Ni kitu cha kusikitisha kuona watoto wadogo kabisa wakiwa vijiweni, kwenye vibanda umiza, au barabarani, wakizurura pasipo uangalizi wa mtu yeyote, kwa kudai eti wanacheza.
Ingawa kitaalamu mtoto anahitaji muda wa kutosha kucheza kwa sababu michezo ni muhimu kwa afya na ukuaji wake, mtoto anatakiwa kucheza kwa wakati maalum, hasa mchana na katika mazingira yanayofaa, akiwa chini ya uangalizi makini wa wazazi, ama wanajamii.
Wazazi na walezi tunajukumu la kumkinga mtoto dhidi ya aina zote za vitendo vya kikatili ambavyo huweza kuathiri mfumo wa ukuaji na maendeleo yake kiakili, kimwili, na kisaikolojia.
Siku zote tunalenga kumlinda mtoto kwa kuangazia masuala mbalimbali yanayoweza kuhatarisha ustawi wake. Kitaalamu, mtoto, tofauti na mtu mzima, anatakiwa kuwa nyumbani mapema na kulala mapema ili kukua vizuri.
Mtoto akiachwa kuzurura hadi usiku kwanza muda wake wa mapumziko unapungua na mitaani huko ndipo anapojifunza tabia zisizofaa kwa umri wake, ambazo mzazi ni vigumu kurekebisha punde unapozigundua.
SOMA ZAIDI: Fahamu Namna Unavyoweza Kusuluhisha Ugomvi Baina ya Watoto Wako
Wakati mwingine unakuta watoto wa shule ya msingi, na hata wa sekondari, wakiwa mitaani wanacheza michezo mbalimbali, huku wakiwa bado wamevalia sare za shule, muda ambao wanatakiwa kuwa darasani.
Wengine hutumia muda huo kwenda kwenye vibanda vya video, maarufu kama vibanda umiza, kwenda kwenye mageto na baadaye taratibu husahau kabisa suala la shule na kuanza kushinda vijiweni.
Wazazi kubanwa na majukumu na kukosa muda wa kutosha wa kuwasimamia watoto wao ni moja kati ya vichocheo vya watoto kuzurura mitaani. Pia, tunaweza kujiuliza uko wapi ule u-Tanzania wa kusema mtoto wa mwenzio ni wako?
Leo hii awe mzazi au mwanajamii akishuhudia suala hili hakuna hatua inayochukuliwa kuwakanya watoto hawa, na hii ni kwa sababu tumepoteza ujamaa, ushirikiano, na upendo tuliokuwa nao kipindi cha nyuma kama jamii.
Zamani, malezi yalifanywa jukumu la lazima kwa kila mwanajamii kwa makusudi makubwa, ikiwemo kutambua kuwa watoto ndiyo warithi wa jamii husika na wanaandaliwa kuwa wazazi wa baadaye.
SOMA ZAIDI: Ifahamu Nguvu ya Maneno ya Mzazi, Mlezi Katika Vipaji vya Mtoto
Ili tuwe na taifa makini, tunahitaji mabadiliko katika malezi. Tamaduni zetu zililipa suala la malezi kipaumbele stahiki kwa kuwajengea mazingira rafiki yenye kuzingatia ukuaji na maendeleo bora ya watoto, inabidi tuzirudie.
Wazazi tusijisahau sana katika suala la uangalizi wa watoto wetu; tunatakiwa kutenga muda wa kuketi na watoto wetu, tukizungumza nao na kuwakanya baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuwa hatarishi kwao.
Pamoja na kwamba kuna sababu za mabadiliko ya kiuchumi, ambazo zinatufanya kujikita zaidi katika kutafuta kipato cha kujikimu, muongozo na usimamizi wa watoto wetu unahitajika katika maisha ya watoto tulionao.
Vilevile, unaweza kutengeneza mazingira rafiki ya ukuaji wa mtoto kwa kumpangia ratiba ya majukukumu yake na kumzoesha kuifuata ratiba hiyo tangu umri mdogo takriban miaka miwili ili kumuepusha na uzuraraji holela.
Hapa atajifunza uwajibikaji na umuhimu wa kutunza muda katika kukamilisha majukumu uliyompangia.
SOMA ZAIDI: Mahusiano Mazuri ya Wazazi ni Muhimu Katika Malezi ya Watoto
Mpe muda mtoto atembeleane na kucheza na wenzake, huku ukifuatilia mwenendo wa michezo yao na wasicheze mbali na maeneo ya nyumbani, na ikiwezekana, unamsindikiza au unahakikisha ana mtu wa kumuangalia.
Hii itasaidia kubaini mabadiliko katika muenendo wa maisha ya mtoto kwa kusikiliza kile wanachokiongea na kama kuna kile kisichofaa, unamkosoa na kumuelekeza kwa maneno.
Labda ni wakati sasa tuanze kujiuliza maswali kama jamii, ni namna gani tutaweza kujenga taifa la kesho lilothabiti? Ni tabia gani Watoto wetu, pamoja na vijana, wanatakiwa wazishikilie?
Tabia hafifu muda mwingine jamii inakua imeziruhusu ama kwa kuzilea na mara nyingine bila ya kuzikemea. Zitakoma vipi? Inawezekana kabisa kulea watoto na jamii yenye maadili na jukumu hili linaanza na mimi na wewe. Inawezekana!
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.