Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo hapa Makao Makuu ya Nchi nayo imeanza kutoa huduma ya kupandikiza huduma ya uloto, au bone marrow kama huduma hiyo inavyojulikana kwa kimombo, ikianza na kutoa huduma hiyo kwa watoto watatu waishio na ugonjwa wa selimundu hapo Mei 10, 2023.
Benjamin Mkapa inakuwa hospitali ya pili nchini kutoa huduma hiyo muhimu baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambayo yenyewe ilianza kutoa huduma hiyo rasmi hapo mwaka 2021.
Matibabu ya uloto huhusisha uvunaji, uchakataji, na upandikizaji wa chembe chembe hai mama za damu. Mbali na wagonjwa wa selimundu, matibabu hayo pia hutolewa kwa watu wenye magonjwa ya saratani za damu na saratani inayohusisha matezi.
Matibabu hayo pia hutolewa kwa wagonjwa wasioweza kuzalisha chembe hai za damu kama aplastic anaemia pamoja na wagonjwa wa thalassemia. Kwa sasa, hata hivyo, Hospitali ya Benjamin Mkapa inatoa huduma hiyo wa watoto wenye selimundu tu.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali imewekeza Shilingi bilioni 2.7 ili kuanzisha huduma hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
SOMA ZAIDI: Wagonjwa wa Selimundu: Sisi ni Binadamu Kama Walivyo Binadamu Wengine
“Huduma hii ni muhimu kwani inaleta nafuu kwa wagonjwa wanaopata maumivu mara kwa mara,” Majaliwa alisema. “[Huduma hii] itawafanya [wagonjwa] kuweza kushiriki shughuli mbalimbali na kupunguza gharama kwa Serikali kuwahudumia wagonjwa hao nje ya nchi.”
Majaliwa alisema kwamba kuendelea kutolewa kwa huduma hizo katika hospitali za nchi siyo jambo dogo, akisema Tanzania ni nchi pekee Afrika Mashariki inayotoa huduma hizo kwa sasa, huku ikiwa ya saba barani Afrika.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kati ya watoto 11,000 wanaozaliwa na ugonjwa wa selimundu nchini, ni watoto 6,000 tu ndiyo wanahudhuria huduma za kliniki, hivyo kuna idadi kubwa ya wagonjwa waliopo mtaani na wanaendelea kuugua au kufariki.
Ummy amesema tayari amekutana na Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba kuangalia namna watakavyoweza kusaidia matibabu ya watoto 40 waliopo kwenye foleni ya matibabu, huku akisema 20 wataanza kupata huduma kwa msaada wa Serikali.
SOMA ZAIDI: Selimundu: Wazazi Walia na Gharama za Matibabu
“Changamoto tuliyobaki nayo ni gharama [za matibabu],” alisema Ummy. “Hapa gharama hii ni kama Shilingi milioni 50 [kupandikiza uloto na] kupandikiza figo ni kama Shilingi milioni 40. Kwa hiyo, hilo ndiyo jambo ambalo tunaendelea kulifanyia kazi ndani ya wizara. Huduma ziko Watanzania hawana hela.”
Gharama za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa selimundu zinatajwa kuwa kati ya Shilingi milioni 50 hadi milioni 55 kwa mgonjwa mmoja nchini wakati nje ya nchi, matibabu hayo hupatikana kwa gharama ya kati ya Shilingi milioni 120 hadi milioni 150.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dk Alphonce Chandika alisema awamu ya kwanza ya utoaji wa huduma hiyo ilianza Januari 19, 2023, na watoto waliopata huduma hiyo wote wanaendelea vizuri.
Dk Chandika alisema huduma hiyo itasaidia nchi kupunguza idadi ya wananchi wanaoishi na selimundu ambao asilimia 50 hadi 90 huwa katika hatari ya kufariki kabla kutimiza miaka mitano.
Mtaalamu huyo aliongeza kwa kusema kwamba Tanzania inakabiliwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu ambapo inashika nafasi ya nne Duniani na takriban watoto 11000 huzaliwa na ugonjwa wa selimundu Kila mwaka.
“Tumeendelea kufanya juhudi za kuanzisha huduma nyingine za kibingwa na bobezi,” alisema Dk Chandika kwenye uzinduzi huo. “Ninayo furaha kuufahamisha umma wa Tanzania na nchi jirani kuwa kwa mara ya kwanza tumefanikiwa kutoa huduma ya upandikizaji Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu nchini.”
Kwa mujibu wa Serikali, mgonjwa wa selimundu huwa hana damu ya kutosha kwa sababu ya seli zake za mwili siyo imara kiasi cha kubeba hewa ya oxygen kwenda sehemu mbalimbali za mwili wa binadamu. IIi mtoto aweze kupata ugonjwa huu ni lazima wazazi wawe na vimelea vya ugonjwa huo.
Mnamo Oktoba 2021, Mratibu wa Huduma za Selimundu kutoka Wizara ya Afya Dk Asteria Mpoto aliiambia The Chanzo kwamba mpaka kufikia mwaka huo, Tanzania ilikuwa ina jumla ya wagonjwa 200,000 wa selimundu, huku Watanzania kati ya asilimia 15 na 20 wakiwa wamegundulika na vinasaba vya ugonjwa huo ambao dalili zake hazionekani mpaka mtoto afikishe umri wa miezi minne.
Moja kati ya malamiko mengi ambayo wazazi wanaouguza watoto wenye selimundu wamekuwa wakilalamikia ni ukosefu wa huduma bora kwa watoto wao hao pale wanapokwenda kuwatafutia matibabu hospitalini, hususani zile za umma.
Baadhi ya malalamiko haya ni gharama za matibabu kuwa juu; uchache wa wataalamu; pamoja na ukosefu wa baadhi ya vipimo.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.