The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Waziri Pindi Chana, Wizara Wasitekwe na Umaarufu wa Soka

Labda tukuulize waziri wetu Pindi Chana na msaidizi wako, MwanaFA, kuna nini kwenye netiboli?

subscribe to our newsletter!

Takriban wiki mbili zimepita tangu Australia itwae ubingwa wa netiboli baada ya kuishinda England kwa mabao 61-45 katika mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika Afrika Kusini.

Lilikuwa ni hitimisho la fainali zilizoshirikisha mataifa 16, huku mataifa sita yakipata tiketi ya moja kwa moja kucheza mashindano hayo; wenyeji na timu tano zinazoshika nafasi tano za juu kwa ubora duniani. Nafasi kumi zilizosalia zilishindaniwa katika kanda tano, kila moja ikitoa timu mbili.

Katika nchi hizo sita zilizopata tiketi ya moja kwa moja, kwa bara letu Afrika Kusini ilifuzu kutokana na kuwa mwenyeji wakati Uganda ilikuwa moja ya timu tano zilizokuwa katika nafasi tano za juu kwa ubora duniani.

Nchi nyingine zilizoiwakilisha Afrika zilikuwa Malawi, ambayo inashika nafasi ya sita kwa ubora duniani, na Zimbabwe ambayo inashika nafasi ya 12 duniani. Malawi na Zimbabwe zilifuzu kupitia Kanda ya Afrika, ambayo kama Tanzania ingekuwa imejiandaa vizuri nayo ingefuzu.

Lakini katika michuano ya ubingwa wa Afrika wa netiboli ambao ulitoa wawakilishi wa Afrika baada ya Afrika Kusini na Uganda, Tanzania ilipoteza mechi zote. Ilifungwa na Namibia 54-30, na Afrika Kusini (58-30), na Zimbabwe (43-33) na ikafungwa na Botswana (54-45) na hivyo kushindwa kwenda hatua ya mwisho kutoka kundi lake kutafuta tiketi.

Mchezo maarufu

Wakati michuano hiyo inaendelea Cape Town, nina uhakika, ni Watanzania wachache sana waliojua kilichokuwa kinaendelea, licha ya mchezo huo kuwa wa pili kwa umaarufu Tanzania baada ya mpira wa miguu.

Siyo siri, netiboli ndiyo mchezo wa kwanza kwa mtoto yeyote wa kike Tanzania kwa kuwa ndiyo anaokutana nao mara tu anapopata akili ya kupenda michezo. Kama ilivyo kwa mpira wa miguu, mchezo wa netiboli hauna matatizo katika kupata sehemu ya kuchezea. Unaweza kucheza barabarani kama watoto wachezavyo gombania goli ya mpira wa miguu au chandimu.

SOMA ZAIDI: Waandishi Bunifu Tanzania Tukisahaulika Sasa, Tutakumbukwa Lini?

Pengine kinachoweza kuwa gharama ni magoli pekee. Nayo yanawezekana bila ya gharama kubwa kama ilivyo kwa mchezo wa mpira wa kikapu. Ni mlingoti mmoja na duara wa chuma tu. Ndiyo maana mtoto yeyote, bila ya kujali hali ya kiuchumi ya mazingira aliyokulia au shule anayosoma, hawezi kushindwa kucheza netiboli.

Na ndiyo maana wakati fulani kulikuwa na klabu za mitaani za netiboli, ukiacha zile za mashirika ya umma, wizara au majeshi zilizofanya kazi kubwa ya kuuwezesha mchezo huo kukua na kuendelea.

Fedheha kwa taifa

Lakini hali ilivyo kitaifa, kimkoa na kiwilaya kwa mchezo huo si nzuri. Miaka michache iliyopita timu ya taifa ya netiboli ilishindwa kushiriki michuano ya Kanda ya Afrika iliyofanyika Afrika Kusini baada ya chama kushindwa kulipia deni la ada ambalo lilikuwa si zaidi ya Shilingi Milioni 2. Ilikuwa ni aibu na fedheha kwa taifa.

Si chama cha netiboli, CHANETA, wala idara husika katika Wizara ya Utamaduni, Michezo na Sanaa ambayo imetoa taarifa yoyote kuhusu jinsi hali ya netiboli inavyozidi kuwa mbaya, huku wasichana wadogo wakianza kuelekeza akili zao katika soka la wanawake.

Si kwamba wizara haipo, au hakuna waziri. La hasha! Wapo.

SOMA ZAIDI: Kabumbu Itusaidie Kujenga Utambulisho, Ufahari Wetu Kama Taifa

Lakini hawa wanaonekana zaidi katika matukio makubwa yanayohusu timu kubwa za soka, au wasanii wakubwa wa huu muziki unaoitwa Bongo Fleva, badala ya kujikita katika malengo ya Sera ya Michezo ya mwaka 1995, ambayo inaelekeza cha kufanya kama kuna mchezo unadorora.

Si ajabu kumuona waziri wa michezo akiwa amesafiri na moja ya klabu kubwa za soka, au timu ya taifa, au akiwa pamoja na msanii mkubwa wa Bongo Fleva. Wizara na Waziri Pindi Chana na wenzake waliomtangulia, wametekwa na umaarufu wa mchezo wa soka na wa wasanii wakubwa. Na nafikiri wanautumia kujiongezea umaarufu badala ya kusaidia kuutangaza mchezo na michezo mingine.

Netiboli ifanye jitihada zake hadi ifuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia ndipo itakapowaona viongozi wa juu wa Serikali wakijihusisha nayo. Haya mambo ya kufufua mchezo unaoelekea kufa, hayaihusu wizara au waziri.

Hakuna ushindani

Wasichana wadogo wanaoshindana kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari (UMISETA), humalizia matamanio yao kwenye mchezo huo mara wamalizapo shule. Hakuna ushindani nje ya shule kwa kuwa hakuna anayecheza netiboli kwa mapenzi yake.

Na kwa kuwa viwanja vya michezo vimevamiwa, huku maeneo mapya yanayotolewa kwa ajili ya ujenzi wa makazi hayazingatii michezo, hakuna matumaini ya wasichana kuendelea kuupenda na kucheza mchezo unaoendana na asili na mazingira yao.

SOMA ZAIDI: Morocco: Chachu ya Soka la Afrika, Duniani

Wizara ina vyombo mbalimbali kwa ajili ya kuratibu na kusimamia michezo kuanzia ngazi ya wilaya, ambako kuna kamati za utamaduni. Lakini ni vigumu mno kusikia kamati hizi zikifanya kazi, hasa zile za maendeleo ya michezo. Labda zile kamati za wilaya ambazo kwenye maeneo yao ya mamlaka kuna klabu kama Simba na Yanga au kuna tukio kubwa ambalo litahitaji kamati kuwajibika.

Huku wilayani ndiko ambako kunatakiwa kuwe na ligi za wilaya ambazo ndiyo msingi wa mchezo huo kwa kuwa hiyo ndiyo ngazi ya kwanza kabisa. Lakini, huwezi kusikia mkoa hata mmoja una ligi ya wilaya ya netiboli.

Ligi za mikoa ndiyo kabisa hazisikiki na ya taifa ndiyo hufanyika kwa bahati. Timu ya taifa itapatikanaje kama hakuna mashindano katika ngazi za awali kabisa?

Wachezaji nyota wa baadaye watapatikanaje kama CHANETA haina hata mashindano ya wasichana walio na umri chini ya miaka 20?

Hata zile shule ambazo zilisifika kutoa wachezaji bora wa michezo mingi, ikiwemo netiboli, hazijaweka mkazo huo tena kwa kuwa hakuna mwanga mbele. Tulizoea kusikia nyota wakitokea shule kama Jitegemee, Lugalo, Filbert Bayi na nyingine, lakini leo hakuna kitu.

Wizara haishtushwi?

Wizara haishtushwi na kudorora huku kwa netiboli? Haijisikii kuinuka na kwenda kuuliza waendeshaji wa mchezo huu kama kuna tatizo linalohitaji msaada wao?

Sera ya Maendeleo ya Michezo ya 1995 inazungumzia jukumu la kuitafutia michezo wadau wanaoweza kuisaidia kifedha, na wataalamu wengine kama wa masoko, ualimu na hata uongozi. Wizara inafanya lolote katika hayo?

Labda tukuulize waziri wetu Pindi Chana na msaidizi wako, MwanaFA, kuna nini kwenye netiboli? Huwezi kutenga muda kidogo kushughulikia kuuhuisha mchezo huu unaopendwa na maelfu ya wanawake?

SOMA ZAIDI: Watanzania 10 Waliong’ara Kitaifa, Kimataifa 2022

Tunajua kuwa kama mwanasiasa ungependa kujihusisha na kitu ambacho kinafuatiliwa na wengi kama unavyofanya kwa Simba, Yanga na Taifa Stars.

Lakini hata huku kwenye netiboli ukifanya jambo kama hilo la kuufufua mchezo huu, jina lako litakua mara kumi ya huko kwenye soka ambako baadhi wanaona kama unaenda ili kujipatia umaarufu na si kutengeneza umaarufu wa mchezo kwa kuurejesha kwenye makali yake.

Rais Samia Suluhu Hassan atalazimika kufuatilia netiboli na kuweka nguvu zaidi iwapo ataona wewe msaidizi wake mkuu katika eneo hilo unafanya kitu kwa wanawake wa nchi hii.

Ni kweli soka ni maarufu, lakini mchezo huu usikuteke wewe waziri, naibu wako wala wizara nzima. Angalieni na kwingine. Iko michezo mingi, lakini netiboli ina upekee kutokana na historia na utamaduni wetu.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *