The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Vavagaa: Jukwaa la Kifeminia Linalolenga Kuondoa Dhana Zilizopitwa na Wakati

“Wanawake kusimulia hadithi zao wenyewe ni njia ya kuwawezesha kusimulia maisha yao na historia walizoshiriki kuzitengeneza.”

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Vavagaa ni neno la Kiswahili ambalo, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu y TUKI, maana yake ni kuenea kwa kitu fulani kwa wingi, au kitu fulani kuwa tele katika sehemu fulani.

Ni jukwaa lililobuniwa na wanawake sita waliofanya kazi kwa miaka kwenye harakati za kupigania haki za wanawake Tanzania, akiwemo Demere Kitunga, moja kati ya wafeminia na waandishi wanaoheshimika nchini, baada ya kujiridhisha kwamba ili  jitihada za kuuondoa mfumo dume zifanikiwe, ni lazima mawazo mbadala yapatikane kila mahala, ni lazima yavavagae.

Wafeminia hutambulishwa kama watu wenye lengo la kujenga jamii yenye kuzingatia usawa wa kijinsia, ambao huubainisha mfumo dume, unaokuza utawala wa jinsia ya kiume, kama kikwazo kikubwa katika jitihada zao hizo za kuboresha ustawi na uhuru wa wanawake na wanaume, na kwa hiyo ni lazima utokomezwe.

“Tangu mwanzo, tulidhamiria kuifanya [Vavagaa] ihusu kusikiliza, kusikia, kuelewa au kuthamini, na kutoa mtazamo mbadala wa masuala yanayoziathiri jamii zetu,” Kitunga, ambaye anaongoza shirika lisilo la kiserikali la Readership for Learning and Development, alieleza kwenye mahojiano na The Chanzo hivi karibuni.

“Kwa kifupi, [tulilenga] kuendesha mazungumzo ambayo yatakuwa ya wazi kulingana na fursa zilizopo na udhaifu; huku washiriki wakiuliza maswali ili kupata msingi mmoja wa mabadiliko ya kijinsia katika jamii,” aliongeza Kitunga. 

Likiwa na makao yake makuu Mikocheni, Dar es Salaam, Readership for Learning and Development, maarufu kama Soma,hujihusisha na masuala ya uhamasishaji usomaji nchini na ni chini ya uangalizi wake ambapo Vavagaa huandaliwa na kuendeshwa.

Demere Kitunga, ambaye anaongoza Shirika la Masimulizi ya Kifeminia, Usomaji wa Kujifunza na Maendeleo, Soma Book Cafe, akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni na kujitafakari iliyofanyika Mei 26, 2023, Dar es Salaam. PICHA | KIRATI JOSEPH

Tekinolojia 

Ili kuendana na maana yake ya kuenea kila mahala, Vavagaa huendesha shughuli zake katika ngazi mbili kuu: mitandaoni na mitaani. Mitandaoni, Vavagaa hutumia njia zilizopo za kitekinolojia katika kuhakikisha kwamba programu zake zinawafikia watu wengi kadri inavyowezekana. 

Kwa mfano, Vavagaa huendesha mijadala ya kila wiki kwenye mtandao wa kijamii unaotumia sauti wa Clubhouse, ukiwavutia washiriki wenye mitazamo na mawazo mbalimbali. 

SOMA ZAIDI: Mwanahamisi Singano: Mfumo Dume Huwabeba Wanaoutetea na Kuwaadhibu Wanaotaka Kuubomoa

Kwenye mijadala hii, ambayo huwa ya wazi kwa kila mtu kushiriki bila kujali jinsia au mtazamo wake wa kidunia, mada kama vile haki za mtoto, uhuru wa kimwili wa mwanamke, malezi, ndoa, afya ya uzazi na unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na nyengine nyingi, hujadiliwa.

Hata watu wanaokosoa dhana ya ufeminia hushiriki kikamilifu katika mijadala hii, ambayo, mara nyingi, hufanyika kwa shauku kubwa na kuambatana na ukinzani mkali wa hoja na mawazo. 

Mary Ndaro, mtayarishaji mwenza na muendeshaji wa Vavagaa, aliiambia The Chanzo kwamba hivyo ndivyo walivyopanga iwe tangu walipoamua kuja na wazo la kuanzisha jukwaa hilo.

“Tulifanya uamuzi wa makusudi kwamba jukwaa letu litajumuisha watu wote na kuvutia maoni tofauti, hata yale yanayopinga ufeminia; tulitaka kupanua mjadala [juu ya ufeminia] ili tusiwe tunazungumza sisi wafeminia tu,” Ndaro, ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kijinsia na maendeleo, alisema.

Mary Ndaro, muanzilishi mwenza na muendeshaji wa jukwaa la Vavagaa, akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni ya kujitafakari iliyofanyika Mei 26, 2023, Dar es Salaam. PICHA | KIRATI JOSEPH

“Tulitaka kuendesha mazungumzo kati ya wanawake na wanaume, na kuunda uwanja salama kwa wao kujadili masuala yanayowapa wasiwasi, ambayo, mara nyingi, yanakandamizwa, au kuonekana kama ni mwiko kuyajadili,” aliongeza Ndaro. 

Kwa kufanya hivi, Ndaro anaamini kwamba Vavagaa inanufaika kwa kujua ni mbinu gani na mikakati ipi itumie kwenye dhamira yake ya kubadilisha hali ya mambo kama ilivyo sasa kwenye jamii nyingi za Kitanzania.

Mijadala ya kwenye Clubhouse ilitanguliwa na mijadala mingine ya kidigitali kama vile Zoom na vipindi vya mazungumzo vya YouTube vilivyohusisha wafeminia na wasio wafeminia nchini kote. Mpaka sasa, hata hivyo, Clubhouse imesalia kuwa jukwaa maarufu la mtandaoni la Vavagaa kufanikisha dhima yake katika jamii.

Sauti za mashinani

Lakini siyo Watanzania wote wapo kwenye mitandao ya kijamii, hali iliyowasukuma Vavagaa kwenda kwenye jamii na kukutana na wananchi kwenye mazingira yao wenyewe na kuzungumza nao kuhusiana na mambo yanayowahusu pamoja na uzoefu wao.

Vavagaa Mtaani,’ kwa hiyo, huwaruhusu waandaaji wa jukwaa hilo kukutana na wananchi hawa moja kwa moja na katika mazingira yao, ambapo wananchi huwa wazi zaidi kueleza uzoefu wao kuhusu mfumo dume na mila nyingine kandamizi katika jamii. 

Katika mahojiano na The Chanzo, Kitunga alieleza kwamba waliamua kufanya hivyo kwa makusudi ili kutatua mgawanyiko uliopo wa kidijitali nchini Tanzania pamoja na kulifanya jukwaa hilo kuwa la watu na linalopaza sauti za watu wote, hata wale ambao hawapo mitandaoni.

SOMA ZAIDI: Pili Mtambalike: Serikali Iwe na Uvumilivu ili Waandishi Waweze Kufanya Kazi kwa Uhuru

“[Vavagaa] Mtaani inaangazia uzoefu wa wanawake na wanaume kuhusu mfumo dume,” alibainisha Kitunga. “Vavagaa Mtaani hufanya kazi na vikundi ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa vikinyamazishwa kama vile madada poa. [Pia], hujikita kwenye kujadili uhuru wa mwili wa mtu binafsi, masuala ya ujinsia, na wanawake walemavu.”

Katika ngazi ya kjamii, timu ya Vavagaa huwalenga vijana wa kike na wa kiume ili kuibua mijadala inayoonekana haifai lakini inaathiri maisha yao ya kila siku katika nyanja za kiuchumi, kijamii, na kisiasa. 

Kwenye mijadala yake ya mitandaoni na ile ya mitaani, Vavagaa hukusanya hadhira kubwa ya wananchi ili kuibua hamasa na ushiriki wao kwenye mchakato mzima wa kupigania jamii yenye usawa wa kijinsia katika jamii.

Baada ya miezi kadhaa ya kufanya kazi, mnamo Mei 24, 2023, timu ya Vavagaa ilikutana na baadhi ya wadau wake iliyokuwa ikishirikiano nao kwa ajili ya tafakuri ya pamoja kuhusiana na shughuli hizo iliyoendana na kupata chakula cha jioni cha pamoja. Tukio hilo lilifanyika makao makuu ya Soma, Mikocheni, Dar es Salaam.

Watu kadhaa walihudhuria, wakiwemo wawakilishi kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wabunifu, wasomi, washirika wa maendeleo, pamoja na waandishi wa habari.

Wawakilishi kutoka sekta ya NGOs, wabunifu, wasomi, wadau wa maendeleo na waandishi wa habari wakiwa katika hafla ya chakula cha jioni ya kujitafakari iliyofanyika Mei 26, 2023, Dar es Salaam. PICHA | KIRATI JOSEPH

Baadhi ya watu hawa wamekuwa wakishiriki mara nyingi kwenye mijadala ya Vavagaa kwenye mtandao wa Clubhouse, huku baadhi yao wakiwa wameshawahi hata kuwa wasemaji wakuu katika mijadala na majadiliano inayofanyika kwenye mtandao huo.

Wakisindikizwa na vinywaji na mbuzi choma, washiriki walisikia kutoka kwa waandaji wa Vavagaa kuhusu mipango ya jukwaa hilo kabla ya washiriki hao kueleza mawazo yao juu ya jukwaa hilo na kutoa mapendekezo kuhusu namna bora Vavagaa inaweza kuboresha shughuli zake ili kufanikisha dhamira yake.

Utatizaji  

Rose Marandu, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Women Fund Tanzania Trust (WFT-T), shirika lisilo la kiserikali linalotoa ufadhili kwa mashirika ya wanawake, alibainisha umuhimu wa kazi inayofanywa na Vavagaa, hususan kupitia mijadala inayohoji vitu vinavyoonekana vya kawaida kwenye jamii.

Rose Marandu, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Women Fund Tanzania Trust (WFT-T), akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni ya kujitafakari iliyofanyika Mei 26, 2023, Dar es Salaam. PICHA | KIRATI JOSEPH

“Kushindwa kuyafanya baadhi ya mambo yaonekane ni matatizo kunasababisha kushindwa kwetu kuyaelewa na kujipanga dhidi yake,” Marandu alisema “Mijadala kama vile ni nani anayemiliki mwili wa mwanamke [ambayo Vavagaa iliwahi kuandaa] husaidia kupinga kile kinachochukuliwa kuwa ni cha kawaida kwenye jamii zetu.”

SOMA ZAIDI: Wanawake Wawili Wauwawa Kikatili Zanzibar. Familia, Wanaharakati Wataka Uwajibikaji

Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa wakati wa majadiliano hayo ni pamoja na kupanua wigo wa zana za kidigitali zinazotumiwa kwa madhumuni kujadiliana, huku baadhi wakipendekeza kuwa mitandao mingine ya kijamii kama vile Facebook na Instagram zijumuishwe. 

Wengine walipendekeza pia kuhusu matumizi ya sanaa kama eneo jingine Vavagaa inaweza kulizingatia kwenye harakati zake.

Kwenye hotuba yake ya kufunga hafla hiyo, Kitunga alisema wanawake kusimulia hadithi zao wenyewe pia ni njia ya kuwawezesha kusimulia maisha yao na historia walizoshiriki kuzitengeneza, ambazo bado kwa kiasi kikubwa zimeendelea kutawaliwa na kusimuliwa na wanaume.

“Kupitia jukwaa hili [la Vavagaa], tunalenga kujhusisha, kama wafeminia wa Kiafrika, na kusimulia hadithi zetu binafsi za kutafuta mabadiliko, katika namna inayohoji mgawanyiko wa madaraka uliopo kwenye jamii, huku tukikujenga mshikamano kati ya wafeminia, kujijali, kulea, na kuboresha ustawi wetu kama watetezi wa haki za wanawake,” alisema. 

Hadija Said ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana mkoani Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia hadijasaid826@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *