The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Waandishi Bunifu Tanzania Tukisahaulika Sasa, Tutakumbukwa Lini?

Bila viongozi wa nchi kutengeneza fursa za makusudi, hakuna mwandishi bunifu atakayehamasika kufika mbali.

subscribe to our newsletter!

Waswahili hunena, ukiwa na jambo unalopaswa kusema, kunyamaza ni sawa na kudanganya. Tangu nilipomaliza kutazama hafla ya uzinduzi wa Ikulu mpya ya Chamwino, jijini Dodoma, nimejaribu kujizuia kusema chochote, lakini nahisi dukuduku likipanda toka kifuani hadi kooni kiasi cha kufanya nihisi koromeo limejaa mithili ya njiwa manga kwenye shamba la mpunga. 

Sina budi kufunua kinywa ili kupata ahueni. Walakini kabla sijasema chochote, naomba kuwaonesha, japo kidogo, umuhimu wa hafla zinazofanyika Ikulu au katika majilisi nyinginezo za Kiserikali katika kuhuisha na kukuza tasnia mbalimbali nchini.

Mwezi Januari 2021, katika hafla ya kuapishwa kwa Rais wa 46 wa Marekani, Joe Biden, mbali na wasanii wakubwa duniani kuhudhuria, pia alialikwa msichana mdogo wa miaka 22—mtunzi wa vitabu vya mashairi—aitwaye Amanda Gorman. 

Mshairi huyu hakualikwa tu kula karanga za Ikulu na kupiga picha, bali pia alipatiwa fursa ya kusoma shairi lake liitwalo The Hill We Climb, fursa ambayo, ndani ya siku moja tu, ilipelekea vitabu vyake viwili – Change Sings: Children Anthem na The Hill We Climb – kupanda chati na kushika nafasi mbili za juu kimauzo kwenye orodha ya Amazon.

Fauka ya hayo, ndani ya siku hiyo hiyo moja, mamilioni ya wafuasi (followers) walifurika katika kurasa zake za mitandao ya kijamii. Mathalani, huko Twitter alikokuwa na wafuasi 7,000 tu, alifikisha zaidi ya wafuasi milioni mbili. Huko Instagram sasa ndiyo hakusemeki. 

Baada ya hafla hiyo, vyombo vikubwa vya habari kama vile CNN, BBC, Al-Jazeera, na vile vya mkondoni kama The Oprah Winfrey Show, vilimsaka kwa udi na uvumba ili kufanya naye mahojiano yaliyokuwa na tija kubwa mno kwake binafsi.

Taasisi mbalimbali nchini Marekani, kama vile Morgan State University, zilimtafuta ili kutaka kumwajiri katika idara nyeti za masuala ya fasihi.

Mafanikio haya makubwa, yaliyochagizwa na kitendo kidogo tu cha Ikulu ya White House kumwalika na kumpa fursa ya kuonekana mbele ya hadhira kubwa, hayakuishia kwa Amanda pekee, bali mrindimo wake uliitetemesha tasnia nzima ya watunzi wa vitabu nchini Marekani. 

Mauzo ya vitabu vingi yaliongezeka mara dufu na ilhali mzani wa hadhi ya watunzi ukipanda juu. 

Kwa tukio hilo, Ikulu ya White House ilipeleka ujumbe duniani namna inavyothamini hadhi na kukuza vipaji vya watunzi wao wa vitabu, sanjari na juhudi zake katika kuhamasisha usomaji wa vitabu—kitu ambacho kinachochea maarifa katika bongo za watu wake, na kusisimua ubunifu katika ukuaji wa vipawa vyao. 

SOMA ZAIDI: Washindi Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu Watangazwa Dar

Tuulizane: ni akina ‘Amanda’ wangapi hapa nchini mwetu Tanzania wanaofisha ubunifu wao na kuzika vipaji vyao kwa kukosa hamasa kutoka katika majukwaa makubwa ya wenye mamlaka?

Nililikumbuka tukio hilo la Amanda na Ikulu ya Marekani baada ya moyo wangu kutamani kuwaona watunzi wa vitabu (riwaya, mashairi, nakadhalika)—kama walivyopanda jukwaani wanamuziki—nao wakipatiwa fursa hiyo adhimu na adimu kabisa katika uzinduzi wa Ikulu mpya ya Chamwino. 

Lakini waapi bwana wee. Siyo tu hawakupata fursa ya kupanda jukwaani wala kutambuliwa hadharani, bali hata kualikwa tu ilishindikana. Walipuuzwa kabisa—au ‘kiungwana’ tuseme walisahaulika.

Kupuuzwa

Lakini, anapoalikwa Ommy Dimpoz, akasahulika mzee Shafi Adam Shafi (wa Kuli, Kasri ya Mwinyifuadi, Mbali na Nyumbani) huko ni kupuuzwa; anapoalikwa Christian Bella, akasahulika Hussein Tuwa (wa Mfadhili, Mkimbizi, Mdunguaji) huko ni kupuuzwa; anapoalikwa Steve Nyerere, akasahulika Profesa Emanuel Mbogo (wa Watoto wa Mama Ntilie, Malkia Sitti bint Saad) huko ni kupuuzwa; anapoalikwa Hajji Manara, akasahaulika Richard Mabala (wa Hawa The Bus Driver, Mabala The Famer), huko ni kupuuzwa. Sasa kwa nini tunawapuuza—au tunawasahau—watu ambao kupitia kalamu zao wanalinda tamaduni zetu na kuchochea maarifa yetu?

Katika hali kama hiyo, unadhani kijana aliyewasoma akina Richard Mabala, Hussein Tuwa, kisha akaishia kuwaona tu Facebook na Twitter, anapokuja kuwaona Ommy Dimpoz na Steve Nyerere—wakiwa na Rais wa nchi—kwenye hafla kubwa za Kiserikali, atatamani kuja kuwa nani baadaye kati ya mwanamuziki na mwandishi? 

Je, kijana huyu atapenda kusoma vitabu au kusikiliza nyimbo? Sisemi kwamba hatuhitaji wanamuziki, waigizaji, nakadhalika, la hasha. Bali tunahitaji mchanyato wa wanasanaa na wanataaluma kutoka katika nyanja mbalimbali, hiyo ndiyo hoja yangu.

SOMA ZAIDI: Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu: Tumaini Jipya Kwa Waandishi Tanzania?

Hivi sasa tuna ombwe kubwa la watunzi wa kike katika tasnia ya vitabu nchini, kiasi kwamba wanawake wanakosa wa kuwasemea mambo yao kinaganaga. 

Sasa hebu pata picha, katika hafla ile ya Ikulu, mbele ya macho ya Rais, wangetambuliwa watunzi kama Zaynab Bahroon, Laura Pettie, Lilian Mbaga, Elizabeth Mramba, na wengineo, ni hamasa kubwa kiasi gani ingewafikia wasichana nchini ambao wanatamani kuwa watunzi wa vitabu, lakini hawaoni mwanga?

Wavaa kofia mbili

Watunzi wa vitabu (riwaya, mashairi, nakadhalika) wanazo kofia mbili vichwani mwao. Moja, ni wanataaluma—kwa sababu vitabu vyao vinaandikwa kitaaluma na vinatumika katika shughuli za kitaaluma. Pili, ni wana sanaa—kwa sababu vitabu vyao, kama ilivyo kwa nyimbo na uigizaji, ni tanzu za fasihi. 

Na fasihi ni tanzu ya sanaa. Kwa hivyo, washairi na wanariwaya ni wasanii pia. Je, unayajua madhara ya kumsahau mtu ambaye asipoigusa jamii kitaaluma ataigusa kisanaa?

Sasa, kasumba hii imekuwa ikichipua kwa kasi mithilii ya uyoga kwenye kichuguu kiasi kwamba si tu katika hafla za Ikulu, bali karibu hafla zote ambazo wana sanaa na wanataaluma mbalimbali hualikwa, watunzi wa vitabu husahaulika. 

Umeshajiuliza ni kwa nini wanenguaji na hata machawa wa wasanii wanaalikwa Bungeni halafu washindi wa tuzo za uandishi wa vitabu (riwaya, mashairi) za Safal-Cornell na Mwalimu Nyerere, wanasahaulika? 

Ni kupuuzwa tu. Tunapeleka ujumbe gani duniani? Kwamba usomaji na utunzi wa vitabu katika nchi yetu ni mpango wa kando?

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis Aichambua ‘Peponi’ Ya Abdulrazak Gurnah

Nchi zilizoendelea duniani kote zinawatunza na kuwatuza watunzi wao wa vitabu kwa wivu mkubwa. 

Rais Barack Obama wa Marekani, katika utawala wake, aliwalika Ikulu mamia ya watunzi wa vitabu, kama vile akina Toni Morrison, Joyce Carol Oates, Daniel Aaron, Stephen King, na wengine wengi—na kuwatuza medani mbalimbali kama sehemu ya kuheshimu na kutambua mchango wao katika jamii.

Mtunzi wa riwaya James Patterson, pia, alipofikiria kuandika riwaya inayohusu masuala ya Urais na Ikulu, alimfikia Rais Bill Clinton na kumshawishi waandike kitabu kwa pamoja. Bill Clinton akakubali. Matokeo yake wakatoka na riwaya kabambe kabisa: The President Is Missing na The President’s Daughter

Kwa heshima hii aliyopewa Patterson, unadhani ni vijana wangapi walikitafuta na kukisoma kitabu hiki? Ni vijana wangapi walitamani kuja kuwa kama Patterson? Bila viongozi kutengeneza fursa hizi hakuna atakayehamasika kufika mbali.

Hata hapa Bongo, miaka ile ambapo usomaji wa vitabu ulikuwa juu sana, haikutokea vile kwa nasibu tu, bali viongozi wa juu wa nchi yetu walishiriki kuamsha ari ya usomaji na kuchochea hadhi za watunzi. 

Mfano wa Nyerere

Utakumbuka Mwalimu Julius Nyerere alishirikiana sana na watunzi kama akina Kaluta Amri Abeid, Shaaban Robert, na wengineo tangu wakati wa kupigania uhuru na hata baada ya kuutwaa. Heshima ya watunzi hawa ikapaa kila kona.

Kuna wakati Mwalimu Nyerere alipata kuwa anawaalika Ikulu watunzi wa vitabu kama akina Elvis Musiba (aliyeandika simulizi za Willy Gamba), Ben R. Mtobwa (aliyeandika simulizi za Joram Kiango), na wengineo wengi ili kupata nao kahawa na kupiga nao soga tu, kitu ambacho kilinyanyua hadhi za watu na thamani ya vitabu walivyoandika.

Unaweza kusema labda hiyo ni kwa sababu Mwalimu Nyerere mwenyewe alikuwa ni mtunzi wa vitabu. La hasha. Kuwa mtunzi pekee hakutoshi, bali wito na utambuzi juu ya tasnia hii nyeti kabisa. 

SOMA ZAIDI: Kabumbu Itusaidie Kujenga Utambulisho, Ufahari Wetu Kama Taifa

Chukua mfano huu: mnamo Machi 2017, Rais Magufuli alimteua mtunzi mahiri wa riwaya nchini, Dk Harrison Mwakyembe, kuwa Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo. Watunzi tukaamini kuwa sasa hata kama hatutofika chumbani, lakini tutatolewa msalani na kuwekwa walau barazani. 

Kumbe ‘mvinyo’ ule ule uliowalevya wengi kiasi cha kudhani sanaa ni ya waimbaji na waigizaji tu, tayari ulikwishamlevya chakari Waziri huyu aliyetunga riwaya ya Pepo ya Mabwege. Mvinyo ule ukawa unamyumbisha tu huku na kule; ikawa leo akipepesukia Bongo Fleva kesho anawewesekea Bongo Muvi.

Kuna wakati, kwa kusaidiwa na mzee wetu mmoja, ambaye pia ni mtunzi wa riwaya, Wanariwaya kutoka Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi) tuliweza kumfikia Dk Mwakyembe hadi ofisini kwake jijini Dodoma—na mabuku yetu makubwa yenye kushajihisha mapito yetu na kupambanua mahitaji yetu. 

Kilichotokea, kama mabuku yetu hayakufungiwa maandazi, basi tutakuwa ni wenye bahati sana!

Hatimaye leo tumempata Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye akiwa Makamu wa Rais, Februari 2021, alihudhuria hafla ya utoaji tuzo za uandishi (riwaya na ushairi) za Mabati-Cornell na kuzungumza mengi yahusuyo uandishi na usomaji. 

Kwenye hafla hiyo, Samia aliwataja akina Mzee Hajji Gora, Shafi Adam Shafi, Mohammed Said Abdulla, na wengine wengi kuashiria namna alivyokuwa mkereketwa na mfurukutwa wa tasnia hii. Sasa, tusipopaza sauti zetu leo tutapaza lini? 

Na kama tutasahaulika wakati huu ambapo Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bi Zuhra Yunus, naye ni mtunzi mwenzetu wa vitabu—tutakumbukwa lini?

Maundu Mwingizi ni mwandishi wa vitabu vya riwaya na hadithi fupi fupi. Pia, ni Katibu Mwenezi wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi). Anapatikana kwa barua pepe maundumwingizi@gmail.com au nambari ya simu +255 754 609 046. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Makala iko vizuri mno! Labda viongozi wanajaribu kuitengeneza Jamii isiyokuwa na fikra pana ili waweze kuwatawala vizuri!! Lakini madhira yake ni makubwa sana hususan kwa Jamii yetu ya baadae.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *