The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Siku 1,000 za Mwanzo za Mtoto Ni Muhimu?

Ukuaji vema wa ubongo wa mtoto unahitaji lishe bora, huduma bora ya afya, mawasiliano chanya, na mazingira salama.

subscribe to our newsletter!

Hivi ni wakina mama, baba na walezi wangapi wanafahamu namna siku 1,000 za mwanzo za utoto zilivyo muhimu kwa maisha ya mtoto, na namna gani tunaweza kufikisha ujumbe wa umuhimu wa siku za mwanzo utotoni katika jamii zote nchini Tanzania?

Wataalamu wanasema ubongo hukua kwa kasi kubwa katika siku 1,000 za mwanzo wa uhai wa binadamu. Hiki ni kipindi kinachoanzia kutungwa kwa mimba hadi umri wa miaka miwili.

Kila mara, mama au baba anapocheza na kucheka, kusoma kitabu, au kushiriki mchezo na mwanawe, ujue kuna maelfu ya hisia chanya zinazojengeka kwenye ubongo wa mtoto huyo mchanga, zinazojenga uwezo wake wa kujifunza, utendaji, kuendana na mabadiliko, na hata kukabiliana na changamoto.

Ripoti mpya ya ulimwengu iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) iitwayo ‘Siku za Mwanzo za Maisha ya Kila Mtoto ni Muhimu (Early Moments Matter For Every Child)’ inasema kipindi cha tangu kutungwa mimba hadi kuanza shule ni muhimu, ni fursa adimu katika kuandaa vema ubongo wa mtoto.

SOMA ZAIDI: ‘Nakuwa Baba Kamili’: Wanaosindikiza Wake Zao Kliniki Waeleza Uzoefu Wao

Huu ndiyo wakati wa kuujenga ubongo wake. Ikiwa watoto watalelewa kwa namna inayojenga vema akili zao, wataweza kujifunza vema, hivyo wataweza kuchangia na kupata kipato bora zaidi. Hii itawasaidia wao, familia zao, na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Watoto wanahitaji huduma bora za afya na lishe, kuchangamshwa, fursa za kujifunza utotoni, na mazingira salama ili ubongo wao uweze kukua vema. Kwa bahati mbaya, duniani kote, mamilioni ya watoto wanakosa fursa hii.

Watoto milioni 155 duniani kote wanaripotiwa kuwa na udumavu, huku watoto milioni 230 wanaishi katika mazingira yaliyoathiriwa na machafuko na wanakabiliwa na msongo wa mawazo. Watoto wengine milioni 300 wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na uharibifu wa mazingira. Mambo yote haya yanaathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto.

Tanzania pia ina maelfu ya watoto wanaokosa vichochezi hivyo vinavyolea ukuaji wa kiwango cha juu cha ubongo wao. Kwa mfano, lishe duni miongoni mwa watoto nchini imefanya asilimia 34 ya watoto walio chini ya miaka mitano kudumaa.

SOMA ZAIDI: Mtaalamu Abainisha Madhara ya Muda Mrefu ya Adhabu ya Viboko kwa Mtoto

Wataalamu wanasema kudumaa humkosesha mtoto fursa ya kukua akiwa na afya bora, kumkosesha uwezo wa kujifunza kikamilifu na hata kupunguza nafasi ya kupata ajira akifikia umri wa kuajiriwa.

Tunawezaje kubadili hali hii?

Wafanyakazi wa afya na lishe waliopatiwa mafunzo stahiki, wanafanya kazi kubwa vijijini kwa kutoa mafunzo kwa wazazi juu ya malezi bora na namna ya kuelewa tabia za watoto wachanga.

Wakina mama, kupitia vikundi na jumuiya zao, wanapewa mafunzo ya namna ya kutengeneza vifaa vya kuchezea vya watoto vya gharama nafuu kutokana na malighafi zinazopatikana katika mazingira yao.

SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni

Mambo yote haya yanasaidia kuboresha malezi ya watoto. Hivyo basi, mara nyingine utakapopata fursa ya kumwangalia mtoto mchanga, tafadhali kumbuka kuwa ukuaji vema wa ubongo unahitaji lishe bora, huduma bora ya afya, mawasiliano chanya, na mazingira salama.

Inaweza kuonekana kuwa ni kitu kidogo, lakini maendeleo ya nchi yanategemea watu wenye uwezo kiakili, na inawezekana kwa Tanzania, kama nchi, kuwa na mamilioni ya watu wenye uwezo wa kiakili.

Makala hizi za maelezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

  1. Hongera Kwa Eimu nzuri.Ipo haja ya kuweka msisitizo mkubwa Kwa wazazi na pengine kuwafundisha namna Bora ya kulea watoto ndani ya siku hizo 1000.Ubongo wa mtoto ni Kama computer ambayo haijawekewa programs.Computer itakufanyia kazi nzuri na za maana kutegemea programs na ma faili uliweka.Kuanzia mimba inatungwa YAMPASA mzazi ajue ni programs zipi na nzuri aanze kuweka Kwa mtoto.Yampasa mzazi ajue ni Mafaili yapi ayaweke kwenye ubongo wa mtoto.Sasa hivi tunashuhudia Vitendo visivyo vya utu vikishamili Kwa sababu program na majalada yaliyowekwa Kwa mtoto ndani ya siku Hizi 1000 hazikuwa za kumjenga kuwa na utu.Ndo maana ubongo wao unawaongoza kutenda maovu. Kuondoa Hali hii au kuipinguza ipo haja ya kuelimisha wazazi wajue namna Bora ya kuiandaa ubongo wa mtoto kuwa na utu.Tukumbuke mbwa MZEE afundishwi tabia MPYA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *