Taifa la Uingereza, kipindi cha Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ilianzisha mpango wa Serikali kuendelea na majukumu yake muhimu hata kama nchi ipo kwenye majanga, ukipewa jina la kimombo Continuity of Government, au COG kwa kifupi.
Mpango huo uliivusha Uingereza salama katika mambo mengi, kubwa lao likiwa ni hilo la vita. Mnamo mwaka 1940, Jeshi la Kifalme la Uingereza, lilidhibiti vema makombora ya anga kutoka Ujerumani, yaliyoitwa Luftwaffe.
Kwa hapa kwetu Tanzania, kukosekana kwa COG, ambayo inaweza kutafsiriwa kama Mwendelezo wa Serikali kwa Kiswahili, ni tatizo ambalo kwa kiasi kikubwa limetufanya kutofika popote. Kutoka Rais hadi Rais na waziri hadi waziri, mambo mengi yanaishia njiani.
Matokeo Makubwa Sasa ya Jakaya Kikwete ilikutana na kifo asilia baada ya kumpisha John Magufuli. Wanafunzi wa Diploma Maalum za Ualimu wa Sayansi, walifukuzwa bila huruma Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Magufuli alipoingia madarakani.
Mipango ya Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Sekondari (MMES) haikutekelezwa kama ilivyopaswa, pale Benjamin Mkapa alipokabidhi Ikulu kwa Kikwete, kisha naye alipompa majukumu ya Uwaziri wa Elimu, Margaret Sitta baada ya Joseph Mungai.
Tatizo sugu
Agosti 3, 2017, Mkapa alisema kuwa tatizo sugu Afrika ni utawala mpya kuacha kila kitu kilichofanywa na uongozi uliotangulia. Mkapa, aliyefariki Julai 24, 2020, aliyasema hayo alipokuwa kwenye mkutano wa Jukwaa la Uongozi Afrika, au African Leadership Forum, Kigali, Rwanda.
Kwenye kongamano hilo lililopewa utambulisho wa Financing Africa’s Transformation for Sustainable Development, yaani kufadhili mabadiliko ya Afrika kwa maendeleo endelevu,
Mkapa aligusia kwamba wakati wa uongozi wake walijitahidi kufikia sekta isiyo rasmi na kuirasimisha, kitu ambacho kiliwasaidia sana watu wa makundi husika.
Mkapa, aliyeioongoza Tanzania kati ya mwaka 1995 na mwaka 2005, alisema kwamba tatizo la Afrika ni mabadiliko ya utawala, kwamba utawala mpya unapoingia madarakani huacha kila kitu kilichoanzishwa na kufanywa na uongozi uliotangulia.
Alichokilalamikia Mkapa kilimkasirisha pia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwamba Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, iliacha hata yale mazuri ambayo yalifanywa katika Serikali ya awamu ya kwanza.
Tafsiri hiyo ni kuwa Rais Mwinyi alianza upya baada ya Mwalimu Nyerere, ni kama ambavyo Mkapa aliingia na Serikali mpya, vivyo hivyo Kikwete na Magufuli. Wakati Mkapa anaondoka madarakani, aliacha Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA).
Kalenda yake ya utekelezaji ilikuwa miaka mitano, yaani kuanzia mwaka 2005 mpaka 2010. Kwa mantiki hiyo, MKUKUTA ulitakiwa kutekelezwa ndani ya muhula wote wa kwanza wa Rais Kikwete.
Oktoba 2004, Serikali ya Tanzania iliingia makubaliano na Serikali ya Norway, kuhusu kufanya mapitio ya biashara na rasilimali za wanyonge ili kuzifanya ziwe rasmi. Mapitio hayo ndiyo yaliyozaa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).
SOMA ZAIDI: Kinachoweza Kukwamisha Mipango ya Serikali Kukabiliana na Njaa
Kuhusu MKUKUTA, Mkapa alikaa na baraza lake Hoteli ya Ngurdoto, mtaalamu kutoka nchini Peru, Jens Clausen, akawapiga msasa mawaziri kuhusu njia na mbinu sahihi za kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa mazingira ya Kitanzania.
Clausen pia ndiye alikuwa kiongozi wa timu ya wataalamu waliofanya mapitio ya rasilimali na biashara za Watanzania kisha kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuzirasimisha. Pitia miaka kumi ya JK, huoni utekelezaji unaoridhisha wa MKUKUTA wala MKURABITA!
Dola za Kimarekani milioni saba, ambazo kwa sarafu ya wakati huo zilikuwa ni sawa na takribani Shilingi bilioni 9.1, zilitumika kwa ajili ya MKURABITA peke yake. Kutotekelezwa kwa mapendekezo ya wataalamu kuhusu MKURABITA, maana yake fedha hizo zilitumika bila faida yoyote!
Rais Samia Suluhu Hassan, tangu aingie madarakani hapo Machi 19, 2021, amejitahidi kuendeleza miradi mikubwa ya mtangulizi wake, Magufuli, aliyefariki Machi 17, 2021. Kuanzia Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), Reli ya Standard Gauge (SGR), nakadhalika.
Baraza la Mawaziri
Hata hivyo, tatizo lipo kwenye mabadiliko ya mara kwa mara ya Baraza la Mawaziri, uamuzi unaonipa mashaka kwamba kwa kufanya hivyo, Rais Samia anasababisha kukosekana kwa mwendelezo katika utendaji kazi wa Serikali yake.
Waziri, au Katibu Mkuu wa wizara, anapoingia ofisini, anakuta mipango ya mtangulizi wake, naye anaweka maono yake na kuanza utekelezaji; anapoondolewa na kuingia mwingine, inabidi maono ya kiutendaji yabadilike.
Katika hali hiyo, kumekuwa na tatizo la viongozi wengi kutoheshimu mawazo ya watangulizi wao. Matokeo yake, kiongozi mpya anapoingia na kila kitu kinaanza upya.
Madhara ya kukosekana kwa mwendelezo wa kiutendaji Serikalini ni makubwa. Ukiongea na mawaziri wa zamani, au hata waliopo lakini waliohamishwa mara kwa mara, watakwambia maumivu yao ya kukatishwa njiani kabla ya kutimiza malengo ya kiutendaji.
Madhara mengine ni Serikali hukosa unyoofu, au consistency kwa kimombo. Kila mara Serikali inabadilika, matokeo yake inakosekana tafsiri inayoeleweka kuhusu uelekeo wa wizara kwa wizara na Serikali yote.
Matamko
Bahati mbaya, nchi hii viongozi wanapenda kutoa matamko. Waziri huyu analeta matamshi haya kwa umma, kesho akiingia mwingine anazungumza lugha tofauti.
Mathalan, Wizara ya Nishati, alikuwepo Waziri Medard Kalemani, aliyesema bei ya kuunganisha umeme nchi nzima, mahali popote, ni Shilingi 27,000; alipobadilishwa na kuingia January Makamba, akasema bei hiyo ni kwa vijijini tu!
Tena, January akasema kabla yake Wizara ya Nishati ilikuwa inaendeshwa kibabe na kwa matamko, kuliko kusikiliza wataalamu, akiahidi kwamba, kwa kushirikiana na wataalamu wa wizara, tatizo la umeme lingekuwa historia ifikapo mwaka 2025.
SOMA ZAIDI: Maswali Fikirishi Kuhusu Falsafa ya 4R ya Rais Samia
January ameondolewa, tatizo la umeme bado lipo, na hakuna dalili kwamba halitakuwepo ifikapo 2025!
Je, unyoofu wa malengo utakuwepo Wizara ya Nishati baada ya kuingia Doto Biteko? Nishati ni mfano tu, lakini wizara nyingi hali ni hiyo hiyo. Wizara ya Elimu, Kilimo, Maji, Maliasili na Utalii, zimekuwa na manung’uniko mengi.
Rais Samia hakatazwi kufanya mabadiliko, ila anahitaji kuanzisha COG yake kwenye Baraza la Mawaziri, itakayoelekeza kwamba kila Waziri, au Katibu Mkuu mpya, akiingia ofisini, lazima aendeleze aliyoyaacha mtangulizi wake.
Kama hayafai kuendelezwa, ripoti iandikwe, Baraza la Mawaziri liridhie; isiwe matakwa, au utashi, binafsi ya Waziri au Katibu Mkuu.
Vinginevyo, kila Rais atakapofanya mabadiliko, atasababisha wizara kuanza upya. Matokeo yake, Serikali haipigi hatua, na nchi itakwama, na lawama, kwa kiwango kikubwa, zitamrudia yeye mwenyewe kama kiongozi wa nchi.
Luqman Maloto ni mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thisluqman@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.