Serikali muda wowote ndani ya mwezi huu wa Julai itaitambulisha kahawa kama bidhaa yake ya kwanza itakayoiuza nje ya nchi chini ya mpango wa Soko la Biashara la Eneo Huru la Afrika (AfCFTA), huku Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ashatu Kijaji, akisema kwamba Serikali haitauza kahawa ghafi, bali ile iliyokamilika.
Uamuzi huu wa Serikali ulifikiwa baada ya majadiliano ya miezi kadhaa baina yake na wadau mbalimbali juu ya ipi iwe bidhaa ya kwanza kupelekwa kwenye soko hilo la watu zaidi ya billioni 1.3. Tanzania ni miongoni mwa mataifa 44 ya Afrika yaliyoridhia mkataba huo.
Ukiacha korosho na tumbaku, kahawa ni bidhaa ya kilimo ya tatu nchini yenye kuchangia pato kubwa la taifa, ikikadiriwa kwamba kwa mwaka wa fedha 2021/2022 zao hilo la biashara lilichangia zaidi ya Dola za Kimarekani millioni 142.
Asilimia 90 ya wazalishaji wa kahawa nchini ni wakulima wadogo wadogo ambao huuza bidhaa zao kwa wafanyabiashara, moja kwa moja au kupitia vyama vyao vya ushirika. Uzalishaji wa zao hilo pia umeendelea kukua mwaka hadi mwaka.
Kwa mfano, uzalishaji uliongezeka kutoka tani 45, 245 kwa mwaka wa 2017/2018 hadi kufikia tani 65, 235 kwa mwaka 2021/2022, huku Serikali ikichukua hatua kadhaa za kuongeza uzalishaji, kama vile usambazaji wa miche bora na uimarishaji wa masoko.
Vinara
Barani Afrika, Ethiopia ni nchi ya kwanza kwa uzalishaji mkubwa na uuzaji wa kahawa ghafi, ikikadiriwa kuuza zaidi ya tani 280, 560 nje ya nchi, ikifuatiwa na Uganda ambayo kwa mwaka 2022, kati ya asilimia 17 na 19 ya fedha zote za kigeni zilipatikana kwenye mauzo ya kahawa.
Kidunia, Ethiopia ni nchi ya tano kwa uzalishaji wa kahawa.
SOMA ZAIDI: Wakulima Mbozi Wagoma Kuuza Kahawa Yao Wakidai Bei Hairidhishi
Ethiopia na Uganda zimekuwa zikifanya biashara zaidi na mataifa kama Italia, Ujerumani, Marekani, Japan, Ubelgiji na mataifa ya Mashariki ya Kati. Uganda pia imepenya hata kwenye soko la China na mataifa ya Ulaya.
Uganda inatajwa kuwa nchi pekee iliyowahi kupata kipato kikubwa kitokanacho na mauzo ya kahawa ndani ya mwaka mmoja kwa kuuza bidhaa hiyo kwa thamani ya Dola za Kimarekani milioni 862. Ivory Coast, Burundi, Rwanda na Kenya pia huzalisha kahawa.
Tanzania pia imekuwa ikiuza kahawa ghafi kwenye mataifa kama vile Japan, Italia na Marekani. Hali hii ya uuzaji wa kahawa katika mataifa haya ya nje ndiyo imepelekea taifa kuendelea kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha zao hili.
Ripoti ya Tasnia ya Kahawa Tanzania: Mkakati wa Maendeleo 2011-2021, imeeleza kwa kina mpango wa ongezeko la uzalishaji kutoka wastani wa tani 50, 000 hadi kufikia tani 100,000 mwaka 2021.
Moja ya njia ya kufikiwa malengo hayo ni kuongeza mauzo kwenye mataifa washirika wa kibiashara, hususan nchi kama Japan ambayo huchangia asilimia 15 ya ununuzi ya bidhaa hii, pamoja na Ujerumani, Italia na Ubelgiji ambazo zote huchangia asilimia 10.
Asilimia 25 iliyobakia inagawanyika kwenye nchi tofauti tofauti kama vile Finland na Uswizi. Ni wazi kwamba Tanzania itatambulisha bidhaa hii katika soko la AfCFTA ndani ya mwezi huu kama Serikali ilivyoahidi.
Hamna tija
Hata hivyo, siioni hatua hiyo ikileta tija kwa wakulima na taifa kwa ujumla. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Afrika imekuwa na matumizi madogo ya kahawa ikilinganishwa na mataifa/jumuiya zingine duniani.
Ukiachilia mbali taifa la Ethiopia ambao hupendelea kahawa ya kwao inayofahamika kama Yirgacheffe ambapo kwa mwaka matumizi ya mtu mmoja ni kilo 2.27, mataifa mengine yamekuwa na utumiaji mdogo wa bidhaa hiyo.
SOMA ZAIDI: Parachichi Inavyokimbiza Kilimo cha Kahawa Mbozi
Kwa mfano, nchini Algeria mtu mmoja hunywa kilo 3.2 tu za kahawa kwa mwaka, huku Madagascar ikiwa ni kilo moja na Ivory Coast kilo 0.9. Nchi za Ivory Coast na Uganda ambazo ni wazalishaji wakubwa wa kahawa Afrika, wananchi wake kwa wingi hutumia kakao na chai badala ya kahawa.
Kwa hiyo, bidhaa kama kahawa, ambayo soko lake kubwa limekuwa kwenye mataifa ya nje, kuiweka kama bidhaa namba moja kwenye ushindani, inaweza isiwe na tija kwa kuwa siyo bidhaa hitajika kwenye soko la Afrika kwa sasa.
Chaguzi za bidhaa hizi pia zinapaswa kusindikizwa na mpango wa kuzilinda kwenye ushindani kupitia bajeti ya wizara na Serikali Kuu pamoja na wataalamu wa soko na ushawishi. Kiujumla, uwekezaji katika ushindani unapaswa kuzingatiwa.
Tanzania inaweza kuitumia fursa hii kuitangaza kahawa katika soko la AfCFTA ili kupata uwekezaji wa viwanda ndani ya nchi kutokana na sheria ya mkataba ya “Rule of Origin” ambayo inahitaji bidhaa izalishwe ndani ya Afrika.
Ezra Nnko ni mchambuzi wa uchumi na siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ezra.nnko@gmail.com au +255 765 571917/+255 784 527018. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
Nina kampun ya kulima kahawa nipo mbozi mkoa wa songwe. Kwa mwaka huu tunatarajia kuzalisha sio chin ya tan 50. Nakuomba tukubaliane kunitafutia wateja wa kahawa wa bei nzuri kutoka nje ya bara la afrika.