Hatua Tano Muhimu Kufikia Upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania

Hatua hizi zinazingatia mazingira ya namna mchakato wa Katiba Mpya ulivyoanza mwaka 2011; namna sheria muhimu za kuongoza mchakato zilivyopitishwa; utata uliojitokeza baada ya kukamilika kwa Rasimu ya Katiba Mpya; na mapungufu yaliyoukumba mchakato wa uwasilishaji rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba.

subscribe to our newsletter!

Nimefarijika sana kupata taarifa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia vikao vyake vya Kamati Kuu na Halmashashauri Kuu Taifa vilivyoketi Dodoma, Juni 21 na 22, 2022, kimeridhia na kuazimia kuwa mchakato wa Katiba Mpya Tanzania, uliokwama mwaka 2014, ufufuliwe na kuanza upya sasa kwa ajili ya ukamilishaji wa hatua zilizosalia hadi kupata Katiba Mpya kuchukua nafasi ya iliyopo sasa ambayo ilitungwa mwaka 1977.

Katika taarifa yake kwa umma kupitia vyombo vya habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka alisisitiza mambo matatu muhimu juu ya kilichoamuliwa na CCM. Kwanza, kwamba CCM imeona umuhimu wa Katiba Mpya kwa mazingira ya sasa. Pili, Serikali inaagizwa kuratibu ufufuaji wa mchakato wenyewe ikiwemo kuukwamua toka kwenye mkwamo kwa lengo la kukamilisha mchakato hadi kupata Katiba Mpya.

Mwisho, CCM pia kimeelekeza kuzingatiwa kwa maslahi mapana ya taifa wakati wa zoezi la ukamilishaji wa mchakato huu wa Katiba Mpya. Kwa maoni yangu, hatua hii ya chama tawala inapaswa kupongezwa na kuungwa mkono ili kutimiza azma ya kupata Katiba Mpya ambayo imekuwa kilio cha Watanzania tangu kukwama kwa mchakato huo mwaka 2014.

Nikiwa mmoja wa Watanzania wachache wenye elimu ya michakato ya Katiba Mpya hususani barani Afrika, nachukua fursa na wasaa huu kujitolea kubainisha hatua muhimu ambazo ni vema kuzingatiwa ili kuhakikisha kuwa mchakato huu unakamilika kwa wakati na pasipo kukumbwa na mkwamo mwingine.

Hatua hizi zinazingatia mazingira ya namna mchakato wa Katiba Mpya ulivyoanza mwaka 2011; namna sheria muhimu za kuongoza mchakato zilivyopitishwa; utata uliojitokeza baada ya kukamilika kwa Rasimu ya Katiba Mpya chini ya uongozi wa Jaji Joseph Sinde Warioba; na mapungufu yaliyoukumba mchakato wa uwasilishaji rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba na kupelekea mgogoro ambao ndicho chanzo cha kukwama kwa mchakato wa Katiba Tanzania mwaka 2014.

Maoni na mapendekezo yangu yanajikita siyo katika ‘kufukua makaburi,’ bali katika kuangaliza na kushauri mambo ya kufuata na kuepuka katika hatua ya mchakato inayoanza sasa. Aidha, kutokana na uzoefu nilionao, nimejaribu pia kutoa taswira ya muda unaotarajiwa kutumika katika kila hatua ya mchakato huu wa kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.

Ni matumaini yangu kuwa makala hii itatoa msaada katika kutengeneza dira (roadmap) ambamo mchakato huu utapitia hadi kukamilika kwake. Zaidi ya yote, nimejaribu pia kushauri mambo ya kufanya baada ya kupatikana kwa Katiba Mpya ili tusije kujikuta kama taifa tunakwama tena katika hatua ya utekelezaji wa Katiba Mpya, kitu ambacho kimetokea sana kwa wenzetu waliotutangulia kupata Katiba Mpya katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki.

Awali ya yote, kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya Tanzania kufuatia tangazo la Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa umma siku ya mkesha wa kuufunga mwaka 2010 kulikuwa na matatizo mawili.

Kwanza, baada ya madai ya wananchi kutaka Katiba Mpya na hususani kupitia Mikutano ya Bahari Beach iliyoratibiwa na Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Rais Kikwete aliona kelele zimezidi na kuamua yeye mwenyewe kukubali pasipo kulipeleka jambo hili katika vikao vya chama chake, kuwa mchakato wa Katiba Mpya uanze mara moja.

Kutokana na hilo, hapakuwa na ridhaa ya chama chake na palikosekana mjadala wenye afya wa kuweza kuunga mkono kauli na maamuzi ya Rais kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kutoka ndani ya CCM. Kwa maoni yangu, jambo hili liliiweka CCM katika njia panda tangu mwanzo na kupeleka taarifa serikalini zenye hisia ukakasi.

Kwa mfano, baadhi ya watendaji wa CCM na Serikali waliendelea kutoa ufafanuzi hasi kuhusu tangazo la Rais hata baada ya kuwa mchakato umeshaanza. Niliongoza Jukwaa la Katiba Tanzania kwenda ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushawishi kuwa mchakato uanze na utungaji wa sheria ya kuongoza mchakato wa Katiba lakini wanasheria wa ofisi hiyo wakaishia kutushangaa na kushangaa kwamba kulikuwa kuna zoezi la kuandika Katiba Mpya.

Kwa maelezo yao, walikuwa hawana taarifa yoyote kuwa kuna kazi ya kuandika Katiba Mpya nchini. Wakati tukijibiwa haya mwishoni mwa mwezi Februari 2011, ilishangaza kuwa kulikuwa na Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 8 wa Mwaka 2011 ilipofika Machi 31. Kiukweli hii ilitushangaza sana, ikifuatiwa na mchakato wa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba baadaye mwezi Aprili.

Maamuzi ndani ya CCM

Hatua ya kwanza muhimu ya kufufua mchakato huu wa Katiba Mpya kwa sasa ni kufanya maamuzi katika chama tawala cha CCM ili maamuzi haya yasiwe ya Rais Samia Suluhu Hassan pekee bali ya chama hicho.

Imenifurahisha sana kuwa Rais ameamua kuanza mchakato kwa kufuata hatua hii muhimu ambayo wadau wa suala hili walianza kushauri tangu baadaya ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Sambamba na maamuzi kupitia vikao hivyo vya juu vya CCM, hatua nyingine muhimu ni ile ya kushawishi wanachama wa CCM katika ngazi zote kupitia vikao ili kuwe na uelewa wa pamoja ndani ya CCM, kuanzia taifa hado tawi na shina kwamba Tanzania tunaanza kuufufua mchakato wa Katiba na kuwa hii ni kwa mujibu wa maagizo ya chama.

Kwa sababu hiyo, nashauri kuwa vikao vya CCM katika ngazi zote za mikoa hadi shina viwe na dondoo ya kudumu kwa angalau miezi sita ijayo inayohusu mchakato wa Katiba Mpya Tanzania katika kila kikao halali cha chama. Hii itasaidia wana CCM kujadili, kujiuliza na kujibiwa kuhusu hofu zinazohusiana na mchakato huu kabla na baada ya mchakato wenyewe kuanza kushika kasi.

Hatua hii itafaa kufuatwa pia na vyama vingine vya siasa, mashirika ya umma, idara za Serikali na asasi za kiraia nchini. Pia, itakuwa vyema kwa viongozi wa kiroho kutangaza ujio wa mchakato huu na kuungana na waumini wao kuliombea taifa kuwa na maono mapana katika zoezi hili.

Uhuishaji wa sheria

Hatua ya pili muhimu ya ufufuaji wa mchakato wa Katiba inahusu uhuishaji wa sheria zinazoongoza mchakato wenyewe. Kwa wasiofahamu, mchakato wa Katiba Mpya unaongozwa na sheria mbili muhimu.

Kwanza, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa na Bunge mnamo Novemba 2011 pamoja na marekebisho yake kadhaa hadi 2014, ndiyo muongozo mkuu wa mchakato wa Katiba Mpya.

Sheria hii ndiyo inayoweka utaratibu wa kisheria wa namna mchakato utakavyoanzishwa na kuendelezwa; malengo na madhumuni ya mchakato; uteuzi, muundo, majukumu na miiko ya tume; Bunge Maalum la Katiba na ufanyaji kazi wake hadi kukamilika kwa Katiba Inayopendekezwa.

Aidha, Sheria hii ndiyo inayoweka utaratibu wa namna Rasimu ya Tume itakavyowasilishwa katika Bunge Maalum a Katiba, jambo ambalo kwa sehemu lilikiukwa na kuleta mgogoro uliopelekea kukwama kwa mchakato.

Kwa mfano, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kupitia Mwenyekiti wake, ilipaswa kuwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya katika Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo kuzinduliwa rasmi na Rais.

Badala yake, mizengwe iliingilia kati na kupelekea Rasimu kuwasilishwa kabla ya Bunge kuzinduliwa rasmi na Rais, jambo ambalo linaifanya Rasimu ya Katiba Mpya kuwa haijawasilishwa mpaka leo kwa kuwa uwasilishaji uliofanyika ulikuwa batili kwa mujibu wa sheria na haukubaliki.

Hata baada ya hoja hii na nyinginezo kuibuliwa na wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kulitokea kupuuzwa kwa hoja yenyewe na kupelekea UKAWA na wajumbe wengine kadhaa wa Bunge Maalum kuondoka bungeni na kutorejea tena hadi mwisho.

Ni kutokana na hilo, Katiba Inayopendekezwa inakosa uhalali wa kuwa mahali pazuri pa kuanzia mchakato huu wa ukamilishaji Katiba Mpya. Hii ndiyo sababu Watanzania wengi wasiojua sheria wamekuwa wakitaka mchakato wa kukamilisha Katiba Mpya uanzie kwenye Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jambo ambalo linapingwa na mahafidhina wa sheria ambao wanadai hatua hiyo ilishapita kisheria.

Kwa sababu hiyo, nashauri hatua inayofuata sasa iwe ni kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83 ya mwaka 2011 na marekebisho yake hadi 2014 kwa lengo la kuhuisha vifungu vyote vilivyopitwa na wakati.

Vivyo hivyo, kuna kazi muhimu ya kuihuisha Sheria ya Kura ya Maoni kwa kuifanyia marekebisho muhimu. Kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, nashauri pia kuingizwe kifungu kipya kitakachoanzisha chombo cha utatuzi wa migogoro inayohusu mchakato wa Katiba Mpya Tanzania ili kutofautiana kwa watu au makundi kimaono kusilazimishe mchakato kukwama kama ilivyotokea mwaka 2014.

Baada ya Maboresho ya Sheria ambayo yatahitaji kuanzia Baraza la Mawaziri na kuiagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Mwandishi Mkuu wa Miswada ya Sheria nchini kuanza mara moja kuandaa rasimu ya miswada hiyo miwili. Miswada hii itapaswa kwenda Bungeni kusomwa kwa mara ya kwanza kati ya Septemba na Novemba mwaka huu, 2022.

Mchakato hauwezi kuingia katika hatua nyingine yoyote pasipo kuwepo kwa Sheria hizi mbili zikiwa hai zinazoongoza mchakato wa Katiba Mpya. Napendekeza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ianzishe Kamati ndogo ya Wataalam wa Masuala ya Sheria na Katiba ili kuweza kufanya kazi ya kuwianisha (harmonization) maudhui ya Rasimu ya Katiba Mpya na Katiba Inayopendekezwa.

Ukisoma nyaraka hizi mbili, hakuna tofauti kubwa ya kimuundo ukiacha suala la ama Muungano uwe wa Serikali mbili au tatu. Shida kubwa iliyopo ni kwamba Katiba Inayopendekezwa imetohoa Maudhui ya Rasimu ya Katiba Mpya kiasi kwamba kuna mahali inajikanganya yenyewe.

Ili kupata mahali pa kutokea, kunahitajika timu hiyo ya watu watulivu na wasiowakilisha maslahi ya kivyama bali maslahi mapana ya kitaifa kuweza kuwianisha maudhui ya nyaraka hizo mbili muhimu. Hoja kuwa Katiba Inayopendekezwa haifai kabisa kufikiriwa wala kutazamwa ni hoja dhaifu na inayoweza kuchochea mgogoro au mkwamo mwingine. Timu ya wataalam wa Katiba itazalisha Rasimu ya Maridhiano ambayo ndiyo itaenda kwa hatua za mbele.

Maandalizi ya kura ya maoni

Hatua nyingine itakayofuata ni Maandalizi ya Kura ya Maoni au Maamuzi ya Watanzania wote kwa kitaalam ikiitwa Referendum. Hatua hii itapaswa kutanguliwa na maandalizi ya aina mbili.

Kwanza, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo ndiyo imepewa dhamana ya kuendesha Kura hiyo ya Maoni kisheria itapaswa kuwa na kipindi cha miezi sita kuendesha elimu ya mpiga kura nchi nzima ili wananchi wafahamu taarifa muhimu kuhusu kura ya maoni ikiwemo tarehe, vituo, swali la kupigia kura, wasimamizi na waratibu wa kura na taarifa nyinginezo kama hizo za kimchakato.

Sambamba na elimu ya mpiga kura, kutahitajika elimu pana zaidi ya uraia kuhusu Maudhui ya Rasimu ya Katiba Mpya itakayopaswa kufanyika pia kwa miezi takriban sita ili wananchi wafahamu kiundani yaliyomo kwenye Katiba hiyo tarajiwa. Nashauri kuwa asasi huru za kiraia ndizo zihusike na utoaji wa elimu ya uraia.

Viongozi wa dini nao watapaswa siyo tu kuendelea kuliombea taifa bali pia kueneza ujumbe wa itifaki na maudhui ya Rasimu ya Katiba inayosubiri kupigiwa kura na Watanzania. Naamini kuwa kupitia nyumba za ibada, wananchi wataweza kufahamu mambo muhimu ya kuzingatia kuelekea upigaji kura na pia maudhui yaliyomo kwenye rasimu.

Baada ya kipindi cha nusu mwaka cha elimu ya uraia na elimu ya mpiga kura, kutafuata kipindi cha siku 90 za kampeni kuunga mkono au kupinga Rasimu ya Mwisho ya Katiba Mpya. Kazi hii itaruhusiwa kufanywa na vyama vya siasa; asasi za kiraia; vyombo vya habari pamoja na idara zozote za kiserikali zinazopenda kufanya hivyo.

Katika kipindi hicho, CCM nayo iitakuwa na fursa ya kufanya kampeni kuunga mkono au kupinga Rasimu ya Mwisho ya Katiba Mpya.

Upigaji kura ya maoni

Hatua ya mwisho ya mchakato wa Katiba Mpya itahusu upigaji Kura ya Maoni au Maamuzi. Hii itafanyika katika siku iliyopangwa na kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itafanya kazi hiyo kwa upande wa visiwa vya Unguja na Pemba kwa vile sheria inatamka bayana kuwa mchakato wa Katiba Mpya, kama ilivyo Katiba yenyewe, ni suala la Muungano.

Endapo kura nyinyi zaidi ya asilimia 50 zitakuwa zimeipa Rasimu kura ya NDIYO, Tanzania itakuwa imepata Katiba Mpya. Kinyume chake, utaratibu uliotajwa na Sheria ya Kura ya Maoni utafuatwa kuweza kurudia upigaji kura kuhusu Rasimu ya Katiba endapo Kura nyingi zitakuwa zimeikataa Rasimu ya Mwisho ya Katiba.

Katika hali ambayo Katiba Mpya imepatikana, utaratibu wa utekelezaji wa Katiba hiyo Mpya na hatua zake utaanza mara moja.

Kwa ufupi, hiyo ndiyo barabara ambayo mchakato wa Katiba Mpya Tanzania ambao umetangazwa wiki iliyopita na vikao vya CCM kufufuliwa itapitia.

Hatua chache zinaweza kuwa tofauti kulingana na maamuzi ya Bunge katika hatua ya maboresho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83 ya mwaka 2014 na Sheria ya Kura ya Maoni ya Mwaka 2014.

Bunge ndilo lenye dhamana ya utungaji wa sheria kwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977.

Mungu ibariki Tanzania na watu wake!

Deus Kibamba ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya siasa Tanzania anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts