa kwenye kitu fulani, si ndivyo?

Ida Hadjivayanis: Ndiyo!

The Chanzo: Na nadhani pia kwa sababu mchakato kuwa shirikishi ni muhimu [kwa sababu] mimi hapa nina kazi inabidi niitafsiri kwa ajili ya chombo chetu cha habari. Kwa hiyo, wamefanya kwa Kiingereza wakaomba kwamba The Chanzo tunaweza kuitafsiri kwa Kiswahili na kaiandika Muingereza, japo inahusu Tanzania, lakini kaandika Muingereza.

Na hapa nimeipitia sasa inabidi nimrudie, nimuambie kuna vitu itabidi tuvibadilishe kulingana na hiyo dhana yako unayosema kwamba unamtafsiria nani. Lakini turudi pengine kwenye uamuzi wa kutafsiri hiki kitabu. Unadhani ni muhimu kiasi gani kwa kazi za fasihi nyingi zaidi kupatikana kwenye lugha ya Kiswahili?

Ida Hadjivayanis: Pengine nilisema pale kwenye tuzo [ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu] siku ile. Nafikiri kwamba hakuna raha duniani, kweli kabisa, hakuna uhondo ambao mtu unapata kama unaposoma kwenye lugha yako mama. Kwa sababu ile ni lugha ambayo unaielewa, ni lugha ambayo itikadi zake umekuwa nazo. Kwa hivyo, unaposoma kwenye yako unaelewa papo hapo.

Vitu vingi yaani unavipata kwamba, mfano mmoja, tuseme kuna wazee watatu kwenye Kiingereza wanasema kuna wazee watatu wanakaa nje ya duka. Tunasema sawa lakini kwa mtu ambaye amekulia kwenye eneo lolote la Tanzania yaani wale watatu wale anawajua.

Kwa sababu kila duka litakuwa lina baraza, sijui benchi, wamekaa wazee wanazungumza au hata mfano tukichulia kule Zanzibar, kuna baraza kila kona, kuna vijiwe kila mahali, watu wamekaa wanapiga gumzo. Kwa hiyo, unaposoma kwenye lugha yako mwenyewe unaelewa na unaona yaani unaweza kuona kabisa kitu gani kinaongelewa.

Lakini kwa yule ambaye mfano anasoma kwa Kiingereza anahisi tu hawa watu wamekaa tu nje ya duka, kwa hiyo? Kuna kitu fulani. Kwa hivyo, ni muhimu sana kusoma kwenye lugha yako wewe mwenyewe.

Kwa sababu kusoma ndiyo kunatanua mawazo yako, kunapanua fikra yako jinsi unavyoona dunia, lazima kusoma na lazima kutafsiri zaidi.

The Chanzo: Mimi kwa uzoefu wangu, kama msomaji, naweza nikasoma kitabu cha Kiingereza na nikaweza kutafsiri, lakini nikakosa maana. Na nadhani pengine hicho ndicho unachomaanisha kwamba ukisoma kwa lugha yako unapata maana, ile halisi, ambayo mwandishi ameikusudia.

Ida Hadjivayanis: Kabisa kabisa, na ndiyo maana kuweza kutafsiri unatafsiri maana kwa maana na siyo maneno kwa maneno. Tafsiri ya maneno kwa maneno haina maana. Juzi niliona kuna filamu, sawa basi, naona tuache hizo, maana yake sitaki kukosoa mtu.

Kulikuwa kuna filamu ambapo watu wanacheza [bao], yule mmoja akasema kwamba, “Wewe umekula, umekula zaidi hapo,” kwenye bao. Lakini tafsiri ikawa kwamba you have eaten. 

Kwa Muingereza lazima atasema amekula nini, kuna keki pale? Hakuna. Hivyo angesema, you are cheating. Kwa hivyo, huyu kwa Kiswahili anasema umekula lakini siyo yaani kama umekula. Kwa hivyo, nafikiri lazima maana, bila maana [tafsiri] inapoteza vitu.

The Chanzo: Sawa kabisa. Na nadhani raha ya kusoma ni kupata maana.

Ida Hadjivayanis: Kweli, kweli kabisa.

The Chanzo: Maana unaweza ukasoma kitabu chote bila ya kupata maana na itakuwa umepoteza muda, hiyo ni nzuri sana. Na sasa hiyo unaizungumziaje kwenye muktadha wa tuzo hii ambayo Serikali imeanzisha, Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Julius Nyerere ya Uandishi Bunifu, japo Waswahili pale walisema wana tatizo na uandishi bunifu, na mimi pia nina tatizo.

Ida Hadjivayanis: Unahisi ingekuwa vipi?

The Chanzo: Ubunifu. Kwa sababu mimi naona kama wametafsiri creative writing – kama hivyo tunavyozungumza neno kwa neno – uandishi bunifu, creative writing. Lakini hamna shida.

Ida Hadjivayanis: Nilipokuwa nimetoka uwanja wa ndege juzi niliona kitu tofauti, niliona tangazo wameandika, “Hii ina bei rafiki.” Nikasema bei rafiki, huh? Friendly price? Ni  nini? Kwa hivyo, ndiyo kama vile nilivyokuambia.

Sasa subiri naomba nikuambie kidogo historia fupi kama tutakuwa sawa. Na wewe ulikuwepo pale kwenye tuzo?

The Chanzo: Na wewe ulikuwepo pale kwenye [ugawaji wa] tuzo.

Ida Hadjivayanis: Nilikuwepo. Kwa hiyo, mimi ninavyofahamu kwamba unajua sisi hapa kwenye Kiswahili tuna historia ndefu sana ya kuandika mashairi.

Mashairi yameandikwa tangu karne nyingi zilizopita na hata mswada mkongwe kuliko wote ambao tunao, mingi iliteketea, unaitwa unaitwa Hamzia, ambalo ni shairi ya shairi lililoandikwa karne ya 13 ndiyo tunayo hiyo sisi hapa.

Na kwa miaka mingi tumekuwa na maandiko ya mashairi lakini riwaya kwa kusema kweli ililetwa na utawala wa kikoloni. Na ilikuja baada ya wakoloni kuamua kwamba Kiswahili kiandikwe kwa Kilatini na siyo kwa Kiajemi, yaani kwa Kiarabu.

Kwa hiyo, sasa wale wameamua kwamba lazima kiandikwe kwa Kilatini walihitaji kuwa na kazi katika lugha ile, katika maandiko yale mapya, watapata wapi hizi kazi waweze kuzisoma, ikabidi tafsiri.

Kwa hiyo, zikafanywa tafsiri nyingi sana kama Mashimo ya Mfalme Suleiman, [ambacho muhisika wake mkuu ni Allan Quatermain. Yaani, zikafanywa nyingi [kama] Alice Katika Nchi ya Ajabu pia zikafanywa tofauti zikiwa nyingi sana. Na zile– Alfu Lela U Lela – zile zikatoa chachu kwa waandishi kuandika.

Kwa hiyo, utaona kama vile miaka ya 50 Shaaban Robert anakuja kuandika Adili na Nduguze [na] Kusadikika ni kwa sababu alipata msisimko kutokana na tafsiri zilizofanywa na wakoloni.

Na pia tunaona kwamba miaka ya [19]70 wakati wa uhuru, 60, 70 wakati wa uhuru utakuta wakati ule pia kuna vitabu vya kikombozi. Kulikuwa na tafsiri kama za Shujaa Okonkwo, [ambacho ni tafsiri ya] Things Fall Apart, Barua Ndefu Kama Hii, [iliyotafsiriwa kutoka] So Long a Letter, na kadhalika.

Na zile zikawapa watu chachu za kusisimua kutaka kuandika. Lakini kumekuwa na kudorora kwa maandiko na kwa muda sasa.

The Chanzo: Ya Kiswahili?

Ida Hadjivayanis: Kiswahili, ndiyo. Yako yanaandikwa lakini sijui kama ni hadhi ambayo labda yetu hasa. Nafikiri kuna umuhimu wa sisi kujaribu kuandika vizuri zaidi, hata kutafuta mada nyingine pana zaidi.

Kwa hivyo, unaposoma kazi kama hizi, unaangalia jinsi huyu mwandishi anavyoandika, au anavyosimulia, wewe inakupa chachu ya kuandika pia. Kwa hivyo, kama mfano ukimsoma Abdulrazak, ukamsoma Ngũgĩ [wa Thiong’o], ukamsoma Chimamanda [Ngozi Adichie], ukamsoma [haisikiki] watu wote hawa unapowasoma wanakushajihisha wewe mwenyewe kupata njia zako za kuandika.

Na ndiyo maana kitabu kama Peponi kilichoambiwa kwamba kimeshinda Nobel, mwandishi kashinda Nobel, kitawapa uwezo wa kuandika kwa sababu kitawasisimua waone kumbe unaweza ukaandika hivi ni hivyo.

The Chanzo: Na hapo sasa tunakuja, unadhani, unatathimini vipi sasa hii tuzo, au uamuzi wa Serikali kuja na hii tuzo? Unadhani [au] unaamini kabisa kwamba inaweza ikachochea mabadiliko chanya kwenye tasnia ya uandishi?

Ida Hadjivayanis: Kabisa kabisa. Mimi nilikutana na [Waziri wa Elimu] Profesa Adolf Mkenda [na] kwa kusema kweli katika mawaziri wachache ambao nimekutananao huyu ni waziri kabambee.

Yaani ni mtu ambaye unaweza ukamuona kwamba ni mwanazuoni, ni mtu ambaye anathamini kusoma, kuandika na kwa kufanya hii yaani kiukweli ukiwaona wale vijana walivyokuwa wanafurahi kushinda tuzo.

Hata wale waliyopewa vyeti furaha iliyowapa, wakasema, “Mwakani mimi nashinda. Leo nimekuwa mtu wa saba, lakini mwakani nakuwa wa kwanza.”

Kwa hiyo, yaani imewasisimua, imewapa ari ya kutaka kuandika na hii tuzo, kwa kusema kweli, mimi nimevutiwa.

Ni kazi nzuri, wana kamati ya watu wa chache ambao wanafahamu wanachokifanya – Aikande Kwayu, Esther [Mngodo], Chambi [Chachage] na Profesa [Penina] Mlama, yaani hawa ni watu ambao wanafahamu kitu gani wanataka, wanaelewa hadhira ya nchi na wameelewa kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa watu kuandika na kusoma na kuchapisha. Tuzo inafanya kazi nzuri!

The Chanzo: Ndiyo, nakubali. Lakini unazungumziaje hii tuzo kwenye muktadha wa uhuru wa mwandishi? Kwa mfano, niseme mimi ni mwandishi wa riwaya, natakiwa niwe huru kwenye kujieleza, kuwa huru kwenye ubunifu. Lakini hapo hapo inabidi Serikali ndiyo inifadhili, ipitie miswaada yangu na nini. Unaona kuna ukinzani wowote, kwa mtazamo wako wewe, kati ya uhuru wa mwandishi na Serikali kufadhili kazi za mwandishi?

Ida Hadjivayanis: Mimi hapa sijaona miswada ambayo imeshinda. Nafikiri kuna umuhimu wa kuona wale walioshinda wanaandika vipi? Tuone jinsi wametumia lugha gani, wameleta mada gani? Labda tutapata kuelewa zaidi.

Lakini nikifikiria Peponi [ambayo] Profesa Mkenda amesema kwamba sasa vitabu hivi vitagawiwa shuleni, Wanafunzi watavisoma, vitaingia kwenye mitaala na vitapelekwa Chuo Kikuu pia.

Na hiki kitabu ni kitabu ambacho mwandishi ana uhuru mkubwa sana. Ametaka kuandika mengi, mengine ambayo yanaweza yakakwaza wengi, na Profesa Mkenda amekisoma, na ameona kwamba kina umuhimu wa kuwepo kwa wanafunzi kusoma.

Kwa hivyo, kutokana na Peponi, ninahisi kwamba suala la uhuru si suala ambalo litaleta tatizo lolote, ninavyofikiri kutokana na Peponi. Lakini kutokana na miswaada, sijaiona hilo, kwa hiyo sifahamu.

Kwa hiyo kwa mawazo yangu ya haraka haraka hakuna kujichuja. Sidhani kama kuna kujichucha ya waandishi. Kwa sababu, tena, Peponi, ni kitabu ambacho mwandishi amejimwaga.

The Chanzo: Lakini kuna kesi nyingine ambazo Serikali za nchi fulani – siyo kwamba lazima iwepo, nauliza tu, kiudadisi – ambapo Serikali inafadhili kazi za waandishi? Kwa sababu pengine wewe upo kwenye hiyo tasnia, [unaweza kutueleza].

Ida Hadjivayanis: Serikali nyingi zinafadhili kazi za waandishi, ndiyo, bila shaka. Kama vile nikifikiria Uingereza. Uingereza wanafadhili sana kazi za waandishi.

Juzi hapa wakati wa Malkia Elizabeth wa Uingereza alipokuwa anatimiza miaka, sijui miaka mingapi ilikuwa, watoto wote wakapewa vitabu, watoto wangu mimi ninao wa miaka tisa [na] kumi, wakepewa vitabu vimefadhiliwa na Serikali ya Kiingereza kuhusu maisha ya Malkia.

Na mle ndani ni hadithi ya mtoto ambaye ni kama Mwafrika, yaani mtoto wa asili ya rangi nyeusi, ambaye anazungumza kuhusu maisha yake na maisha ya Malkia Elizabeth. [Watoto] wamepewa bure nchi nzima.

Kwa hivyo, nafikiri Serikali zote hufanya hivyo. Na ni muhimu. Serikali ndiyo inayowawezesha wasanii. Kama Serikali haitaweza kuwawezesha wasanii hawataweza kufanikiwa. Ni muhimu sana na ni lazima wafanye hivyo.

The Chanzo: Kabisa. Labda tukiwa tunamalizia, tayari tuna juhudi, au jitihada, kama hizi za kwako wewe na akina Mkuki [na Nyota] na umezungumza kabisa kwamba huu mradi unaendelea, kwamba hiki siyo kitakuwa kitabu cha mwisho. Tumeona pia kuna tuzo, mimi na wewe tulikuwepo pale [Hoteli ya] Rotana ilikuwa ni shughuli iliyofana. Ilikuwa, kusema kweli, watu wana bashasha. Kama vile kuna matumaini fulani.

Ida Hadjivayanis: Yaani mimi nimefurahi sana. Nilifanyiwa mahojiano na kijana ambaye yeye aliniambia yeye ana ulemavu wa macho, si kama yule Sheikh aliyesema kwamba yeye kipofu, na akanifanyia mahojiano na ile braile na akanukuu kila kitu ambacho nilikisema, [akiniambia] kwamba umesema hivi umesema hivi.

Nikasema Mungu wangu ulikuwa unasikiliza umeandika. Yaani kulikuwa na msukumo, kulikuwa kuna vijana ambao mmoja wao ameshinda, alikuwa amevaa suti, watanashati vijana. Walikuwa wanafurahi. Wanatuambia mwaka ujao sisi ndiyo tunashinda. Yaani unaona kwamba watu wanafuraha sana. Kuna matumaini.

The Chanzo: Na inashajihisha. Mimi nilikaa na baadhi ya waandishi wachanga. Ikawa inashajihisha kwamba mwakani na mimi nitatuma mswada wangu. Kwa hiyo, kuna hizo juhudi, kuna hizo jitihada. Lakini unadhani kuna kingine ambacho pengine ungependa kukiona kikifanyika kwenye tasnia ya uandishi bunifu, hususan wa kazi za Kiswahili, kuhakikisha kwamba tuna kazi za Kiswahili nyingi? Na umezungumza vizuri pale mwanzo kwamba tupanue wigo wa mada ambazo tunaziandikia.

Ida Hadjivayanis: Unajua nini? Mimi nafikiri kuna umuhimu wa sijui kama Serikali, au jumuiya tofauti, labda kama kuwapa mafunzo vijana, mafunzo ya kuandika. Kwamba unaandika vipi, yaani huku wanafanya kwa ajili ya hadithi fupi fupi.

Warsha za kuwasaidia, hata ikiwa ni siku tatu [au] siku nne, yaani kama zinakupa muelekeo wa jinsi ya kuandika. Unakumbuka yule Mwenyekiti alipozungumza, Profesa [Fikeni E.M.K.] Senkoro, nafikiri, alisema kwamba kulikuwa na wengi waliotuma [miswada] lakini hawakuweza, alisema nini, zile kazi zao zilikuwa hazifai, hazikufaa kwa sababu hawakufuata masharti.

Sasa labda kama wao wenyewe wangekuwa na warsha labda ndogo ndogo za kuwafundisha hawa vijana, waandishi chipukizi, ambao kwamba labda inabidi iwe hivi, inabidi uandike hivi, inabidi ufikirie hivi. Kama ni kufikiri kwenye tafsiri wangefanya warsha.

Ningewaambia kwamba kitu cha kwanza ukumbuke kwamba kuna hadhira, kuna lugha, na kuna utamaduni. Yaani vitu kama hivi kuwapa vijana nafikiri ni muhimu.

Cha pili, nafikiri, inabidi wawahusishe watu kama nyinyi, vyombo vya habari kama nyinyi, ambao mnaweza kuonesha, kufahamisha, vitu gani vinafanywa na Serikali kwa sababu sijui kama watu wengi walipata habari ya ule wito uliotokea mwaka jana.

Nafikiri labda kwenye miji mikubwa watu walisikia, lakini sijui kwenye pembe tofauti za nchi, kama Sumbawanga walisikia, sina hakika. Kwa hiyo, nafikiri vyombo vya habari kama nyinyi mnaweza kupeleka hizi habari kirahisi zaidi ili watu zaidi wapate kutuma maombi yao. Mimi ningesema hivyo, nafikiria zaidi elimu.

The Chanzo: Labda pengine warsha ianzie hapa na hii tutakuwa tunamalizia.

Ida Hadjivayanis: Ndiyo!

The Chanzo: Wewe ni mtafsiri, umetafsiri vitabu kadhaa, kikiwemo hiki cha Peponi. Mimi nataka nitafsiri.

Ida Hadjivayanis: Anha!

The Chanzo: Mimi moja kati ya vitabu ambavyo nimewahi kusoma, na ambavyo vimekuwa na ushawishi mkubwa kwenye maisha yangu, ni kitabu cha Pedagogy of the Oppressed cha Paul Freire.

Ida Hadjivayanis: Freire, ndiyo!

The Chanzo: Nadhani unakifahamu?

Ida Hadjivayanis: Ndiyo.

The Chanzo: Nikitaka kutafsiri kile kitabu naanzia wapi na amefariki mwenyewe?

Ida Hadjivayanis: [Anacheka].

The Chanzo: Na amefariki mwenyewe.

Ida Hadjivayanis: Anha, kwa hiyo, kitu cha kwanza ni kwamba inabidi uangalie ni nani aliye na haki, nani mwenye hakimiliki, na unazungumza nao na inategemea kuna waandishi ambao hakimiliki si tatizo, watakuambia endelea.

Kama mimi saivi nimeshinda tuzo ya Africa Institute, Sharjah, nitatafsiri kazi ya Adam Shafii ya Kasri ya Mwinyi Fuad kwenda Kiingereza na hakujakuwa na suala la hakimiliki. [Shafi ameniambia], “unataka kutafsiri, tafadhali fanya hivyo.” Kwa hiyo, ilikuwa hivyo.

Lakini kuna vitabu ambavyo, kwa mfano, kama hapa ilibidi Mkuki na Nyota walipe hakimiliki ya kupata haki ya kutafsiri [hiki kitabu cha Peponi]. Kwa hiyo, hiki hakikuwa bure. Kwa hivyo, inabidi kwanza uangalie mchapishaji kwamba itakuwaje.

Lakini kama mwandishi amefariki zaidi ya miaka 70 liyopita, basi chapisho litakuwa linapatikana kwa jamii. Unaweza ukatafsiri unavyotaka, ukafanya unavyotaka.

The Chanzo: Kisheria kabisa?

Ida Hadjivayanis: Kisheria.

The Chanzo: Sheria za kimataifa?

Ida Hadjivayanis: [Sheri za] kimataifa, ndiyo. Miaka 70, haki yako. Wewe mwenyewe utaamua.

The Chanzo: Basi nitasubiri [Kicheko].

Ida Hadjivayanis: Itabidi usubiri? [Kicheko]. Hilo ni la kwako. Pili, ni kwamba ufikirie ni nani unayemtafsiria? Ni nani ambaye atasoma kile kitabu? Kwa hiyo, ukishamfahamu, utajua ni lugha gani utumie, na maneno gani yatafaa, na [yepi] hayatafaa. Basi unakwenda zako!

The Chanzo: Da Ida, mimi nakushukuru sana.

Ida Hadjivayanis: Asante sana!

Omari Mikoma amebadilisha mahojiano hayo kutoka sauti kwenda maneno. Lukelo Francis amehariri mazungumzo haya. Stephan Gimbi amesimamia uzalishaji wa mahojiano haya. Kwa mrejesho, wasiliana nasi kupitia: editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *