The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Kuzipatanisha Saudia na Iran, China Imelamba Dume Kwenye Siasa za Kimataifa

Hatua ya kuwapatanisha mahasimu hao wawili inaiweka China kwenye nafasi ya kuaminika zaidi katika kutafuta suluhu za amani duniani.

subscribe to our newsletter!

Baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa takriban miaka saba, Iran na Saudi Arabia hatimaye zimeamua kufufua uhusiano wao wa kidiplomasia, huku zikitangaza kwamba balozi zao kwenye nchi hizo pia zitafunguliwa. Hatua hii ilikuja kufuatia mapatano yaliyoongozwa na Rais wa China Xi Jinping jijini Beijing, China.

Nchi hizo mbili zimeitangazia dunia kwamba kufuatia hatua hiyo, zitaandaa mipango ya kubadilishana mabalozi katika muda wa miezi miwili. Ingawa makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mazungumzo yaliyofanyika nchini China, katika hatua za awali Oman na Iraq pia zilisaidia mchakato huo wa mapatano.

Saudi Arabia na Iran zimesisitiza umuhimu wa kila nchi kujiamulia mambo yake ya ndani bila ya kuingiliwa na nchi nyingine. Walikubali pia kutekeleza makubaliano ya ushirikiano wa usalama yaliyosainiwa mnamo mwaka 2001, pamoja na makubaliano ya 1998 kuhusu ushirikiano katika biashara, uwekezaji, ufundi, sayansi, utamaduni, na michezo.

Makubaliano haya yaliyofikiwa Machi 10, 2023, ni zaidi ya kuanzisha uhusiano wa kibalozi. Ni ushirikiano kamili kati ya nchi hizi mbili zilizokuwa zikihasimiana tangu mapinduzi ya Iran ya mwaka 1997. Na kwa muda wa miaka saba iliyopita nchi hizo zimekuwa zikihusika na vita inayoendelea nchini Yemen.

Saudi Arabia na Iran zimeonesha kwa mfano kwamba kwa kufanya mazungumzo ya amani inawezekana kutatua matatizo yao bila ya kuingiliwa na mataifa makubwa, na bila ya kutumia silaha. Nchi hizo mbili zimeonesha kuwa nchi za Mashariki ya Kati zinaweza kujiamulia mustakbali wao bila ya kutegemea mataifa ya kibabe.

Umoja wa Mataifa (UN) ulizipongeza Saudi Arabia na Iran kwa hatua hiyo, huku Katibu Mkuu António Guterres akiipongeza pia China kwa uamuzi wake wa kuendesha mazungumzo hayo, akisema: “Ujirani mwema kati ya Saudi Arabia na Iran ni muhimu sana kwa amani na utulivu katika maeneo yote ya Ghuba ya Uajemi.”

Uhasama wa muda mrefu

Uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran haukuwa mzuri tangu mwaka 1979 wakati Iran ilipompindua Mfalme Shah aliyekuwa kibaraka wa Marekani na rafiki wa Saudi Arabia. Tangu wakati huo, Serikali ya Iran imekuwa ikipigwa vita na Marekani na marafiki zake.

Saudi Arabia ikavunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 2016 wakati Wairani wenye hasira walipovamia ubalozi wa Saudi Arabia jijini Tehran. Chanzo kilikuwa ni hatua ya Saudi Arabia kumyonga mkuu wa madhehebu ya Shia, Sheikh Nimr Baqir al-Nimr, aliyekuwa mpinzani wa utawala wa Saudi Arabia.

Uhasama huo uliendelea hadi Aprili 2021 wakati Iraq ilipofanikiwa kuzikutanisha nchi hizo katika mji wake mkuu wa Baghdad. Baada hapo vilifanyika vikao vitano. Oman nayo iliunga mkono mazungumzo hayo ambayo pia yalifanyika Oman. Hata hivyo, hakuna makubaliano yaliyofikiwa. Ndipo China ikaamua nayo isaidie.

Mnamo Disemba 2022, Xi Jinping alifanya ziara nchini Saudi Arabia ambako alizungumzia suala la Iran. Mnamo Februari 2023, Xi alimkaribisha Rais wa Iran Ebrahim Raisi ambaye alitembelea China, akiambatana na mawaziri wake sita. 

Raisi akamueleza Xi kuwa Iran iko tayari kufikia makubaliano na Saudi Arabia. Ndipo mazungumzo yakapamba moto, na jitihada hizo mwishowe zikazaa matunda wakati mkataba ulipotiwa saini mjini Beijing hapo Machi 10, 2023.

Wafuatiliaji wameielezea hatua hii kuwa ni ya kihistoria, wakibainisha faida kadhaa zinazoweza kupatikana kutokana na hatua hiyo. 

Kubwa kabisa ni uwezekano wa kumalizika kwa vita ambayo imeendelea kupiganwa nchini Yemen inayopakana na Saudi Arabia, vita iliyoanza mwaka 2014 wakati wapiganaji wa kabila la Houthi waliposhika sehemu kubwa ya nchi hiyo pamoja na mji mkuu wa Sanaa.

Houthi wamekuwa wakiungwa mkono na Iran. Kwa upande wa pili, Saudi Arabia imekuwa ikiwaunga mkono watawala waliopinduliwa. Nchi za Magharibi, kama vile Marekani na Uingereza, zimekuwa zikitoa silaha kwa Saudi Arabia zilizokuwa zikitumika kuwashambulia Houthi. 

Majeshi ya Saudi Arabia yakayakalia maeneo ya Yemen kusini, hali iliyopelekea maelfu ya wananchi kuuwawa na wengi kuyakimbia makazi yao. Wadadisi wana matumaini kwamba kufuatia makubaliano ya Beijing, kuna uwezekano kwa Wayemeni wenyewe wakazungumza jinsi ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mwaminifu China?

Labda faida nyengine kubwa ambayo inategemewa kupatikana kutokana na hatua hii ni kuibuka kwa taifa la China kama msuluhishi anayeaminika, hatua ambayo bila shaka ni pigo kwa taifa la Marekani ambalo siku zote limekuwa likijitapa kama baba wa dunia. 

Hata hivyo, badala ya kutumia hadhi hiyo kupatanisha mahasimu, Marekani imekuwa ikiwafanya marafiki kuwa mahasimu!

Ndiyo maana haishangazi kuona Serikali ya Marekani ikibeza makubaliano hayo kati ya Saudi Arabia na Iran, huku ikidai eti Iran haiaminiki kwani wakati wowote inaweza kujitoa. 

Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani John Kirby amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, “Ingawa tungependa kuona vita vya Yemen vinamalizika, lakini Iran siyo nchi inayoheshimu ahadi zake.”

Lakini ni Marekani iliyoshindwa kuheshimu ahadi yake kwenye makubaliano yake yaliyolenga kudhibiti utengenezaji wa silaha za nyuklia (JCPOA) kwa kuanzia na Rais Donald Trump aliyeitoa Marekani kwenye makubaliano hayo, hadhi iliyodumishwa na Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden.

Kwa ufupi, tunaweza kusema kwamba China imeweza kuwa msuluhishi pale ambapo Marekani haikuweza kufanya kazi hiyo. Rais Biden aliwahi kusema kwa hasira kuwa atafanya kila bidii kuiadhibu Saudi Arabia kutokana na mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi. 

Hata hivyo, vita ya Ukraine ilipoanza Biden akabadili msimamo, akazuru Saudi Arabia na kuiomba iongeze uzalishaji wa mafuta.

Saudi Arabia ikakataa na Biden akarudi mikono mitupu. Sasa kwa Saudi Arabia kusaini makubaliano ya amani na Iran ni sawa na kumbeza Biden na kumuambia kuwa Saudi Arabia haitainyenyekea tena Marekani.

Baada ya kusuluhisha Saudi Arabia na Iran, China sasa inafanya juhudi za kusuluhisha Urusi na Ukraine. China tayari imependekeza hatua 12 za kufikia makubaliano. Tatizo ni kuwa katika vita hivi, Urusi haipigani na Ukraine bali inapigana na NATO. Kwa hiyo, si rahisi kusema iwapo China itafanikiwa au la.

Hata hivyo, Rais Xi tayari amezuru Moscow na kuonana na Rais Vladimir Putin. Baada ya hapo, Xi anategemewa kuzungumza na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine. Wafuatiliaji wa siasa za kimataifa wataangalia kwa hamu ni kwa namna gani Xi anaweza kukwepa vihunzi na kuzipatanisha Urusi na Ukraine!

Mkataba na Israel kufifia?

Kuna tukio jingine kubwa linaweza kutokea kufuatia hatua hii ya Saudi Arabia na Iran kuweka uhasama wao kando na kuamua kushirikiana. Na hili linahusiana na uwezekano wa Saudi Arabia kukataa kusaini mkataba unaodhaminiwa na Marekani wa kutafuta amani kati ya mataifa ya Kiarabu na Israel.

Ikijulikana kwa jina la The Abraham Accords, mpaka sasa tayari Marekani imeweza kuzisainisha nchi za UAE, Bahrain, Morocco na Sudan kwenye mkataba huo, na Marekani inategemea Saudi Arabia itasaini pia makubaliano hayo.

Kukubali kwake kwamba uhasama wake na Iran uishe kumewafanya baadhi ya wadadisi kuuliza endapo kama Saudi Arabia bado inaweza kuona tija ya kudumisha amani na Israel, taifa ambalo ni hasimu wa taifa la Iran. 

Lengo kuu la The Abraham Accords ni kuhalalisha uvamizi wa Israel dhidi ya Palestine, pamoja na kuitenga Iran na kuifanya iwe adui wa Waarabu. Baada ya “kuyamaliza” yeye na Iran, ni ngumu kuiona Saudi Arabia ikishiriki kwenye mkataba huo.

Kwa uamuzi wake wa kumzuia Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Eli Cohen kuingia nchini humo kushiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu utalii, Saudi Arabia tayari imetuma ujumbe kwamba kuna uwezekano mdogo sana kusaini mkataba huo wa The Abraham Accords.

Cohen alishindwa kuingia Saudi Arabia baada ya taifa hilo kusema kwamba wakati haiwezi kumzuia Waziri huyo kuingia nchini mwao, Saudi Arabia haitamuhakikishia usalama wake atakapokuwa nchini humo, na hivyo kumfanya Cohen asitishe ziara yake!

Nizar Visram ni mchambuzi wa siku nyingi wa siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 673 004 559 au nizar1941@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *