Jinamizi la Mauaji Holela Linavyoitesa Zanzibar

Wananchi wadai hatua ya Serikali kutowafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wanaoshukiwa kufanya vitendo hivi inapelekea kushamiri kwake.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Wananchi, wanaharakati na vyombo vya sheria nchini hapa wanaendelea kuumiza vichwa wakifikiria ni nini kinaweza kuwa ni chanzo cha mauaji holela yanayoendelea kutokea visiwani humu, huku familia zilizopoteza wapendwa wao kwenye matukio hayo wakilitupia lawama Jeshi la Polisi waklituhumu kushindwa kutimiza wajibu wao. 

Jumla ya matukio ya mauji 208 yameripotiwa katika vituo mbali mbali vya polisi vya Zanzibar kati ya mwaka 2015 na 2020, kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mtakuwimu Mkuu Zanzibar. Taarifa hizi zinaonesha kuwa kwa mwaka 2015, vifo 24 viliripotiwa. Mwaka 2016, vifo 34. Mwaka 2017, vifo 42. Mwaka 2018, vifo 41; mwaka 2019, vifo 34 na mwaka 2020, vifo 33.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini Tanzania (TAMWA), upande wa Zanzibar, moja kati ya Asasi za Kiraia zilizo mstari wa mbele katika kupaza sauti kuhusiana na matukio haya, inayobainisha kwamba kati ya mwaka 2016 hadi 2021, jumla ya mauaji ya wanawake na watoto 19 yaliripotiwa kwenye ofisi zao, huku mauaji ya wanawake yakiwa 15 na watoto wanne.

“Zanzibar ina miongozo inayowalinda wanawake na watoto ila bado mkazo haujawekwa kwenye hili,” Dk Mzuri Issa, Mkurugenzi wa TAMWA – Zanzibar, anaiambia The Chanzo wakati wa mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake Septemba 27, 2021. “Na kuhusu suala la kuchukuliwa hatua [kwa wanaodaiwa kufanya mauaji] changamoto ni kwenye uchunguzi. Ndiyo maana kesi hizi zinashindwa kufikia mwisho na wahusika kuwajibishwa.”

Kitendo cha vyombo vya sheria Zanzibar kushindwa kuwachukulia hatua watu wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya mauwaji ni jambo ambalo familia nyingi zilizopoteza wapendwa wao kutokana na matukio haya wamelilamikia sana, huku wakionesha kukata tamaa katika juhudi zao za kupata haki kwa ajili ya wapendwa wao. 

‘Nimeamua kumuachia Mungu’

Moja kati ya wafiwa hawa ni Khamis Ali Haji, baba wa watoto 15, ambaye mnamo Novemba 4, 2017, alimpoteza mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 23 aliyejulikana kwa jina la Asia Khamis Haji. Licha ya kwamba kifo cha Asia kilitokea katika mazingira yenye utata mwingi, Khamis, 59, anadai kwamba hakuna chochote kinachoendelea kwenye uchunguzi wa kifo cha binti yake, akidai kwamba hata jalada la kesi ya Asia halionekani liko wapi.

“Mimi nimekosa haki ya mtoto wangu kwa sababu sina pesa wala uwezo na nishamuachia Mungu, najua waliohusika wametumia mamlaka na pesa kunikosesha haki ya mtoto wangu,” mkazi huyo wa Mkele, kisiwani Unguja, anayejishughulisha na kazi ya udereva, anaiambia The Chanzo huku akitokwa na machozi. “Hakuna kesi wala kitu kilichoendelea.”

Akisimulia namna alivyopata taarifa za kifo cha binti yake, Khamis anaeleza siku moja Asia aliwaaga wazazi wake kwenda Paje, sehemu mashuhuri visiwani hapa kwa shughuli za utalii na sherehe, akisema kwamba amealikwa kwenye sherehe, akiwa na marafiki zake. 

Lakini Asia hakurudi nyumbani siku hiyo, kitu ambacho kilimpa wasi wasi sana baba yake mzazi, Mzee Khamis. Asubuhi wakati akijiandaa kwenda kazini, walikuja watu nyumbani kwake na kumueleza kwamba wamepata taarifa kwamba binti yake amefariki kwa shoti ya umeme.

“Nilipopata taarifa sikushtuka na niliona ni ajali tu,” Khamis anasimulia. “Nikatoka  na kwenda kuifuata maiti ya mwanangu hospitali Makunduchi kwa ajili ya kuanza utaratibu wa maziko. Kitu kilichonishangaza [ni kwamba] wakati nafika hospitali nikamsikia daktari akizungumza na simu na mtu mwengine  akisema, ‘Hawa askari wabaya wamesema kuwa huyu mtu kafariki kwa shoti ya umeme na wamemleta hapa na PF3.’

“Yule daktari aligundua kuwa nimesikia na kuanzia hapo suala la kupewa tu maiti ya mtoto wangu ilichukua zaidi ya saa tano, kitu ambacho niliona ni kuendelea kuficha ushahidi wa tukio hilo. Nilipopewa maiti ya mtoto wangu niliomba pia kupewa taarifa ya uchunguzi ila niliambiwa nitaletewa huko huko [mazikoni], kitu ambacho kilinipa wasiwasi ila sikuwa na nguvu za kuendelea kuuliza juu ya hayo nikachukua maiti na kuondoka.

“Wakati napewa maiti ya mtoto wangu, niliambiwa kuwa mizigo mengine ya mtoto wangu iko kituo cha polisi Paje. Nilipokwenda nilipewa mizigo yake na  simu moja, wakati Asia alikuwa na simu mbili, ila hata hio niliyopewa ilitolewa laini na kublokiwa pia ikawa haifanyi kazi.

“Kitu kilichonishitua ni kwamba walioosha maiti ya Asia wanasema mwili wake ulikuwa mbichi na damu zinatoka puani na maskioni. Kama alikuwa amepigwa na shoti ya umeme angekakamaa, ila haikuwa hivyo kabisa. Hapo ndipo nilipopata hofu juu kifo cha mwanangu. Baada ya kuzika nilirudi tena kituo cha polisi Paje na kuuliza ni nani alileta vitu vya mtoto wangu pale, polisi hawakunijibu. Nikaenda tena hospitali ya Makunduchi kuuliza Asia alipelekwa na nani pale sikupata majibu wala karatasi ya uchunguzi.

“Kwa vile na mimi nina uenyeji hapa [Unguja] nikahangaika kutaka kupata haki ya mtoto wangu. Nikaenda mpaka kwa Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar kuomba usaidizi. Ila wakati anatafuta jalada likawa halionekani na sijawahi kuliona na hata sijawahi kupewa taarifa ya uchunguzi wa kifo cha mtoto wangu zaidi ya yale niliyosikia pale hospitalini.”

Auwa na ujauzito wa miezi mitatu

Uzoefu wa Mzee Khamis si uzoefu wa kipekee kwani watu wengi tu ambao wamepoteza wapendwa wao kwenye vitendo hivi vya mauaji wanakiri kukabiliana navyo. Mansour Juma Mwinyi ni baba mkwe wa Asha Khamis, aliyeuwawa mwaka 2019 akiwa na umri wa miaka 23, yeye na mume wake Issa Mansour Issa, huku Asha akiwa na ujauzito wa miezi mitatu.

Mzee Mansour, 65, mkazi wa Kibele hapa Unguja, anasema  mtoto wake aliuza shamba na kupata pesa nyingi na alianza kuzitumia kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yake na siku hio ilikuwa ni siku ya mwisho kwenda kuzitoa pesa hizo. Anasimulia namna alivyopata taarifa za kifo cha kijana wake na mkwe wake  wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo, Septemba 23, 2021:

“Ni kawaida yangu kupita asubuhi kuwauliza hali nikiwa naenda kwa mke wangu mwengine. Lakini siku hio asubuhi wakati napita nikamuona mtoto wake [Issa] akaniambia, ‘Babu, baba amekufa na nyumbani kuna damu.’ Ila nikadharau na kuona  ni mambo ya kitoto. 

“Mjukuu wangu akanifuata na kuniambia tena. Hapo ndipo nikashtuka na kwenda na nilipofika nikakuta Issa yupo ukumbini amekakamaa na mkononi alikuwa na kipande cha tikiti. Walimuua kwa kumpiga sehemu za mbavuni  na kumtoboa na kumkata kidevuni na shingoni.

“Baada ya kuona vile nikaanza kumtafuta mkewe na nikaenda kumkuta mkewe chumbani, nikamkuta amelala chali na wamempiga shingoni na kichwani nae alikuwa ashakufa na huku akiwa na ujauzito wa miezi mitatu. Kama ningeweza kuchagua ningetaka wamuache yule mkwe wangu maana sidhani kama anahatia yoyote. 

“Polisi wakaja na kuanza kuchunguza kisha wakachukua miili yote na kuipeleka hospitali kwa ajili ya uchunguzi kisha tukapewa maiti na kuzika. Baada ya siku kadhaa kupita nikaitwa kituo cha polisi Tunguu na kuambiwa kuwa kuna taarifa za kiuchunguzi  kwamba mtu aliyehusika na mauji yupo Kunduchi hivyo tutakupa taarifa zaidi. Lakini mpaka leo sijawahi kupata taarifa zozote.”

Polisi: Uchunguzi haujakamilika

Alipoulizwa kwa nini familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na mauaji hawapewi taarifa ya nini hasa kilichochea mauaji hayo na washukiwa kutiwa nguvuni, Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar Zuberi Chembela ameiambia The Chanzo kwamba ni kwa sababu uchunguzi haujakamilika, akisema: “Upepelezi wa makosa ya jinai ni mchakato kwa maana kwamba tukio linapotokea na kuripotiwa katika kituo cha polisi ndo uchunguzi unapoanzia hapo.”

Ali Chikira ni Meneja Mradi wa shirika la Search for Common Ground, linalojishughulisha na utatuzi wa migogoro  kwenye jamii anayeiambia The Chanzo kwamba suala la kudumisha amani katika jamii ni la kila raia, akisisita umuhimu wa malezi katika kudumisha amani na kuondokana na vitendo kama hivi vya mauaji.

“Kuwepo kwa vitendo hivi kunaweza kuharibu amani ya nchi maana kila mtu ana kiwango chake cha kuvumilia iwapo mauaji yanayoteka yanashindwa kufanyiwa kazi na watuhumiwa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” anasema Chirika wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyofanyika ofisini mjini hapa. “Ni muhimu kwa mamlaka zinazohusika kuharakisha uchunguzi wa matukio haya unakamilika haraka iwezekanavyo na haki ionekane imetendeka.”

Najjat Omar ni mwandishi wa habari za kijamii kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najjatomar@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na makala haya, unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts