Hivi karibuni tulijaribu kuzungumza na wazazi tofauti kupata mawazo yao juu ya umri upi wangependa kuwapeleka watoto wao shule za bweni.
Kuna ambao walisema hawatawapeleka watoto wao shule za bweni kamwe. Mzazi mmoja alisema umri sahihi ni kuanzia miaka 16 na kuendelea. Mwingine alisema kuanzia miaka 14 na kuendelea.
Wazazi hawa wote walikua na sababu zao za msingi za majibu yao, hivyo tunaona utofauti wa fikra uliopo kuhusu suala zima la umri wa kumpeleka mtoto shule za bweni.
Kufikia muafaka wa swali hili, ni vyema tukaanza kwa kuangalia uwezo wa mtoto kulingana na umri wake na kisha tutahitimisha na maoni yetu kuhusu umri unaoshauriwa kumpeleka mtoto shule ya bweni.
Kuanzia umri wa miaka miwili hadi minne, mtoto huwa hajawa na ufahamu wa kutosha kujua mabaya na mema. Anachokipenda yeye ndicho kizuri na asichokipenda siyo kizuri.
SOMA ZAIDI: Mtoto Anapaswa Kuwafahamu Wazazi Wake, Ndugu na Familia Tandaa
Ni muhimu mzazi kuelewa hili ili kutoa muongozo na uangalizi kwa mtoto kwa upendo pasipo kumuhukumu kuwa ana tabia mbaya kwani bado uwezo wake wa kupambanua baya na jema ni mdogo mno.
Ingawa bado hajawa na uwezo binafsi wa kung’amua mwenyewe mambo mema na mabaya, mtoto mwenye umri wa miaka mitano hadi sita anaweza kufuata maelekezo ya mzazi vyema zaidi.
Mtoto wa umri huu anakiamini kila anachosema mzazi. Bado hana uwezo wa kujua kwa utashi wake mwenyewe lakini anao uwezo mkubwa wa kufuata maelekezo ya mzazi au mlezi.
Wataalamu wa makuzi wanashauri wazazi wawe makini katika kutoa maelekezo katika umri huu kwani unachomweleza huwa ni kama mbegu unayoipanda maishani mwake.
Misimamo yako katika yale unayoyaamini kama ibada, aina za vyakula, nakadhalika kwake hupokelewa kama kilivyo.
SOMA ZAIDI: Tuzungumze Kuhusu Umuhimu wa Michezo kwa Watoto
Mtoto anapofikisha umri wa miaka saba mpaka minane mfumo wake wa kung’amua jema na baya huimarika. Mtoto anaanza kujua mifumo ya maisha ya jamii husika na anao uwezo wa kuelewa madhara ya kutenda mabaya.
Mara nyingi katika umri huu, wataalamu wa makuzi wanaeleza kuwa kutokutenda makosa hujengwa katika uoga wa adhabu zinazotolewa na si kwa sababu nyinginezo.
Kwa mfano, mtoto anajua kuwa sababu kubwa ya watu kutokuiba ni kukamatwa na polisi na si kwa sababu maadili mema yanaelekeza hivyo.
Mara nyingi unaweza kusikia watoto wa umri huu wakitishiana kuwa wakifanya hivyo watakamatwa na polisi au mzazi atawaadhibu. Kama mzazi, ni vyema kumuelewesha mtoto kuwa watu hawaibi kwa sababu wanaogopa polisi tu bali wizi ni tabia mbaya na si maadili mema.
Jambo jema katika umri wa kuanzia miaka tisa na kuendelea, ni mtoto anaanza kuelewa maumivu ya kutenda kosa na faraja ya kutenda mema. Kadiri alivyolelewa, mtoto huumia anapotenda jambo analohisi si jema.
SOMA ZAIDI: Je, Watoto Wako Wanamheshimu Dada wa Kazi?
Uelewa wa dhana ya kuwa watendee wengine vile ambavyo ungependa utendewe wewe huingia. Kwa hiyo, ni vyema mzazi au mlezi kuwa mfano mwema kwa mtoto. Usimtendee vitendo vya kionevu mtoto ukadhani kuwa haelewi, anaelewa.
Jitahidi kutenda haki kwani utamuandaa kupenda kutenda haki kwa wengine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba watoto wanajifunza kwako zaidi kuliko kwa mtu mwingine.
Muongoze mtoto awe na uelewa wa kung’amua jema na baya pasipo kushurutishwa.
Kutokana na mifano hiyo ya kitaalamu kuhusu uwezo wa mtoto kutegemea na umri wake, pamoja na uhalisia wa hali ya maisha ya Kitanzania, bila kusahau maoni ya wazazi tofauti tofauti, tunashauri kwamba iwapo inakubidi kumpeleka mtoto shule ya bweni, basi mpeleke pale atakapomaliza shule ya msingi na kuingia shule ya sekondari.
Hapa mtoto anakua na umri kati ya 12 na kuendelea kutegemea na umri alioanza shule ya awali.
SOMA ZAIDI: Je, Unamshirikisha Mtoto Wako Katika Kufanya Maamuzi ya Kifamilia?
Kabla ya kumpeleka mtoto wako shule ya bweni una fursa ya kujenga ukaribu naye kwa kumuonyesha upendo, kumfundisha maadili mema yatakayomsaidia kuishi na watoto wenzake, kumfundisha jinsi ya kujitegemea na kujisimamia, pia, hakikisha unajenga ukaribu na waangalizi au waalimu wake.
Hivi ni vitu muhimu kuhakisha kwamba mtoto wako yuko salama na yuko tayari kwa maisha bila wewe.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.