The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wanawake Wawili Wauwawa Kikatili Zanzibar. Familia, Wanaharakati Wataka Uwajibikaji

Ni Khairat Juma Bakari na Laura Msemwa, wanawake wawili waliouwawa kikatili Zanzibar, kwenye matukio mawili tofauti.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Polisi visiwani hapa wametangaza msako mkali dhidi ya watu waliohusika na mauaji ya wanawake wawili, katika matukio tofauti, yaliyoacha majonzi na huzuni kwa familia zilizoathirika, huku wanaharakati wa haki za binadamu wakitaka wahusika wa mauaji hayo kufikishwa mbele ya vyombo vya dola haraka iwezekanavyo.

Khairat Juma Bakari na Laura Msemwa wameripotiwa kuuwawa kikatili kwenye mazingira yaliyojawa na utata ambayo wanaharakati wa haki za binadamu wameyatafsiri kama mwendelezo wa mashambulizi dhidi ya wanawake visiwani Zanzibar yanayoashiria kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia visiwani humo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia yake, Khairat, 23, aliuwawa hapo Mei 20, 2023, kwa kukatwa na kitu chenye chenye ncha kali shingoni, huku akiong’olewa meno pamoja na nywele kabla ya kutupwa kwenye nyumba ambayo haijakamilika maeneo ya Mbuzini, kisiwani Unguja.

Hamisa Hassan Maalim, mama mlezi wa Khairat, aliiambia The Chanzo kwamba mauji hayo yalitokea punde tu baada ya Khairat, mkazi wa Donge, Kaskazini Unguja, kutoka benki na Shilingi milioni nne, fedha zilizokusudiwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa nyumba yao waliyokuwa wanajenga.

Hamisa, akiongozana na mtu mwengine, walimsindikiza Khairat mpaka kwenye kituo cha daladala maeneo ya Darajani, Unguja, na ndiyo ulikuwa mwisho wa mama huyo wa watoto sita kumuona binti yake.

Hakurudi nyumbani

“Tulimuacha pale na hakurudi nyumbani,” Hamisa, ambaye kitaalamu ni mwalimu wa shule, alisema. “Mpaka asubuhi tuliposikia kuwa kuna mtu ameokotwa Mbuzini, amevaa baibui jeusi na mtandio mweupe, ameuliwa. Nikajua ni Khairat.”

Faki Juma Bakari, baba mlezi wa Khairat, alisema kama familia walishtushwa na tukio la kuuwawa kwa binti yao aliyemaliza kidato cha nne mwaka 2021, akizitaka mamlaka zinazohusika kuwasaka waliohusika na kifo chake.

SOMA ZAIDI: Watoto 1,173, Wanawake 185, Wanaume 3 Wafanyiwa Ukatili Zanzibar 2022

“Wamemuua vibaya na si haki wala ubinaadamu,” Bakari aliiambia The Chanzo. “Kuna mtu palepale benki aliona kila kitu ndiyo akafanya hivyo. Haiwezekani itokee bahati mbaya. Tunahitaji haki itendeke.”

Kwa upande wake, Laura, 23, mwenyeji wa Iringa aliyekuja Zanzibar kufanya kazi za hotelini, mwili wake ulipatikana ukiwa tayari umeharibika huko maeneo ya Bububu Kijichi, kisiwani Unguja, baada ya kufariki siku kadhaa kabla ya watu kugundua.

Kwenye mahojiano na The Chanzo, Tumaini Amos, jirani yake Laura waliokuwa wanaishi kwenye nyumba moja ya kupanga, alisema kifo cha binti huyo kilitanguliwa na ugomvi kati yake na aliyekuwa mpenzi wake aliyekuwa akiishi naye hapo, ugomvi ambao ulishuhudia wawili hao wakigawana vitu.

Tumaini alieleza kwamba jioni ya siku Laura aligombana na mpenzi wake huyo alimkaribisha mwanaume mwengine nyumbani kwake hapo ambapo binti huyo hakutoka tena mpaka alipogundulika kuwa amefariki.

Nilisikia harufu

“Alhamis kimya, Ijumaa kimya na si kawaida yake,” Tumaini alisimulia. “Sasa Jumamosi asubuhi nimeamka kufanya usafi, nikipita hapa kwenye mlango wake naskia harufu. Ndipo nilipotoa taarifa kwa mama mwenye nyumba.”

Ndipo polisi walipofika na kuvunja mlango na kuukuta mwili wa Laura ukiwa umeshaanza kuharibika na kuuchukua na kwenda kuuzika.

The Chanzo ilishuhudia chumba cha Laura kikiwa kimefungwa, huku ndugu zake wakichukua baadhi ya vitu, wakiahidi kurudi na kuchukua vilivyobaki.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ukatili Baina ya Wapendanao Siyo Jambo la Kifamilia

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Richard Mchomvu alisema polisi mkoani humo linafanyia uchunguzi matukio hayo mawili yaliyohusisha mauaji ya kikatili ya Khairat na Laura.

“Uchunguzi wa kesi zote mbili unaendelea [na] tutahakikisha huyu aliyefanya hivi tutawapata na sheria kuchua mkondo wake,” Mchomvu aliwaambia waandishi wa habari hapo Mei 25, 2023.

Wahalifu wasakwe

Kwa upande wao, wanaharakati wa haki za binadamu visiwani hapa wamelaani vikali mauaji hayo ya kikatili dhidi ya mabinti hao, wakitaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wale wote waliohusika na uhalifu huo.

Kwenye taarifa yao ya pamoja waliyoitoa hapo Mei 28, 2023, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) – Zanzibar na Jumuia ya Wanaseheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) walilitaka Jeshi la Polisi kuwatia nguvuni watu waliohusika na matukio hayo ya kihalifu.

“Kupatikana kwa haki kutawatisha wahalifu wengine ambao wana nia ya kufanya vitendo hivyo vya kikatili na kuhakikisha kwamba matukio kama haya hayaendelei kutokea Zanzibar,” yalisema mashirika hayo kwenye taarifa yao hiyo.

Ingawaje ni matukio yaliyoshtua watu wengi visiwani humu, haya si matukio ya kwanza ambayo yanahusisha wanawake kuuwawa kikatili.

SOMA ZAIDI: Jinamizi la Mauaji Holela Linavyoitesa Zanzibar

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya pamoja ya TAMWA – Zanzibar na ZAFELA, tangu mwaka 2016, jumla ya matukio 23 yanayohusisha mauaji ya wanawake na watoto yameripotiwa Zanzibar.

Kwenye matukio yote hayo, TAMWA – Zanzibar and ZAFELA wamesema kwamba upatikanaji wa haki umekuwa mgumu kufikiwa.

“Tunaamini kwa nchi ndogo kama Zanzibar, kukiwepo na upelelezi na mashirikiano mazuri na jamii, wahalifu wanaweza kupatikana kwa muda muafaka,” mashirika hayo yalisema kwenye taarifa yao hiyo.

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *