The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Nakuwa Baba Kamili’: Wanaosindikiza Wake Zao Kliniki Waeleza Uzoefu Wao

Utamaduni huo unahusishwa na kujengeka kwa mahusiano mazuri kati ya baba na mtoto atakayezaliwa.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Hapa katika kliniki ya watoto ya the Aga Khan Polyclinic, unaweza kuona akina mama wengi wamepanga foleni wakiwa na watoto wao, wakisubiri zamu zao zifike kwenda kumuona mtoa huduma. Wengi wao hawajaambatana na baba watoto zao kwani wanaume hapa ni wachache sana.

Miongoni mwa hao wanaume wachache, hata hivyo, ni Godwin Banzi, baba wa mtoto mmoja ambaye leo ameongozana na mke wake kumleta mtoto wao kliniki ili kuangalia afya na ukuaji wake. Banzi anaonekana ni baba anayejivunia, akionekana mzoefu kwenye eneo hilo la kliniki asubuhi hiyo ya Mei 24, 2023.

The Chanzo inaamua kumfuata Banzi baada ya kutoka kumuona mtoa huduma, ikitaka kujua ni nini kinamshawishi kuwa tofauti na wanaume wengine kwenye eneo hilo la kusindikiza mama watoto kliniki. The Chanzo inagundua kwamba siyo mtoto tu kwani Banzi alikuwa pia anamsindikiza mke wake kliniki wakati wa ujauzito wake.

“Unajifunza vitu vingi,” Banzi, 29, aliiambia The Chanzo kuhusu kumsindikiza mke na mtoto wake kliniki. “Na kitu kingine, ni vyema kufanya hivyo, ni njia ya kutengeneza familia bora. Pia, napata uzoefu wa kutosha juu ya afya na makuzi ya mtoto.”

SOMA ZAIDI: Ukosefu wa Vituo vya Upataji Nafuu Waacha Waraibu wa Dawa za Kulevya Njia Panda Mtwara

Lakini Banzi, fundi bomba, anawezaje kutenga muda wa kufanya hivyo na wakati huo huo akaweza kuendelea na shughuli zake za kujipatia kipato? The Chanzo ilitaka kujuwa, iikizingatiwa kwamba hii ni moja wapo ya sababu kubwa zinazotajwa na wanaume kutokuhudhuria kliniki.

“Hiki ni kitu cha muda; ninaweza nikapanga siku fulani napeleka mtoto kliniki na ikawa hivyo,” alisema Banzi, kijana mweusi na mwenye urefu wa makamo. “Kwa upande wangu, ningewashauri wanaume wenzangu wawe na tabia ya kuwasindikiza wake zao kliniki.”

Wanaume wachache

Banzi ni moja kati ya wanaume wachache sana nchini Tanzania waliojenga utamaduni na mazoea ya kuwasindikiza wenza wao kliniki. Ingawaje hakuna taarifa rasmi, maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Afya waliiambia The Chanzo kwamba muamko bado ni mdogo sana miongoni mwa wanaume linapokuja suala hilo husika.

Changamoto hii ni kubwa sana na inayowachanganya maafisa afya nchini, hali iliyoipelekea Serikali kuandaa mpango maalumu wa kubadilisha hali ya mambo uliopewa jina la Mwongozo wa Kitaifa wa Ushiriki na Ushirikishwaji wa Wanaume Kwenye Masuala ya Afya ya Uzazi.

Gerald Kihwele, Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi kwa Vijana na Jinsia kutoka Wizara ya Afya, aliiambia The Chanzo hivi karibuni kwamba kutokana na hali ilivyo, wamelazimika kuutumia Mwongozo huo, ambao mchakato wake wa kuutengenezwa ulianza 2021, bila ya hata kukamilika.

SOMA ZAIDI: Unavyoweza Kusababisha Kuenea kwa VVU Licha ya Kutokuwa Mwathirika

“Tulitengeneza mwongozo baada ya sisi kama Serikali kuona umuhimu wa wanaume kushiriki,” Kihwele alisema kwenye mahojiano hayo. “Mwongozo upo katika hatua za mwisho japo utekelezaji wake umeanza hata kabla haujafikia mwisho.Tunatarajia kuwa ikifika Julai mwaka huu [wa 2023] uwe umeshakamilika.”

Wataalamu wanashauri wanaume wahudhurie kliniki ili waweze kupata elimu ya afya ya uzazi pamoja na malezi ya mimba hadi kujifungua, wakisema endapo kama wanaume watapata elimu hiyo itasaidia kupunguza vifo vitokananvyo na uzazi. Pia, utamaduni huo unahusishwa na kujengeka kwa mahusiano mazuri kati ya baba na mtoto atakayezaliwa.

Licha ya uwepo wa faida hizi, na licha ya kuthibitika kwamba wanaume wengi wanazielewa faida hizo, bado wanaume wengi nchini wanaripotiwa kuwa na mwamko hafifu wa kusindikiza wenza wao kliniki. Hata hivyo, siyo wanaume wote wenye tabia hiyo.

Baba kamili

Ronald Sonyo ni baba wa watoto wawili ambaye amekuwa na utamaduni wa kumsindikiza mke wake kliniki kila mara inapotokea haja ya kufanya hivyo. Sonyo, 32, aliiambia The Chanzo kwamba kitendo hicho kinamfanya ajihisi kuwa baba kamili mwenye kutimiza wajibu wake.

“Kumsindikiza mke wangu kunaleta faida nyingi,” Sonyo, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, alisema. “Nitakuwa najua nimeongezewa uzito wa majukumu yangu kama baba. Nitakuwa najua mke wangu anatakiwa kujifungua wakati gani ili nianze kujiandaa. Nitajua vitu gani hatotakiwa kufanya katika kipindi cha ujauzito.”

SOMA ZAIDI: Mtaalamu Aeleza Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Saratani ya Shingo ya Kizazi

Salim Abdallah, mzazi mwengine aliyejenga tabia ya kumsindikiza mke wake kliniki, alikikataa kisingizio cha wanaume wengi kutokufanya hivyo wakidai hawana muda kwani hutumia muda wao mwingi kutafuta pesa kulisha familia, akisema kutenga masaa machache ya kwenda kliniki hayawezi kuathiri kipato cha mtu.

“Kwanza kipato ni masuala ya Mwenyezi Mungu,” Abdallah, baba wa watoto wanne, alisema. “Kwa hiyo, nikienda na mke wangu [kliniki] pia Mwenyezi Mungu anajua riziki yangu ipo sehemu gani. Nampeleka, anapata huduma, baada ya hapo nampeleka nyumbani, naendelea na shughuli zangu.”

Lakini kuna utayari pia, hoja ambayo Juma Ibabe, baba wa watoto watatu anayemsindikiza mke wake kliniki, anaamini ndiyo huamua mwanaume afanye hivyo au asifanye. Kwa mujibu wa Ibabe, 38, kama utayari haupo, mwanaume anaweza kubuni kila aina ya kisingizio kitakachomzuia asimsindikize mke wake kliniki.

Kipaumbele

Hata hivyo, suala la uhudhuriaji wa kliniki kuingiliana na shughuli za wanaume kujipatia kipato linaonekana kuthibitika kuchangia kwa kiwango kikubwa wanaume kutokuwa na utamaduni wa kuhudhuria kliniki, na afua kadhaa zinachukuliwa kutatua changamoto hiyo.

SOMA ZAIDI: Walazimika Kujifungulia Nyumbani Baada ya Kituo cha Afya Kukosa Wahudumu

Dk Paulo John ni Mratibu wa Huduma ya Mama na Mtoto wa Kanda ya Kati ambaye aliiambia The Chanzo hivi karibuni kwamba ni muhimu sana kwa vituo vya kutolea huduma kuwapa kipaumbele akina mama wanaosindikizwa na waume zao, akisema hatua hiyo itachangia kurekebisha hali ilivyo hivi sasa.

“Kwa nchi zetu ni kwamba ukimuambia baba aje hospitali, hakikisha hakai muda mrefu,” Dk John anasema. “Hiyo ndiyo changamoto ambayo wanaume wengi wanapata, na haya mambo yanawezekana. [Mwanaume] anapewa ratiba kwamba wewe utakuja saa tano. Saa tano anakuja, ndiyo muda wao. Wamekuja, wanapimwa, wanaondoka.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackine@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *