Dodoma. Wadau wa afya ya mtoto wamebainisha mbinu kadhaa ambazo wazazi ambao watoto wao wanapata tumbo la chango wanaweza kufanya ili watoto hao warudi katika uchangamfu na afya imara.
Wadau hao wameeleza mbinu hizo wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyofanyika hivi karibuni kuhusiana na tatizo hilo ambalo wazazi wengi, hususan wale wanaonyonyesha, wameripoti kukabiliana nalo, huku wengi wakiwa wanauliza namna bora za kukabiliana na hali hiyo.
Kwa mujibu wa wataalamu, watoto wachanga husumbuliwa na chango, au colic kwa kimombo, wanapokuwa na umri wa wiki mbili baada ya kuzaliwa. Chango ni maumivu makali ya tumbo anayopata mtoto na kulia mara kwa mara ikiwa usiku, mchana au jioni.
Wataalamu wanasema mtoto anaweza kulia zaidi ya masaa matatu kwa siku, hali inayoweza kuathiri ustawi wa mtoto husika. Wataalamu wanabainisha kwamba aghlabu chango huchukua muda wa miezi mitatu kupona.
“Tatizo hili mara nyingi husababishwa na hewa kujaa tumboni na huwapata watoto walio chini ya umri wa miezi mitatu ambao bado hawajaanza kukaa,” alisema Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya Elieth Rumanyika wakati wa mahojiano hayo na The Chanzo.
“Inaweza kusababishwa na namna mama anavyomuweka mtoto kwenye titi wakati wa kunyonyesha,” aliongeza Rumanyika.
SOMA ZAIDI: Zaidi ya Watoto 1,000 Dodoma Wana Uzito wa Ujifunzaji Shuleni
Rumanyika anasema kuna uwekaji wa mtoto wakati wa kunyonyesha ambao hupelekea mtoto kuvuta hewa kwa wingi na hivyo kupelekea kuwa na tatizo hilo la tumbo la chango.
Hapa, Rumanyika anafafanua zaidi: “Hewa inapoingia tumboni inamsababishia mtoto kujisikia vibaya na hivyo kumfanya alie. Mtoto akiwekwa vizuri, na akasaidiwa, hiyo hewa itatoka.”
Sophia Selemani ni Mkurugenzi wa Save Community Healthy Initiative (SACOHEI), shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na afya ya mtoto, ambaye anabainisha namna nzuri ya unyonyeshaji huepusha kumsababishia mtoto tatizo la chango.
“Mwisho wa siku kama mama hajui jinsi ya kumcheulisha mtoto, kumuweka begani, kumfanyia masaji ili azidi kubeua, [kwamba] akimaliza kunyonyesha anamlaza hapo, anamyonyesha mara mbili, mara tatu, tumbo la mtoto unakuta limejaa ndii, yaani ukilipiga piga hivi linalia kama ngoma,” alisema Selemani.
“Kuna njia tofauti tofauti za kupunguza hiyo gesi,” aliendelea kueleza Selemani ambaye amekuwa akishauri wazazi namna bora za unyonyeshaji.
“Kuna ile ya kumuweka begani, kuwaweka kwenye bega la mama na kumsugua sugua, yaani kama anamfanyia masaji tumboni ili aweze kubeua. Kwa hiyo, kupitia hiyo njia mtoto anakuwa anapunguza gesi tumboni,” alifafanua.
SOMA ZAIDI: Ofisi ya Mufti Zanzibar: Vitendo vya Udhalilishaji Watoto Vinahuzunisha
Lakini kuna nyingine mama anaweza akamlaza mtoto halafu akamfanyia masaji pale tumboni kwa mafuta, kwa kutumia mafuta ya nazi, kwa mujibu wa Selemani.
“Baada ya kumlaza, unamfanyia mtoto kama zoezi la kuendesha baiskeli, anamzungusha ile miguu kama anaendesha baiskeli,” alisema. “Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo, mtoto anapumua. Kwa hiyo, kuna njia hizi ambazo ni rahisi kuzifanya na akamsadia mtoto.”
Baadhi ya wazazi ambao The Chanzo imezungumza nao wamelalamikia kutokupewa elimu ya kutosha wanapokwenda kliniki kabla na baada ya kujifungua, na hivyo kushauri elimu zaidi itolewe kwa akina mama kuepusha matatizo kama hayo kwa watoto.
“Mimi sijawahi kupata elimu kuhusu unyonyeshaji,” alisema Joyce Kasiki, mama mwenye mtoto wa miaka mitatu. “Kuanza kwenda kliniki kumpleka mtoto sijapata elimu kuhusu lishe. Hawatoi elimu yoyote, ni porojo tu.”
SOMA ZAIDI: Wanawake Wanaolea Watoto Peke Yao Waelezea Uzoefu Wao
Naye Bahati Msanjila, mama mwenye mtoto wa miaka miwili na miezi saba, anasema: “Unapokwenda kwenye kituo cha afya upate ushauri, yaani wanakuhudumia kama unasubiria mvua, kama vile umeenda kujificha mvua ili ikiisha uondoke.”
Selemani anakiri kuwepo kwa tatizo hili, akilihusisha na uhaba wa watumishi kwenye sehemu nyingi za kutolea huduma nchini.
“Nadhani ni eneo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi,” alipendekeza Selemani. “Ni muhimu kwamba watu wote wanapata elimu ya unyonyeshaji mzuri kwa ajili ya afya ya akina mama na watoto wao pia.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dodoma. Anapatikana kupitia jackline@thechanzo.com.
4 Responses
What are the symptoms and how could a baby react
Mimi mtoto wangu anasumbuliwa n chango ndo mimba ya kwanza lakini nilivo anza klinic sikuwahi kupewa mafunzo yoyote yale
Habari daktari naomba kujua ,eti mtoto akishapata tatizo ilo kunadawa maalum ya kutibu moja kwa moja
Mtoto wangu anasumbuliwa na tumbo