The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fahamu Kwa Nini Watoto Wachanga Hucheua

Siyo vyema kwa mzazi, ama mlezi, aonapo mtoto anacheua nae akapuuzia kwa kujua kuwa ni tendo la kawaida.

subscribe to our newsletter!

Kucheua kwa mtoto ni kitendo cha mtoto kutoa mabaki ya chakula yanayopitia mdomoni muda mfupi tu baada ya kula ama kunyonya. Kwa wazazi na walezi wengi, ni kitendo cha kawaida na mara nyingi baada ya mtoto kunyonya kauli kama ‘mcheulishe mtoto’ husikika.

Kucheua kwa mtoto hutokea mara baada ya mtoto kunyonya, ndani ya saa moja au mbili. Watoto wachanga, mathalan wa umri wa miezi mitatu, hucheua angalau mara moja kwa siku.

Baadhi ya watoto wachanga huanza kucheua meno yanapoanza kuota, wanapoanza kutambaa, na wanapoanza kula vyakula vigumu.

Kucheua kwa watoto hushika kasi zaidi pindi wanapofikisha umri wa miezi miwili hadi minne, lakini pia kasi hiyo hupungua pindi wafikishapo umri wa miezi saba hadi nane na huacha kabisa kucheua pindi wafikishapo umri wa mwaka mmoja.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Siku 1,000 za Mwanzo za Mtoto Ni Muhimu?

Siyo vyema kwa mzazi, ama mlezi, aonapo mtoto anacheua nae akapuuzia kwa kujua kuwa ni tendo la kawaida. La hasha! Kucheua kwa mtoto wakati mwingine huweza kuashiria tatizo kubwa zaidi kwa afya ya mtoto.

Mathalan, inaweza kutokana na kuziba kwa mrija unaopitisha chakula, mzio, au allergy, sambamba na ugonjwa wa tumbo ambao kwa lugha ya kimombo hujulikana kama “Gastroesophageal Reflux Disease (GERD).”

Kucheua baada ya kula

Wataalam wa afya, hususan madaktari bingwa wa tiba na uchunguzi wa magonjwa ya watoto, yaani pediatrics, wanakubaliana kwamba sababu kuu ya watoto kucheua ni kutokuimarika kwa maumbile ya asili ya misuli ya watoto, hususan misuli ya umio ambayo kwa kitaalam hujulikana kama lower and upper esophageal sphincter.

Misuli hii hufunga na kufungua mirija inayotoka kooni hadi tumboni ili kuruhusu chakula kifike tumboni. Kwa watoto wachanga, misuli ya umio la chini, yaani lower esophageal sphincter ambayo huunganisha mrija wa kupitisha chakula na tumbo, huwa haijatengemaa, na hivyo huruhusu chakula kama vile maziwa kurudi juu (kuelekea mdomoni) badala ya kwenda tumboni moja kwa moja.

SOMA ZAIDI: Fanya Hivi Mtoto Wako Akipata Tumbo la Chango

Misuli hii hufanya kazi maalumu ya kufungua njia ili kuruhusu chakula kielekee tumboni na kisha hufunga ili kuzuia chakula kisipate kurudi kilipotoka, yaani mdomoni.

Hivyo basi, kutotengemaa kwa misuli hii ndiyo hasa hupelekea tendo la kucheua miongoni mwa idadi kubwa ya watoto wachanga mara baada ya kupata mlo ama kunyonya.

Vilevile, maziwa wayapatayo watoto wachanga kutoka katika ziwa au titi la mama pamoja na yale yasiyotoka kwa mama, yaani maziwa ya kopo, ambayo hutumika kama chakula, mara zote huwa katika hali ya majimaji, au kimiminika, jambo ambalo hupelekea urahisi wa hali ya kucheua.

Hata hivyo, uwepo wa hewa ndani ya tumbo la mtoto ambayo aghalabu hutokana na sababu kama vile mtoto kunyonya titi la mama haraka haraka, kunyonya kupita kiasi, mtoto kuchezea titi la mama pindi anyonyapo pamoja na mama kutofahamu namna sahihi ya kumnyonyesha mtoto pia hupelekea mtoto kucheua mara kwa mara.

SOMA ZAIDI: Je, Unafahamu Kwamba Hata Mtoto Anaweza Kupata Kifua Kikuu?

Ni vyema wazazi na walezi kutambua kwamba kucheua huweza kupelekea mtoto pia kutapika.

Vilevile, ieleweke kuwa inapotokea mtoto anacheua mpaka matapishi yanaruka nje kwa nguvu sana, anahangaika na kujikamua sana kabla ya kucheua au kutapika huku akiugulia maumivu, akikataa kunyonya, akipumua kwa shida, akipata tabu amezapo chakula, maumivu ya koo, kucheua macheuo ya rangi ya kijani ama njano basi hapo wazazi, ama walezi hatupaswi kupuuzia.

Tutambue kwamba kucheua huko si kwa kawaida bali ni dalili mbaya kuhusu afya ya mtoto na hivyo ni muhimu kumuwahisha mtoto katika kituo cha afya ili afanyiwe uchunguzi na kupatiwa matibabu haraka iwezekanavyo.

Makala hizi za maelezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *