The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Watanzania na Kilio cha Samaki Kwenye Maji Katika Kiswahili

Kwa nini Tanzania inakitangaza sana Kiswahili lakini watu wake hawanufaiki na fursa za lugha hiyo?

subscribe to our newsletter!

Rafiki yangu mmoja Mwingereza, Tom Carragher, aliwahi kuniuliza swali la kufikirisha sana: Kwa nini Watanzania mnakitangaza sana Kiswahili lakini fursa zake mnawaachia watu wa mataifa mengine?

Carragher alikuwa anashangaa kwamba huko ughaibuni, kwa asilimia kubwa, fursa zilizokuwa zinahusu Kiswahili watu kutoka mataifa mengine ndiyo walikuwa wananeemeka nazo kuliko Watanzania aliyosema wanakitangaza. 

Nilitaka kumwambia kwamba mbona hiyo siyo kwenye Kiswahili tu, kwani soko la madini ya Tanzanite lipo Afrika Kusini, huku uchimbaji wake upo Mererani, Arusha, ni hali inayoshangaza sana kwa kweli! Lakini rafiki yangu huyu ana hoja ya msingi.

Ni ukweli usiopingika kwamba ulimwenguni kote, kila inapotajwa lugha ya Kiswahili, kwa haraka haraka jina la taifa hili lililopo mashariki mwa bara la Afrika limekuwa kama kielelezo cha lugha hii adhimu.

Pamoja na jitihada nyingi zinazochukuliwa kuhakikisha lugha hii inaenea ulimwenguni kote, hata hivyo, umewahi kujiuliza ni Watanzania wangapi wananufaika na fursa kede kede zitokanazo na lugha hiyo?

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Hakuna Kiswahili Kimoja

Kitu kilichomshangaza zaidi rafiki yangu Carragher ni kwa namna ambavyo Watanzania wanatajwa kuwa wajuzi halisi wa lugha ya Kiswahili, akijiuliza inawezekana vipi wakakubali kuporwa fursa za lugha hiyo? 

Kila uchao kuna kundi kubwa la wageni ambao wanaingia nchini Tanzania kujifunza lugha ya Kiswahili. Baada ya muda, wanafunzi hawa hurudi kwenye mataifa yao kama wataalamu, wakipiga hela wakati sisi tunaojitapa eti ni wenye Kiswahili tukibaki tumeduwaa tu.

Kuna mambo mawili ambayo nadhani yanaweza kuwa yamepelekea hali hii. Kwanza, nadhani inabidi tu tuukubali ukweli mchungu kwamba Watanzania tulio wengi tumekuwa wanyonge kwenye kudaka fursa.

Tumefikaje hapo, nadhani ni swali ambalo kila mtu anaweza kuja na jibu lake. Lakini kama taifa tumekwama mahali, pengine ni mfumo wa ujamaa ndiyo umetulemaza, tumekuwa wanyonge kweli katika kutanua mbavu kupamabania fursa za lugha yetu kimataifa.

Jambo la pili nadhani ni kushindwa kwa taasisi zilizopewa dhamana ya kukistawisha na kukipaisha Kiswahili zimeshindwa kazi zao kwa kushindwa kuwafanya wazawa wanufaike na lugha hii. Zimebaki jitihada binafsi na ujanja wa mtu kuweza kupenya na kunufaika na lugha hiyo.

Hata ukiwasikiliza viongozi waliopewa dhamana kutaka kujua mipango ya kisera kama taifa kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa za lugha hii utakutana na majibu yaliyojaa siasa na mipango ya kwenye makaratasi.

SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Lakini unakuja kujiuliza, ni mahali gani kama taifa tumefaulu na kujipongeza? Tupo hoi kwenye kila nyanja mpaka kwenye lugha ambayo tunajinasibu ni yetu. Wakenya na watu wa mataifa mengine wamekuwa wakituzidi katika kuzikimbilia fursa hizo. 

Kwenye nchi za wenzetu, Serikali zimekuwa zikitoa kipaumbele kwa kuhakikisha wataalamu wa lugha wanazinyaka fursa na siyo za ndani tu bali mpaka zile za kimataifa kupitia balozi zao. 

Lakini hapa kwetu ni tofauti, ukitaka kufika huko sharti ujiongeze na ujanjaujanja mwingi. Ukikutana na Watanzania walionufaika kupitia lugha yetu basi watakueleza kwamba ni jitihada zao binafsi na ujanja mwingi tu ndiyo uliyowapelekea ‘kutoboa.’

SOMA ZAIDI: Hatua Zilizobaki Ili Kiswahili Kiwe Lugha ya Kufundishia Tanzania

Hakuna mfumo maalumu ambao unazalisha watalaamu ambao wanaenda kunufaika na hizo fursa moja kwa moja. Balozi zetu zilizopo ughaibuni zimebaki kutoa matamko tu lakini utekelezaji wao katika kuzitengneneza fursa za lugha umebaki katika ombwe.

Tukitaka tujivunie Kiswahili chetu na kunufaika nacho, basi tuhakikishe kuna jitahada za lazima zinafanyika kuweka mifumo imara inayoandaa watalaamu ambao wanaenda kunufaika na hizo fursa moja kwa moja. 

Tuachane na hizi siasa za kujaza idadi kubwa ya wataalamu kwenye kanzi data huku wanufaikaji wakiwa ni wachache!

Steven Mbosa amejitambulisha kama mtaalamu wa Kiswahili aliyehitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia mbosasteven99@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *