The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mabadiliko ya Tabianchi Ni Nini? Mtaalam Afafanua

Ni mabadiliko yanayotokea katika vile viwango vya wastani wa hali ya hewa katika eneo fulani kwa muda mrefu.

subscribe to our newsletter!

Maelezo yanayofuata yametolewa kutoka sauti kwenda kwenye maneno kutoka kwenye mahojiano maalum ambayo The Chanzo imefanya na Dk Baruani Mshale, mtaalamu wa masuala ya maliasili na mabadiliko ya tabianchi. Uhariri umefanyika kuboresha usomaji.

Mabadiliko ya tabianchi, ama kwa lugha ya Kiingereza tunasema climate change, inamaanisha mabadiliko katika wastani wa hali ya hewa. Hapa kuna tabianchi na hali ya hewa, na huwezi kuzungumzia mabadiliko ya tabianchi bila ya kuzungumzia hali ya hewa.

Hali ya hewa nadhani wengi wetu tunafahamu maana yake ni nini. Tunapozungumzia hali ya hewa utasikia kwamba kiasi cha joto kitakuwa nyuzi kadhaa, ama mvua itanyesha ama haitanyesha, vipindi vya jua vitakuwa hivi, nakadhalika. Kwa hiyo, hiyo ndiyo hali ya hewa.

Tabianchi ni hali ya hewa ya eneo fulani ambayo inapatikana kwa kutafuta wastani wake kwa muda mrefu. Yaani, kwa mfano, ukiwa Dar es Salaam, au ukanda wote huu wa pwani, inajulikana kwamba ni eneo ambalo lina joto japokuwa kuna tofauti ya kiwango cha joto asubuhi, mchana, na jioni.

SOMA ZAIDI: Wananchi Mkuranga Walia Na Athari Za Mabadiliko Tabia Nchi

Mwezi Januari, mwezi Machi, mwezi Juni, na mwezi Disemba. Lakini tunajua kabisa kwamba Dar es Salaam hali ya hewa yake, au tabianchi ya Dar es Salaam, ni ya joto.

Ukienda Arusha, ama Lushoto mkoani Tanga, unajua kwamba hali ya hewa ya Lushoto ni baridi japokuwa na yenyewe itabadilika, yaani kile kiasi cha joto kitabadilika asubuhi, mchana, jioni na miezi tofauti katika mwaka. Lakini tunajua, kwa wastani, hali ya hewa ya Lushoto ni baridi kuliko Dar es Salaam.

Kwa hiyo, tunasema tabianchi ya Lushoto ni tofauti na tabianchi ya Dar es Salaam. Kwa sababu hali ya hewa, wastani wa hali ya hewa ya Lushoto ni baridi au ni joto la chini zaidi kuliko Dar es Salaam. Kwa hiyo, ile hali hali ya hewa ya eneo fulani katika muda mrefu, takribani miaka 30, ndiyo inaitwa tabianchi. Hiyo ndiyo maana ya tabianchi.

Kwa hiyo, tunapozungumzia mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya tabianchi maana yake ni kwamba kama tumezoea Lushoto kuna baridi, na labda wastani wa baridi ya Lushoto kwa mwaka ni nyuzi 14, tutasema tabianchi ya Lushoto imebadilika pale ambapo kiwango cha joto kule Lushoto labda kimeongezeka au kimepungua.

SOMA ZAIDI: Ni Upi Mtazamo wa Wakulima Wadogo Juu ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi?

Badala ya kuwa nyuzi joto 14 imekuwa labda 16, huo ni mfano tu. Hapo ndiyo tunasema kwamba tabianchi ya Lushoto imebadilika. Lakini pia inaweza ikabadilika kwa kuangalia vipimo vingine vya hali ya hewa.

Kwa mfano, mvua, upepo na viashiria vingine tunavyovitumia kuangalia hali ya hewa ya eneo fulani. Halafu hiyo hali ya hewa eneo fulani ndiyo inatupa tabianchi ya hilo eneo.

Kwa hiyo, tukizungumzia mabadiliko ya tabianchi tunazungumzia yale mabadiliko yanayotokea katika vile viwango vya wastani wa hali ya hewa katika eneo fulani kwa muda mrefu.

Siyo kwa kuangalia labda asubuhi, mchana, jioni au vipindi tofauti katika mwaka. Hapana. Ni ile hali ambayo sasa inaenda ikibadilika kwamba ukiangalia tabia nchi, au hali ya hewa ya Lushoto ya sasa hivi mwaka 2023, ni tofauti na mwaka 1970. Kwa hiyo, tunasema tabianchi ya Lushoto imebadilika.

Mfano mwingine ni katika mvua. Unaweza kukuta katika eneo fulani tulizoea mvua zinanyesha kuanzia mwezi Machi mpaka mwezi Juni na zinanyesha kwa kiwango fulani.

Lakini unakuta kwamba eneo lilelile sasa siku hizi mvua zinaanza kunyesha labda mwezi Aprili halafu zinanyesha tu kwa muda mfupi, mvua kubwa sana, na mwezi Mei mvua zimekata.

Kwa hiyo, hapo tunasema tabianchi ya lile eneo, kwa kuangalia kigezo cha mvua, imebadilika kwa sababu sasa mvua zinanyesha katika kipindi ambacho sicho tulichozoea na kiasi cha mvua kinachonyesha sicho tulichokizoea vilevile.

Na kwa Tanzania hiyo hali imeshatokea. Ushahidi upo na kila mwananchi anaweza akaangalia eneo lake. Ndiyo maana unasikia watu wengi wanaweza kusema zamani palikuwa hivi na siku hizi pamekuwa hivi.

SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Yatajwa Kuathiri Kilimo cha Korosho Lindi, Mtwara

Hiyo ndiyo inaashiria kwamba tabianchi ya lile eneo imebadilika kwa sababu ile hali ya hewa sasa katika muda mrefu imebadilika.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *