The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je,  Zanzibar Inaweza Kuwa na ‘Mamlaka Kamili’ Ndani ya Jamhuri ya Muungano?

Ismail Jussa anasema ‘Mamlaka Kamili’ haimaanishi wito wa kuvunja Muungano bali kuiwezesha Zanzibar kufaidi ‘mamlaka ya pamoja ya kidola.’

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha upinzani ACT-Wazalendo, Ismail Jussa, ametolea ufafanuzi kile kinachoitwa ahadi ya chama hicho kwa Wazanzibari – Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili – akisema kwamba ahadi hiyo hailengi kuvunja Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Jussa, sauti muhimu kwenye vuguvugu la kudai mamlaka zaidi ya Zanzibar kwenye Muungano, alitoa ufafanuzi huo kwenye mahojiano maalum aliyofanya na mwandishi wa The Chanzo Najjat Omar hapo Februari 27, 2023.

Kwenye mazungumzo hayo, Jussa, ambaye amewahi kuhudumu kama Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa vipindi tofauti, alisema kwamba ahadi yao hiyo inalenga kuiwezesha Zanzibar kunufaika na ‘mamlaka ya pamoja ya kidola’ yaliyotokana na Muungano ambayo kwa sasa alidai ni Tanganyika tu ndiyo inayonufaika na mamlaka hiyo.

“ACT-Wazalendo tunachotaka ni kuubadilisha Muungano wa sasa kutoka kwenye muundo wa kikoloni uliokusudiwa kuidhibiti Zanzibar kuwa kweli ni ushirika wa nchi mbili ambao utazipa nchi hizi haki na fursa sawa sawa,” Jussa alieleza kwenye mahojiano hayo.

“Na ndiyo maana tunasema, katika lugha nyingine, tunasema tunachotaka ni Muungano wa haki, Muungano wa heshima na Muungano wa usawa baina ya washiriki wawili wa Muungano huu,” aliongeza.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo na hapa Jussa anaanza kwa kueleza namna chama chake kilivyopokea uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kufungulia vyama vya upinzani kufanya mikutano yao ya hadhara:

Ismail Jussa: Siasa zetu Zanzibar, na Tanzania kwa ujumla, unaweza kusema pengine kwa Afrika, bado ni siasa ambazo, kwa kiasi kikubwa, watu wamezoea kuwasiliana moja kwa moja kwa kumuona anayezungumza na hadhara kuwa kubwa [na] watu wakaweza kusikiliza.

Sasa mnapokuwa mnazuiliwa jambo kama lile, mnatafuta njia zingine, lakini haziwi kama vile ambavyo watu wamezoea. Kwa hiyo, bila shaka [katazo la mikutano ya hadhara] imeathiri kwa kiasi kikubwa na naweza kusema kwamba watu waliingia kama uduwanzi wa namna fulani kwa kukosa kitu kama kile.

Lakini jingine pia imeathiri haki za watu, kwa sababu mikutano inasaidia kuibana Serikali, kuiwajibisha Serikali, kuwasemea watu mambo yao. Yote hayo yalikuwa yamekosekana katika miaka sita mpaka saba iliyopita, na sasa kwa kuruhusiwa tena inarudhisha haki ile ya watu ya kuweza kuzungumza, kupata habari lakini pia kusemewa, na sisi vyama vya upinzani kuiwajibisha Serikali.

Kwa hiyo, tumefurahi. Si kwamba tumepewa fursa, ni haki yetu ambayo ilikuwa imeporwa. Tunafuraha kwamba imerudhishwa na watawala kutambua kwamba jambo lile halikuwa sahihi.

The Chanzo: Kufunguliwa kwake kumeleta maana gani kwa chama cha ACT-Wazalendo, hususani mwanachama wa Zanzibar?

Ismail Jussa: Nadhani wanachama wamefurahi na hilo limedhihirika jana [Februari 26, 2023,] katika mkutano wetu wa mwanzo wa uzinduzi ambao tuliufanya pale Nungwi.

Unaona jinsi watu walivyokuwa na furaha, watu walivyoitika kwa wingi, siyo tu ndani ya kijiji cha Nungwi lakini pia watu kutoka maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Unguja kama ilivyokuwa utamaduni wa watu wa Zanzibar kuja kusikiliza na hamasa ambazo zilionekana tangu njiani, au barabarani, wakati watu wanaelekea Nungwi, Nungwi kwenyewe na hata wakati wa kurudi.

Yote haya yanadhihirsha kwamba watu walikuwa wameyakosa mambo haya tokea zamani na sasa yamerudi basi yamerejesha furaha ya namna fulani kwa wananchi wa Zanzibar.

The Chanzo: Februari 25, 2023, wakati mnazindua ahadi yenu kwa wananchi, kuna maneno ambayo ulikamilisha sentensi moja ni maneno sita. Ulisema Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili. Maneno haya sita yana maana gani kwa mtu ambaye hakuwepo kwenye mikutano, hakuwepo kwenye uzinduzi wa ahadi yenu kwa wananchi lakini kichama maana yake halisi ni ipi haswa?

Ismail Jussa: ‘Brand Promise,’ au Ahadi Yetu, kwa Wazanzibar kwa maana hii ambayo tunaizungumzia maana yake ni kitu gani ambacho chama chetu kinasimamia.

Na kama alivyosema Kiongozi wa Chama [Zitto Kabwe] wakati tunazindua ‘Brand Promise,’ au Ahadi Yetu kwa Watanzania pale Dar es Salaam, kwamba chama cha siasa bidhaa yake ambayo kinaipeleka katika soko, ambalo ndiyo nchi nzima, ni mawazo.

Kwa hiyo, ‘Brand Promise’ ni mawazo ya nini ACT-Wazalendo tunakisimamia. Sasa kwa upande wa Zanzibar, tunasimamia Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili.

Tunakusudia nini katika haya? Tunaposema Zanzibar Mpya ni kwamba haturidhiki na Zanzibar hii iliyopo sasa. Kwamba Zanzibar inaoneka imechakaa, au imechakazwa, [kwamba] mambo mengi hayaendi vizuri.

Huduma za kijamii kwa watu wake hazipatikani pamoja na kwamba wanalipa kodi kupitia shughuli zao za maisha, haki zao hazipatikani, uendeshaji wa nchi umekuwa ni wa shaghala baghala, hauzingatii misingi ya uwajibikaji.

Kwa hiyo, tunasema hii ndiyo Zanzibar ya sasa ambayo imechakazwa na [chama tawala, Chama cha Mapinduzi] CCM. Kwa hiyo, Zanzibar Mpya ni ile ambayo inakwenda kutibu mambo haya kwa kuleta mbadala wake. Nafikiri baadaye tutapata fursa ya kuichambua.

Lakini tunaposema Zanzibar Moja, kwa upande mwingine, tunachokusudia ni kwamba ni kinyume cha Zanzibar iliyopo sasa chini ya CCM ambayo ni Zanzibar yenye migawanyiko, Zanzibar  yenye ubaguzi, Zanzibar ambayo imepelekea watu wake kutenganishwa na kwa hivyo kujikuta kwamba inakosa jambo la msingi kabisa ambalo ndiyo umoja wa watu wake.

Na tutambue kwamba hakuna nchi ambayo inaweza ikapiga hatua za kimaendeleo na kubadilisha maisha ya watu wake ikiwa watu wake wametengana, wana mfarakano.  Tunahitaji watu ambao wako kitu kimoja, ni wamoja. Kwa hiyo, lengo letu [ni] hilo tunaposema Zanzibar Moja.

Na kwenye suala [la] Mamlaka Kamili, tunachokusudia ni kwamba vilevile, Zanzibar haitaweza kwenda mbele ikiwa haitaweza kuwa na mamlaka ya kujiamulia mambo yake wenyewe, hasa katika eneo la uchumi, katika eneo la masuala ya fedha na mipango yake, utakuta bado mamlaka yake yamedhibitiwa katika hiki kinachoitwa Muungano.

Kwa hiyo, tunaposema Mamlaka Kamili tunakusudia Zanzibar kurejesha haki yake ya msingi, kurejesha sauti yake, kurejesha maamuzi yake ili iweze kufanya maamuzi ya kisera ambayo yanahitajika kuikwamua Zanzibar kutoka hapa ilipo ambapo katika mfumo wa sasa haiwezekani.

Kwa kifupi, hayo ndiyo tunamaanisha tunaposema Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili.

The Chanzo. Niulize swali kuhusiana na Mamlaka Kamili. Nifafanulie kidogo kwa undani mamlaka kamili ipi ambayo ACT Wazalendo mumekuwa mkiizungumza kwa hizi siku mbili, ni kwa mtazamo upi, kabla sijauliza swali jingine.

Ismail Jussa: Tunaposema Mamlaka Kamili, kwanza labda tuwafahamishe watu wengi kwamba hili neno Mamlaka Kamili unaweza kulitafsiri kwa maneno tofauti katika lugha ya Kiingereza lakini maana moja unaweza ukaitafsiri ni Exclusive Authority.

Na hili neno Exclusive Authority, kwa maana ya Mamlaka Kamili, lipo ndani ya Mkataba wa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar. Mkataba wa Muungano unaanzisha mamlaka tatu. Na kila moja imeitwa Exclusive Authority [yaani,] Mamlaka Kamili.

Inazungumzia Exclusive Authority ya Muungano kwa Mambo ya Muungano ambayo inashughulika na Jamhuri yote ya Muungano. Halafu vilevile, inazungumzia Exclusive Authority, yaani Mamlaka Kamili kwa Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano. Na vilevile, inazungumzia Exclusive Authority, yaani Mamlaka Kamili kwa Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano.

Bahati mbaya sana katika muundo wenyewe ni kwamba mamlaka mbili – mamlaka ya Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano na mamlaka ya Muungano – zikachanganywa pamoja.

Hilo linalosemwa siku zote kwamba kupitia muundo huu Tanganyika ikavaa koti la Muungano na ikajigeuza yenyewe kuwa ndiyo Muungano.

Sasa kilichokwaza Zanzibar katika hili ni kwamba ukishakuwa una mshirika mmoja ndiyo ambaye amevaa koti la Muungano ameyachukua mamlaka yake kwa mambo yasiyo ya Muungano na mamlaka ya Muungano kwa mambo yote ya Muungano.

Imekuwa sasa Zanzibar imefanywa kama ni mgeni na hii lugha hii hata Pius Msekwa, ambaye alikuwa ni Karani wa Bunge la Tanganyika wakati Mkataba wa Muungano unaidhinishwa, ametumia maneno hayo hayo katika maandishi yake mengi.

Kwamba Zanzibar imegeuzwa kuwa invited guest, yaani mgeni mwalikwa katika Muungano. Na maana yake ni kwamba Zanzibar imekua sasa tofauti na Tanganyika kwa sababu Tanganyika imeingia ndani ya Muungano, haitaki ruhusa ya mtu kufanya maamuzi, inatumia mamlaka ambayo imeyabeba yenyewe.

Lakini Zanzibar kinyume chake imekuwa kwa yale mambo ya Muungano haiwezi kujiamulia mpaka ipate ruhusa ya Muungano ambaye ni Tanganyika aliyejigeuza kwamba ni Muungano.

Sasa tunaposema Mamlaka Kamili tunasema la kwanza, mnapounganisha nchi kuna kitu kinaitwa sovereignty, yale mamlaka ya kidola yanayokutambulisheni nyie kama ni dola kamili ndani na nje ya mipaka yenu. Mkiunganisha nchi mnaunganisha sovereignty zenu, yaani haya mamlaka ya kidola.

Lakini ilivyo ni kwamba mnapaswa ndani ya Muungano, au ushirika, mliouunda, haya mamlaka ya pamoja sasa yaweze kufaidisha pande zote mbili na yamilikiwe na pande zote mbili kwa usawa kwa sababu katika sheria ya kimataifa ukubwa na udogo wa nchi, [au] uchache na wingi wa watu, siyo hoja.

Na ndiyo maana katika Umoja wa Mataifa, kuna kijinchi kinaitwa Nauru, kina watu 7,000 tu. Ina kura moja sawa sawa na Marekani au India au China, hizo nchi mbili za mwanzo zina watu zaidi ya bilioni moja na Marekani ina watu kwa mamilioni, lakini wote wana kura moja moja tu katika Baraza la Umoja wa Mataifa.

Sasa na katika Muungano wetu tunazungumzia hilo na la kwanza Mamlaka Kamili tunalolitaka ni kwamba kwa sasa tunachoona suala hili limepotoshwa kwa muda mrefu, haya mamlaka ya pamoja ya kidola, yaani shared sovereignty yamekuwa yanatumika upande mmoja dhidi ya upande mwingine ambayo si sahihi.

Sisi tunachotaka katika hilo ni kuona kwamba inatungwa sheria itakayotafsiri vipi mamlaka ya kidola – shared sovereignty – tunaipeleka kwenye muungano inaweza kutumiwa na pande zote mbili kwa usawa baina yao, hilo moja.

La pili, tunazungumzia katika Mamlaka Kamili ni mamlaka katika masuala yanayohusu sera za kodi. Ni sawa kwamba kodi imefanywa kuwa Suala la Muungano lakini huwezi ukawa na kodi za namna moja kwa nchi mbili ambazo chumi zake ni tofauti kabisa.

Zanzibar ni nchi ya kisiwa, kwa vyovyote vile haina rasilimali kubwa kama ilivyo Tanganyika. Tangayika tunazungumzia wana madini kama dhahabu, wana almasi na Tanzanite lakini pia wana ardhi kubwa ya kilimo, wana eneo kubwa la kuweza kutumia kuzalisha.

Zanzibar ni kisiwa kidogo, au visiwa vidogo viwili. Zanzibar, kwa maumbile yake, unapaswa kuwa unaitwa uchumi wa huduma, yaani service-oriented economy. Kwa hiyo, katika hali kama hiyo, kodi za uchumi wa huduma hazipaswi kuwa sawa sawa na kodi za uchumi wa rasilimali.

Na kwa hivyo unaweza ukawa na mamlaka moja lakini unapotengeneza kodi ikatambua kwamba inapaswa kutenganisha aina na viwango vya kodi baina ya pande mbili.

Sasa huwezi kufanya uchumi ambao unategemea bidhaa sawa na uchumi wetu wa huduma. Na ndiyo maana, kwa mfano, sisi uchumi wetu unategemea mno bandari, biashara ya mpito. Vipi utaweka viwango sawasawa vya kodi baina ya hizi nchi mbili? Haiwezekani!

Kwa hiyo, tunataka mamlaka ya Zanzibar kuweza kujiamulia. Kama mtakumbuka, kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa kila kiongozi anayekuja huko nyuma alikuwa akiimba kuanzisha Zanzibar ambayo ina bandari huru.

Huwezi kuanzisha bandari huru ikiwa huna mamlaka ya kikodi katika nchi yako. Waziri wetu wa Fedha wa Zanzibar anaitwa tu Waziri wa Fedha lakini ni Waziri wa Fedha gani duniani ambaye hana mamlaka ya kikodi?

Huyu ndiyo maana wengine wanamuita ni glorified finance officer, ni karani wa fedha aliyepewa hadhi tu akaitwa waziri lakini hamiliki mamlaka ya kikodi. Kwa hiyo, tunachotaka la pili ni eneo la kodi.

La tatu ni katika masuala vilevile yanayohusu sera za fedha. Tuna Benki Kuu ya pamoja, baada ya suala la sarafu, mabenki na fedha za kigeni kuingizwa kinyemela katika [Mambo ya] Muungano mwaka 1965, mwaka mmoja baada ya kuundwa Muungano, matokeo yake Zanzibar yenye uchumi wa huduma ingependa kuwa kituo cha fedha na mabenki katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ili kuvutia wawekezaji tofauti wanaokwenda Kenya, wanaokwenda Uganda, wanaokwenda Tanganyika kwenyewe pengine wanaokwenda Rwanda, wanaokwenda Burundi, wanaokwenda Kongo, wanaokwenda kuwekeza huko lakini wakaamua kwamba wanataka kusajili kampuni zao Zanzibar.

Wanataka kuanzisha akaunti zao za fedha katika mabenki ambayo yako Zanzibar yatakayokuwa salama. Zanzibar ili kuweza kuweka vivutio vya kufanya hayo haina mamlaka hayo kwa sababu mamlaka hayo yapo katika benki kuu na bahati mbaya vilevile kama ilivyo kwenye suala la kodi kwenye suala fedha, Benki Kuu inajisahau kwamba inahudumia chumi mbili tofauti.

Kwa hiyo, hayo ni baadhi ya maeneo. Yako mengi mengine tunazungumzia katika suala la mafuta na gesi kuwa na Mamlaka Kamili. Tunazungumzia masuala, kwa mfano, hata elimu ya juu, Zanzibar elimu yake inapaswa izingatie mahitaji ya Zanzibar katika uchumi wa huduma na mengi mengine. Lakini hii ni mifano michache nimeitaja ambayo tunadhani kwamba Zanzibar inapaswa iwe na Mamlaka Kamili.

Kwa hiyo, tunavyosema Mamlaka Kamili tunakusudia hilo lakini haya yote kubwa lao lile nililoanza mwanzo la shared sovereignty kwa sababu hili linakusudia nini na nimalizie katika nukta hiyo kwamba hata kwa mambo yasiyo ya Muungano kwa sasa hivi kwa sababu hatuna hii shared sovereignty, [yaani] mamlaka ya pamoja ya kidola tunayofaidika nayo Zanzibar inajikuta haiwezi kufaidi fursa zake kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano.

Kwa mfano, afya siyo Suala la Muungano lakini Zanzibar siyo mwanachama Shirika la Afya Duniani (WHO). Elimu na sayansi siyo Masuala ya Muungano lakini Zanzibar haiwezi kuwa mwanachama wa UNESCO. Kilimo si Suala Muungano lakini Zanzibar haiwezi kuwa mwanachama wa FAO, Shirika la Kilimo na Chakula Duniani.

Michezo ambayo vijana inawakera mno, wana vipaji vingi vijana wa Kizanzibari, wanataka wakacheze kimataifa waweze kuuza vipaji vyao, waweze kuitangaza Zanzibar, hawawezi kwa sababu ikifika kwenye milango ya kimataifa, Zanzibar inapigwa stop kwa sababu sovereignty ya pamoja imehodhiwa na Tanganyika.

Kwa hiyo, tunachosema kwenye shared sovereignty ni kwamba hata katika mahusiano ya kimataifa, kwa mambo yote yasiyo ya Muungano, Zanzibar haiwezi kufaidi kikamilifu na kunufaika na fursa zake.

The Chanzo: Asante sana na maana yake kwenye mazungumzo haya, mazungumzo yako yanayohusu dola ni kama vile unataka kusema kwamba ACT sasa wameamua kuitoa Zanzibar kwenye Muungano, kwa maneno machache.

Ismail Jussa: Hapana. Tunazungumzia kuusanifu upya Muungano. Tatizo si Muungano. Dunia nzima ziko nchi ambazo zimeungana. Suala ni Muungano wenyewe ni wa muundo gani? Muungano wenyewe kweli ni Muungano?

Kwa sababu kama Muungano unapaswa wote walioungana wafaidike sawa sawa katika haki na fursa zinazotokana na muungano ule. Lakini huwezi ukawa na Muungano ambao mmoja amemdhibiti mwenzake. Huo si Muungano, ni ukoloni.

ACT-Wazalendo tunachotaka ni kuubadilisha muungano wa sasa kutoka kwenye muundo wa kikoloni uliokusudiwa kuidhibiti Zanzibar kuwa kweli ni ushirika wa nchi mbili ambao  utazipa nchi hizi haki na fursa sawa sawa.

Na ndiyo maana tunasema, katika lugha nyingine, tunasema tunachotaka ni Muungano wa haki, Muungano wa heshima na Muungano wa usawa baina ya washiriki wawili wa Muungano huu.

The Chanzo: Lakini haya maneno ni kama yanatofautiana sasa kwenye haki, ushirikiano na usawa na Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja yenye Mamlaka Kamili. Maana yake sasa ni ipi ambayo iko sawa ni maridhiano ya muungano, ni kurekebishwa kwa Muungano au ni kupata mamlaka kamili. Maana yake mtu ukimpa kitu kamili maana yake unatakiwa umpe chote, siyo umpe kwenye maridhiano na Muungano. Mheshimiwa Jussa hapo umeniacha kidogo.

Ismail Jussa: Hapana, wala hakuna mgongano. Mgongano unakuja kwa sababu ya mazoea na mimi siwalaumu wenye wasiwasi kwa sababu tumeishi takribani kwa miaka 60 sasa, mwaka huu ni miaka 59 mwakani tunakwenda miaka 60 katika mfumo huu wa kikoloni ambao tunadhani kwamba ndiyo Muungano.

Kwa hiyo, fikra zozote mpya, [au] mbadala, zinapokuja na ndiyo kawaida mabadiliko siku zote huwa yanashitua, mtu akisikia mnataja Mamlaka Kamili yeye anafikiri kuvunja Muungano.

Lakini nitawapa mfano kwamba mkishaamua kwamba mna shared sovereignty ndiyo maana nimetumia mamlaka ya pamoja ya kidol,a hakuzungumzii kuvunjwa Muungano lakini tunazungumzia haya mamlaka ya pamoja kila mmoja ayafaidi kikamilifu, ndiyo mamlaka kamili hayo.

Kwa sababu mnaweza kuwa na taasisi za pamoja zinazowaendesha lakini tunachokikataa sisi katika mfumo wa sasa ni kwamba katika kuziendesha hizi taasisi za Muungano – iwe Benki Kuuu, iwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iwe hata vyombo vingine vyote tunavyovizungumza – unakuta mmoja amejitwisha umiliki na mwingine anakwenda kubembeleza.

Kwa hiyo, hakuna kupingana. Tunachozungumza sisi ni Mamlaka Kamili ya Zanzibar ni kuweza kutetea haki zake ndani ya huohuo mfumo wa Muungano kwa sababu ina mamlaka yake kamili.

Kama ambavyo Tanganyika inapaswa iwe nayo kwa sababu hatupaswi kuwa na mfumo ambapo Tanganyika ndiyo hiyo hiyo ni Muungano, hiyo ndiyo inayonyang’anya Zanzibar kuwa na Mamlaka Kamili.

Tanganyika ina Mamlaka Kamili, ipo ndani ya Muungano lakini ina Mamlaka Kamili kwa nini? Kwa sababu imejivika koti la Muungano na kubeba maamuzi ya mambo yote yaliyokuwa ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa Zanzibar, inatuamulia sisi.

Tukiwa na Mamlaka Kamili, Zanzibar inabakia vilevile ndani ya Muungano lakini ina sauti sawasawa na mshirika mwenzake. [Hicho] ndiyo tunachokusudia.

The Chanzo: Maana yake hii unataka kusema kwamba baada ya Zanzibar kupewa mamlaka yake kamili, maana yake chama cha ACT Wazalendo Tanganyika na Zanzibar kitakuwa kina muundo huu huu ambao unaendelea au kutakuwa na mabadaliko kwenye utendaji?

Ismail Jussa: Vyama ni juu yake wenyewe kuamua. Bila shaka moja katika mambo ambayo hata katika mjadala wa katiba mwaka 2014 yalikuwa yakizungumzwa sana ni mambo yapi yabakie katika orodha ya Mambo ya Muungano.

Moja katika suala ambalo lilikuwa linajadiliwa ni vyama vya siasa. Kwa sababu suala la vyama vya siasa tutakumbuka liliingizwa mwaka 1992, kabla ya hapo halikuwa Suala la Muungano. Kwa hiyo, ikiwa vyama vya siasa vitabakia kuwa Suala la Muungano ni vyama vyenyewe kuamua sasa muundo wake.

Mimi sioni tatizo kwa sababu sisi hata kama sasa hivi chama chetu kinalitekeleza hilo ambalo tunalihubiri. Muundo wa chama chetu sisi [ni] tofauti na vyama vingine vyote. Na kwenye hilo natoa changamoto, chama chochote Tanzania hakina muundo kama ACT-Wazalendo.

ACT-Wazalendo tuna vyombo vya pamoja, tunaweza kusema vya Muungano. Kwa maana ya Mkutano Mkuu wa Taifa, Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu ya Taifa. Lakini baadaye kila upande, Tanganyika na Zanzibar, kuna sekretarieti yake ambayo inapokaa peke yake inaitwa Kamati ya Mashauriano.

Kwa hiyo, kuna Kamati ya Mashauriano Zanzibar, kuna Kamati ya Mashauriano Tanzania Bara au kwa kugha nyingine tunasema Tanganyika na zinapokaa hizi zinafanya mazungumzo kuhusu pande hizi mbili.

Baadaye, bila shaka, vinapelekwa katika vyombo vya umoja na hata katika vyombo vya maamuzi kuna Kamati Maalumu ya Zanzibar na Kamati Maalumu ya upande wa Bara halafu baadaye kuna Kamati Kuu ya Taifa ya pamoja.

Kwa hiyo, nadhani hata tuwe na mfumo huo bado ACT itakuwa imetangulia mbele katika kutengeneza mfumo ambao utafanya kazi vizuri sana kwa kuwa na vyombo ndani ya chama ambavyo vina mamlaka ya kuzingatia masuala ya upande wa Zanzibar na vina yombo ndani ya chama vinavyozingatia mambo yanayohusu Tanganyika na tuna vyombo vya kitaifa ambavyo tunakutana sote na kuamua yale yanayotuunganisha kwa pamoja.

The Chanzo: Ina maana unataka kusema Mheshimiwa Jussa kwamba chama ndiyo kitaamua baada ya Zanzibar kupewa Mamlaka Kamili kwamba kivunje uwiano wa wanachama wa Bara ama kiendelee kubaki kama ambavyo mnavyofanya kazi sasa?

Ismail Jussa: Hapana. Kwanza, tusichanganye mambo. Suala la Mamlaka Kamili ni sera ya chama kwa sasa, ndiyo maana tumezindua katika ‘Brand Promise.’ Lakini bila shaka haitotekelezeka kwa kuwa sera ya chama mpaka mmeshika madaraka ya nchi au mmekuwa na nguvu  ya kushawishi mabadiliko katika mfumo wa sasa.

Kwa mfano, moja ambalo linazungumzwa ni suala la kuwa na Katiba Mpya. Na unakumbuka lugha hii ya Mamlaka Kamili ingawa nimesema kihistoria inarudi katika Mkataba wa Muungano wa mwaka 1964 lakini ilikuja ikapata nguvu zaidi katika mjadala wa mabadiliko ya Katiba mwaka 2012 mpaka mwaka 2014. Kwa hiyo, kama tunakamilisha Katiba Mpya wala haitakuwa suala la chama, sisi tutapeleka hiyo hoja.

Lakini ikishapatikana, itakuwemo ndani ya mifumo ya kikatiba na sheria katika nchi. Chama chenyewe, kama ulivyosema, kitaongozwa pia na Sheria ya Vyama vya Siasa, pia kinaongozwa na Katiba yake na kama nilivyosema mimi hata kwa mfumo wa Katiba ya sasa ulivyo sioni kama unaizuia Zanzibar kuweza kufanya maamuzi yake kama ambavyo haizuiwi Tanganyika kufanya maamuzi yake na vilevile kukutana pamoja katika vyombo vya kitaifa ambavyo nimevitaja.

Kwa hiyo, suala la muundo wa chama halitobadilika kwa kuwa na mamlaka kamili. Mamlaka kamili itakuwemo ndani ya Katiba za nchi na muundo wa chama utaamuliwa ndani ya Katiba ya chama na miongozo yake mengine.

The Chanzo: ACT-Wazalendo mpo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, je hamuoni kwamba kutakuwa kuna kikwazo cha kupata Mamlaka Kamili ikiwa nyinyi ni wanachama wa maridhiano au makubaliano na miongozo kadhaa ya Zanzibar kwa kwenye kutoa maamuzi hii inawezekanaje kufanyika maana yake mmekubali huku halafu leo mnataka hivi?

Ismail Jussa: Wala si suala geni duniani. Labda ndiyo hali inarejea Watanzania tujizoeshe kuangalia mambo yanayofanyika vipi duniani huko. Nitakupa mfano. Scotland kuna chama kinaitwa Scotish Nationalist Party (SNP).

[Chama hiki] kipagania Mamlaka Kamili ya Scotland, wao wanataka kujitoa kabisa katika Muungano wa Uingereza, tofauti hata na sisi. Lakini chama hicho hicho kina wabunge ambao wanaingia ndani ya Bunge la Uingereza na kinaendeleza hoja zake kule, umeona? Na vilevile,  kwenye Scotland kinapigania mamlaka yake.

Sisi tunachozungumza katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kwamba kwanza litabaki suala hili kwa sasa ni msimamo wa ACT Wazalendo. Bila shaka tunarai na kushawishi na kujenga hoja wengi waliunge mkono, wakiwemo kutoka upande wa pili.

Na kama utakumbuka, hata wakati ule ilipokuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010 [na] 2015, baadhi yetu hatukuwa ACT Wazalendo lakini suala hili lilikuwepo na vilikuwa vyama tofauti na kila mmoja alikuwa kwenye msimamo wake.

Tungefurahi, na tulijaribu sana, kwamba tunapokwenda katika Bunge la Katiba tuwe na msimamo mmoja lakini bahati mbaya wenzetu [kutoka CCM] wakakengeuka. Palikuwa na mazungumzo mengi hapa.

Sasa mpaka sasa kwa sasa hivi tulichozindua sisi ni ahadi ya ACT kwa Wazanzibar, ndiyo maana ya ‘Brand Promise’ hii ya Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili, ni ahadi ya ACT kwa Wazanzibar.

Tunakusudia, kama ulivyosema, ni bidhaa yetu tunaipeleka katika soko, soko ni wapiga kura, ni wanachi waamue. Kwa hiyo, wakiamua kwamba ACT-Wazalendo iongoze nchi maana yake wamekubali suala la Mamlaka Kamili na wengine wote watapaswa kufuata.

Kwa hiyo, si suala ambalo tunatarajia ndani ya kipindi hiki ambapo Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaongozwa na CCM kwamba ndiyo litatekelezwa, likitekelezwa sawa na pengine nguvu yetu ya ushawishi ndani ya muundo wa sasa wa Serikali si kubwa kiasi hicho.

Lakini kwa sasa hivi, kama nilivyosema, hii inabakia kwamba ni bidhaa yetu sokoni, tunawapelekea Wazanzibari waamue. Na tunaamini kwamba Wazanzibari walio wengi, kama ambavyo ilithibitishwa katika vipindi vingi, wanaunga mkono hoja hii.

Kwa hiyo, wakituunga mkono, wao watatukabidhi madaraka ya nchi na kupitia madaraka ya nchi ndiyo tutapoweza kusimamia sasa hoja hii kwa sababu sasa tuna madaraka ya kiserikali ya kutekeleza kile ambacho wananchi wa Zanzibar walikuwa wamekiunga mkono kupitia katika Uchaguzi Mkuu.

Kwa hiyo, tusichanganye haya mambo. Sisi suala ambalo tunalipeleka sasa hivi serikalini, kwa sababu tunaamini kwamba CCM kwa vyovyote hawezi kulikubali suala hili katika msimamo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Lakini huu ni msimamo wetu kama chama tutakwendanao na kuwashawishi Wazanzibari baina ya sasa hadi 2025. Na tunaamini kwamba bidhaa hii inatakiwa sana Zanzibar na itachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na baada ya hapo ACT-Wazalendo itasimamia utekelezaji wa suala hili kupitia mamlaka ambayo itakuwa imeyapata katika uchaguzi wa mwaka 2025.

The Chanzo: Kwa mfumo wa sasa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba iliyopo, unaona kwamba mtapata ruhusa hata kidogo ya nyinyi kuzungumzia Mamlaka Kamili pasi na kuchanganya Wazanzibari juu ya Muungano?

Ismail Jussa: Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano, kama ilivyo Katiba ya Zanzibar, inatoa haki ya watu kuwa na mawazo na kutoa mawazo yao nje. Lakini mbali ya hilo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano inazungumzia kwamba nchi yetu ni ya vyama vingi.

Katiba ya Zanzibar inazungumzia kwamba Zanzibar ni nchi ya vyama vingi na inaruhusu kila chama kuwa na sera na misimamo yake. Kwa hiyo, hakuna kikwazo chochote cha kikatiba, wala cha kisheria, ambacho kinazuia ACT-Wazalendo isisimamie inachokiamini.

Na ndiyo maana suala la Mamlaka Kamili labda kwa sasa tu kwa sababu tumelileta kama ni hoja ya pamoja labda linaonekana jipya lakini kama mtu anafuatilia siasa za Zanzibar si suala jipya kuzungumza katika majukwaa ya kisiasa na kama nilivyosema tunarudi hicho cheti ambacho ndiyo kimezaa muungano, huu Mkataba wa Muungano, Hati ya Muungano, yenyewe inazungumzia Mamlaka Kamili – Exclusive Authority – tafsiri yake ni Mamlaka Kamili imo ndani ya Katiba ya Muungano.

Kwa hiyo, si suala ambalo liko nje ya Katiba, si suala ambalo liko nje ya mfumo wa kisheria katika nchi yetu. Tunayo haki hiyo tumekuwa tukilitetea huko nyuma na tutaendelea kulizungumza kwa kasi zaidi sasa hivi ndiyo Wazanzibari waliunge mkono na liwe ndiyo chachu ya kubadilisha Muungano wetu kuwa Muungano wa haki, heshima na usawa ambao utazipa Zanzibar na Tanganyika, zote, nafasi, haki na fursa sawa katika Muungano huu badala ya mmoja kumdhibiti mwingine.

The Chanzo: Hii mnaweza kufanyaje, ni njia gani ambazo mnaweza kutumia kuleta huo mtiririko mzima wa Zanzibar kuwa na Mamlaka Kamili?

Ismail Jussa: Kama nilivyosema, kuna njia mbili: Moja, ni kupitia mjadala wa Katiba Mpya, kufanya ushawishi ili tuone kwamba muundo wa sasa wa Muungano haujaisaidia nchi hii na tunahitaji kubadilisha muundo wa Muungano ambao utaakisi Zanzibar na Tanganyika kila mmoja kuwa na mamlaka yake kamili na kushirikiana katika maeneo ambayo tutaamua kushirikiana kupitia Serikali ya Muungano. Kwa hiyo, hii ni hatua moja.

Lakini kama inashindikana kupitia mfumo huo, njia ya pili ni kuhakikisha tunashinda uchaguzi na ndiyo maana nikasema ‘Brand Promise’ ni bidhaa yetu, tunawapelekea watu.

Wakiiunga mkono, ACT-Wazalendo ikachaguliwa, na mimi naamini kwamba kwa bidhaa hii watatuunga mkono Wazanzibari na hata Watanganyika. Kwa hiyo, ACT-Wazalendo ikishika madaraka, njia yake ya kufikia Mamlaka Kamili sasa ushakuwa na mamlaka ya kiserikali wewe sasa ndiyo unasanifu sera na mwelekeo wa nchi yako.

Kwa hiyo, wakati huo tutakuwa na mamlaka ya kuweza kulisukuma kwa nguvu zote. Kwa hiyo kuna njia mbili, ama kupitia mjadala wa Katiba Mpya ikiwa imeshindikana hapo ni kupitia kushinda uchaguzi na mkishinda uchaguzi maana yake wananchi walio wengi wameunga mkono sera hiyo na kwa hivyo sasa mnakuwa na madaraka, au ridhaa, ya kutekeleza kile ambacho wananchi wanakitaka kupitia kukichagua chama chetu.

The Chanzo: Mheshimiwa Jussa, bado mna matumaini na wananchi kwenye kuwachagua kama ACT-Wazalendo kwenye kuongoza Zanzibar licha ya kupitia changamoto kadhaa miaka yote hiyo?

Ismail Jussa: Tunaamini na kama tungekuwa hatuamini tungevunja chama. Misukosuko tunaona sisi ni sehemu ya safari. Na wala sisi hatutokuwa wa mwanzo katika dunia, katika Afrika.

Kuna mifano mingi sana ya nchi ambazo zilikuwa na mifumo ya kikandamizaji ambayo haikuruhusu sauti ya watu kuheshimiwa kupitia katika chaguzi lakini hatimaye mabadiliko yamekuja.

Hapa hapa katika Afrika kuna vyama, kwa mfano, katika nchi kama za Senegal na wagombea ambao waligombea mara saba na hatimaye mwisho wakaongoza nchi. Zambia kulifanyika kila aina ya vituko lakini hatimaye mabadiliko yamekuja mwaka uliopita. Malawi na mifano mingine.

Kwa hiyo, na sisi tunapitia misukosuko mingi. Bado mifumo yetu ya kikatiba, ya kisheria, ya kiutawala haijafanywa kuheshimu maamuzi ya watu. Na tunarudi pale pale kwamba tangu mfumo wa vyama vingi uliporuhusiwa [tena mwaka 1992] bahati mbaya kulifanywa mabadiliko madogo tu ya kusema sasa nchi ni ya vyama vingi lakini mfumo mzima wa kikatiba, kisheria, na kiutawala ulibakishwa vilevile wa chama kimoja.

Sasa hivi kuna mazungumzo ambayo yamefanyika na nashukuru kwamba ACT-Wazalendo wakati kilikuwa kinabezwa na kufanyiwa kila aina ya dhihaka kwa kuamini katika suala la kufanya majadiliano na Serikali.

Wengine wakaamua kususa lakini mwelekeo wa ACT-Wazalendo ulipelekea hatimaye kuishawishi Serikali kikaundwa Kikosi Kazi. Na leo tunamzungumza mikutano ya hadhara, umeanza kunihoji hilo.

Mikutano ya hadhara yenyewe imeruhusiwa pamoja na kwamba ni haki yetu lakini iliporwa, imerejeshwa kupitia mazungumzo ambayo yamefanyika kupitia Kikosi Kazi, ni moja katika mapendekezo yake.

Lakini uzuri wake ni kwamba bado tunazungumza na katika mapendekezo yamo hata siku wanaruhusu mikutano ya hadhara mtakumbuka Rais Samia Suluhu Hassan kazungumzia suala la Katiba Mpya. Kazungumzia suala la mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi, kazungumzia mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Hivi sasa ninavyojua imeundwa tume ya kutazama masuala ya haki jinai katika nchi. Kwa hiyo, tunaamini kwamba tumeanza. Pengine tungependa twende kwa kasi zaidi. Pengine tungependa twende mbali zaidi. Lakini tunafurahi kwamba kuna hatua zimeanza kupigwa.

Tunaamini kwamba tutafika pahala tupata mabadiliko ambayo yatawezesha kufanyika uchaguzi unaoheshimu maamuzi ya watu. Na hata hapa Zanzibar kumeundwa Kikosi Kazi lakini mbali na Kikosi Kazi sisi kama ACT-Wazalendo tangu tulipoamua kuingia katika siasa za Umoja wa Kitaifa tulipeleka hoja zetu za msingi na karibuni kabisa tumezikumbushia na nafurahi pengine bado mapema kuzungumzia zaidi lakini kwamba kuna hatua zimeanza za kuhakikisha hayo yanatekelezwa.

Niwahakikishie tu wananchi kupitia kipindi chako hiki Najjat Omar na kupitia The Chanzo kwamba chama hichi hakitakubali hata siku moja kurudi tena katika hali ile ambayo tulikuwa huko nyuma.

Na ndiyo maana tumesema suala la muundo wa Tume ya Uchaguzi, kuwe na tume huru ya uchaguzi Zanzibar. Suala la Sheria ya Uchaguzi, mambo ya sijui kupiga kura siku mbili, haya hatutaweza kuyakubali hata siku moja na tunaona kuna mwelekeo wa kuweza kubadilika.

Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba tunayo imani na ndiyo maana bado chama kipo, sisi tupo tunaendelea kuwahamasisha watu kutuunga mkono na tunafurahi kwamba bado watu wana imani na sisi kama tulivyoona jana Nungwi na naamini hali itakuwa hivyo hivyo wiki hii kisiwani Pemba, Jumamosi [ya Machi 4, 2023,] kwamba watu wanaamini kwamba bado chama hiki ndiyo chombo sahihi cha kuwavusha kuelekea katika mabadiliko wanayoyahitaji katika visiwa hivi vya Unguja na Pemba.

The Chanzo: Kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, muna wawakilishi watatu, maana yake muna Makamu wa Kwanza wa Rais, muna waziri ambaye anasimamia masuala ya viwanda na maendeleo ya biashara na mna waziri kutoka wizara ya afya. Wakiwa kama wawakilishi wenu, munaona wanawatendea haki Wazanzibari kwenye kuwatetea masuala kadhaa ambayo yanawahusu? Kwa sababu wanapowakilisha timu kubwa inatoka Chama cha Mapinduzi. Munaona wanapiga hatua kwenye kuwasemea, au ni kwa sababu munazungumza haya wakati munasahau mambo mengine ambayo kama Wazanzibari wanayahitaji?

Ismail Jussa: Hapana. Mimi naamini wanatenda haki na ushahidi wa hilo hao viongozi wa upande wa pili, wa Chama cha Mapinduzi, wametoka hadharani kukiri kwamba katika mawaziri wanaotenda kazi na kuwajibika ipasavyo ni mawaziri hawa wanaotoka ACT-Wazalendo. Kwa hiyo, hilo wamelithibitisha.

Kikwazo ambacho kipo Najjat, wala hichi hatukikatai, na hichi kimekuwa siyo katika kipindi hichi tu, hata katika kipindi cha mwanzo cha Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya mwaka 2010 mpaka 2015, ni kwamba yale ambayo tuliyatarajia kwamba muundo huu usingeishia pale tulipoanzia tu kidogo kidogo tungepiga hatua zaidi. Bahati mbaya hilo halijafanyika.

Kwa hiyo, tunahitaji kuwa na mabadiliko hayo yanafanyika na moja katika jambo ambalo tunalisukuma katika haya mazungumzo ambayo yanaendelea ni kuona hilo linfanyika.

Mtakumbuka hata katika mkutano ambao ulifanyika [hotel ya] Golden Tulip pale wahusika mbalimbali wa masuala ya kidemokrasia walizungumzia haja ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuteremka hadi ngazi ya chini.

Sasa kwa nini nimelisema hili? Kwa sababu unaweza kuwa na mawaziri, unaweza kuwa una Makamu wa Kwanza wa Rais, lakini mfumo mzima ambao uko pale anaosimamia bado ni ule ule wa kizamani, pengine nguvu ya ushawishi kama ulivyosema kutokana na uchache katika Baraza la Mapinduzi ambalo ndiyo Baraza la Mawaziri kwa Zanzibar si kubwa.

Na kwa hivyo pengine kunakuwa na uzito na ugumu fulani katika kushawishi mabadiliko ya kisera. Na ndiyo maana tunachosema tunarudi pale pale, tunaamini mabadiliko ya kisera yatakuja pale ambapo ACT-Wazalendo inaiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

 

Na ndiyo maana tunarudi pale pale ‘Brand Promise’ ni ahadi yetu kwa Wazanzibari kwamba haya mabadiliko makubwa mnayoyataka ya kisera, ya kimfumo, yatakuja ikiwa ACT-Wazalendo ni kiongozi wa Serikali.

Lakini kwa sasa angalau kwa ngazi ya kiutendaji na ngazi ya kiusimamizi, ngazi ya kiuwajibikaji, wameonekana mawaziri wetu, wameonekana Makamu wa Kwanza wa Rais kiasi gani wamekuwa wakitumia ule mtindo na mifumo ya kufanya kazi ya ACT-Wazalendo ambayo inahimiza uwajibikaji.

Na niseme tu ni bahati mbaya kwamba wanaoongoza Serikali hawajakwenda hatua zaidi kwa sababu mnapokuwa na mtu kama Makamu wa Kwanza wa Rais aliyekuwepo sasa Mheshimiwa Masoud Othman Masoud, hiki ni kichwa kwa Zanzibar na watu wote wanamuoana anapozungumza tu huyu mtu ana maarifa makubwa katika mambo mengi ya Zanzibar, ya Tanzania ya ulimwengu kwa ujumla.

Ndiyo maana mtu huyu alifika kiaminiwa na shirika la WIPO la Umoja wa Mataifa la World Intellectual Property Organization. Kuliwakilisha bara zima la Afrika kama mjumbe wake.

Sasa ana maarifa makubwa lakini bahati mbaya  wakati mwingine watawala wanashindwa kutumia maarifa na uzoefu aliokuwa nao. Mimi naamini kwamba yangetumika tungefika mbali zaidi.

Lakini kwa sasa pale ambapo wanapewa nafasi ya kushiriki wametoa mchango wao na nafikiri hilo linaonekana. Moja nafikiri ambalo bado mnaliona leo dogo lakini siyo dogo, suala la bei ya karafuu.

Kwa miaka mingi watu walikandamizwa hapa, ni msukumo wa mawaziri wetu kwamba ikiwa hakujafanyika ubinafsishaji wa zao hili, basi angalau tufike pahala kwamba wakulima walipwe asilimia 80 ya bei ya soko la dunia. Na hilo limefanyika.

kwa hiyo, ni katika hatua ambazo tumezipiga kupitia mawaziri wetu. Lakini nakubali kwamba ili waweze kutoa mchango mkubwa zaidi tunahitaji ACT-Wazalendo iongoze Serikali na mimi naamini kutokea 2025 Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar itaongozwa na Rais kutoka ACT-Wazalendo itaongozwa na Serikali ambayo wengi wa mawaziri wake watatoka ACT-Wazalendo.

The Chanzo: Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alizungumzia kwenye taarifa yake wakati anasoma kama taarifa kwa wanachama na viongozi kadhaa wa ACT-Wazalendo Februari 25, 2023 pale kwenye ukumbi wa kuzindua ‘Brand Promise.’ Ni mara nyingi zaidi ametamka neno makubaliano, maridhiano, makubaliano, maridhiano. Kwa nini ACT mnapenda maridhiano na makubaliano na mnataka makubaliano na maridhiano na nani ikiwa nyie mnatamani kukiondoa Chama cha Mapinduzi?

Ismail Jussa: Swali zuri sana. Kukiondoa Chama cha Mapinduzi ni lengo la kila chama cha siasa ambacho kinajitambua. Kwa sababu kila chama kinaundwa kwa sababu kinaamimini katika sera ambazo inakwenda kuzitekeleza na unaweza kuzitekeleza tu ikiwa unaongoza Serikali.

Lakini kwa Zanzibar, tulifanya maamuzi makusudi kabisa mwaka 2009 kwamba kwa kutizama historia yetu, tumegundua kwamba siasa zetu zimekuwa za ushindani ambao umevuka kiwango cha kifikia uhasama.

Kwa hiyo, matokeo yake ungetegemea katika hali ya kawaida vyama vinakwenda katika ushindani, chama kimoja kinashinda, kinaongoza Serikali, chama kingine kinakuwa cha upinzani, kinasubiri miaka mitano kijenge tena ushawishi, kama kitakubalika kirudi tena madarakani.

Lakini bahati mbaya kwa Zanzibar tukagundua kwamba ule uhasama umefika pahala kwamba hakuna kuaminiana na ndiyo maana upinzani iwe [ni] ACT-Wazalendo au huko nyuma chama kingine umekuwa ukishinda chaguzi zote tangu mwaka 1995.

Na ripoti mbalimbali za waangalizi wa uchaguzi zimekuwa zikithibitisha hayo na ndiyo maana unafutwa uchaguzi mwaka 2015 alivyofanya [aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar] Jecha [Salim Jecha] kwa sababu CCM imeshakwama tayari, haiwezi njia nyingine ya kufanya zaidi ya kufuta uchaguzi.

Mwaka 2020 ndiyo kabisa hata uchaguzi wenyewe haukufanyika, maana yake unafika pale mimi nilikuwa mgombea. Hata kuruhusiwa kuingia katika kituo cha uchaguzi hauruhusiwi mgombea.

Kwa hiyo, wameona kwamba hawakubaliki. Sasa [mwaka] 2009 ndiyo tulijaribu sisi ilikuwa ni kuona kwamba pengine inafika hivi kwamba watu hawako tayari kukabidhi madaraka, hawako tayari kuheshimu maamuzi ya watu kwa sababu ya hofu kwamba watapoteza kila kitu na pengine kutokana na siasa zetu zilivyo labda kutakuwa na ulipizaji wa visasi na mambo mengine kama hayo. Tukasema mfumo huu wa mshindi kuchukua kila kitu ndiyo unaokwaza hilo.

Kwa hiyo, tukiwa na mfumo wa kufanya kazi pamoja kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa italeta msingi wa kwamba ndiyo mmoja ameibuka mshindi kwa watu wengi kwa maana kwamba ameungwa mkono na walio wengi kwa hiyo sera zake kwa kiasi kikubwa zitaongoza lakini amshirikishe na mwenzake ili ile hofu ya kwamba huyu akipata amepata kila kitu na huyu akipoteza amepoteza kila kitu.

Huo ndiyo msingi kwa nini kila wakati Makamu Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Othman Masoud Othman na chama chetu cha ACT-Wazalendo na sisi sote kila wakati tunasisitiza suala la maridhiano na makubaliano kwa sababu tunaamini katika dunia ya leo pengine mfumo huo ndiyo mfumo bora zaidi wa kuendesha nchi.

Na bahati nzuri imethibitika kile ambacho kuna vyama vilitukejeli wakati ule hatukuwa ACT-Wazalendo, lakini walitukejeli, walituita kila majina mabaya hapa mwaka 2010 kwa sababu ya kukubali Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini pia kwa sababu ya kuzungumzia maridhiano.

Tukaambiwa waponyaji wa nchi lakini leo lugha hizi tunazisikia kutoka katika vyama vilevile vilivyokuwa vikitufanyia kejeli zile. Wao ndiyo wamekuwa wahubiri wakubwa zaidi na kutaka kujimilikisha kwamba wao ndiyo waasisi wa hoja za maridhiano, hoja za kuponya nchi.

Kwa hiyo, tunathibisha kwamba sisi siku zote tumekuwa tukitangulia, tukiwaonesha wengine njia. Kwa hiyo, suala la makubaliano na maridhiano ni mifumo ya kisasa.

Nadhani tumefika pahala kwamba dunia itafika pale ije ijifunze kwamba uchaguzi unapaswa kuamua yupi aongoze nchi lakini haina maana ya kwamba yule ambaye ameshindwa atoke kabisa katika uendeshaji wa nchi.

Kwa hiyo, ndiyo tunaamini kwamba maridhiano na makubaliano [ni] jambo la msingi kwa sababu tunaamini ndiyo njia pekee ya kuwaleta pamoja Wazanzibari ambao siasa za uhasama zimewatenganisha kwa zaidi ya miaka 60.

The Chanzo: Kabla hatujahamia upande mwingine, tukiacha mambo ya Zanzibar Moja, Zanzibar Mpya, Mamlaka Kamili. Ni kwa nini ACT-Wazalendo inataka kuifanya kama Scotland, kwa nini ufananishe Zanzibar kama Scotland kama Singapore, kama Dubai kama Hong Kong? Kwa nini ACT-Wazalendo haitaki kuona kwamba ina haki ya kuisimamia Zanzibar kama Zanzibar na watu wengine wakatuiga lakini mnataka kuifananisha Zanzibar na miji, ama na nchi, zingine zilizopiga maendeleo zaidi?

Ismail Jussa: Waswahili wanasema chema chajiuza kibaya chajitembeza. Na ni kawaida katika lugha mnakuwa mnapiga mifano. Kwa hiyo, mifano nitakayochukua ni ile ambayo ni mifano mema, mifano ambayo imefanikiwa vizuri zaidi.

Sasa tunaposema kwamba tunataka kuifanya Zanzibar kuwa kama Singapore, au wegine wameizungumzia Dubai, wengine wamezungumzia Hong Kong, ni kwa sababau gani?

Kwanza, mazingira ya maeneo haya, au nchi hizi, yanafanana na Zanzibar. Ni maeneo madogo ambayo yametumia maeneo yake yalipo kimkakati, Wazungu wanaita strategic location.

Kama ambavyo Zanzibar ipo ikaweza kwamba kuwa vituo vikuu vya kibiashara, ikaweza kuwa ni vituo vikuu vya huduma za kifedha na mabenki, ikaweza kuwa ni vituo vikuu vya uchumi wa huduma kama ambavyo nilizungumza pale, kwamba Zanzibar kwa kukosa kwake Mamlaka Kamili inakosa nguvu za kuweza kutekeleza hayo.

Sasa tunapotumia mifano hii sisi tunataka kuwafanya Wazanzibar waone kule ambako tunataka kuifikisha Zanzibar. Na ikishafika wakati huo Zanzibar haitakuwa tena Singapore au Dubai. Zanzibar itakuwa ni Zanzibar.

Lakini wakati huo sasa itakuwa labda itakuwa imefikia kiwango kile, au pengine zaidi ya kile, Zanzibar yenyewe ikawa mfano kwa wengine. Kuna kitu hapa kinazungumzwa Najjat na wazee wanasema wakati fulani Zanzibar ilipokuwa Zanzibar ikitikisa katika dunia hii.

Aliyekuwa mtawala wa Dubai, Marehemu Rashid bin Saeed Al Maktoum, alikuwa mwenyewe akifanya usafiri wa majahazi kuleta biashara. Na inasemekana mara moja, au mbili, mwenyewe aliwahi kuja na siku zote ilikuwa Zanzibar ndiyo kigezo chao kwa miaka ile.

Na ndiyo maana watu wengi walihama wakaja wakahamia Zanzibar kutokana na kivutio chake. Kwa hiyo, tumeipoteza katikati fursa hii kutokana na siasa za magomvi, kutokana na kutokuwa na Mamlaka Kamili baada ya kuingizwa katika mfumo wa Muungano ambao unainyima Zanzibar haki na fursa za kujiamulia sera zake.

Ninachoamini kwamba kupitia sera, mtazamo, ahadi ya ACT-Wazalendo kwa Zanzibar tukiitekeleza kwamba Zanzibar itaweza kuvuka hata kule ambako ilikuwa zamani. Na kwa hivyo, kwa sasa hivi kigezo chetu ni kuwa Singapore ya Afrika Mashariki.

Lakini inafika pahala pengine nchi zingine za duniani ziseme tunataka kuwa kama Zanzibar katika eneo letu, ndiyo malengo yetu hayo.

The Chanzo: Jana na juzi tarehe 25 na tarehe 26 [Februari], mna sentensi moja mara kadhaa mnaitumia kusema kwamba Wazanzibari wanataka elimu bora, Wazanzibari wanataka afya bora, Wazanzibari wanataka vitu kadhaa vya ubora. Lakini Mheshimiwa Jussa, mnakumbuka hawa Wazanzibari mnaowazungumzia siyo Wazanzibari wa ACT-wazalendo tu, ni Wazanzibar ambao wana vyama vingine vya upinzani. Kwa nini munaona wanataka hivyo ilihali kuna watu wanafuata vyama vingine vya mrengo mwingine. Na pengine wameridhika, mmejuaje kwamba wanataka vitu vyote hivyo.

Ismail Jussa: Hizi ni lugha. Unaposema kwa lugha ya jumla Wazanzibari tunakusudia walio wengi, haina maana kwamba asilimia 100  ya watu watakuwa na mtazamo unaofanana.

Lakini unapozungumzia zaidi ya nusu ya watu ndiyo kundi linatumika kutambulisha watu wa nchi. Kwa hiyo, tunaposema kwamba Wazanzibari wanayataka haya kwa sababu wamethibitisha kwa miongo kadhaa sasa kupitia chaguzi mbalimbali ya kwamba wanataka mabadiliko na hoja ambazo vyama vinavyopigania mabadiliko tumekuwa tukizieleza ni hoja hizi hizi, pengine kwa lugha tofauti tu.

Kwa hiyo, linalotupa nguvu na ujasiri na kujiamini tunaposema kwamba Wazanzibari wanataka tunaweza kuwa pengine una asilimia 10, pengine asilimia 20, ndiyo binadamu. Kuna mwingine labda ile dhiki yake anaipenda – ingawa mimi ni tabu kuamini kwamba kuna mtu ambaye hataki elimu bora, kuna mtu ambaye hataki afya bora, kuna ambaye hataki badala ya kutoka na madumu ya maji akateke nje ambaye hatamani kuona kwamba mfereji ndani ya nyumba yake akifungua kama ambavyo tulivyokulia tunavyokumbuka unatoka maji bila kuwasha pampu akatumia umeme wa ziada wala kuhangaika.

Kwa sababu zamani hatukuwa na mambo haya na unapokuwa na miundo sawasawa ya huduma hizi, hutegemei mambo haya. Sidhani kama Mzanzibari hataki kuwa na uchumi mzuri ambao unatoa ajira ili kuondokana kila nyumba leo tumekuwa tunafuga vijana.

Si kama wanapenda lakini hawana la kufanya. Kijana tangu anasomeshwa na mzee wake mpaka anakuwa amefika pahala na yeye ahudumie jamii bado anaendelea kutegemea baba na mama nyumbani. Sidhani kama kuna mtu anaridhika na hali kama hiyo.

Ndiyo maana tukasema kwamba Wazanzibari wanataka haya kwa sababu kila Mzanzibari anataka kuishi maisha ya heshima yenye kipato stahiki na ajira yenye heshima.

Tunaamini kwamba kila Mzanzibari anataka kuishi katika jamii ambayo ina haki na ina usawa na inatemndea kila mtu vile ambavyo sheria inamtendea kila mwingine. Siyo kwamba kuna watu wako juu ya sheria, kuna wengine wako chini ya sheria.

Na tunaamini vilevile kwamba kila Mzanzibari anataka kuishi katika Zanzibar ambayo ina heshima yake, hadhi na haiba yake ikiwa na Mamlaka Kamili, siyo kugeuzwa kuwa koloni la nchi nyingine.

Kwa hiyo, ndiyo maana tunachosema haya matatu – maisha ya heshima yenye kutoa ajira na kipato stahiki, maisha ambayo ndani yake mtu anaishi katika haki, usawa, umoja na maridhiano [na] maisha ambayo Zanzibar ina heshima yake, ina haiba yake kama nchi miongoni mwa nchi – naamini haya ni mambo ambayo kila Mzanzibari mwenye kuipenda nchi yake anayataka.

The Chanzo: Maalim Seif Sharif Hamad, ukiwa kama mtu wake wa karibu sana kwenye mrengo wa kisiasa, unaendeleaje tugeukie huko sasa. Kwa kidogo sana.

Ismail Jussa: Mimi mwenyewe binafsi?

The Chanzo: Wewe mwenyewe binafsi, kwa upande wa chama lakini ukiwa binafsi lakini kwa upande wa chama.

Ismail Jussa: Hakuna mtu ambaye atasema kwamba hakuonekani kule kukosekana kwa Maalim Seif kwamba hakuonekani athari yake. Utakuwa unajidanganya. Maalim Seif ni aina ya viongozi duniani, ni aina ya viongozi duniani ambao wanazaliwa mmoja kwa karne moja au miaka 50, wakaishi na wakawa wameathiri kila nyanja ya maisha ya watu.

Tunazungumzia, kwa mfano, unapomzungumzia Mahatma  Gandhi wa India mpaka leo anakumbukwa. Unapomzungumzia Nelson Mandela wa Afrika Kusini mpaka leo anakumbukwa. Unapomzungumzia kwa mfano Fidel Castro wa Cuba na viongozi wengine kama hao.

Kwa hiyo, ni viongozi ambao Mwenyezi Mungu anawaleta kama ni hidaya katika jamii. Na Maalim [Seif] alikuwa ni wa namna hiyo. Tumeona siku alipoondoka duniani kama kuna mtu alikuwa ana shaka nadhani siku ile alijua kwamba yupi alikuwa chaguo la umma siku zote kuwa Rais wao.

Kutokana na jinsi nchi ilivyokuwa imejiinamia na umma ulivyotoka mabarabarani. Kwa hiyo, hakuna mtu anaweza kukataa kwamba kuondoka kwa Maalim Seif hakujaacha pengo, hakujaacha athari.

Lakini nitatumia lugha ambayo amewahi kuniambia ndugu yangu Mansour Yusuph Himid. Siku moja wakati tunazungumzia na tunatafakari, tunajadili juu ya kuondoka kwa Maalim Seif na ni vipi tunapaswa kuwa, akaniambia kwamba Maalim ulikuwa mwamba na kujaza nafasi yake huo mwamba mwingine kama yeye haupo. Isipokuwa tunapaswa kukusanya miamba midogo midogo kila mmoja ikiwa na nguvu yake ichanganye nguvu kufikia huu mmoja.

Kwa hiyo, ndiyo akasema yeye miamba hiyo ni nani? Uchukue nguvu aliyokuwanayo Othman Masoud, ichukue nguvu ambayo anayo Mansour Yusuph Himid, ichukue nguvu ambayo aliyokuwa nayo Juma Duni Haji, uichukue nguvu ambayo anayo Nassor Mazrui, ichukue pengine nguvu anayo Salum Bimani, anayo Fatma Fereji, anayo Jussa, kwa Zanzibar, na kwa [Tanzania] Bara pengine uchukue nguvu ambayo anayo Zitto Kabwe anayo Doroth Semu, anayo Ado Shaibu Ado, anayo Jorum Bashange wanayo wengine, wote kwa pamoja hii ikikusanyika ndiyo inaweza ikaziba nafasi ya ule mwamba kwa pamoja.

Kwa hiyo, sisi tunalichukulia hivyo kwamba tuna dhamana kubwa sana ya kuhakikisha kwamba yale ambayo Maalim Seif aliyasimamia, yale ambayo alitufunza, tunayaendeleza, tukitambua kwamba mmoja wetu miongoni mwetu hawezi akalifanya lile peke yake lakini sote, kwa umoja wetu, tunaweza kufanya yale ambayo alikuwa anayaamini.

Na mimi naamini huko aliko Maalim [Seif] roho yake iko radhi, ina furaha, kwa kuona kwamba aliowaacha nyuma wanaendeleza kile kile ambacho yeye alikisimamia katika uhai wake wa kisiasa.

The Chanzo: Unaona kuna pengo kubwa kwenye chama chenu kwa Mwenyezi Mungu kumtanguliza yeye?

Ismail Jussa: Tunamkumbuka lakini tukisema, kama nilivyosema, nafikiri nilijibu kwamba kwa yeye kama kiongozi mmoja bila shaka. Lakini tunaweza kusema hatuoni pengo kwa sababu naona kama tumekuja na ari kubwa zaidi ya sote kila mmoja kujituma kwa nguvu zaidi na kutoa mchango wake ili lile pengo lisionekane.

Nafikiri tumeona watu wengi walikuwa wakifanya dhihaka kwamba labda Maalim Seif akiondoka kwamba harakati hizi zitayumba lakini nadhani wiki hii wamepata jawabu na Jumamosi watapata jawapo kubwa zaidi Tibirinzi.

Kwamba umma wa nchi hii ulihitimu kwa Maalim wao wa siasa na kile ambacho alikisimamia wanakiendeleza kupitia viongozi wao na kwamba kuondoka kwa Maalim Seif badala kukuhesabu kwamba ni pengo na pigo kunawaongezea ari ya kusimamia kile ambacho amekisimamia wakati wa uhai wake hata baada ya yeye kuwa hayupo na sisi.

The Chanzo: Kuna msemo ulikuwa unasemwa wiki mbili mpaka tatu nyuma kabla ya mikutano ya hadhara kuanza. Wanasema watu mmelamba asali, nataka kujua kwa Zanzibar na nanyi mmelamba asali, kwamba mnawazungumzia Wazanzibari mbele ya sura kwamba mnataka mabadiliko lakini mna ajenda zingine za siri?

Ismail Jussa: Bahati nzuri katika waliotuhumiwa kulamba asali sisi wa ACT-Wazalendo hatukuwemo. Wako watu na mwenyewe katoka hadharani kusema kwamba wenzake wanamtuhumu kulamba asali na inamsumbua sana.

Sisi tunashukuru Mungu sote tunaaminika kwa sababu tunajenga imani miaka nenda, miaka rudi, watu wanatuamini na ndiyo maana hata katika chama chetu husikii watu kushutumiana, wala hujamsikia kiongozi wetu akitoka hadharani kusema wenzake wanamshutumu kalamba asali. Kwa hiyo, hilo tumuachie yule ambaye anatuhumiwa, alijibu, sisi kwetu halipo.

The Chanzo: Nataka kumalizia swali la mwisho sana. Mamlaka Kamili ikipatikana, narudi kidogo kule nyuma maana yake ndiyo nahitimisha, Mamlaka Kamili ikipatikana, ACT-Wazalendo mmeichora Zanzibar kwenye muonekano upi?

Ismail Jussa: Mamlaka Kamili yakipatikana ambayo ndani yake pia kutapatikana Zanzibar Mpya na Zanzibar Moja, taswira yetu tunayoichora ni ile ambayo mwananchi wa Zanzibar atakuwa anaishi katika nchi ambayo kwanza ina amani ya kweli, kwa sababu ndani yake haki za kila mmoja zinaheshimiwa.

Zanzibar ambayo kijana hatokaa barazani akashtukizia ghafla anavamiwa, iwe na mazombi au makundi ya watu wasiojulikana au hata vikosi vingine kwa sababu tu ameamua kutumia uhuru wake wa kukaa na wenzake wakazungumza.

Tunataka kila mmoja aishi vizuri kabisa. Lakini tuna imani pia ya Zanzibar ambayo itakuwa inaongozwa na ACT-Wazalendo chini ya Mamlaka Kamili ambapo Zanzibar itakuwa haiendi tena kupiga magoti kwa nchi nyingine, au kiongozi wa nchi nyingine, ili kuweza kufanya maamuzi yake ya kisera.

Ni Zanzibar ambayo inaweza kusimama kwa miguu yake ikafanya maamuzi sahihi ya kisera, yawe sera za fedha, sera za uchumi, sera za kodi, sera za elimu, sera za mawasiliano ambazo zitakuwa na maslahi na watu wake.

Tunaichora Zanzibar ambayo itakuwa kila kijana na kila mtu anaweza kupata ajira ambayo itampa maisha ya heshima na ambayo itampa kipato stahiki.

Siyo ajira tu ile ambayo tumezoea kusema hapa ya kumpatia pesa ya sabuni. Mtu hahitaji kufua tu. Mtu anahitaji kwanza ale vizuri, apate milo mitatu, tena mlo ambao una heshima ambao anastahiki kula binadamu.

Tunahitaji kuona kwamba mtu halali akiwaza kesho asubuhi akiamka nitakula nini na hayo yanawezekana kabisa. Tunahitaji kuona kwamba tunaichora Zanzibar ambayo ndani yake watu wote wanapendana, wanasaidiana [na] hawabaguani.

Lakini zaidi tunahitaji kuona Zanzibar ambayo mtu akiumwa hahitaji kujitazama mara mbilimbili, kwamba mimi nikiwa sina siwezi kutibiwa, anakwenda katika hospitali ambazo zina vifaa vyote, zina madaktari bingwa, zina wauguzi wenye heshima na wanaweza kupata haki zao zote.

Tunataka kuona kwamba Zanzibar ambayo watu wataamka wakiishi chini ya ACT-Wazalendo ambapo vyombo vya ulinzi na usalama vinawatumikia watu badala ya kuwakandamiza watu. Badala ya kuwa na Jeshi la Polisi tuwe na Huduma ya Polisi.

Yaani badala ya kuwa na Police Force tuwe na Police Service. Vikosi vya SMZ hivi tuvione vikitumikia watu. Kama KMKM imeundwa ili kulinda mwambao wetu na watu wanapopata ajali pengine kuweza kuhudumiwa ifanye kazi hiyo badala ya kuonekana mitaani ikidhuru watu.

Tunataka kuiona Zanzibar ambayo imekuwa kituo kikubwa cha huduma za biashara. Zanzibar ambayo bandari yake ina harakati saa zote, bandari kubwa itakayoweza kuhudumia siyo tu Zanzibar, [bali] ukanda wote wa Afrika Mashariki.

Tunataka kuona uwanja wa ndege wa kisasa siyo ambao unapendelea kampuni fulani kwa sababu pengine watu wana maslahi fulani huko lakini iwe inatoa fursa kwa Wazanzibari wenyewe, kampuni za ndani ziweze kupata nafasi, Wazanzibari waweze kupata ajira, nchi iwe na harakati saa zote, kila mtu aweze kuishi kwa furaha kabisa.

Hiyo ndiyo aina ya Zanzibar ambayo tunaitarajia na In Shah Allah itapatikana chini ya ACT-Wazalendo.

Najjat Omar amefanya mahojiano haya. Omari Mikoma alibadilisha mahojiano hayo kutoka sauti kwenda maneno. Lukelo Francis amehariri mazungumzo haya. Shafii Hamisi na Nassor Nassor walisimamia mahojiano haya. Kwa mrejesho, wasiliana nasi kupitia: editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *