Kabla ya anguko la uchumi wa viwanda muongo wa tatu hadi wa nne katika karne ya 20, ambalo kwa kimombo lilikuja kujulikana kama Great Depression, mwishoni mwa karne ya 19, Marekani ilikumbwa na kitu ambacho wachumi hukiita commodity glut.
Tafsiri yake ni wingi wa bidhaa, au malighafi, kuliko mahitaji. Viwanda vilizalisha kuliko mahitaji, ikawa ndiyo mwanzo wa elimu ya masoko, kwamba ni muhimu kwa ugavi na mahitaji viende sawia. Vilevile, pawepo mzani wa bei na upatikanaji wa bidhaa, au demand curve kama wasemavyo wataalamu.
Mwanasayansi ya siasa, Profesa Stanley Kelley Jr, katika kitabu chake Professional Public Relations and Political Power cha mwaka 1956, alitambulisha msamiati political marketing, au masoko ya kisiasa, kwa tafsiri isiyo rasmi.
Kisha, gwiji wa elimu ya masoko wa Marekani, Philip Kotler, alitafsiri nadharia ya masoko ya kisiasa kuwa ni mahitaji na matamanio ya jamii kisiasa. Mwanasiasa anapaswa kujielekeza kwenye mahitaji na matamanio ya watu kwa sababu hilo ndiyo soko lake.
Kujitafuta
Safari ya mwanasiasa kujiundia soko lake husindikizwa na mapito ya kujitafuta. Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa na Wadau wa Demokrasia, imetoa ishara kuwa sasa kiongozi huyo anajitafuta upya.
Hotuba yake hiyo ya Septemba 11, 2023, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), imemtofautisha na Samia mwenye sauti ya upole, aliyezoeleka na kumleta mpya.
Rais Samia aliwahi kusema mwenyewe kuwa hahitaji kuongea kwa vishindo ili ujumbe wake ufike. Hata hivyo, nyakati zinabadilika. Hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa siyo tu alihutubia kwa vishindo, bali pia alisimama pembeni ya kitovu cha uvumilivu.
SOMA ZAIDI: Sakata la Tanga Cement na Upande Mwingine wa Rais Samia
Je, ule upole na uongeaji wake wenye nakshi za utulivu ndiyo hulka yake? Kama ndivyo, basi hulka imebadilika. Ikiwa alikuwa akijitahidi kuuishi uvumilivu, basi ama uvumilivu umemshinda au amechoka kujitahidi.
Endapo nyakati zilizopita alikuwa anaficha kucha, ameamua kuyaacha makucha wazi. Anavyoonekana, Rais Samia yupo tayari kumrarua yeyote ambaye hatakwenda naye vema. Samia wa sasa si yule!
Aprili 2023, Rais Samia alipopokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hesabu za mwaka 2021-2022, kwa mara ya kwanza alionesha ‘umbogo’ wake. Alichukizwa na ubadhirifu na udanganyifu wa wasaidizi wake Serikalini.
Kutoka ripoti ya CAG hadi nyongo aliyotema kwenye mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa, bila shaka Rais Samia hawezi tena kusema “siyo mpaka nizungumze kwa vishindo ndiyo ujumbe ueleweke.”
Kumbe, si wakati wote uzungumzaji wa vishindo ni utashi, wakati mwingine inakuwa siyo hiyari. Yaliyojaa kifuani, yanaweza kumtawala mzungumzaji, matokeo yake mdomo ukaruhusu maneno ambayo hayakuwa kwenye mpangilo.
SOMA ZAIDI: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Mkataba wa DP World: ‘Kuna Makosa ya Kimkakati’
Hotuba ya Rais Samia iligusa vipengele nane: Mapendekezo ya Kikosi Kazi; demokrasia; mikutano ya hadhara; uhuru wa maoni; Katiba; mmomonyoko wa maadili; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025; na Dira ya Maendeleo 2025-2050.
Tafsiri tofauti
Japokuwa alitaja vichwa husika, Rais Samia alikuwa akihama mara kwa mara na kujielekeza kuwashughulikia aliowaita “watukanaji.” Yupo mtu muda huu anasema Rais Samia alitoa hotuba mbaya.
Mwingine anawaza, mbona siku zote alizungumza kwa upole na ustaarabu mwingi. Yupo ambaye atakumbusha uhusika wa Samia Bunge la Katiba 2014: mwanamke mtulivu, mvumilivu, mkomavu na mstahimilivu.
Atakuwepo mwenye kumhukumu Samia kwa sababu alidhihirisha hasira. Hapo kuna somo la mwasisi wa kanuni ya uongozi ya Peter Principle, Laurence Peter, aliyefariki dunia mwaka 1990.
Peter aliacha wosia, akisema: “Speak when you are angry, and you’ll make the best speech you’ll ever regret.” Kwa Kiswahili, alisema: “Zungumza ukiwa na hasira, na utatoa hutuba bora kabisa ambayo utakuja kuijutia.”
SOMA ZAIDI: Rais Samia, Tunaomba Utuachie Kitabu Chenye Hadithi Nzuri
Hekima nyingine zinatoka kwa Rais wa Tatu wa Marekani, Thomas Jefferson, aliyewahi kusema: “When angry, count to ten before you speak. If very angry, count to one hundred,” akimaamanisha, “Ukiwa na hasira, hesabu mpaka kumi kabla hujazungumza. Kama una hasira sana, hesabu hadi 100.”
Hakosekani wa kusema kuwa Rais Samia amevumilia mengi. Sakata la Bandari lilipoibuka, alisakamwa kuwa yeye ni Mzanzibari lakini ameuza bandari za Watanganyika. Je, hakuumia kwa mashambulizi hayo?
Kabla ya kuunda Tume ya Mipango, Rais Samia aliomba watu wapendekeze majina ya wale ambao inaonekana wanafaa. Taifa linajengwa moja, alisema, badala ya wengine kukosoa tu, kama wana uwezo na mawazo mazuri, basi watumike kwa masilahi ya nchi.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Tanzania Bara), Tundu Lissu, alipotakiwa kutoa maoni kuhusu ombi hilo la Rais Samia, alijibu, “Hiyo akili ni matope.” Ni kosa kubwa kuamini kwamba hilo jibu halikumuumiza Rais Samia.
Hakuna binadamu mwenye uvumilivu wa kudumu. Hata ajaaliwe moyo wa subira kiasi gani, zipo nyakati atatetereka. Hivyo, tukubali kuwa Rais Samia alitoa hotuba akiwa mwenye jazba, ila usisahaulike uchokozi dhidi yake.
Hofu
Hofu yangu ndani ya hotuba ya hasira ya Rais Samia ni maneno aliyotumia, kama vile hakuna uhuru wa maoni usiyo na mipaka. Ni kweli, ila changamoto ni tafsiri ya mipaka. Vilevile, mkazo wake kuwa mchakato wa Katiba lazima uanze na elimu.
Mtangulizi wa Rais Samia, John Magufuli, aliwaambia waandishi wa habari, “Msidhani mna uhuru huo.” Kuhusu Katiba Mpya, hayati Magufuli aliwaomba wananchi wamwache kwanza afanye maendeleo. Samia yeye anataka aachwe kwanza atoe elimu ya Katiba.
SOMA ZAIDI: Kauli ya Samia Kwamba Alitofautiana na Magufuli Kwenye Mambo Mengi Inatufundisha Nini?
Bila kupotosha maana, alichokisema Rais Samia kuhusu watu kutoijua Katiba, na wengine kukosa utiifu wa Katiba, nakubaliana naye. Hata hivyo, hapaswi kutumia kigezo hicho kama mwavuli wa kuchelewesha mchakato.
Kuanzia onyo la uhuru wa maoni hadi Katiba, jumlisha ukali wake alipohutubia Baraza la Vyama, ni dhahiri Rais Samia ameanza kujitafuta upya ili kusimika soko lake la kisiasa; chondechonde, asijipate katika mtindo wa Magufuli, akaminya demokrasia na kufuta jitihada za kupata Katiba Mpya.
Namkumbusha, nadharia ya masoko ya kisiasa inataka mwanasiasa akidhi mahitaji na matamanio ya jamii. Akifanikisha Katiba, Rais Samia atajiuza vema na kutanua soko lake kisiasa. Katiba ni mahitaji na matamanio ya Watanzania!
Luqman Maloto ni mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thisluqman@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.