Wakiadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari, waandishi wa habari mkoani Mwanza wamesisitiza juu ya kuimarisha mazingira ya upatikanaji habari hasa mahusiano na watoa habari kama mamlaka mbalimbali.
Maadhimisho ya siku uhuru wa vyombo vya habari hufanyika kila mwaka Mei 3, kwa waandishi wa habari wa Mwanza tukio hilo limefanyika katika ukumbi wa Nyakahoja uliopo Nyamagana, Mei 16,2023, ikihusisha waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Uhuru wa habari
Mwandishi wa kujitegemea Kwilasa Mahigu akiwasilisha mada iliyoibua mjadala mkubwa kuhusu nafasi ya wadau wa habari kusimamia uhuru wa kujieleza amesema jamii ikipata uhuru wa kujieleza hata taaluma ya uandishi itachochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Haki nyingi za binadamu zinachochewa na uwepo wa haki ya kijieleza. Unapominya haki ya mtu ya kujieleza unamuondolea nafasi ya kutoa maoni yake ambayo yanaweza yakawa chachu ya maendeleo” Kwilasa anaeleza.
Vilevile amesema kumekuwa na tabia ya wadau kuweka jicho la uadui kwa waandishi wa habari pale ambapo wanaona wametoa habari ambazo zinaibua madhaifu yao.
“Unakuta habari ina manufaa kwa jamii ila sasa anakufuata anakukataza kutoa taarifa hiyo, hapo ndipo unagundua huna uhuru” anaeleza Kwilasa.
Aidha Kwilasa amesema mara nyingi wadau wamekuwa wakisema uhuru wa habari lazima uwe na mipaka, hata hivyo mipaka wanayoisema ni ile inayowanufaisha wao tu.
“Ukiwasifia hawakumbuki suala la mipaka, wakiharibu sasa wanakuja kukwambia unapaswa kuwa na mipaka” anafafanua zaidi Kwilasa.
Changamoto ukusanyaji wa habari
Akichangia mada mwandishi wa Raia Mwema, Manga Msalaba amesema kwa kiasi kikubwa baadhi ya wadau wamekuwa wakikwamisha kazi za uandishi kutokana na kulazimisha wanapofanya vibaya wasiandikwe.
Huku akieleza ni kwa namna gani baadhi ya taasisi hufikiri kuwa wanaweza kufanya vizuri tu kuliko kukosea, Manga amebainisha kuwepo kwa vitisho kutoka kwa taasisi hizo pale wanapohisi wameguswa masilahi yao
“Kuna mdau mmoja ambaye nilipaswa kuzungumza naye kutokana na jambo ambalo nilitaka ufafanuzi, ni kuhusu kupungua kwa mapato mkoa wa Mwanza. Aliniambia kijana jiangalie usijekuwa umeanza kwa mguu mbaya kuja kwangu” Manga anaeleza.
Hata hivyo Manga amesema kumekuwa na changamoto katika kushirikiana na vyombo vya usalama katika shughuli za uandishi ambapo vyombo vya usalama vinakuwa vinaingiza hisia zao binafsi.
“Kuna kesi tulikuwa tunaifuatilia mahakama kuu, ikafika hatua wale wenzetu wa jeshi la polisi wakaingiza hisia zao binafsi wakataka tuache kuandika hiyo stori kwakuwa wanadai tunawaandika vibaya. Kulikuwa na purukushani kubwa sana hadi kupelekea uongozi wa mahakama kuu kuingilia kati” anasema Manga
Miiko ya uandishi wa habari
Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kanda ya ziwa Mhandisi Francis Mihayo amesema suala weledi kwa waandishi wa habari ni changamoto kubwa kuliko masuala ya sheria
“Ni lazima muangalie miiko ya taaluma ya uandishi siyo kukimbilia kuzungumzia sheria. Mtakimbilia kuchokonoa kanuni lakini kama weledi hamna ni kazi bure” anasema.
Vilevile Francis amesema baadhi ya vyombo vya habari kama redio wanafanya kile ambacho hakiakisi taaluma ya habari, “watu wanachambua magazeti hadi unacheka, kwasababu watu wanapenda vichekesho basi wanapenda. Sasahivi tunawaangalia, tunawaita tunazungumza nao sana tu.”
Kamanda wa Polisi Wilbroad Mutafungwa amesisitiza sekta ya habari kuhakikisha wanawashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo jeshi la polisi na taasisi zingine za kiserikali katika mijadala ya kutatua masuala ya haki na uhuru.
“Hakuna jambo muhimu katika maisha ya watanzania katika kufikia malengo ya kimaendeleo kama suala la haki. Kama haki isipotolewa basi hakuna maendeleo” anasema.
Vilevile Kamanda Wilbroad amewataka waandishi wasimamie weledi wa taaluma yao kwa kuhakikisha wanafuata sheria wanapokuwa katika maeneo ya kazi. Akitoa mfano sehemu zenye utepe kumaanisha mtu asikatize eneo hilo lakini unamkuta mwandishi anaingia.
Wilbroad ameeleza pia changamoto ya waandishi kwenda kwenye matukio bila kuwa na vitambulisho, hali inayopelekea mara nyingine kutokea kwa kutoelewana na kutishia amani na usalama.
Aidha Jeshi la polisi limetoa ahadi ya kuwalinda waandishi pale ambapo watakutana katika shughuli mbalimbali, “kazi yenu nyinyi ni kutafuta habari, kazi yetu sisi ni kuwalinda waandishi na mali zao wanapokuwa wanatafuta hizo habari. Sisi sote tunakutana katika matukio mbalimbali kama mikutana na maandamano”
Katika majadiliano yaliyoendeshwa na Mwenyekiti wa chama cha waandishi mkoa wa Mwanza Edwin Soko, Soko amesema ili kuhakikisha taaluma ya uandishi inalindwa waandishi wamekubaliana kukumbushana mara kwa mara katika kusimamia miiko ya taaluma.
Rahma Salumu ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: salumurahma1@gmail.com.