The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mustakabali wa Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar

Suluhisho sio kujiunga ama kutojiunga kwa ACT-Wazalendo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Suluhisho ni kufanyika kwa mjadala wa kina kuhusu tuhuma za kasoro za kimfumo zinazoibuka kila wakati wa uchaguzi na kuzifanyia kazi.

subscribe to our newsletter!

Picha ya kupeana mkono kati ya Amani Abeid Karume, Rais wa awamu ya nane wa Zanzibar na Maalim Seif Sharif Hamad, wakati huo Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi-CUF, huku wakitabasamu tarehe 5 Novemba 2009, ni moja wapo ya picha muhimu katika historia ya Zanzibar. Picha hio  ilisadifu na kuelelezea hatua za kutaka kuhitimisha karne nyingi za siasa za uadui na chuki visiwani Zanzibar. Ishara hii ya kupeana mikono baina ya wawili hawa ilishadidi maana nyingi katika muktadha wa siasa za Zanzibar. Michakato ya awali ya mazungumzo ya kuondoa mitafaruku iliyojikita katika historia ya siasa za rangi (racial politics) iliyochagiza Mapinduzi ya 1964 ilifeli. Kuibuka kwa makubaliano ya kiungwana (gentleman’s agreement) mwaka 2009 ilikua ni furaha kubwa kwa Wazanzibari wapendao amani na maendeleo. Makubaliano haya yalikuja kufahamika kama Maridhiano (reconciliation).

Mwaka wa 2010 ulikuwa ni mwaka muhimu sana kwenye historia ya Zanzibar. Mwishoni mwa mwezi wa Januari, 2010 kuliletwa Hoja Binafsi na aliyekuwa Mwakilishi wa CUF marehemu Abubakar Khamis Bakari kwenye Baraza la Wawakilishi. Hoja hiyo lilipendekeza marekebisho ya katiba ya Zanzibar ya 1984 ili kuongeza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Pamoja na mambo mengine, hoja hiii pia lilipendekeza kuundwa kwa nafasi mbili za Makamu wa Rais na kugawanywa kwa nafasi za uwaziri kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) baina ya vyama viwili vitakovyopata kura nyingi kwenye uchaguzi. Muhimu zaidi, hoja hii ilichangia katika kuweka wazi kwamba Zanzibar ni moja wapo ya nchi mbili kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ilikidhi haja ya Wazanzibari wengi walioona kwamba nchi yao imemezwa na Jamhuri ya Muungano, na kama Wanzazibari wengi wanavyoiita, Tanganyika. Wazanzibari walifanya kura ya maoni Julai 2010 kuidhinisha makubaliano ya kugawana madaraka kulingana na matokeo ya uchaguzi wa 2010. Matokeo ya kura ya maoni yalionyesha utayari wa Wazanzibari kuweka nyuma uadui na chuki uliotawala kwa muda mrefu. Asilimia 66.4 walipiga kura ya kukubali Maridhiano na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Kampeni na matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 2010 pia yalidhihirisha dhana na Maridhiano. Licha ya wasiwasi wa uhalali wa ushindi wa Ali Mohammed Shein wa CCM, dhana ya Maridhiano iliwalazimu CUF kukubali matokeo. Matokeo yalionyesha Ali Mohammed Shein alishinda kwa kura kiduchu kwa kupata asimilia 50.1 ya kura na Maalim Seif Shariff Hamad kupata asilimia 49.9.

Rais Shein alipokea nchi ambayo ilikua imesheheni ahadi ya matumaini, amani na mshikamano. Japo kugawanywa kwa madaraka kulikua kwenye ngazi ya uwaziri pekee, uhasama miongoni mwa watu ulipungua sana. Zamani kulikua na misemo ya “hatuzikani” baina ya wafuasi wa CCM na CUF. Chuki, ubaguzi na fitna zilitawala. Ila Maridhiano yalibadilisha mitazamo ya watu Zanzibar. Mfano mzuri ni mshikamano wa kipekee tuliouona pale meli ya MV Spice Islander ilipopata ajali Septemba 2011. Tulishuhudia mashikamo wa wananchi katika uokozi na pia uwajibikaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Tuliona pia maendeleo katika sekta mbali mbali za uchumi hasa Pemba, baada ya miaka mingi ya kutengwa.

Marekebisho ya Katiba na Kuanza kwa Mtanziko

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2010 alihutubia taifa kuhusiana na masuala mbali mbali. Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete aliainisha umuhimu wa katiba mpya nchi itakapokuwa inatimiza miaka hamsini ya Uhuru (Uhuru wa Tanganyika) mwaka 2011. Moja wapo ya mambo ambayo alisema katiba mpya itatatua ilikuwa ni sintofahamu na mikwaruzo katika muungano. Kuanza kwa mchakato wa katiba mpya, jambo ambalo lingeleta neema zaidi katika kufafanua sehemu ya Zanzibar katika muungano, kwa ajabu ndio ulikuwa mwanzo wa kuyumba kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mchakato wa kupokea maoni ya wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba kulianza kuchafua hali ya hewa visiwani Zanzibar. Mihemko na tofauti za vyama viwili vikuu vya CCM na CUF vilianza kuonekana tena. Licha ya kasoro zilizokuwa katika muundo wa SUK na zaidi nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika serikali, kulikuwa na maelewano na kuheshiminiana.

Katika mchakato wa kukusanya maoni, hususan kwenye suala nyeti la muundo wa muungano, vyama hivi viwili vilitofautiana. Wakati CCM walitaka mfumo wa serikali mbili kuendelea, CUF kilipendekeza muungano wa mkataba. Katika kipindi hiki tuliona kuibuka kwa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) almaarufu kama UAMSHO. Kikundi hiki, kupitia mihadhara kilizungumzia masuala mbali mbali likiwemo suala tata la utaifa wa Zanzibar (nationalism) – jambo ambalo liliwagawanya zaidi Wazanzibari. Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka 2013, alitangaza wajumbe watakao elekea Dodoma kwenye Bunge Maalamu la Katiba (BMK) kujadili mapendekezo ya Katiba Mpya (Rasimu ya Warioba). Wajumbe hawa walikuwa ni pamoja na wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge, pamoja na wajumbe wateule waliowakilisha asasi mbali mbali. Kuelekea Dodoma tulianza kuona migawanyiko ambayo ilichangia kuyumba kwa dhana ya Maridhiano. Mchakato mzima kwenye BMK ulisheheni vituko, vibwanga na hatimaye maoni ya wananchi kutupiliwa mbali baada ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutoka nje na kususia.

Uchaguzi wa 2015 na Kufa kwa Maridhiano 

Dhana ya Maridhiano ilikuwa imekufa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015. Licha ya kuwepo kwa SUK, kauli za chuki zilirudi. Kampeni zilikuwa tofauti na zile za mwaka 2010 wakati maridhiano ya kijamii yalikuwa. Katika hatua ambayo haitawahi kusaulika, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) chini ya mwenyekiti Jecha Salum Jecha, alifuta uchaguzi. Itakumbukwa kwamba hadi pale Jecha alipotangaza kufuta uchaguzi, matokeo ya majimbo 31 kati ya 54 yalishakwisha tanganzwa. Katika taarifa yake, Jecha alisema uchaguzi ulikuwa umegubikwa na kasoro nyingi na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi, ikiwemo jambo la kushangaza la kupigana kwa makamishna wa ZEC. Kilichofuata ni kuitishwa uchaguzi wa marudio Machi, 2016. Juhudi za suluhu na mazungumzo baina ya CCM na CUF zilishindakana. Hapa ndipo Maridhiano yalikufa. Maridhiano yalizikwa rasmi baada ya CUF kujitoa kwenye uchaguzi wa marudio jambo ambalo lilipelekea ‘ushindi’ wa kishindo wa CCM kwenye ngazi ya urais na Baraza la Wawakilishi. Zanzibar ilibaki bila Makamu wa Kwanza wa Rais baada ya uchaguzi wa 2016.

Rais Shein alipokea madaraka wakati Wazanzibari walikuwa wamoja. Kulikuwa na mshikamano zaidi ya kipindi chochote kile cha historia ya Zanzibar. Lakini Rais Shein ameondoka akiiacha utengano na simanzi miongoni mwa wengi. Hofu ilitawala uchaguzi wa mwaka huu wa 2020. Ripoti zimeonyesha watu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi, wengine kupigwa na kuteswa na kuumizwa. Wengine, ikiwemo wanasiasa, kukamatwa na kuzuiliwa na polisi. Matukio haya yameleta simanzi nyingi kwa wote. Wengi wameamua kutua nyoyo zao na kunyamaza wakitafakari.

Mtanziko wa ACT-Wazalendo: Je Wajiunge ama Wasusie?

Marekebisho ya Katiba ya Zanzibar (2010) kama nilivyoeleza awali yaliweka utaratibu wa SUK. Ibara ya 9 (3) inasema muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa. Ibara inayofuata inaendelea kutaja malengo na maamuru muhimu katika SMZ. Kwa kuwa chama cha ACT-Wazalendo kilipata asilimia 19 ya kura za urais na kushika nafasi ya pili, kwa mujibu wa katiba kinastahili kuwa kwenye SUK ikiwa ni pamoja na kutoa Makamu wa Kwanza wa Rais na pia kupata viti katika Baraza la Mawaziri katika SMZ. ACT-Wazalendo, walitanganza kutoridhika na mwenendo mzima wa uchaguzi na pamoja na maazimio mengine kutotambua matokeo ya uchaguzi. Baada ya maandamano waliyoitisha kugonga mwamba, ACT-Wazalendo wanajikuta katika mtanziko: Wajiunge ama wasijiunge na SUK.

Ndugu Hussein Mwinyi ambaye alishinda urais wa Zanzibar amekuwa akizungumzia Maridhiano tangu aapishwe. Katika hotuba yake baada ya kuaapishwa alitaja umuhimu wa Maridhiano katika kujenga ‘Zanzibar Mpya’. Alirudia kauli hiyo wakati akihutubia Baraza la Wawakilishi. “Ninaheshimu maridhiano na matakwa ya Katiba ya kushirikiana na vyama vingine vya siasa katika kuendesha serikali na niko tayari kuyatekeleza maridhiano kama katiba ya Zanzibar inavyoeleza,” alieleza Rais Mwinyi. Kwa upande wao, ACT-Wazalendo kimesema kinatafakari kuhusu kujiunga na SUK. “Kamati kuu (ya Chama) iliamua tufanye tafakuri ya kina,” alisema Seif Shariff Hamad.

Maridhiano ni Imani, Siyo Maneno

Rais Mwinyi alifanya uteuzi wa Baraza la Mawaziri na kuacha nafasi mbili wazi. Nafasi hizi zitazibwa na ACT-Wazalendo endapo watajiunga na SUK. ACT-Wazalendo wako katika hali ya mtanziko (dilemma). Kuna minong’ono miongoni mwa wafuasi wa ACT-Wazalendo kwamba endapo ACT-Wazalendo watakubali kujiunga na SUK itakuwa imesaliti walioathirika na matukio ya uchaguzi. Wapo wanaosema kuafiki na kujiunga SUK ni kuhalalisha kasoro za uchaguzi. Kwa upande mwingine, kuna wanaosema ni muhimu ACT-Wazalendo wajiunge na SUK ili kupigania haki wakiwa kama washirika wakuu wa shughuli za serikali. Katika uchaguzi wa 2015, wakati huo wakiwa CUF, waliweza kutumia nyenzo za uwepo wao katika serikali kujijenga na kupata kinga itokanayo na kuwa ndani ya SUK.

Ukiondoa matakwa ya kisheria, Maridhiano ni imani. Maridhiano sio maneno bali vitendo. Maridhiano ni haki. Dhana ya maridhiano haipo katika hotuba wala uteuzi. Mataifa yaliyopitia nyakati ngumu katika historia zao yaliweka tume za haki, ukweli na maridhiano. Mataifa kama Afrika Kusini, Kenya, Sierra Leone, Rwanda, Liberia na kadhalika ziliunda tume za ukweli, haki na maridhiano. Msingi wa Maridhiano upo katika kutafuta ukweli, haki, amani na kuleta marekebisho ya kisiasa, kisheria na kijamii.

Suluhisho sio kujiunga ama kutojiunga kwa ACT-Wazalendo katika SUK. Mambo yanayopaswa kujadiliwa kwa uzalendo ni: ukweli kuhusu tuhuma za kasoro za kila mara za uchaguzi, ukweli kuhusu tuhuma za ‘kugandamizwa’ kwa Zanzibar na Dodoma, marekebisho ya mfumo, marekebisho ya sheria za uchaguzi ikiwemo tume huru ya uchaguzi pamoja na uwezo wa kupinga matokeo mahakamani na kadhalika. Yakizingatiwa haya basi tunaweza kusema kuna Maridhiano.

Nicodemus Minde ni mtafiti wa masuala ya siasa za muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Amejikita zaidi katika utafiti wa michakato ya suluhu za Muafaka na Maridhiano Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni nminde96@gmail.com au kupitia Twitter @decolanga. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

  1. Mijadala kuhusu muwafaka na maridhiano sio suala geni karika siasa za zanzibar,. lakini hakujapatikani mafanikio ya kudumu kwa awamu zote ambazo chama tawala wamediriki kukaa chini na upinzani. Mimi nadhani sababu ni kutokuwa na utashi na nia njema kwa watawala kuhusu suala hili. hivyo wengi wetu hatuamini kile anachokisema Rais Mwinyi hasa tukikumbauka vitendo vya kihàramia walivyofanyiwa wananchi na vyombo vya dola kipindi cha uchaguzi. Vitendo vya mauaji, utesaji, na unyanyasaji wa wananchi bilà ya kosa lolote walilofanya jambo hilo linaakisi moja kwa moja kwamba hakuna maridhiano yoyote yatakayoleta faida bila ya na taasisi huru za kusimamia uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *