Tangazo la Shirikisho la Soka (TFF) kwamba limeboresha kanuni za udhamini, ambazo sasa zinawapora wachezaji haki yao ya kujiimarisha kiuchumi kutokana na uwezo au umaarufu wao, limestua wengi na si habari nzuri kwa wachezaji.
Ni tangazo ambalo linaonesha tunajitahidi kurudi nyuma wakati baadhi ya wawekezaji wanakesha kufikiria wafanye nini kuboresha timu wanazodhamini au kuzimiliki na kuboresha uchumi wa wachezaji ili wacheze mpira bila ya mawazo yoyote.
Ni tangazo la kushtua hata kwa wachezaji kutoka nje ambao, katika miaka ya karibuni, wamekuwa wakimiminika nchini kuja kuuza nguvukazi yao, huku kwa namna fulani wakisaidia wazawa na kuchangamsha ligi yetu ambayo sasa inashika nafasi ya tano kwa ubora barani Afrika.
Hicho kitu kinachoitwa maboresho ya kanuni za ligi kinazungumzia kuzuia wachezaji kuingia mikataba binafsi ya udhamini na kampuni ambazo ni washindani wa mdhamini mkuu wa Ligi Kuu, yaani benki ya NBC, ambayo ina haki peke, au exclusive rights, za Ligi Kuu.
Katika kanuni hizo kumeongezwa sentensi inayosema, “Hairuhusiwi kwa mchezaji kuingia mkataba binafsi wa udhamini na mshindani kibiashara wa mdhamini mkuu wa Ligi Kuu. Atakayekiuka atafungiwa kwa kipindi cha kati ya mwezi mmoja na mitatu.”
Haiendi ndani kwa kina kuzungumzia ni shughuli gani ambazo zitachukuliwa kuwa zimeingiliana na mdhamini mkuu. Ni sentensi ya kiujumla ambayo inaweza kutafsiriwa vibaya kwa lengo ovu.
Marekebisho hayo yamekuja wakati tayari wachezaji wanne—Stephane Aziz Ki, Farid Mussa, Mohamed Hussein, na Cloutus Chama wakiwa na mkataba wa udhamini, maarufu kama endorsement, na benki ya CRDB.
Haijulikani uamuzi huo umeathiri vipi mikataba ya nyota hao, yaani kama imeshaisha au inaendelea, lakini kilichopo ni kwamba sura zao bado zinaonekana kwenye mashine za kutolea fedha (ATM) za CRDB, kitu kinachomaanisha kwamba bado wanaendelea kutangaza huduma za benki hiyo.
Hayastahili kuwepo
Hata kama mikataba yao ingekuwa imeisha, bado marekebisho hayo hayastahili kuwepo, achilia mbali kwamba yamechelewa na hayakupewa muda wa kutosha kujadiliwa, hasa na wachezaji wenyewe ambao kiutaratibu wanatakiwa wawakilishwe na mameneja wao, mawakala wao, au Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA).
Ni jambo la ajabu kwamba wakati huu ambao ligi mbalimbali duniani zinatengeneza chapa zake – La Liga, Premier League, Bundesliga, Serie A au Ligue 1 – ili kuondokana na mizozo ya kiuchumi dhidi ya klabu na wachezaji, sisi ndiyo kwanza tunapiga hatua kurudi nyuma kurudi kwenye udhamini wa kiujumla wa Ligi Kuu ya NBC.
SOMA ZAIDI: Waziri Pindi Chana, Wizara Wasitekwe na Umaarufu wa Soka
Ligi Kuu ya England imefanya kazi kubwa kujenga chapa, au brand, yake ya Premier League na kuondokana na udhamini wa pamoja kama ule wa Barclay Premier League. Hivi sasa klabu zinaweza kudhaminiwa na kampuni yoyote bila ya muingiliano na Premier League, ambayo ni taasisi tofauti kabisa na Chama cha Soka cha England (FA).
Kilichofanywa na Ligi Kuu ya England ni kutengeneza bidhaa tofauti ndani ya ligi na kuziuza kwa kampuni zinazotaka kudhamini. Kampuni zinazonunua bidhaa hizo hujulikana kama washirika, au partners. Kwa mfano, mshirika mkuu wa Premier League ya England ni EA Sports, ambayo inahusika na michezo ya video, au video games.
Pamoja na kwamba EA Sports ina haki peke, au exclusive rights, katika eneo hilo, hakuna muingiliano wa udhamini na klabu wala wachezaji.
Hawa wana haki ya tangazo lao kuonekana kwenye runinga wakati wa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mechi zote za Ligi Kuu duniani, wanadhamini mchezaji bora wa mwezi na wa msimu na wanaendesha shindano la video la ligi hiyo. Sidhani kama klabu inaweza kutafuta mdhamini anayefanya shughuli hizo.
Kapu hilo la washirika pia linahusisha benki ya Barclays. Taasisi hii ya kifedha inahusika na kutoa huduma zote za kibenki kwenye ligi kuu. Lakini klabu hazikatazwi kudhaminiwa na benki nyingine. Liverpool inadhaminiwa na benki ya Standard Chartered.
SOMA ZAIDI: Kabumbu Itusaidie Kujenga Utambulisho, Ufahari Wetu Kama Taifa
Kapu hilo la washirika pia lina kampuni za Budweiser, Hublot, Castrol, Nike na Oracle.
Bidhaa nyingine za Ligi Kuu ya England ni kutoa leseni kwa kampuni kwa ajili ya shughuli maalum. Mfano ni Avery Dennison, ambayo kazi yake ni kuchapa chapa.
Hawa ndiyo waandishi wa majina yote kwenye jezi rasmi za timu zote, namba na beji za mkononi. Ni bidhaa iliyotengenezwa kwa ajili fulani na klabu haziwezi zikasema eti jezi zao zitaandikwa na mtu wao wa Kariakoo.
Pia, kuna washirika wanaohusika na urushaji wa matangazo ya televisheni, yaani kampuni za Sky Sports, TNT Sports, Prime Video na BBC Sports. Kwa sheria za soka, mmiliki wa haki za matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ni chama cha soka cha nchi husika.
Nimejaribu kuonyesha uhusiano wa kiuchumi kati ya chama cha soka cha nchi na klabu na jinsi chama kilivyotengeneza bidhaa, au brand packaging ambazo zinaondoa muingiliano wa udhamini kati yake na klabu.
Klabu ndiyo ziko karibu sana na chama cha soka cha nchi ambacho huzidhibiti, lakini wachezaji wako mbali sana na si rahisi chama kuwasogelea na kuwadhibiti. Kama England imetengeneza njia ya kukwepa migogoro ya kiuchumi na klabu, vipi kwa wachezaji?
Ni dhahiri kwamba FA inakutana na wachezaji uwanjani tu na si kwenye mashine za ATM au mabango mengine barabarani au kwenye TV kama TFF inavyotaka kufanya.
Ni kitu kibaya kwamba katika enzi hizi, TFF inaibuka na kanuni inayobana wachezaji kiuchumi badala ya kuwatengenezea mazingira mazuri na kuwalinda.
Uzoefu kwengineko
Ni muhimu TFF ikaangalia mifano ya sehemu nyingine ili kujua ijenge vipi hoja wakati wa kusaini mikataba ya udhamini badala ya kukimbilia kuandika kanuni ya hovyo kama hiyo kupendezesha wadhamini wakati enzi za kanuni hizo zimeshapita. Hebu tuangalie uhusiano wa klabu na mchezaji kiuchumi.
Mdhamini mkuu wa vifaa wa klabu ya Paris Saint Germain (PSG) ni Nike ambayo ilikuwa pia na mikataba binafsi na wachezaji kama Kylian Mbappe na Marco Verrati, lakini hiyo haikuzuia Puma kumdhamini Neymar na Adidas kumdhamini Lionel Messi.
SOMA ZAIDI: Morocco: Chachu ya Soka la Afrika, Duniani
Iko mifano mingi ya wachezaji kuidhinisha kampuni kutumia jina na taswira yake kutangaza bidhaa zinazolingana na huduma za mdhamini mkuu wa klabu au ligi. Kinachotakiwa ni kutengeneza bidhaa na kuiwekea maeneo ambayo mdhamini atatakiwa kuwa na haki peke na si kila mahali.
Yaani kama Aziz Ki, Chama, Farid na Tshabalala hawatangazi bidhaa za CRDB wakati wa mechi za Ligi Kuu ya Bara, NBC haathiriki kwa lolote kwa kuwa eneo lake halijaguswa. Labda kama TFF imewauzia NBC kila kitu!
Ni kwa vipi udhamini wa CRDB kwa akina Aziz Ki, Tshabalala, Farid na Chama unaingilia udhamini wa benki ya NBC? Hawavai fulana za CRDB uwanjani wala jezi zilizo na nembo ya NBC wakati wa mechi au mazoezi. NBC wanaathirikaje? Kama TFF haikuliona hilo, ni ajabu.
Kwa sasa vyama, klabu na wawakilishi wa wachezaji wanahangaika jinsi ya kutafuta fedha katika fursa ambazo mchezo wa soka unazitoa na si kufikiria jinsi ya kudhibiti fursa hizo. Ni vyema TFF ikawa inafanya utafiti wa kutosha, ikishirikisha wadau halisi badala ya chawa wakati wa kujadili mambo muhimu kama uchumi wa wachezaji na klabu!
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.