The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Maswali Fikirishi Kuhusu Falsafa ya 4R ya Rais Samia

Je, mageuzi yanayotafutwa Tanzania ni kwa maslahi ya wanasiasa tu au kwa maslahi ya kila Mtanzania?

subscribe to our newsletter!

Nitapita kwenye zile zile 4R za Rais Samia Suluhu Hassan kuibua maswali ambayo yoyote atakayejisikia kufanya hivyo, tutakapopewa fursa na mwenyekiti, anaweza akachangia katika maswali hayo, ama kuibua maswali mengine ambayo yatatuongoza katika kujenga taifa letu jipya.

Suala la kwanza ni la maridhiano. Maridhiano ni muhimu sana, na maridhiano yanaleta uponyaji. Lakini lazima tujiulize, tunaponya nini na nani wanahusika katika huo uponyaji? Nani alifanyiwa nini hivyo anastahili huo uponyaji ili aweze kupata ahueni na yeye aweze kuchangia katika mustakabali wa taifa letu?

Tumepitishwa kwenye historia yetu na kuoneshwa kwamba hata hizi tofauti tulizonazo sasa, nyingine si mpya; zimeanza tangu kabla ya ukoloni, na zimeendelea mpaka sasa. Kwa hiyo, lazima hilo tuweze kulizingatia. 

Na cha muhimu kabisa, hoja yangu ninayoiweka hapa ni kwamba historia yetu lazima tuiseme kwa ukamilifu wake, na swali la kujiuliza hapa ni kwamba je, historia yetu, jinsi ambavyo tumekuwa tukiifunza na kuambizana, imekuwa ni kwa mtindo wa funika kombe mwanaharamu apite, au imekuwa ni historia kwa maana ya kwamba tunajifunza kutoka kwenye ile methali inayosema mficha maradhi kifo kitamuumbua

Kwa hiyo, hilo ni suala ambalo lazima tujiulize.

Na hapa nitatoa mifano ya nchi takribani tatu. Tunafahamu kuhusu yale mauaji ya Kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994. Na ikaanzishwa ile Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda (ICTR) ambayo Tanzania ndiyo tulikuwa wenyeji, Arusha. 

Ile Mahakama, katika kuleta yale maridhiano, na kuleta uponyaji, ina manufaa yake, na mafanikio yake ambayo yalifikiwa, lakini jamii ya Rwanda waliona kwamba wanahitaji kwenda zaidi ya kile ambacho kimepatikana katika Mahakama ile.

SOMA ZAIDI: Mustakabali wa Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar

Watu wanaoishi katika jamii kuna ambao walifanyiana vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu, nakadhalika, walichoamua wao sasa ni kurudi katika Mahakama zao za kijadi, na zimeweza kusaidia katika zoezi la uponyaji. 

Katika zile Mahakama za kijadi wanaongea kwa uwazi kabisa vitu ambavyo vinaumiza kabisa: nani alifanyiwa nini na nani na lini. Na ile inamsaidia yule ambaye alifanyiwa kile kitendo kama ni ndugu zake, jamaa zake waliuwawa, kuweza kupata uponyaji kamilifu. Tunajifunza nini kwa historia kama hiyo?

Ujerumani ya Hitler na yote yale ambayo yalitokea, wameimiliki historia yao na wanaisema kwa ukamilifu, na imewasaidia kuweza kusonga mbele. Taifa la Marekani na ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa aina tofauti tofauti, kuna mikakati ambayo wameifanya, lakini ukilinganisha na Ujerumani, ni kwa kiwango kidogo.

Marekani, ninaweza nikasema kwamba, wametumia utaratibu wa funika kombe mwanaharamu apite, ndiyo maana zile tofauti mpaka leo bado zipo. Ukatili, unyanyasaji, na ubaguzi unaendelea kuwepo. Kwa hiyo, na sisi tujifunze kutoka kwa wenzetu.

Ustahimilivu

Suala la pili la ustahimilivu, au resilience. Ustahimilivu ni muhimu sana. Tumeoneshwa hapa tulikotoka, tofauti zetu pale ambapo tulitofautiana, tukaumizana, tukajeruhiana, nakadhalika. 

Lakini mimi nataka kuongezea kwamba ustahimilivu pia ni muhimu kwa muktadha ambao tuko sasa na huko tuendako. Kuwa na ustahimilivu katika dunia ambayo ina mabadiliko mengi ni muhimu sana. 

Kuna mabadiliko ya kisiasa. Tumeona jinsi ambavyo kumekuwa na mapinduzi ya kijeshi katika nchi kadhaa hivi karibuni na wananchi wanashangilia na kuunga mkono yale mapinduzi. 

SOMA ZAIDI: Mwenezi Khamis Mbeto: CCM Ndiyo Baba wa Demokrasia Tanzania

Yale ni mabadiliko ambayo wananchi wanaonyesha kabisa hawana imani na demokrasia; kile kilichokuwa kinaitwa demokrasia hakikuwa kikiwaletea wao maendeleo na kuwafaidisha wao. 

Kwa hiyo, yale yaliyotokea wameyaunga mkono, wananchi wanashangilia mitaani katika baadhi ya nchi kwa yale mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika. Sasa mabadiliko hayo yanatulazimisha tuweze kuzingatia sana suala la ustahimilivu. 

Kuna mabadiliko mengine ya kijamii, kuna mabadiliko ya kiteknolojia, kuna mabadiliko ya kiuchumi, mabadiliko ya mazingira, nakadhalika. Siasa ina jukumu muhimu sana katika kutengeneza utaratibu wa namna ambavyo tutakaa na kujadiliana na kutengeneza mustakabali wetu wa baadaye. 

Lakini je, siasa zetu zikoje? Siasa zetu zinazingatia ustahimilivu ama hazizingatii ustahimilivu? 

Kingine cha muhimu katika suala la ustahimilivu ni kuzingatia kwamba kuna nyakati tutaenda mbele na kuna nyakati tutarudi nyuma; kuna nyakati tutakosea, kuna nyakati tutapatia, ni kujifunza. Cha muhimu ni kujifunza na siku zote kuweza kwenda mbele.

Mageuzi kwa nani?

R ya tatu inazungumzia mageuzi. Suala la muhimu sana kujiuliza katika haya mageuzi ni kwamba, mageuzi haya kwa maslahi ya nani? Je, ni kwa maslahi ya wanasiasa au kwa maslahi ya kila Mtanzania?

Rais Samia Suluhu Hassan, wakati wa ufunguzi wa mkutano huu hapo Septemba 11, 2023, alisema kwamba mchakato wa Katiba Mpya si wa wanasiasa peke yao. Hii itukumbushe kwamba lazima tuangalie raia wa kawaida anataka nini. 

Na hiyo kauli ya kukumbushana kwamba huu mchakato wa mabadiliko ya Katiba na michakato mingine iweze kuzingatia mahitaji na maslahi ya mwananchi wa kawaida; itusaidie kuweza kuona yale mageuzi tunayotaka kuyaleta, kweli yanagusa maisha ya wananchi wa kila siku?

SOMA ZAIDI: Je,  Zanzibar Inaweza Kuwa na ‘Mamlaka Kamili’ Ndani ya Jamhuri ya Muungano?

Kama yanagusa maisha ya mwananchi ya kila siku je, tumeonesha hiyo connection iko wapi na iko vipi? 

Mwananchi akisikia kwamba wanasiasa wanazungumzia marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi, marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, wanaona kabisa kwamba hawa wapo kwa ajili ya wao kujitengenezea fursa zao za kuingia madarakani, fursa zao za kubakia kuwa na uhalali, nakadhalika. 

Lakini hawazungumzii kupanda kwa gharama za maisha za mwananchi na kuoanisha kuona kwamba haya mageuzi yanagusa vipi ile hali ya mwananchi wa kawaida. 

Nani anashiriki katika kuleta haya mageuzi? Tukiangalia hii ni fursa adhimu tuko nayo. Hapa ndiyo washiriki ni wengi na Msajili wa Vyama vya Siasa alisema lengo lilikuwa ni washiriki 500 lakini wakafika 700. 

Katika hawa 700 waliofika, wangapi ni wanawake? Wangapi ni vijana? Wangapi ni watu wenye ulemavu? Takwimu zetu za sensa ya mwaka jana zinatuonesha nini? Je, tuliopo hapa, tulivyo humu ndani, tunaakisi matokeo ya sensa ya mwaka jana? 

Kama zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wana umri chini ya miaka 35 je, majority ya watu ambao wamo humu ndani wana umri gani? Tunapozungumzia mageuzi, ni nani tunamuacha katika hii michakato ya kuleta haya mageuzi? 

Vijana wako wapi? Je, tunajua wako wapi na wanafanya nini sasa hivi, wanawaza nini, au tunafanya haya huku tukiwa tumewaacha?

Kwa hiyo, lazima katika mageuzi tujiulize vilevile mageuzi kwa maslahi ya nani? Tunatumia taratibu gani kuleta hayo mageuzi na wale ambao ndiyo wengi na wale ambao ndiyo wanaathirika hasa na ile hali ambayo ipo na tunataka kuibadilisha, wako wapi? 

SOMA ZAIDI: Tutegemee Mageuzi Makubwa ya Kisiasa Tanzania 2023?

Wanashiriki katika haya mageuzi ama hawashiriki katika haya mageuzi? Na matumizi ya teknolojia vilevile. Wengi wetu ni vijana na wanawake ambao wanaweza kutumia teknolojia. Sisi tunatumia vipi hizo teknolojia? 

Kingine ambacho ningependa kuongezea hapa katika suala la mageuzi ni matokeo ya takwimu za taasisi ya Afrobarometer duniani ambayo zinaonesha kwamba wananchi wengi duniani wanapoteza imani kwa taasisi na mamlaka ambazo zimekuwepo. 

Iwe ni vyombo vya habari, iwe ni Serikali zao, iwe ni taasisi zisizokuwa za Kiserikali ambazo zimekuwepo kwa miaka mingi, wananchi wanapoteza imani kwa hizo taasisi, au hayo mamlaka. 

Kwa hiyo, tunapozungumzia mageuzi, ni lazima tuzingatie kwamba kama wananchi wanapoteza imani kwa hizo taasisi, ni mbinu gani m’badala tunaweza tukazitumia kuweza kuwashirikisha wananchi, hasa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ambao imani yao katika taasisi zetu inaenda ikipungua? Lazima tuzingatie sana hilo.

Ujenzi mpya

Kwenye R ya mwisho ya ujenzi mpya wa taifa, tumekumbushwa hapa tunu zetu: utu, umoja, udugu, maelewano, ushirikiano, pamoja na amani.

Nataka niulize swali angalau moja kwa kila tunu tulizonazo, na kujaribu kuchokoza wengine waje wazungumzie. Je, kwa sasa tukijitafakari, kinachotuongoza ni tunu yetu ya utu au ni tunu yetu ya uchawa? 

Uchawa, kwa mtazamo wangu, naona sasa imekuwa kama ni tunu. Tujiulize, tumetoka kwenye utu kwenda kwenye uchawa na itatupeleka wapi? 

Tukija kwenye umoja, tunatambua kuna nyufa nyingi katika umoja wetu. Tofauti nyingi tu iwe za kijinsia, iwe za itikadi, za vyama, iwe kitabaka, mwenye nacho, asiokua nacho, nakadhalika. 

SOMA ZAIDI: Yaliyowapatanisha, Kuwafarakanisha Serikali, Upinzani 2022

Hata Rais Samia alizungumzia watu kukashifiana kwa imani zao, kwa dini zao, hizi ni tofauti ambazo pia zipo. Je, umoja wetu bado upo kweli? Tunaongeleaje hizi nyufa ambazo zipo katika umoja wetu?

Udugu. Tukijiuliza ndugu yako ni nani? Je, ndugu yako ni yule unayefanana naye, kwa maana ya kwamba labda mko katika chama kimoja? Au ndugu yako ni yule ambaye mnafanana naye, labda mna jinsia moja, ama mko katika tabaka moja la kiuchumi, nakadhalika? Au ndugu yako ni kila Mtanzania?

Teknolojia imeibuka na mitandao ya kijamii na tunaona kabisa inazidi siyo kutuleta pamoja, kwa sababu hizi teknolojia zinatakiwa zitusaidie kupata taarifa na maarifa na habari kwa haraka na kutuunganisha na watu tofauti tofauti. 

Lakini tukiangalia, ukisema ukaangalie Twitter, uende ukaangalie sijui Clubhouse, unakuta kinachotokea ndo hizi zinazoitwa echo chambers, kwamba watu walewale, wenye mitazamo ileile, ndiyo wapo katika hiyo mitandao wanajumuika pamoja na kujadiliana. 

Ikatokezea tu mmoja amekuwa tofauti na wao, atasulubiwa vya kutosha, atapigwa ‘spana,’ na atatengwa. Kwa hiyo, tunapozungumzia undugu, tuangalie pia athari ya teknolojia. Tunazitumiaje, na jinsi ambavyo zinazidi kuonesha zile nyufa ambazo tunazo.

Mashirikiano na maelewano yapo chini sana na hasira za watu ziko juu sana. Tumefikia mahali ambapo inakuwa kana kwamba mtu anasema nikanyage kwa bahati mbaya nikulipizie kwa makusudi, yaani anakungoja tu. Ni kwa sababu hakuna maelewano, hakuna mashirikiano. 

Tunakosa ile imani ya kwamba huyu hiki alichokifanya inawezekana amekifanya kwa nia njema kwangu, embu nimpe fursa, nimsikilize, nione kama kuna jema katika yale anayoyafanya, ama kuyatenda.

SOMA ZAIDI: Hatua Tano Muhimu Kufikia Upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania

Lakini tumefikia mahali ambapo mtu kama ana utofauti na wewe, iwe ni kisiasa, iwe ni tofauti nyingine yeyote, unaona kama vile hakuna jema linaloweza kutoka kwa yule mtu.

Suala la amani kama tunu yetu, na tunu ya mwisho tuseme, amani maana yake nini? Je, tunaitumia amani kweli kujenga utu, umoja, undugu na mashirikiano, au tunatumia kauli za kulinda amani yetu kuweza kunyamazishana na kufunika kombe mwanaharamu apite?

Na kuna jingine la unyenyekevu, kwamba tuwe wanyenyekevu, tuwe na subira, ni kitu muhimu sana, ndiyo, lakini nani anapaswa kuwa mnyenyekevu? 

Je, ni kiongozi-mwanasiasa kuwa mnyenyekevu kwa raia, au ni raia ndiyo wanapaswa kuwa wanyenyekevu kwa viongozi na wanasiasa?

Baruani Mshale ni mtafiti na mtaalamu wa masuala ya sera kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Hii ni sehemu ya hotuba aliyotoa kama mchokoza mada kwenye mkutano wa demokrasia uliofanyika Dar es Salaam Septemba 12, 2023. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Big up. It is true that, people don’t trust organisation and their leaders eg village leaders and Parliaments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *