Dar es Salaam. Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Tanzania, kwenye ripoti yake iliyoiwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan Julai 15, 2023, imeanisha athari kadhaa zinazotokana na uwepo wa taasisi nyingi za upelelezi wa makosa ya jinai, ikishauri kuundwa kwa chombo kimoja kitakachotekeleza majukumu hayo.
Msingi wa pendekezo hilo umetokana na imani ya tume hiyo iliyoundwa Januari 31, 2023, kwamba ubora wa upelelezi na uchunguzi ndiyo msingi wa haki kupatikana kwa wakati, ikitaja uwezo na weledi wa wapelelezi, vitendea kazi, uadilifu, uwajibikaji na ufanisi kama masuala ya msingi katika kuboresha mfumo na utendaji wa taasisi za Haki Jinai nchini.
Kwa mujibu wa tume hiyo iliyofanya kazi yake chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, yote hayo kwa sasa yanashindwa kufikiwa kwani Idara ya Upelelezi imeshindwa kutenganishwa na shughuli nyingine za Jeshi la Polisi, hali inayochangia ucheleweshaji wa upelelezi, ukosefu wa ubobevu, na ufanisi mdogo katika upelelezi.
SOMA ZAIDI: Tume Yataka Mkakati wa Kitaifa Kubaini, Kuzuia Uhalifu Tanzania
Tume imeanisha athari sita zitokanazo na uwepo wa taasisi nyingi zinazojihusisha na upelelezi wa makosa ya jinai nchini, ambazo ni:
- Kwanza, migongano baina ya vyombo pelelezi kwa kutoelewa mipaka ya majukumu kati ya taasisi moja na nyingine kutokana na makosa ya jinai kuwa na muunganiko katika utendaji wake, kama vile makosa ya dawa za kulevya, rushwa na ujangili ambayo yana mfungamano na utakasishaji fedha haramu, ambapo makosa hayo yanapelelezwa na taasisi tofauti. Tume inasema hali hii imesababisha baadhi ya taasisi za kiupelelezi kufanya majukumu yasiyo na mamlaka nayo kisheria na hivyo upelelezi kutofanyika kwa ukamilifu. Hali hii pia, kwa kuruhusu wahusika kuwa wengi, inaathiri eneo muhimu la uwajibikaji.
- Pili, ongezeko la gharama kwa Serikali kutokana na mgawanyo wa rasilimaliwatu na fedha pamoja na vitendea kazi kama vile maabara za kisasa kwa ajili ya uchunguzi, boti, magari, ofisi, samani, vyumba vya mahabusu na taasisi za mafunzo ili kutosheleza mahitaji ya taasisi hizo nchi nzima.
- Tatu, taasisi tajwa hazina mfumo wa usimamizi na udhibiti wa matumizi ya mamlaka yake hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.
- Nne, uwepo wa taasisi nyingi zinazohusiana na upelelezi umesababisha changamoto za uratibu na utunzaji wa takwimu za uhalifu.
- Tano, mbali na Jeshi la Polisi, taasisi zinazotekeleza majukumu ya upelelezi hazijaenea maeneo yote nchini na gharama kubwa itahitajika ili kuziwezesha taasisi hizo kufika maeneo yote.
- Sita, vikosi kazi vinavyoundwa na taasisi za upelelezi na uchunguzi ili kushughulikia kwa dharura jinai vimelalamikiwa kwa kukosa ufanisi, uwajibikaji na muendelezo.
Kwa kuzingatia uzoefu kutoka nchi nyingine, tume hiyo iliyokuwa na wajumbe tisa ilisema kwamba uwajibikaji na ufanisi unaongezeka zaidi endapo taasisi ya upelelezi na uchunguzi itakuwa moja na itajitegemea, ikipendekeza yafuatayo:
- Ili kuweka usimamizi na mfumo madhubuti wa upelelezi na uchunguzi, Serikali iunganishe nguvu ya upelelezi na uchunguzi iliyopo sasa katika taasisi mbalimbali za upelelezi wa makosa ya jinai na kuanzisha Mamlaka mpya na huru ya upelelezi inayojitegemea itakayojulikana kama Ofisi ya Taifa ya Upelelezi (OTU), ambayo itakuwa na jukumu la kupeleleza makosa yote makubwa ya jinai.
- Pia, inapendekezwa mamlaka mpya iwe na bajeti inayojitegemea, uwezo wa kuajiri watumishi, kuwa na chuo bora cha mafunzo na maabara moja ya kisasa kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi, mifumo ya TEHAMA na kuimarisha ubobevu wa wapelelezi. Aidha, muundo, majukumu na mipaka ya utendaji itabainishwa katika sheria.
- Sheria iweke ukomo wa muda wa upelelezi kwa makosa yanayosikilizwa na Mahakama Kuu.
SOMA ZAIDI: Wakuu wa Mikoa, Wilaya Wasiwe na Mamlaka ya Kukamata Watu, Tume Yashauri