The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mtaalamu Abainisha Madhara ya Muda Mrefu ya Adhabu ya Viboko kwa Mtoto

Kati ya madhara hayo ni mtoto kujenga tabia ya uongo pamoja na kutokujiamini.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mtaalamu wa masuala ya ustawi wa jamii, malezi, makuzi na maedeleo ya mtoto Fatuma Kamramba amebainisha kwamba wakati adhabu ya viboko kwa watoto inaweza kuleta suluhu ya muda mfupi kwa anayeitoa, adhabu hiyo ina madhara mengi na ya muda mrefu kwa mtoto husika.

Kamramba, anayefanya kazi na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na ulinzi na makuzi ya mtoto la C-Sema, alitoa tathmini hiyo alipofanya mahojiano maalum na The Chanzo ofisini kwake mnamo Machi 3, 2023.

“Ukiacha kuondoa hasira kwa mpigaji, [viboko] vinatengeneza tabia za uongo, watoto wengi wanaopigwa njia yao mbadala wa kuepuka fimbo ni uongo,” alisema Kamramba, akieleza kwamba tabia hiyo mtoto hukua nayo mpaka ukubwani kwake.

“Lakini pia tunapata watu ambao kazi yao ni kusema tu ‘ndiyo’ katika kila jambo, hata kama ana maoni yake anaogopa kuyatoa kwa sababu toka mdogo anahisi kuna mamlaka juu yake,” aliongeza mtaalamu huyo.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo na hapa mtaalamu huyo anaanza kwa kueleza kwa nini adhabu ya viboko, hususan shuleni, inapaswa iondolewe:

Fatuma Kamramba: Sababu ya kwa nini adhabu ya viboko shuleni iondolewe, nadhani sisi wote tukitazama tangu viboko vianze kutumika havijawahi kukoma, havijawahi kuacha kutumika.

Kwa hiyo, tunavyojua kwamba shule inakuwa na madarasa mbalimbali, ina maana kama vingekuwa vinasaidia basi walimu tangu waanze kutumia viboko wangekuwa wameshapata suluhisho kwamba viboko ni suluhisho au ni sababu ya kujenga tabia.

Mimi nasema viboko visitumike kwa sababu watoto ni binadamu. Na wengi wetu kama walezi, ama wazazi, hatuangalii watoto kwa namna ya kuwaona kama binadamu wenye ubongo ambao wanaweza kufanya maamuzi, ambao wana fikra, ambao wana mawazo mbalimbali.

Kwa hiyo, ili uweze kuacha kutumia viboko sasa inabidi kwanza uanze kwa kuthamini utu wa mtoto. Lakini pia, uanze kutumia njia mbadala ambayo inaweza kuwa ni mazungumzo ya wewe na mtoto katika umri mdogo.

Viboko shuleni vinakuwa vingi kwa sababu tumejenga huo msingi nyumbani na walimu pia ukiacha kuwepo shuleni bado nyumbani kwao ni wazazi na wanatumia hivyo viboko.

Na mara nyingi makosa ya watoto wanaochapwa yanakuwa ni yaleyale yanayojirudia, ndiyo maana nasema viboko siyo suluhisho.

The Chanzo: Ni kwa namna gani sasa tunaweza kutoka kwenye hii adhabu ya viboko kama taifa?

Fatuma Kamramba: Kwa hiyo, kama wazazi wanatakiwa kabla mtoto hajaenda kuandikishwa shule kwanza, inabidi wawe wameshaanza msingi wa kumlea yule mtoto bila fimbo.

Lakini kwa sababu hatuwezi kuwafanya wazazi wote, kwa wakati mmoja, waanze kuwalea watoto wao bila ya fimbo ina maana kutakuwa na mchanganyiko wa watoto ambao wamelelewa bila fimbo na ambao wamelelewa kwa fimbo.

Kwa hiyo, inabidi suala la malezi shuleni lisimuhusu mwalimu shuleni peke yake. Mara nyingi viboko vinaendelea kwa sababu hatuna mpango wa pamoja, hatuna mpango kazi wa pamoja, baina ya walimu na wazazi katika namna ya kulea watoto wetu.

Mzazi unapomzaa mtoto wako ili uweze kuacha kutumia viboko unatakiwa uwe na mpango kazi, au mpango mkakati, ambao umeuweka kwamba wewe unahitaji mtoto wako katika miaka 20 tangia sasa ulipomzaa anatakiwa kuwa mtu wa aina gani katika masuala mazima ya tabia, uhusiano na watu ndani na nje ya familia.

Kwa hiyo, ili uweze kutengeneza hayo mambo lazima mtoto wako uanze naye mapema. Kwanza ujue namna ambavyo watoto wanafikiri, wanafikiria vipi, halafu jifunze tabia za watoto katika kila umri ili uweze kupata mbinu za kuwasaidia.

Kwa hiyo, sasa ukishafanya hivyo ina maana wakati shule inafunguliwa, kwa maana sasa hivi viboko vimeshakuwa ndiyo tamaduni sasa hivi, tunakuja sasa na mpango wa kuviondoa.

Tuanze kufanya tafiti, tatizo sisi huwa hatufanyi tafiti, hebu tufanye shule ya mfano hata waandishi wa habari ambao wanaandika hizi habari pamoja na Serikali ambayo inaweka katazo la viboko na wazazi ambao bado mtazamo wao haukubaliani na viboko tufanye kwa pamoja, tufanye utafiti kwenye shule ambazo za awali yale madarasa ya awali.

Kuwepo na ushirikiano kati ya walimu na wazazi, tukubaliane kwamba malengo ya watoto wetu katika ukuaji wanapofikia miaka 20 ni watu wazima wawe na tabia za aina gani na tunataka hizi tabia zitokee bila ya kutumia fimbo.

Sasa utafiti unaanzaje? Mnaanzia pale wanapoanza darasa la awali, mzazi ana mpango gani, mwalimu ana mpango gani, wote tunaweka mkakati wa kumthamini mtoto kama mtu, kuthamini utu wa mtoto, halafu tunaamua hatutumii fimbo halafu tunakuja na njia mbadala ambazo tunaweza kutumia nyumbani na shuleni zikaenda sambamba.

Ufuatiliaji wa watoto shuleni ukawa wa karibu sana kwa wazazi kwa maana wazazi wengine mtoto akiwa mkorofi wanampeleka akashinde shuleni na mwalimu pale shuleni ana watoto wengi sana wa kushughulika nao na unakuta wengine labda wana hizo-, bado wapo katika ile hali ya utoto ya kujifunza, ndipo hapo makosa yanapotokea.

Wengi wetu tunajua watoto ni wakorofi, ni watukutu lakini kikubwa ni kwamba watoto wale wapo katika umri wa kujifunza, ndiyo maana unakuta wanakosea sana na wanapigwa mara kwa mara kwa makosa yaleyale.

Kwa hiyo, tukija na mbinu ya pamoja kwamba ngoja tupime hili darasa sasa hivi tunaandikisha watoto wa chekechea mwaka huu, ngoja tuwe na mikakati ya pamoja sisi kama familia pamoja na shule halafu tuone namna gani wanakwenda.

Kwa sababu tafiti zilizofanywa – kwa watu ambao wameamua kufanya tafiti za viboko – mara nyingi zinamuondoa hasira yule mtu ambaye anapiga, yaani ndiyo suluhisho kwa sababu wewe una mamlaka hata katika kupigana kwa kawaida, kwa watu wazima, hakuna mtu mzima anayempiga mwingine aliyemshinda nguvu, aliyemshinda mamlaka.

Kwa hiyo, wewe unakuwa na maamuzi ya kumpiga mtoto kwa sababu unajua muda wowote unavyotaka kumpiga unao uwezo wa kufanya hivyo na yeye hana uwezo wa kukataa kupigwa.

The Chanzo: Viboko vina athari gani vinapotumika kama adhabu kwa mtoto?

Fatuma Kamramba: Kwa hiyo, sasa tafiti zinaonyesha kwanza fimbo zinaleta matokeo ya muda mfupi ambayo sisi tunayataka. Kwa mfano, umekuta mtoto amefungua friji, amepanda mule, tuseme wa miaka minne, mitatu, cha kwanza kama mzazi wa Kiafrika utakachokifanya ni kumnyanyua kule kwenye friji na kumtatindika vibao au kutumia fimbo au kandambili, chochote kile.

Lakini kiukweli kwenye ubongo wa mtoto kitakachoendelea kwa wakati huo atakua surprised, yaani atapata mshtuko kwa sababu yeye pale alipo kwenye kichwa chake hajui kama anafanya kosa.

Yaani yeye anafanya tu kile ambacho akili yake imemtuma kama mtoto – fungua friji, fuata yale matunda au yogurt ama kitu gani, anaingia mpaka ndani ya friji. Sasa wewe ukimkurupusha kule na kumtwanga fimbo ina maana pale kuna namna unazisumbua neuroni zake, unamjengea woga.

Kwa hiyo, siku nyingine ndiyo utakuta watoto mara nyingi wanaopigwa, ukiacha kuondoa hasira kwa mpigaji, lakini pia zinatengeneza tabia za uongo. Watoto wengi wanaopigwa njia yao mbadala wa kuepuka fimbo ni uongo.

Na unamtengenezea anakuwa na ile akili ya kuhakikisha ataepuka fimbo kwa namna yoyote ile. Hata ukienda kutuhoji watu wazima kama sisi yale makosa ambayo tulikuwa tukiyafanya utotoni ni namna gani tulikuwa tunaepuka tusipigwe mara nyingi ni kufanyaje? Kuongopa. Na mtoto akiamua kuongopa si rahisi wewe kugundua kama anasema uongo.

Kwa hiyo, kwa nini msimamo wangu mimi kwenye fimbo ni kuzikataa ni kwa sababu, kama mtaalamu, kama mlezi, ambaye nimeweza kulea watoto kwa kutumia mbinu mbadala, nikimaanisha mbinu mbadala wa fimbo, nimeona kwamba fimbo inatengeneza nidhamu ya kufikiria, yaani nidhamu ambayo mtoto anajua kwamba yaani anapokuwa anatenda kosa kwanza unatakiwa umeleweshe kwamba hili ni kosa toka yupo mdogo.

Kwa hiyo, adhabu mbadala zinatibu tatizo kwa sababu zinampa muda mtoto wa kufikiri, wa kujua kwamba nimetenda kosa, nimepewa adhabu fulani, au mama au baba amefanya kitu fulani ambacho kimemuumiza na kumpa muda wa kufikiria.

lakini fimbo ukimtandika ni ghafla ghafla umeshamvamia, umemtandika, maumivu yanaisha wewe umefurahi umetoa adhabu kama mtoto mamlaka yako umeyatimiza. Mtoto kesho yake atakudanganya lakini hatapata muda wa kufikiria ile adhabu.

Kwa hiyo, mimi nafikiri, kama wazazi, kama jamii, tuwekeze kwanza kwenye utafiti tuanze na watoto wadogo na tuelewe hasa kama jamii, kama Serikali, tuanze kufundisha elimu ya makuzi na maendeleo ya mtoto, sayansi ya makuzi na maendeleo ya mtoto.

Ili watu waweze kuamini vitu kwa ushahidi kwa sababu mimi nafanya kazi na wazazi na walimu, wengi wao wanaamini mtoto wa Kiafrika hawezi kukua bila ya fimbo.

Wakati ubongo unatengenezwa hakuna tofauti ya ubongo wa mtoto wa Kizungu wala mtoto wa Kiafrika. Bongo zinavyotengenezwa za binadamu ni vilevile ila misingi uliyojiwekea ya malezi ndiyo itakusaidia wewe usitumie fimbo na mwanao awe sasa kama yule ambao unahisi wa Mzungu analelewa bila ya fimbo.

Watoto wote wanaweza wakalelewa bila ya fimbo. Mimi naongea kama mtoto niliyelelewa kwa fimbo lakini uongo nimefanya sana. Lakini nikiangalia watoto niliowalea bila ya fimbo baada ya kuongeza taaluma ya namna gani watoto wanatakiwa kulelewa ubongo wao unakuwaje, wanapokeaje adhabu zinawajengea misingi gani na tabia gani nikaona kabisa kwamba inawezekana tukalea bila ya fimbo.

Ndiyo maana unakuta kwa sababu ya fimbo mtoto anajenga woga lakini kadri anvyokuwa mtu mzima anakuwa ni mtu mzima ambaye siyo mwaminifu, ambaye hawezi kujituma kwa hiari yake.

Mwingine kama unavyoona maofisini anasubiri bosi amwambie jambo hata kama anaona anaweza kufanya, au mtu anawahi kazini kwa sababu bosi wake atamgombeza, siyo kwa sababu yeye anataka kuchapa kazi na kuweka mchango wake kwenye maendeleo ya hili taifa.

Lakini pia tunapata watu ambao kazi yao ni kusema tu “ndiyo” katika kila jambo, hata kama ana maoni yake anaogopa kuyatoa kwa sababu toka mdogo anahisi kuna mamlaka juu yake.

Kwa hiyo, kwenye mamlaka tukijengeana heshima ya majadiliano, unamlea mtoto kwa majadiliano, unamueleza kwamba wewe ni, pia pengine tusisahau hata suala la dini tunavyowalea watoto wetu tuwalee kwa misingi ya dini.

Kwa hiyo, unamwambia wewe ni mtoto wa Kikristo, wewe ni mtoto wa Kiislam, hatupaswi kufanya jambo hili, haupaswi kufanya jambo lile. Lakini umemkuta amepanda kwenye friji, unamtoa, unacheka naye lakini unamwambia hatupaswi kupanda kwenye friji, muelezee kwa nini hatakiwi kupanda kwenye friji, yaani tujenge mawasiliano, majadiliano.

Wengi wetu tunahisi kwamba watoto hawana uwezo wa kuelewa mambo. Lakini kiukweli, watoto wanaelewa, kisayansi, wanaelewa kuliko hata watu wazima kwa sababu wana huo muda wa kuweka kitu ambacho unawaambia kichwani kwa muda mrefu kwa sababu wao hawawazi wakati ujao, hawawazi wakati uliopita, wanachokiwaza ni sasa hii, yaani wakati uliopo tu.

Kwa hiyo, tukiwekeza kwenye wakati huu itasaidia kuweza kuondoa hizi adhabu za viboko.

Na tuanze hasa mtoto akiwa mdogo, mazungumzo ya mtoto yanaanza mtoto akiwa tumboni. Kwa hiyo, sayansi ya makuzi na maendeleo ya mtoto inasema tabia unayoitaka kuijenga kwa mtoto ijenge kuanzia umri wa sifuri mpaka miaka tisa.

Wataalamu wa makuzi na malezi tunakiita kipindi cha usajili, dirisha la usajili limefunguliwa pale ikishafika miaka tisa. Miaka tisa ikifunga pale ina maana kurekebisha tabia ya mtoto inakuwa ngumu kwa sababu ameshakuwa na hisia za kujitegemea.

Kwa hiyo, ndiyo pale uongo utakuwa mwingi, makosa yatakuwa mengi, kwa sababu anazidisha utundu.

Kwa hiyo, katika hicho kipindi tujifunze kuzungumza na watoto kuwatengenezea misingi. Lakini pia sisi watu wazima tujue kwamba ndiyo maana vitu ambavyo ni vya kuharibika, au ni vya hatari, mara nyingi vinakuwaga vimeandikwa weka mbali na watoto.

Kwa hiyo, kwa sababu makosa mengine tunayowapigia watoto hasa wadogo siyo makosa yao. Kwa mfano, wewe umeacha simu yako hapo na kuna ndoo ya maji, lazima mtoto ataweka kwenye ndoo ya maji.

Umeacha dawa mtoto atameza kwa sababu anaona watu wanakula dawa, hajui mantiki ya zile dawa. Umeacha vitu hovyo hovyo mtoto atavuruga. Umeacha kompyuta yako, umeacha nini, atavuruga tu.

Kwa hiyo, kumpiga hakutokusaidia zaidi utamharibu ubongo wake, utakuwa hauwezi kujifunza mambo mazuri.

Watoto ambao ni wadogo hawajaweza kung’amua mambo, hasa kuanzia miaka mitatu na nusu kushuka chini, tujaribu kuwaepusha mazingira ya kufanya makosa kwa sababu sidhani mtoto wa miaka mitatu na nusu kama hata anafanya makosa, lakini wanapigwa na makosa yao ni kama ya kumwaga vitu, kuungua, sijui kamwagia maji labda hivi vyombo vya umeme ambavyo tunakaa navyo watu wazima.

The Chanzo: Kwa hiyo, ukiachana na viboko ni adhabu gani mbadala zinaweza kutumika?

Fatuma Kamramba: Lakini wale ambao wameanza kufanya mazungumzo na kuelewa mambo wale, unampa adhabu mbadala ambayo, kwa mfano, mtoto anapenda kuangalia katuni, mnakubaliana kwamba hautoangalia katuni kwa sababu moja, mbili, tatu.

Kwa mfano, unakuta mtoto kuna watoto wanapenda labda umejenga nyumba yako unakuta kachafua ukuta, au kachana madirisha, labda yale ya nyavu au kavunja vitu.

Mtoto kama yule, kwa mfano, ulikuwa akienda shule unampakia sijui soseji, sijui vitu gani, unampa labda Sh1,000, hebu kaa naye chini mwambie kwa sababu umechafua ukuta na huu ukuta ni gharama, natakiwa nipake tena rangi, inabidi tupunguze pesa yako ya shule kwa muda fulani, inabidi tupunguze kama tulikuwa tunaweka mkate na soseji tukuwekee mkate peke yake.

Kwa hiyo, ile kitu inamfanya mtoto aanze kufikiria kwamba nilifanya kosa na nimepewa adhabu sawa.

Lakini haya makosa mengine unajaribu kufanya mazungumzo. Muondoe mtoto katika kitu anachokipenda kama, kwa mfano, anapenda kucheza na wenzake baada ya muda wa shule, akitenda kosa, hebu muondolee ile ratiba ya kucheza.

Yaani, fanya kumnyima vile vitu anavyovipenda ili aweze kupata muda wa kujua kwamba mimi kuna kosa nimefanya.

Wote tunajua mapenzi watoto waliyonayo kwenye kuangalia runinga. Sasa umwambie kwamba kila ukitoka shule, ukimaliza kula, unaenda chumbani hapa sebuleni kukaa kuangalia runinga, utangalia baada ya wiki mbili au wiki moja.

Kwa hiyo, yule mtoto, kwa namna ambavyo anapenda ile runinga, hatoweza kufanya hivyo.

Labda mtoto yuko shule anashiriki kwenye timu ya mpira, au kwenye timu za michezo, au muda wa kutoka nje kucheza, unamwambia wewe kwa sababu nimekupa kazi ya nyumbani hukufanya, hautaenda kucheza na wenzako.

Fanya hivyo kwa siku tatu uone mtoto hawezi kurudia kosa kwa sababu inamfikirisha, anakaa pale anaona wenzake wanacheza yeye hajatoka tofauti na ukimpiga. Ukimpiga yeye anaishia pale, kesho anaendelea kufanya mambo mengine, anarudia kosa lile lile.

Kwa sababu ukiangalia sasa hivi watoto wadogo asipofanya homework anakuwa muoga sana ni kwa sababu shuleni anatandikwa asipofanya homework.

Lakini ili umuepushe na fimbo mzazi kuwa na muda wa kufuatilia homework za mtoto. Kwa nini mtoto arudi shuleni hajafanya homework na wewe mzazi upo? Kwa hiyo, muepushe na zile adhabu ili asiweze kupata zile adhabu lakini pia jaribu kumuondolea vitu ambavyo anavipenda.

Kwa hiyo, niseme wote tuwekeze lakini wenye uwezo tuweke kwenye utafiti tuache kuzungumza na maneno. Mimi binafsi nimeshafanya utafiti, uzoefu wa nyumbani kabisa wa kulea watoto bila ya fimbo.

Hebu tujaribu kuona tunawezaje kuwekeza kwa wale watoto wadogo kufanya utafiti ambao una matokeo kwa sababu wenzetu tayari wameshafanya tafiti na tafiti zinafanya kazi. Naweza kusema hayo.

Hadija Said amefanya mahojiano haya, kuyasimamia na kuyabadilisha kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno. Kwa mrejesho, wasiliana nasi kupitia: editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Huyu Bidada analeta Mambo ya Wazungu Nchini na anasahau kuwa hili Taifa liweze kupona lazima tupambane na maadui wakuu watatu, UJINGA, MARADHI NA MALAZI sasa huu Ujinga hautolewi kwa negotition, Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, Hata kwa sisi wakristo Biblia inasema kuwa usimnyime mtoto mapigo kwa maana hayatamtoa Roho…

    Tena Fimbo imezungumzwa kwenye Biblia Takatifu Ya MUNGU, Mimi ni Mwalimu toka Nianze Kutumia Fimbo kama Baba Nyumbani kwangu lakini Fimbo Shuleni, Watoto wamekuwa na Maendeleo Chanya, Yaani Mjengeo Faida, Na baada ya Masomo Watoto huja kunishukuru kwa kuwafunza tabia njema na kuwasaidia ktk Masomo yao, Huwezi kumwadhibu mtoto kwa kumuonea, Adhabu zinatolewa kwa kufuata sheria lakini ukizingatia Afya, Umri na aina ya Kosa….

    Tukiacha hawa watoto hivi kuna siku tutakuja kugundua tayari Taifa Limeshakwisha ingia mtaroni….

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *