Kuna msemo usemao malezi ya mtoto ni jukumu la kijiji kizima, na kwa tamaduni zetu za Kiafrika siyo jambo la kushtusha kwa bibi, shangazi au mjomba kuchukua jukumu la kumlea mtoto wa familia mwenye uhitaji.
Hii hutokea kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kifo cha wazazi, kutengana kwa wazazi, ujauzito ulokuja bila mipango, nakadhalika. Pia, wakati mwingine, mzazi unahitaji kupumzika na kuchukua muda wa peke yako bila watoto, hivyo ni vizuri kuwa na watu wa karibu kama ndugu ambao wanafahamika na watoto wako kukusaidia pale changamoto yoyote itakapotokea.
Siku hizi, hata hivyo, desturi hii imepungua. Watoto wengi sasa wanakuzwa bila kujua wazazi na ndugu zao wa familia tandaa kwa sababu nyingi, ikiwemo umbali wa familia, kutelekeza ujauzito, kutelekeza watoto na baadhi ya wazazi, hasa wa kiume, kukimbia majukumu yao ya kuwahudumia watoto au familia kwa ujumla.
Ikitokea mzazi mmoja au wote wawili wamefariki na watoto hawajaachwa katika mikono salama, watoto hawa huishia katika vituo vya misaada au mitaani. Je, watoto wangapi wangenusurika kuishi katika hali hizi kama wangekua na ndugu wanaowafahamu na kutaka kuwalea?
Kuna wazazi wanaowaficha watoto chimbuko lao bila kujua wanatenda kosa la jinai. Kwa kiasi kikubwa, wazazi wa kike wanaongoza kwa kitendo hiki, labda kwa sababu wao ndiyo huachwa na ujauzito na mara kadhaa hutelekezewa watoto au mimba na wazazi wenzao wa kiume.
SOMA ZAIDI: Tuzungumze Kuhusu Umuhimu wa Michezo kwa Watoto
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inamtaka mlezi kumfahamisha mtoto wazazi wake wa kumzaa na ndugu zake wengine.
Vilevile, katika kuhakikisha mtoto kamwe hapatwi na ndugu zake, wazazi hawa huwabadilisha watoto majina ya baba zao na kuwaita ya wajomba zao au ya babu zao wa upande wa mama, na pengine huwaambia watoto kuwa baba zao walishakufa ingawa wanajua wako hai.
Kwa mtazamo wa kawaida unaweza kuwalaumu sana wazazi wa namna hii kwa vitendo hivi, lakini ukifuatilia mlolongo wa matukio yaliyowapelekea wao kufanya hivi, ikiwemo maumivu ya kutelekezwa na ujauzito, unaweza ukawaelewa kwa kiasi fulani.
Lakini hii haiwapi haki ya kumnyima mtoto kuujua ukweli wa chimbuko lake. Kifungu cha sita cha Sheria ya Mtoto kinamkataza mzazi kumnyima mtoto haki ya kujua chimbuko lake.
“Mtoto atakuwa na haki ya jina, utaifa na kuwafahamu wazazi wake wa kumzaa na ndugu wengine wa familia tandaa,” kifungu hicho kinaeleza.
SOMA ZAIDI: Je, Watoto Wako Wanamheshimu Dada wa Kazi?
Kwa upande mmoja, jamii imechukulia vitendo hivi kuwa vya kawaida bila kujua ni kwa kiasi gani vinamuathiri mtoto katika makuzi na maendeleo yake hasa kisaikolojia.
Matokeo ya athari ambazo hutokana na suala hili hubainika pale mtoto anapoanza kuhoji kuhusu chimbuko lake kwa kumuuliza mama kuwa baba yuko wapi au kumuuliza baba kuwa mama yuko wapi au pengine ndugu wanaomzuguka.
Wakati mwingine wazazi huingia katika ugomvi mkubwa na watoto wao kiasi cha kujibizana kwa ukali kwa sababu tu mtoto anataka kujua chimbuko lake. Wakati akiwa mdogo ni vigumu kugundua ni kwa kiasi gani mtoto anateseka kwa kutokujua wazazi ama mzazi wake.
Hii ni kwa sababu wazazi, ukiacha kuwaficha watoto juu ya chimbuko lao, pia huwaeleza kuhusu ugomvi uliopo au uliowahi kutokea baina ya wazazi.
Kumhusisha mtoto katika ugomvi wa wazazi si jambo zuri kwani mtoto hahusiki, kwa namna yeyote ile, katika ugomvi wenu, hasa unaohusu maamuzi na mipango ya kumleta duniani.
SOMA ZAIDI: Je, Unamshirikisha Mtoto Wako Katika Kufanya Maamuzi ya Kifamilia?
Ni vyema kama mzazi mwenzako alikukosea kwa namna yeyote ile muwekee kinyongo yeye na si kupanda chuki kwenye akili ya mtoto juu ya baba au mama yake! Wahenga husema funika kombe mwana haramu apite, kwa hiyo, kama mzazi, jitahidi kumueleza mazuri juu ya mzazi wake hata kama alikukosea.
Makosa na maovu ya mzazi mwenzako jitahidi kuyaweka kifuani ili kumsaidia mtoto kukua bila kuwa na chuki juu ya mzazi wake. Ukipandikiza chuki hiyo kwa mtoto huweza kumuathiri na kumjenga kuwa mkatili juu ya watu wengine.
Watoto ambao wamefichwa ubini wao hupata wakati mgumu sana wakiwa katika mazingira ya shule, mara nyingine wanataniwa sana na watoto wenzao hasa pale minong’ono kuhusu chimbuko la huyu mtoto inapofika shuleni.
Hali hii humuathiri mtoto kisaikolojia na kumpelekea kufanya vibaya kwenye masomo yake na wakati mwingine kuacha shule kabisa kwa kuogopa kutaniwa.
Mtoto wa namna hii huwa na msongo wa mawazo anaposikia wenzake wakiongelea kuhusu baba, mama, mjomba na shangazi wakati yeye hajawahi kusikia watu wa namna hiyo katika maisha yake.
SOMA ZAIDI: Fahamu Maadili Mema Yanavyojenga Mwenendo Mzuri wa Maisha ya Mtoto
Ijulikane kuwa, ukuaji chanya wa mtoto na uangalizi mzuri unapatikana katika familia inayojumuisha ndugu, jamaa na marafiki.
Usimnyime mtoto wako haki ya kuwafahamu watu wanaomjali katika maisha yake. Mwambie mtoto ukweli kuhusu chimbuko lake na pia, mpe fursa ya kusalimiana na kutembeleana na ndugu zake na hata wazazi walio mbali kama wazazi wametengana.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.