Zaidi ya Watoto 1,000 Dodoma Wana Uzito wa Ujifunzaji Shuleni

Uzito wa ujifunzaji ni ile hali inayomkabili mtoto na kumsababishia ugumu fulani kwenye kusoma, kuandika au kuhesabu.

subscribe to our newsletter!

Dodoma: Halmashauri ya Jiji la Dodoma imebaini uwepo wa watoto wenye uzito wa ujifunzaji shuleni zaidi ya 1,400, kwa mujibu wa Afisa Elimu Maalum wa Jiji la Dodoma na Mwenyekiti wa Maafisa Elimu Maalum Tanzania Bara, Issa Omary Kambi.

Kambi alitoa tathmini hiyo alipokuwa akiongea na The Chanzo mara baada ya kutoa mafunzo kwa walimu wa Shule ya Msingi Bahi Sokoni, wilayani Bahi. Mafunzo hayo yalilenga kuwapatia walimu mbinu bora za kuwafundisha watoto hao.

Kambi alibainisha kwamba kundi la watoto wenye uzito wa ujifunzaji shuleni limekuwa likiachwa nyuma kutokana na watu wengi kukosa uelewa wa namna ya kulisaidia, huku akitaja walimu kama mawakala muhimu wa kubadilisha hali hiyo.

“Namna ya kujua watoto wenye matatizo haya ni pamoja na kufuatilia historia zao,” Kambi alisema pembezoni mwa mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni.

“Baada ya kuona darasani hayuko vizuri ni vizuri kujiridhisha kupitia historia zao [kwa] kumuita mzazi na kumshirikisha,” anaongeza. “Wakati mwingine jamii inayomzunguka pia kuangalia makuzi yake yalikuwaje. Lakini ni rahisi kwa walimu kwa sababu wamekaa nao kwa muda. Kwa hiyo, wanajua mtoto huyu ni mzito, huyu ni mwepesi katika kujifunza.”

Kambi anashauri wazazi kwamba wakigundua watoto wao wanaonesha dalili za uzito wa kujifunza wanapaswa kuongeza upendo kwao, akisema moja kati ya tatizo sugu ambao wao kama wataalamu wameligundua ni wazazi kuwanyima watoto hao upendo wanaostahiki.

Kwa mujibu wa wataalamu, uzito wa ujifunzaji ni ile hali inayomkabili mtoto na kumsababishia ugumu fulani kwenye kusoma, kuandika au kuhesabu. Wataalamu wanaeleza kwamba hali hii haisababishwi na upungufu wa akili au motisha ya kusoma kwa mtoto. Bali, hali hiyo hutokana na ubongo wa mtoto husika kuwa tofauti na bongo za watoto wengine.

Watoto, na hata watu wazima wenye uzito wa ujifunzaji, huona, husikia na huelewa vitu kwa namna tofauti, hali ambayo inaweza kuwaletea shida kwenye kujifunza taarifa na ujuzi mpya na kuzitumia taarifa na ujuzi huo kwenye maisha yao ya kila siku.

Wataalamu wanabainisha kwamba hali hii inaweza kubadilika endapo kama kutakuwa na miundombinu rafiki ya kuwawezesha watoto hawa kujifunza.

“Kikawaida tunaposoma, tunasoma kwenye vyuo vya ualimu vya kawaida,” anasema Sara Chizeva, Afisa Elimu Maalum wilayani Bahi. “Kuna kitengo ambacho kinaitwa Kitengo cha Elimu Maalum [ambako] walimu wanakwenda kusomea hiyo elimu maalumu. Lakini [hivuo vitengo] tunavyo vichache sana.”

Sara anasema kwamba wilayani Bahi, kwa mfano, tatizo la kusahaulika kwa watoto wenye uzito wa ujifunzaji ni kubwa sana, ambapo walimu wengi hukimbia kumaliza mada bila ya kuzingatia maslahi ya kundi hilo la watoto.

John Josephat ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Bahi Sokoni ambaye anakiri kuwepo kwa watoto wa aina hiyo shuleni kwake na kubainisha kwamba baadhi yao wamekuwa wakiacha shule, wakisema shule imewashinda.

“Lakini hili tatizo, baada ya kupatiwa haya mafunzo, tumebaini kwamba tutatumia mbinu tulizopewa kwa ajili ya kuwasaidia wale watoto ambao ni wazito katika kuelewa,” anasema Josephat. “[Hii ni muhimu] ili wafanye vizuri [na] wasikimbie shule. Kwa sababu, imekuwa unaanza na watoto 200 lakini wanaomaliza unakuja kukuta labda ni watoto 160.”

Mratibu wa Mradi wa Elimu Jumuishi unaotekelezwa na Kanisa la FPCT ambao umelenga kutatua changamoto za uzito wa ujifunzaji miongoni mwa watoto, Janey Mgidange, anasema kwamba lengo la kutoa mafunzo hayo kwa walimu ni kuwajengea uwezo walimu ili kuwasaidia wanafunzi hao.

“Sisi tukaona kwamba kuna haja ya walimu kuelewa kwamba kuna hili kundi la watoto wenye mahitaji maalumu ambao wana uzito wa ujifunzaji shuleni,” anasema Janey. “Kwa hiyo, ndiyo maana tukaamua kuwapitisha walimu wazifahamu aina za watoto hawa. Dalili ni zipi na namna ya kuzitatua hizo changamoto wanazozipitia.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts