The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ofisi ya Mufti Zanzibar: Vitendo vya Udhalilishaji Watoto Vinahuzunisha

Ofisi hiyo inahusisha vitendo hivyo na ushawishi wa shetani na watu kukosa hofu ya Mungu.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Zanzibar inaweza kuwa inajulikana kwa vivutio vyake vingi vya utalii na harakati za kisiasa. Lakini kama kuna kitu kingine ambacho Zanzibar inajulikana basi ni kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto.

Unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto unatajwa kuwa ni jambo la kila siku visiwani hapa, huku asilimia 14 ya wanawake wakiripotiwa kukumbana na vitendo hivi.

Matukio ya udhalilishaji Zanzibar ni maarufu sana kiasi ya kwamba Rais wa nchi hiyo Dk Hussein Mwinyi ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali yake za kupambana na matukio hayo.

Kwa kuzingatia ukweli kwamba Zanzibar ni jamii ya kidini, ikiwa na waumini wengi wa dini ya Kiislamu, The Chanzo ilitamani kufahamu mtazamo wa Kiislamu kuhusiana na vitendo hivi na juhudi gani taasisi za kidini visiwani humo zinachukua kukabiliana na janga hilo.

Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ni taasisi rasmi ya Serikali ya Zanzibar iliyoanzishwa mwaka 1992, na baadaye kuanzishwa upya kwa sheria mwaka 2001, ambayo kazi yake kuu, pamoja na mambo mengine, ni kutolea ufafanuzi masuala kadhaa ya Kiislamu yanayojitokeza katika jamii.

Katika mahojiano haya maalum, The Chanzo inazungumza na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Othman Muhammed Saleh ili kuweza kupata mtazamo wa ofisi hiyo kuhusiana na matukio ya udhalilishaji visiwani hapa na hatua inazochukua kukomesha matukio hayo.

Na hapa Saleh anaanza kwa kutueleza kile Uislamu unasema kuhusiana na suala zima la ukatili wa kijinsia na udhalilishaji wa watoto. Endelea …

Othman Muhammed Saleh: Ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto ni muamala, au matendo yaliyokuwa mazuri, [matendo] yaliyokuwa na upendo au mapenzi kwa watoto. Ni matendo ambayo yanahusiana kwanza kutokupewa haki zao za msingi, ikiwemo ya elimu, matibabu, lugha nzuri za kuwapenda watoto na ikawa kinyume chake kuwatukana, kuwabagua, [na] kuwapiga.

Na njia yoyote ambayo watoto, kama walivyo watu wengine, wanahitaji kuenziwa zaidi, kupewa moyo zaidi, kuwekwa katika mstari nzuri kwa sababu wao ndiyo vijana wa kesho na ndiyo viongozi wa kesho.

Lazima tuwatayarishe katika matayarisho mazuri. Ikiwa hatukuwatayarisha, tumewanyima kila haki yao ya msingi, tumewanyanyasa, ikiwemo unyanyasaji wa kimwili, unyanyasaji wa kijinsia, unyanyasaji wa kuwaingiza katika biashara wakati umri mdogo, kufanya hivyo, tunahesabu ni katika miongoni mwa mambo ya unyanyasaji.

The Chanzo: Zanzibar inasemekana kuwa na idadi kubwa ya Waislamu lakini inaripotiwa kuwa na vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia, hususani kwa watoto na kujumuisha mambo kama, ulawiti, na vitendo vyengine. Wewe kama Mkurugenzi kwenye Ofisi hii ya Mufti inakushtua kwa kiwango fulani?

Othman Muhammed Saleh: Tunayo idadi kubwa ya Waislamu. Asilimia 99 [ya] Waislamu walioko Zanzibar na asilimia 1 ni dini nyenginezo. Lakini Uislamu ni kuwa na imani kwanza halafu kutekeleza. Vitu vyote viwili lazima viambatane. Udhalilishaji wa kijinsia ni suala ambalo lipo dunia nzima.

Lipo katika Bara la Ulaya, lipo katika Bara la Asia, lipo katika nchi nyengine za Afrika na lipo Tanzania. Kila mtu anapolia anasema mamaangu mimi. Kwa hiyo, sisi tuna wajibu wa kujitathmini sisi wenyewe.

Wala hatuna haja ya kusema wenzetu wanafanya na siku zote jambo baya anapofanya mtu wa kawaida linakuwa ni baya sana lakini mtu anaenasibishwa na dini jambo hili huwa ni baya zaidi.

Uislamu si kuwa tu na jina la Kiislamu. Uislamu sikuwa umezaliwa na baba Muislamu na mama Muislamu. Uislamu ni kunyenyekea na kutekeleza yale yote aliyokuja nayo Bwana Mtume Muhammad.

Kwa hiyo, lazima vitu viwili viambatane: imani na matendo mema, na pamoja na kuacha yote yaliyokatazwa. Mtu kuwa na imani halafu akatekeleza mambo machafu, mambo mabaya ikiwemo hili la udhalilishaji, basi anahesabika kwamba imani yake ina mapungufu na hii itamuweka pahala pabaya hapa duniani na huko akhera.

The Chanzo: Kwa mtazamo wako, unadhani vitendo hivi vinasukumwa na nini?

Othman Muhammed Saleh: Kwa mtazamo wangu mimi, na bila shaka itakuwa baadhi ya watu wanaweza kuniunga mkono, inatokana na shetani. Shetani mara zote anapenda kuwashawishi watu katika njia zote.

Kuna mambo ambayo shetani anapenda kuwepo karibu, kwa sababu kuna vitu vingi ambavyo vinashawishi watu kuyafanya hayo. Kwanza mfanyaji mwenyewe anakuwa imani yake iko dhaifu.

Mtu ambaye hamuogopi Mwenyezi Mungu anaweza kufanya chochote. Atafanya udhalilishaji. Anaweza hata akalewa. Akafanya hujuma. Akafanya wizi wa mali za umma. Akafanya uzembe katika shughuli zetu za kazi.

Yaani asiwajibike kuonesha kwamba yeye anamuogopa Mwenyezi Mungu. Unapo muogopa Mwenyezi Mungu ni pahala ambapo kuona kwamba huyu Mungu mimi ananichunga.

“Hakika ya Mwenyezi Mungu anampenda mja anapofanya amali yake, basi aifanye kwa kuitakasa.” [Aya ndani ya Qur’an]. Afanye kazi katika mazingira ya heshima. Sasa tunaporejea katika suala la udhalilishaji tunakuta kwamba kunakosekana hofu ya Mwenyezi Mungu.

The Chanzo: Unadhani taasisi yako inamchango gani katika kukomesha maswala ya ukatili wa kijinsia Zanzibar?

Othman Muhammed Saleh: Sisi tunawasimamia watoto kwa kupitia madrasa zao. Kwa hiyo, watoto wale tunasikia baadhi ya siku wamefanyiwa udhalilishaji. Kwa hiyo, linapotokezea la mtoto ambae yuko madrasa [na] kwa kuifahamu madrasa hiyo, kwa kufahamu walifanya mambo hayo tunasima kidete kuhakikisha kwamba mtoto huyu kapatiwa haki zake.

Hii ni taasisi ya Kiislamu ambayo inatamani watu watekeleze Uislamu wao kwa asilimia 100. Kwa hiyo, yanapotokezea matukio haya Ofisi [ya Mufti], pamoja na watendaji wote, wanahuzunika sana.

Hata Mheshimiwa Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi [Dk Hussein Ali Mwinyi] toka ananadi Ilani ya Uchaguzi alisema jambo hili la udhalilishaji atalivalia njuga kuona kwamba haliendelei.

Sheria zimebadilishwa [na] utekelezaji unafanyika. Lakini kila siku mambo haya yanazidi. Ni huzuni kubwa kwa sababu sisi ni wasaidizi wa Mheshimiwa Raisi katika masuala haya.

The Chanzo: Wito wako ni upi kwa jamii ya Wazanzibari, pamoja na mamlaka husika, linapokuja suala la ukatili wa kijinsia visiwani humu?

Othman Muhammed Saleh: Kila mmoja atumie nafasi yake kuhakikisha kwamba tunamuogopa Mwenyezi Mungu popote tulipo. Ikiwa sisi tunaona Mwenyezi Mungu hatuoni lakini [tujue] yeye anatuona sana. Na hakuna chochote kitakacho jificha kwa wakati wowote, siku yoyote.

Ni vyema tukatengeneza mazingira ya kuhakikisha kwamba kila kwenye mwanya wa aina yoyote wa udhalilishaji, ama wa watoto au wa wanawake, mambo haya tunayaondoa kabisa kwa asilimia 100. Kila mtu atekeleze wajibu wake.

Tushirikiane kwa pamoja. Tunaweza.

Salim Khamis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Anapatikana kupitia salimkombo437@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *