The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Maji Yalivyohatarisha Vita Kati ya Iran na Afghanistan

Mapigano mafupi kati ya nchi hizo jirani yalipelekea watu angalau wanne kupoteza maisha, huku maji yakitajwa kuwa katikati ya mzozo huo.

subscribe to our newsletter!

Afghanistan na Iran ni nchi za Kiasia zinazopakana. Kati yao, kuna Mto wa Helmand unaotiririka kutoka Afghanistan kwenda Iran. Hivi karibuni, Iran imekuwa ikilalamika kwamba Afghanistan inazuia maji ya mto huo na kusababisha ukame nchini Iran.

Malalamiko hayo yakaongezeka hadi majeshi ya nchi hizo yakafyetuliana risasi mnamo Mei 27, 2023. Risasi zikarindima kwenye mpaka wa nchi hizo katika jimbo la Nimroz, ikisemekana watu wanne walipoteza maisha, watatu wakiwa ni Wairani na mmoja Muafghani. Wengine wakajeruhiwa.

Wanajeshi wa Afghanistan wamedai kuwa ni Wairan ndiyo walioanza kufyetua risasi. Wairan nao wanadai ni wapiganaji wa Taliban ndiyo walioanza kushambulia. Kufuatia mapigano hayo, Iran ikafunga mpaka wake na Afghanistan. Biashara kati ya nchi hizo mbili zikasimama.

Kabla ya mapigano haya, Rais Ebrahim Raisi wa Iran aliwaonya Taliban wasivunje mkataba uliosainiwa mnamo 1973 kwa kuzuia maji ya Mto Helmand yanayoingia Iran, akiiagiza wizara yake ya Mambo ya Nje na ile ya Nishati zifuatilie suala hilo kwa ukaribu.

Taliban wakakanusha shutuma hizo za Rais Raisi.

Mkataba husika

Ni vizuri, hata hivyo, tukauelewa mkataba huo wa 1973. Mto Helmand, wenye urefu wa kilometa 1,126, unaanzia kutoka milima ya Hindu Kush nchini Afghanistan na kuelekea Iran. Mamilioni ya wananchi kutoka pande mbili hizi hutegemea sana maji kutoka mto huo katika umwagiliaji, uvuvi, na matumizi mengine ya nyumbani.

SOMA ZAIDI: Miaka 20 Tangu Marekani Ivamie Iraq kwa Udanganyifu. Je, Kuna la Kujifunza?

Ndipo mkataba kuhusu utumiaji wa maji ya Mto Helmand baina ya Iran na Afghanistan (Helmand River Water Treaty) ukatiwa saini mnamo Machi 13, 1973. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Afghanistan inatakiwa kila mwaka iruhusu maji angalau mita za ujazo milioni 850 zitiririke hadi Iran, “katika hali ya kawaida.”

Hata hivyo, mkataba huo haujawahi kutekelezwa kikamilifu. Iran imekuwa ikilalamika kuwa imekuwa ikipata asilimia nne tu ya maji hayo. Ilitakiwa nchi mbili zikae na kujadili jinsi ya kutekeleza mkataba wa 1973, lakini Afghanistan imekuwa siku zote katika hali ya kivita.

Kila Serikali inapobadilika ndivyo mazungumzo yanavunjika na Serikali mpya inakuja na msimamo mpya.  Mnamo Agosti 2021, wavamizi wa Kimarekani walitimuliwa na wapiganaji wa Taliban wakachukua nchi. Hawa wakaahidi kutekeleza mkataba wa 1973. 

Hata hivyo, wakaitaka Iran ielewe kuwa Afghanistan imekuwa ikikabiliwa na ukame wa muda mrefu.

Iran nayo ikaitaka Afghanistan itambue kuwa imekuwa ikiwapokea wakimbizi wengi kutoka Afghanistan. Kwa mujibu wa takwimu kutoka Umoja wa Mataifa, takriban Waafghan milioni 3.5 wamekimbilia Iran, hasa tangu Taliban waliposhika madaraka.

Hawa nao wanahitaji maji. Tatizo limeongezeka kwa vile Iran imekataa kuutambua utawala mpya wa Taliban, wakidai kuwa utawala huo unawabagua raia kwa misingi ya kikabila na kijinsia kwa kuwakandamiza wasichana na wanawake. Hata hivyo, Iran haijavunja kabisa uhusiano wake na Afghanistan.

SOMA ZAIDI: Kwa Kuzipatanisha Saudia na Iran, China Imelamba Dume Kwenye Siasa za Kimataifa

Inakisiwa kuwa nchini Afghanistan mito ya Helmand na mengineyo inatoa jumla ya maji takriban mita za ujazo bilioni 75 kila mwaka. Maana yake, Afghanistan inapata maji ya kutosha. 

Hata hivyo, tatizo lake ni kuwa nchi hiyo haina mpango wa kuhifadhi maji. Matokeo yake ni kuwa maji hayo yanaelekea nchi za jirani kama vile Iran, Pakistan, Uzbekistan, na Turkmenistan. Hali hii inazidi kuwa mbaya pale mvua inapopungua nchini Afghanistan.  

Kwa muda mrefu nchi hiyo pia imeshindwa kutumia mito yake kuzalisha umeme na kwa hiyo inalazimika kununua umeme kutoka nchi za jirani kama Iran. Hata hivyo, Afghanistan imeanzisha mradi wa kutumia maji ya Helmand kwa kujenga bwawa liitwalo Kamal Khan, lengo kuu likiwa ni kumwagilia mashamba na kuzalisha umeme.

Uhaba wa maji

Iran imelalamika kuwa bwawa hilo litaongeza upungufu wa maji nchini Iran. Tayari nchini Iran wakulima wanalalamika kuwa wanakosa maji ya kutosha. Mwaka 2021, wakulima hao walidiriki kuandamana. Afghanistan, kwa upande wake, inadai bwawa hilo halipingani na mkataba wa 1973.

Kwenye miaka ya 70, Iran ilikuwa tayari kusaidia ujenzi wa bwawa hilo kwa kuligharamia iwapo Afghanistan ingehakikisha kuwa Iran itapatiwa maji ya kutosha. 

Hata hivyo, utekelezaji wa mkataba huo umekuwa ukiyumba kwa vile Afghanistan imekuwa katika migogoro ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na kushambuliwa na mataifa ya Magharibi. 

SOMA ZAIDI: Hadithi ya ‘A Walk in the Night’ Na Uhalisia wa Ubaguzi wa Rangi Afrika ya Kusini

Iran nayo imekumbwa na vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi. Tumeona jinsi wakulima wa Iran walivyoandamana wakidai maji. Kwa mujibu wa shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na ukame kwa takriban miaka 30 sasa. 

Na idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini humo inakisia kuwa asilimia 97 ya nchi huwa inakabiliwa na upungufu wa maji.

Wakati Iran inalalamika kuwa Afghanistan imeshindwa kutekeleza mkataba wa 1973, jibu la Afghanistan ni kuwa shutuma za Iran si za kweli kwa sababu Afghanistan nayo imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa maji kiasi kwamba wakulima wake wamelazimika kuyahama mashamba yao. 

Wanasema mkataba wa 1973  hausemi kuwa Afghanistan iyaachie maji ya Helmand hata nchi hiyo inapokabiliwa na ukame. Inaongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, maji yameadimika kila mahali. Kwa hiyo, Iran haitakiwi ilalamike bali itafute usuhuhishi kwa njia ya mazungumzo na diplomasia.

Balozi wa Iran nchini Afghanistan, Hassan Kazemi Qom, amekutana mara kadhaa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan, Amir Khan Muttaqi, kuzungumzia mzozo huu na kuona namna ya kuutatua. 

Mazungumzo pia yamefanyika baina ya Muttaqi na waziri mwenzie kutoka Iran, Hossein Amirabdollahian. Ni matumaini ya wengi kwamba mazungumzo haya yatasaidia kurejesha mahusiano mazuri kati ya nchi hizo mbili na kuiepusha dunia na vita nyingine!

Nizar Visram ni mchambuzi wa siku nyingi wa siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia au nizar1941@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts