Washindi Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu Watangazwa Dar

Washindi wa kumi mpaka wa saba watunikiwa vyeti maalum, huku wa tatu mpaka wa kwanza wakijishindia fedha taslim.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Washindi wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu walitangazwa jijini hapa hapo Alhamisi, Aprili 13, 2023, kwenye hafla iliyohudhuriwa na wageni mbalimbali, huku Rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano, akiwa kama mgeni rasmi wa shughuli hiyo.

Tuzo hiyo iliyozinduliwa rasmi mnapo Septemba 12, 2022, imeandaliwa ikiwa kama ni sehemu ya juhudi za Serikali kuunga mkono uandishi wa kazi bunifu, tasnia ya uchapishaji, pamoja na kukuza utamaduni wa kujisomea miongoni mwa Watanzania.

Ikipewa jina la Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, kama sehemu ya kuenzi mchango wa mwanasiasa na mwanafalsafa huyo katika eneo la uandishi wa kazi bunifu, tuzo hiyo imetolewa Aprili 13 ili kuendana na sherehe ya kuzaliwa kwa kiongozi huyo anayeheshimika ndani na nje ya nchi.

SOMA ZAIDI: Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu: Tumaini Jipya Kwa Waandishi Tanzania?

Kwenye hafla hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Rotana, jumla ya washindi 20 walitangazwa – kumi wakiwa ni wa riwaya na kumi wakiwa wa ushairi – ambapo saba, kutoka kila tanzu, walipewa vyeti vya kuwatambua, huku watatu, kutoka kila tanzu, wakipewa vyeti na fedha taslimu.

Mshindi wa tatu kutoka kila tanzu alizawadiwa Shilingi milioni tano; mshindi wa pili Shilingi milioni saba, huku mshindi wa kwanza akijizolea Shilingi milioni kumi. Mbali na fedha hizo taslimu, washindi hao wa kwanza pia walizawadia ngao, kama ishara ya tuzo husika.

Amri Rajab Abdalah, mwandishi bunifu kutoka Kilimanjaro, ndiye aliyeibuka mshindi kwa upande wa tanzu ya ushairi, huku akiupa mswada wake huo jina la Mtale wa Ngariba. Hamis Hussein Kibari, kutoka Dar es Salaam, aliibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa riwaya.

Washindi hao wa kwanza pia watanufaika na ufadhili wa Serikali wa kuchapishiwa miswada yao kuwa ya vitabu. Serikali pia itabeba gharama za kusambaza vitabu hivyo kwenye shule zote za umma pamoja na maktaba za umma.

Mchuano mkali

Akizungumza kabla ya utoaji wa tuzo hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo hiyo, Profesa Penina Mlama, alisema kwamba zoezi zima la kupokea miswada ya waandishi lilianza hapo Septemba 12, 2022, na kukamilika rasmi mnamo Novemba 30, 2022.

Mnamo Disemba 21, 2022, Tume ya Majaji ilianza kazi ya kuipitia miswada iliyokidhi vigezo vya kushindana, zoezi ambalo lilikamilika Machi 30, 2022. Jumla ya miswada 283 ilipokelewa mbele ya kamati, miswada 193 ikiwa ni ya ushairi, 85 ya riwaya na miswada mitano ya kazi ambazo zilikuwa hazishindanishwi.

Kati ya miswada hiyo, 79 haikukidhi vigezo vya kushindana, huku 204 ndiyo iliyokidhi vigezo vya kushindana ili kumpata mshindi. Kwa ujumla, miswada 254 ilitokea Tanzania Bara na miswada 29 ilitokea Zanzibar. Idadi ya wanaume walioshiriki ilikuwa ni 223 na wanawake walikuwa ni 60.

SOMA ZAIDI: Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria

“Naomba nichukue fursa hii kuwapongeza waandishi bunifu wote walioshiriki katika kushindania tuzo hii,” Mlama, moja kati ya waandishi nguli wa tamthiliya za Kiswahili Afrika Mashariki, alisema. 

“Hata kama hutabahatika kuwa mshindi, ukumbuke kuwa kwa kuthubutu kwako kukaa na kubuni ushairi, au riwaya, umeupaisha uandishi bunifu wa Kiswahili nchini kwetu kwenda kwenye kiwango kingine,” aliongeza Profesa Mlama.

Mlama alitoa wito kwa waandishi bunifu kujiandaa kwa msimu unaokuja wa mwaka 2024, ambao utatangazwa rasmi hapo Juni 1, 2023, ambao dirisha la kupokea miswada litafunguliwa.

“Kuhitimishwa kwa zoezi la tuzo hii leo ni mwanzo wa mchakato mpya wa tuzo hii kwa mwaka unaofuata,” alibainisha mwanafasihi huyo. “Tunawataarifu waandishi kuwa miswada ya tuzo ya mwaka 2024 itaanza kupokelewa kuanzia Juni 1, 2023, na kutakuwa na muda hadi Oktoba 31, 2023.”

Kiswahili kitukuzwe

Kwenye hotuba yake kabla ya kutoa tuzo hiyo, Chissano, ambaye akiwa kama Rais wa pili wa taifa la Msumbiji alihudumu kutoka mwaka 1986 mpaka mwaka 2005, alisema ni muhimu kwa Serikali na wadau wengine kuendelea kuutambua mchango wa watu wanaoandika kwa kutumia lugha ya Kiswahili ili kulinda uhai wa lugha hii inayotumiwa kwa kiasi kikubwa na wakazi wa Afrika Mashariki.

“Sote tunafahamu kuwa Kiswahili nyumbani kwake ni Tanzania,” alisema Chissano katika hotuba yake aliyoitoa kwa kiasi kikubwa kwa Kiswahili. “Hivyo, juhudi kama hizi za kutambua mchango wa wadau wa maandiko bunifu kwa lugha ya Kiswahili ni kitu muhimu sana.” 

SOMA ZAIDI: Sifa Kedekede Zamwagwa Dunia Ikiadhimisha Siku ya Kiswahili

Kwa maoni yake, kiongozi huyo alisema kwamba ipo haja ya juhudi hizo kuendelezwa, akibainisha kwamba uhai wa lugha yoyote duniani ni kuwapo na machapisho yaliyoandikwa kwa lugha hiyo.

“Natoa wito kwa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la nchi wanachama, kuendeleza matumizi ya Kiswahili katika maeneo muhimu ya kiutawala na kijamii kwani Kiswahili ni tunu na utambulisho wa Afrika na Mwafrika,” Chissano alihitimisha.

Nyenzo ya utamaduni

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Profesa Kitila Mkumbo, alisema kwamba ni muhimu sana kwa nchi kuwa na watu wanaoandika kwani maandishi ni moja wapo kati ya nyenzo ya vita ya utamaduni. 

SOMA ZAIDI: Wadau wa Elimu Wahoji Ukimya wa Dira ya Taifa Katika Kutambua Nafasi ya Kiswahili Kwenye Elimu

“Kupitia maandishi, utamaduni unaweza kulindwa au kubomolewa,” alisema Mkumbo ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chama cha Mapinduzi – CCM). “Nyenzo mojawapo ya vita ya utamaduni duniani ipo kwenye maandishi. Na nchi zote ambazo zinahifadhi utamaduni wa nchi yao wapo makini sana watoto na jamii yao wanasoma nini.”

“Kwa sababu nyenzo ya propaganda ni kupitia vitabu, nyenzo ya kuendeleza, ama kuua, utamaduni ni kupitia kwenye vitabu,” aliongeza Mkumbo, moja kati ya wadau muhimu wa elimu Tanzania.  

“Kwa hiyo, nchi nyingi [ziko makini watoto wao wanasoma nini], hata nchi ambazo zinajifanya zina demokrasia sana,” aliongeza. “Wewe huwezi kutoka tu hapa, ukaenda Marekani, ukaweka kitabu chako maktaba. Hicho kitu hakipo. Lazima wajue [watoto wao] wanasoma nini.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts