Dar es Salaam. Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Tanzania imeonesha kwamba taifa hilo la Afrika Mashariki halina mkakati mahususi wa kitaifa wa kubaini na kuzuia uhalifu, ikiitaja kasoro hiyo kama moja ya changamoto kadhaa zinazoukabili mfumo wa haki jinai wa Tanzania.
Tume hiyo iliyokabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan hapo Julai 15, 2023, imebainisha kwenye muhtasari wa ripoti yake hiyo kwamba mkakati huo, pamoja na mambo mengine, ungeainisha majukumu ya taasisi mbalimbali pamoja na vyombo vya utekelezaji na jamii kwa ujumla.
Ikiwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, tume hiyo pia ilibaini kwamba vyombo vya utekelezaji sheria nchini vimejikita zaidi katika ukamataji baada ya uhalifu kutokea na siyo kubaini na kuzuia uhalifu usitokee.
Mbali na ukosefu wa mkakati, tume pia ilibaini upungufu wa vitendea kazi. Kutatua changamoto hii, tume hiyo imependekeza yafuatayo:
- Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI); Wizara ya Fedha na Mipango; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na wadau wengine wa Haki Jinai waandae na kusimamia utekelezaji wa Mkakati Mahususi wa Kubaini na Kuzuia Uhalifu, yaani Crime Detection and Prevention Strategy, ikiwemo uhalifu wa majini na mitandaoni.
- Mfumo wa nyumba kumi uhuishwe kisheria na kutambulika rasmi katika mfumo wa Serikali za Mitaa ili kurahisisha wananchi kutambuana kwa lengo la kuwezesha mkakati wa kuzuia uhalifu kuwa endelevu.
- Mifumo ya huduma za kijamii na kibiashara zifungamanishwe na mifumo ya utambuzi na usajili – ikiwemo anuani za makazi, RITA, Ardhi na NIDA – ili kila mwananchi awe na namba moja ya utambuzi.
- Serikali ichukue hatua za kupunguza uchumi wa fedha taslimu, au cash- based economy, ikiwemo kuondoa vikwazo vilivyopo kwenye mifumo ya malipo na uhamishaji pesa kimtandao.
- Mifumo ya kushirikisha jamii katika kuzuia uhalifu kama vile mfumo wa Polisi Jamii na TAKUKURU – Rafiki iimarishwe na wahusika wapewe mafunzo ya msingi kuhusu majukumu yao na watakiwe kutekeleza kazi zao kwa kuheshimu sheria na haki za binadamu.
- Serikali ihamasishe na kuwekeza, kwa kushirikiana na sekta binafsi, kwenye matumizi ya CCTV camera na TEHAMA ili zitumike kwa kiwango kikubwa katika kuzuia na kubaini uhalifu na wahalifu.
- Elimu itolewe kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuzuia vitendo vya uhalifu.
Kwenye uchunguzi wake, tume pia ilibaini kwamba vyombo vyenye mamlaka ya kukamata, mara nyingi hutumia nguvu kubwa kupita kiasi na kusababisha mateso kwa watuhumiwa.
Uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka ya kukamata pia umelalamikiwa na wananchi kuwa inakuwa vigumu kutambua taasisi iliyomkamata ndugu yao na mahali alipohifadhiwa, tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia imebaini.
Aidha, tume imegundua kwamba uwepo wa vyombo vingi vya ukamataji na vyenye mahabusu umetafsiriwa na jamii kuwa ni sababu mojawapo ya watu waliokamatwa kupotea wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Kufuatia changamoto hizo, tume imependekeza yafuatayo:
- Mamlaka ya kukamata waliyonayo mamlaka za usimamizi (regulatory bodies) yatekelezwe kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
- Taasisi nyingine zenye mamlaka ya kukamata zifanye ukamataji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
- Mahabusu za Jeshi la Polisi ndizo pekee zitumike kuhifadhi watuhumiwa wa makosa ya jinai.
- Mamlaka husika zichukue hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wanaokiuka taratibu za kazi ya ukamataji na uhifadhi wa watuhumiwa.