Maneno, tabia, na matendo ndiyo huonyesha picha halisi ya mwenendo wa maisha ya mwanadamu, na kwa kiwango kikubwa hutokana na malezi mtu aliyoyapata akiwa mdogo.
Hii maana yake ni kwamba, mwenendo wa maisha yako mzazi, ikiwemo mahusiano uliyonayo na mwenza wako, majirani, ndugu, marafiki, nakadhalika, pamoja na jinsi mnavyozungumza, hujenga tabia na mwenendo wa maisha wa mtoto wako.
Tafiti mbalimbali za saikolojia ya makuzi ya mtoto zinamuonyesha mzazi kama kiongozi wa familia, ina maana awe mfano wa kuigwa kwa watoto, ajiheshimu na kuheshimu wenzake kwa kutenda matendo mema na yanayofaa.
Pia, achague maneno ya kusema mbele ya watoto, hasa awapo na hasira. Tutambue kuwa, watoto hawazaliwi na misamiati ya matusi na maneno ya ovyo; wanapata tabia hizi kutoka kwa jamii zinazowazunguka.
Tunafahamu kuwa malezi ya mtoto hayaishii katika kumpatia mahitaji muhimu tu. Urithi muhimu anaoupata mtoto kutoka kwa mzazi wake ni jinsi ya kuishi na watu.
SOMA ZAIDI: Tujadili Kuhusu Upakiaji Picha za Watoto Mitandaoni
Hivyo, ukijisahau, ukaendelea kupiga soga-zembe na rafiki zako, huku mkitumia maneno makali yasiyofaa masikioni mwa watoto, utakuwa huwajengei msingi wa maadili mema na itachukua muda mwingi kuwarekebisha kinidhamu watoto wako kama ukiwalea katika mazingira hayo.
Tafiti pia zinatoa ushahidi juu ya wanaume na wanawake wanaowapiga wenzi wao wa ndoa. Si vyema wazazi ndani ya familia kupigana na kutoleana lugha chafu mbele ya watoto.
Mwenendo huu wa maisha una athari kubwa kwa makuzi na maendeleo ya watoto kisaikoloja.
Kwanza, huwafanya watoto kuwa na chuki dhidi ya mzazi mmoja lakini pia humjengea mtoto imani kuwa matusi na vipigo ni mambo ya kawaida katika mahusiano, hivyo huweza kuendeleza matendo hayo kwenye familia zao huko baadaye.
Mwenendo huu wa maisha ndiyo moja ya sababu kubwa ya muendelezo wa tabia na vitendo vya kikatili katika jamii zetu.
SOMA ZAIDI: Tuongee Kuhusu Matumizi ya Simu, TV na Mitandao kwa Watoto
Watoto wanaolelewa na wazazi wenye mwenendo mzuri wa maisha huwa na maadili mema, nidhamu, busara na uwezo mkubwa wa kuchanganua na kukabiliana na changamoto za maisha wakiwa wakubwa.
Pia, hujituma katika utendaji kazi na ni rahisi kufuata ushauri na muongozo wanaopatiwa na wazazi wao na watu wazima wengine katika jamii.
Kama mzazi, ufanye nini ili watoto wako wawe na mwenendo mzuri wa maisha?
Kwanza, jitathmini mwenendo wako wa maisha, jiulize, unaongea maneno gani na kwa namna gani ukiwa na watoto wako? Una mahusiano ya namna gani na jamii inayokuzunguka?
Marafiki zako ni watu wa aina gani? Na mnasemezana vipi na mzazi mwenzako mbele za watoto wenu? Kisha angalia mtoto wako anaiga vitu gani kutoka kwako?
SOMA ZAIDI: Je, Wazazi Tunajua Watoto Wetu Wanashinda, Kucheza Wapi?
Majibu yako ndiyo yatakayoonyesha mabadiliko unayopasa kufanya. Usisahau kwamba wewe ndiyo mwalimu wa kwanza wa mtoto wako; kama unatamani aje kuishi maisha yenye maadili mema, huna budi kuwa mfano bora wa kuigwa.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.