Mafanikio ya timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, ya kufuzu kucheza fainali zijazo za Mataifa ya Afrika, yamepokelewa na zomeazomea dhidi ya wachambuzi ambao walihoji sababu za kutoitwa kwa nyota watatu.
Ni Mohamed “Tshabalala” Hussein, Shomari Kapombe na Feisal Salum ambao walikuwemo kwenye kikosi kilichoishinda Niger jijini Dar es Salaam, lakini hawakuitwa kwa mechi hiyo ya mwisho ya Kundi F dhidi ya Algeria iliyochezwa ugenini.
Masuala yao yamekuwa na utata tangu mwanzo. Mara ya kwanza, Feisal “Fei Toto”, aliitwa na kocha Amrouche, akiwa hajacheza soka la ushindani kwa takriban miezi minne. Wengi walihoji sababu za kuitwa kwa mchezaji ambaye hakuwa na utimamu wa mechi, au match fitness. Amrouche aliziba masikio na akamuanzishia benchi na kumuingiza mwishoni mwa mchezo.
Na kwa Kapombe na Tshabalala, kikosi cha kwanza kabisa cha kocha Amrouche hakikuwa na majina ya wawili hao, kitu kilichofanya wengi wahoji, nikiwemo mimi.
SOMA ZAIDI: Kocha Adel Amrouche Awajibike Kwa Watanzania
Nilihoji kwa sababu kwa wakati huo usingeweza kuzungumzia mabeki wa pembeni wenye uzoefu zaidi ya Kapombe na Tshabalala, ukitilia maanani kuwa wakati huo Simba SC ilikuwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mashindano ambayo yaliwapa utimamu wa mwili na uzoefu mkubwa.
Lakini baada ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Amrouche alipigwa picha akiwa anaongea na wawili hao, kitu kilichomaanisha kuwa kuna kitu alikuwa akiwaeleza ambacho angependa wakiongezee ndipo awaite. Na kweli. Katika mechi dhidi ya Niger akawaita na kuwatumia.
Kwa hiyo, kwangu binafsi, kocha Amrouche alishawaona, alishakaa nao karibu mazoezini na kwenye mechi na alishajua uzuri na udhaifu wao na wapi awatumie. Sikushangaa alipotangaza kikosi bila ya kuwajumuisha nyota hao watatu.
Mijadala ya wachambuzi
Kitendo chake kiliibua mijadala mingi kwa wachambuzi, wengine wakisema alitakiwa ajitokeza hadharani kuzungumzia sababu za kuwaacha nyota hao watatu. Nilijua asingefanya hivyo kwa kuwa makocha wa timu za taifa hupenda kuzungumzia wachezaji wanaowaita tu kwa kuwa asiowaita ni wengi na hivyo hawezi kuzungumzia kila mchezaji ambaye hajamuita.
Lakini hakuna aliyejua kocha huyo raia wa Algeria atatoa majibu ya aina gani, hadi baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa mwisho wa Kundi F kwa sare ya bila kufungana, matokeo ambayo yameipa Tanzania tiketi ya kwenda Ivory Coast mwezi Januari kushindana na mataifa mengine makubwa barani Afrika yaliyofuzu.
SOMA ZAIDI: Kukosa Uvumilivu Kunaigharimu Azam FC?
Kwa nafasi ya Kapombe, Amrouche alianza na Dickson Job, mmoja wa mabeki wenye nidhamu ya kufuata mbinu na juu yake akamuweka Haji Mnoga, ambaye ana uwezo wa kucheza kama beki wa pembeni na beki wa kati.
Alikuwa anajua kuwa Algeria, ambayo ilichezesha vijana wengi, ni hatari upande wa kushoto na hupata mabao yake kwa mipira ya krosi. Mnoga alifanya kazi kubwa ya kuziba eneo la kulia wakati Job alipoingia kati kulinda lango.
Novatus Dismas alicheza namba ya Tshabalala upande wa kushoto. Watatu hao walionyesha nidhamu kubwa ya mbinu ya mchezo na ni kwa nadra sana walipanda mbele kwenda kuongeza nguvu katika mashambulizi, na isitoshe hakukuwa na haja ya kushambulia katika mechi ambayo Algeria anacheza nyumbani.
Ni dhahiri kuwa pamoja na uzuri wa Kapombe na Tshabalala, mechi hiyo haikuhitaji ustadi wao wa kushambulia wakati wote kwa kuwa Algeria ni wazuri sana kwa mashambulizi ya kushtukiza na isitoshe timu ilikuwa inahitaji sare tu hivyo ingekuwa ni kujihatarisha kujaribu kushambulia wakati wenyeji hawajatangulia kufunga.
Nafasi ya Fei Toto, ambaye bado hajajihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha taifa, alicheza Bajana, kiungo anayesumbuka wakati wote kuziba mianya inayoweza kusababisha hatari na juu yake alikuwepo Mzamiru, mchezaji mwingine anayejishughulisha sana uwanjani.
Nje alikuwepo Jonas Mkude na Himid Mao. Mkude huwa hachezi mbali na eneo la kati mbele ya mabeki wake na hivyo angeweza kuingia wakati wowote kama Bajana angepata tatu, wakati Himid anacheza sana kwa kufuata maelekezo na hata alipoingia mwishoni mwa mchezo alionyesha nidhamu hiyo ya kutulia eneo alilopewa.
SOMA ZAIDI: Kanuni Mpya TFF Inaua Uchumi wa Wachezaji
Na pamoja na ustadi wa Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca katikati, ngome ya Taifa Stars ililindwa vyema kwa staili hiyo kiasi cha kuruhusu shuti moja tu lililolenga bao. Hicho ni kiwango kizuri sana dhidi ya Waarabu nyumbani kwao na tuombe kuwa kiwango hicho kitaongeza uzoefu kwa wachezaji wetu ili wajue zaidi nidhamu ya kucheza ugenini.
Majibu tosha
Kwa hiyo, Amrouche alikuwa ametoa majibu tosha kwa waliohoji sababu za kutowaita Kapombe, Tshabalala na Fei Toto. Si kwa sababu viwango vyao vimeshuka, la hasha. Bali kwa sababu ya mahitaji ya mchezo na staili yao ya uchezaji.
Na isitoshe, kumuita mchezaji mzoefu wakati huna mpango wa kumtumia, ni kujitwisha mzigo mkubwa katika kufanya maamuzi kiasi kwamba unaweza kulazimika kumtumia kwa hoja ndogo sana. Zaidi ya yote, unaweza kulazimika kumtumia kwa sababu ya shinikizo kutoka sehemu mbalimbali.
Kungeweza kutokea hoja kwa nini kocha amchezeshe Dickson Job, ambaye kiasilia ni beki wa kati na kumuacha Kapombe, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akicheza upande wa kulia, licha ya ukweli kwamba kiasilia ni beki wa kati.
Halikadhalika, kwa Fei Toto hoja ingekuwa kama hiyo, kwamba wakati alikuwa hajacheza kwa miezi minne aliitwa Taifa Stars, lakini sasa amecheza na anaongoza kwa ufungaji, anaachwa benchi.
SOMA ZAIDI: Waziri Pindi Chana, Wizara Wasitekwe na Umaarufu wa Soka
Busara ilikuwa kama humtumii Fei Toto, Kapombe na Tshabalala kutokana na staili yao ya uchezaji, basi ni bora usiwaite kabisa hadi pale utakapowahitaji kulingana na mchezo unaofuata.
Na natumaini kwamba huo haukuwa mwisho wa Kapombe, Tshabalala na Fei Toto kuitwa na Amrouche. Lakini kama kuna maelekezo kocha huyo amewapa, ni muhimu kwa wachezaji hao kufanyia kazi maelekezo yake ili waitwe tena kupeperusha bendera ya nchi.
Wakati mwingine ni muhimu kuwaachia wataalamu wafanye kazi kulingana na mahitaji ya taaluma zao kuliko kuanza kuwapa maelekezo kwa kutumia ufahamu tunaoupata kwa kusoma Google. Kunahitajika kitu cha ziada kujua mahitaji ya kitaalamu.
Binafsi, naona Amrouche ametoa majibu safi kwa waliohoji bila ya kufungua mdomo wake.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.