Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, itakuwa na mechi muhimu ya kuamua hatima yake kwenye jaribio lake la kufuzu kwa mara ya tatu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) itakapokuwa mgeni wa Algeria Septemba 7 kwenye Uwanja wa Mei 19, 1956.
Tanzania inasaka pointi moja tu ili ijihakikishie tiketi ya kucheza fainali hizo, pointi ambayo itaiweka ju zaidi ya Uganda. Tanzania ina pointi saba, wakati Uganda ina pointi nne na iwapo itaifunga Niger katika mechi ya mwisho inaweza kuipiku Tanzania katika nafasi ya pili.
Ingawa Tanzania ina faida ya kuwa na tofauti ndogo ya magoli ya kufunga na kufungwa (-1), ikipata kipigo kwa Algeria tofauti hiyo itaongezeka kulingana na idadi ya mabao, wakati iwapo Uganda itashinda itapunguza tofauti yake ya kuanzia -3 na kuwa imara zaidi.
Taifa Stars inakwenda kucheza mechi hiyo kukiwa hakuna hamasa yoyote kwa mashabiki wa soka wa Tanzania, hasa kutokana na historia ya Waalgeria inapocheza nyumbani, matokeo ya mechi ya kwanza ya kipigo cha mabao 2-0, na ukimya wa kocha kuzungumzia kikosi chake.
Tangu kocha Adel Amrouche atangazwe kuwa kocha wa Taifa Stars ameongea na vyombo vya habari mara moja tu baada ya timu hiyo kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uganda, lakini akamtuma msaidizi wake kuzungumza na vyombo vya habari baada ya kutoka sare na Niger.
Kikosi alichotangaza kwa mara ya kwanza hakikuwa na majina ya mabeki wawili wa Simba, Shomari Kapombe na Mohamed “Tshabalala” Hussein na hivyo kuibua mjadala kwa mashabiki kutokana na utimamu waliokuwa nao wachezaji hao waliouonyesha wakati Simba ikisaka tiketi ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, na uzoefu wao, ukitilia maanani kuwa kikosi hicho kilikuwa cha kwanza kwake.
SOMA ZAIDI: Kukosa Uvumilivu Kunaigharimu Azam FC?
Ni kawaida kwamba makocha huwa hawawajibiki kueleza sababu za kuacha wachezaji kwenye kikosi cha taifa kwa kuwa walio nje ni wengi kuliko aliowaita. Lakini anapozungumzia wachezaji aliowaita, moja kwa moja anakuwa anazungumzia sababu za kuwaacha wengine.
Hakuwahi kuzungumzia lolote kati ya mawili hayo, lakini baada ya mechi ya Simba ya Ligi ya Mabingwa, kocha huyo Mualgeria alipigwa picha akizungumza na wachezaji hao wawili na baadaye akawaita kwa ajili ya mechi iliyofuata, kitu kilichoimarisha imani kuwa hakuhusika kikamilifu kuandaa kikosi cha kwanza.
Mashabiki kupoteza upendo
Kitendo cha kocha huyo kuwaacha tena wawili hao kimeibua tena mjadala, kiasi cha baadhi ya mashabiki kupoteza upendo kwa timu yao ya taifa. Mbali na Tshabalala na Kapombe, safari hii pia amemuacha Feisal Salum wa Azam, ambaye alimuita katika kikosi cha kwanza wakati akiwa hajacheza mechi yoyote kwa miezi minne.
Yote hayo yameibua maswali mengi kwa umma na kupoteza mapenzi na timu yao ya taifa. Na iwapo itakosa tiketi ya kufuzu, idadi ya mashabiki wasio na imani na Taifa, itaongezeka na itaweza kuvutia wachache uwanjani itakapokuwa inacheza mechi zinazofuata.
Si lazima sana kocha wa timu ya taifa azungumze na vyombo vya habari, lakini anawajibika kufanya hivyo kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuonyesha kuwaheshimu mashabiki au wananchi wa Tanzania, ambao kwa njia fulani ndiyo waajiri wake.
Maswali yanayokosa majibu ndiyo huibua sintofahamu kwa timu hiyo na iwapo matokeo yanakuwa mabaya, hali inazidi kuwa mbaya.
Katika siku za karibuni, kumekuwa na idadi ndogo ya mashabiki wanaokwenda uwanjani kuishuhudia Taifa Stars, na hata watu wanaovalia fulana za rangi ya timu hiyo ni ndogo, hali inayoonyesha kuwa hakuna mapenzi na timu ya taifa.
SOMA ZAIDI: Kanuni Mpya TFF Inaua Uchumi wa Wachezaji
Mitaani zinaonekana jezi za Simba na Yanga tu na ukiona mtu kavaa jezi ya Taifa Stars ujue ana uhusiano na watendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa maana kwamba hajainunua bali amepewa.
Mechi ya mwisho kucheza nyumbani iliweza kuvutia mashabiki baada ya wanasiasa kuweka hamasa ya kununulia tiketi mashabiki, wakiongozwa na raia namba moja, Rais Samia Suluhu Hassan. Kama wanasiasa wasingetia hamasa hiyo, kuna uwezekano uwanja ungekuwa mtupu. Hakuna anayewahamasisha kwenda uwanjani na kocha ametulia kimya, labda anasubiri matokeo ndiyo yazungumze.
Pengine Amrouche hana ratiba ya kuzungumza kila mara na vyombo vya habari na huenda TFF haimlazimishi kufanya hivyo.
Mpango wa mawasiliano
TFF inaweza kumlazimisha awajibike kwa Watanzania kwa kumpa mpango wake wa mawasiliano na umma unaoonyesha kuwa kabla ya kutangaza kikosi, ana wajibu wa kuzungumza na waandishi kuhusu mipango yake, matarajio yake, hali ya maendeleo ya timu, kuwasihi mashabiki wajitokeze na kuiunga mkono timu au kuzungumzia mipango ya kiufundi itakayoweza kuzalisha timu bora ya taifa.
Haya ndiyo mambo ambayo husababisha mashabiki waanze kuijadili timu ya taifa na kuona mwanga kidogo wa huko tunakoelekea. Hii ni kwa sababu mashabiki watakuwa wanajua sababu za timu kutofanya vizuri katika mechi zilizotangulia, marekebisho yaliyofanywa, na imani ya kocha kwa kikosi chake.
SOMA ZAIDI: Waziri Pindi Chana, Wizara Wasitekwe na Umaarufu wa Soka
Hapo kocha atakuwa anawajibika kwa Watanzania hata kama matokeo hayatakuwa mazuri. TFF inatakiwa imuonyesha Amrouche kuwa anawatumikia Watanzania na si watu wachache wenye mamlaka kwenye chombo hicho.
Kocha Marcio Maximo alifanikiwa sana katika kuhamasisha wananchi kuipenda timu yao na haikuwa ajabu kuona uwanja umejaa rangi ya bluu kila wakati timu ya taifa inapocheza.
Kujaa huko kwa mashabiki ni nguvu ya ziada kwa wachezaji, ambao hulazimika kufanya jitihada zote kufurahisha umati ulioacha kazi zao kwa ajili ya kwenda kuwaangalia. Hali hii kwa sasa haipo. Kuna mpango gani kwa TFF kuhakikisha hamasa ya mashabiki kwa timu yao ya taifa inarudi?
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.