The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Ni Muhimu Kumjengea Mtoto Tabia ya Kujitegemea Mapema

Malezi ya watoto ni jambo lenye kuhitaji subira na uvumilivu. Muamini mtoto. Hatokuangusha.

subscribe to our newsletter!

Wakati mwingine, wazazi na walezi tunapata wasiwasi juu ya maisha ya baadaye ya watoto wetu. Tunajiuliza: Watakuwa na maisha ya aina gani? Watakuwa watu wazima wa namna gani? Hivi watafanikiwa kielimu? Biashara?

Lakini kimsingi, sisi wazazi na walezi ndiyo watu pekee wenye jukumu la kuhakikisha kuwa tunalea watoto wetu katika mienendo ambayo tunaona ni mema, kama usemi maarufu wa wahenga usemavyo, mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo.

Tabia ya kujitegemea, kwa kiasi kikubwa, huja kutokana na msukumo wa wazazi na namna makuzi yanavyotolewa. Ni muhimu kwa mzazi au mlenzi kuanza kwa kumpa fursa mtoto kujifanyia vitu, au mambo madogo-madogo kadiri anavyozidi kukua.

Mtoto anatakiwa aanze kujua, kwa mfano, dhana ya kunawa mikono peke yake kuanzia umri wa miaka mitatu au mapema zaidi. Mueleze kwa nini kunawa mikono ni muhimu. Mfunze kuoga pekee yake mapema. Aanze kufua nguo nyepesi kama kanga au shati la shule mapema.

SOMA ZAIDI: Watoto Wanaoangalia Sana TV Wanaweza Kuharibu Miundo ya Ubongo

Taratibu ajue akitoka shule pana kazi kadha wa kadha zinazomsubiri. Mtie moyo kwa kumsifu pindi anapojaribu kujifanyia jambo mwenyewe pasi kuambiwa. Hii itamfanya aendelee kujihusisha na jambo hilo mara kwa mara na mwishowe atavuna uzoefu katika hilo.

Heshimu mawazo ya mtoto. Watoto wetu hupenda sana kutoa maoni yao kama sehemu ya utatuzi wa changamoto za siku hata siku katika familia zetu. Zungumza na mtoto wako, kubaliana naye – lakini mpe sababu kwa nini unajua anachoshauri hakiwezekani.

Unamjengea uwezo wa kusimama pekee yake katika hoja. Mpe fursa ya kuchagua nguo anayopenda kuvaa – haya mambo madogo yanatafsiri ya uhuru wa kuamua. Huku nako ni kukuza dhana ya kujitegemea.

Upo ushahidi wa kutosha kuwa baadhi ya wazazi huwafanyia watoto wao kila kitu majumbani mwao kwamba wanawapenda sana. Lakini swali la kujiuliza ni kuwa je, utaishi na watoto wako maisha yao yote?

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ni Muhimu Mzazi Kumuomba Mtoto Wake Msamaha?

Mapenzi kwa watoto ni pamoja na kuwaandalia kesho yao kupitia kazi kama kufagia nyumba, kufuta vumbi madirishani, kuosha vyombo, kutandika kitanda, kujipangia ratiba ya siku, nakadhalika.

Mpe usaidizi wa masuala ambayo dhahiri ni magumu kwake. Namna ya kukabiliana na msiba, changamoto za kielimu, namna ya kujenga uhusiano bora wa kirafiki na watoto wengine, kuwaheshimu wakubwa, nakadhalika, ni baadhi ya mambo ambayo yanahitaji ukaribu na miongozo ya kutoka kwako mzazi.

Mtambulishe kwa ndugu wa familia tandaa – apate kujenga mahusiano na shangazi zake, wajomba zake, bibi na babu pasi wewe kuingilia-ingilia. Awasiliane nao binafsi kadiri anavyokua.

SOMA ZAIDI: Fahamu Kwa Nini Watoto Wachanga Hucheua

Bahati mbaya sana wazazi na walezi, hasa wa mijini, tunatumia muda wetu mwingi kazini na hata tunaporudi majumbani hatutaki watoto wetu wamsaidie mfanyakazi wa nyumbani kazi.

Wazazi wengine, mtoto akianza kupata marafiki anaambiwa akome. Ataishi vipi dunia hii bila kuhusiana na binadamu wengine? Uzoefu wa kuwa na marafiki – tabia za watu mbalimbali na mambo ya namna hii hawezi kupata ndani ya nyumba yako.

Malezi ya watoto ni jambo lenye kuhitaji subira na uvumilivu. Muamini mtoto. Hatokuangusha!

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *