Dar es Salaam. Vyama vipya viwili vya siasa vimeitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itimize wajibu wake kwa kuvipatia vyeti vya usajili wa muda ili viweze kuendelea na majukumu yake baada ya kudai kukidhi matakwa yote ya kisheria yaliyokuwa yanahitajika katika mchakato wa usajili.
Vyama hivyo ni Action for Human Justice (AHJ Wajamaa) kilichoanzishwa mwaka 2016 na kukamilisha stahiki zote tangu Disemba, 2022 pamoja na Independent People’s Pary kilichoanzishwa Mei mwaka jana.
Kwa mujibu wa waanzilishi wa vyama hivyo wamedai kuwa kwa muda sasa wamekuwa wakifuatilia kwa wahusika wa ofisi hiyo na kuambiwa kwamba wasubiri mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa ukamilike.
Jambo ambalo hawakubaliani nalo kwani kwa sasa Tanzania tayari ina Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 2019, ambayo ni halali na inaweza kutumika kukamilisha kuvisajili vyama vyao.
“Chama chetu kimsingi kimeanzishwa mwaka 2016. Lakini baada ya kuanzishwa Ofisi ya Msajili [wa Vyama] kwa kweli ilitukwamisha toka wakati huo,” Magnus Msambila ambaye ni Mwenyekiti Mwanzilishi wa chama cha AHJ Wajamaa aliiambia The Chanzo mnamo Disemba 21, 2023.
“[Ofisi hiyo] ikawa inatueleza [kuwa] tusubiri sheria mpya [ya vyama vya siasa]. Sasa kwa kawaida siamini kwamba mtu [anatakiwa] asubiri mambo yake yasifanyike mpaka sheria [mpya] itakapokuja.”
Msambila anaendelea kusema “kwa kweli ni kitu ambacho ni kama cha kihuni, tunakiona cha kihuni. Kwa sababu mtu hawezi kusubiri sheria itakayokuja wakati sheria ipo. Kwa wakati huo sheria ipo, kama hakuna ni suala lingine lakini sheria ipo. Sasa kwa nini tusubiri sheria nyingine? Lakini ndiyo hayo yametukuta ni katika moja ya ukandamizaji tunaoufikiria, huu ni ukandamizaji, hamna kitu kingine.”
Kwa upande wa chama cha IPP nao waliwasilisha maombi yao tangu Mei 4, 2023. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliwaandikia barua mbili ambazo The Chanzo imeziona za kuwataka warekebishe makosa yaliyobainishwa kwenye nyaraka zilizowasilishwa.
Licha ya kurekebisha kama walivyoelezwa pamoja na kulipia ada ya usajili wa yenye thamani ya Shilingi 1,000,000 ofisi hiyo bado haijawapatia cheti cha usajili wa muda.
“Ni zaidi ya miezi sita sasa tumetuma maombi hayo. Ofisi hiyo ingekuwa inafanya kazi sawa sawa kwa kadri ile sheria [iliyopo ya vyama vya siasa] inavyoeleza, ilipaswa leo tuwe tupo kwa umma tunafanya kazi ya kutafuta wanachama na mambo mengine ambayo chama chochote kipya kinapaswa kufanya.
“Lakini mpaka sasa hivi tunataabikia kupata huo usajili wa muda ambao hatujaupata bado,” Gregory Urima ambaye ni Mwanzilishi wa chama cha IPP anasema.
Januari 3, 2024, The Chanzo ilimtafuta Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa anayeshughulikia usajili na ufuatiliaji Sisty Nyahoza, ili kufahamu kuhusu usajili wa vyama hivyo ambapo alitueleza kuwa “vyama hivyo bado havijakamilisha masharti ya usajili wa muda na tumeshawaandikia barua kadhaa kuwafahamisha.”
Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 2019, kipengele cha pili kinachozungumzia usajili wa chama cha siasa, kifungu cha 4(a) kinamtaka Msajili wa Vyama vya Siasa atangaze kwenye magazeti mawili baada ya kupitia nyaraka za maombi jambo ambalo linadaiwa kutofanyika.
Lakini pia kifungu cha 4(c) kinamtaka Msajili baada ya kupitia nyaraka hizo za usajili na kujiridhisha ndani ya siku 30 awe ametoa cheti cha usajili kitu ambacho kinaelezwa kutofanyika.
Hivyo vyama hivyo kwa sasa haviruhusiwi kufanya jukumu lolote mpaka pale cheti cha usajili wa muda kitakapotolewa.
Chama cha mwisho kilisajiliwa 2014
Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tanzania ina jumla ya vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu. Chama cha mwisho kupata hadhi hiyo kilikuwa ni Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), kilichopewa usajili mnamo Mei 5, 2014.
Hivyo mpaka sasa ni takribani miaka 10 inakwenda bila ya ofisi hiyo kukipa hadhi ya usajili wa kudumu chama kipya cha siasa.
Mnamo Mei 12, 2023 Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, alinukuliwa akisema kuwa ofisi yake imepokea maombi ya vyama vipya 18 vya siasa ambavyo vinahitaji usajili wa muda.
Mutungi aliendelea kueleza kuwa kati ya vyama hivyo ni vyama sita pekee ndivyo vilivyokidhi vigezo vya kupata usajili wa muda ingawa hakuvitaja majina
Barua kwa Rais Samia
The Chanzo imeiona barua iliyoandikwa na chama cha AHJ Wajamaa kwenda kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kumuonba aondoe zuio la kusajiliwa kwa vyama vipya vya siasa kwenye ofisi ya msajili.
Sehemu ya barua hiyo ya Disemba 19, 2023 imeeleza kuwa, “Mheshimiwa Rais,tulipoanzisha chama tulikuwa na tegemeo kubwa la kushiriki katika chaguzi kuu zote za nchi hasa uchaguzi mkuu yaani uchaguzi wa Serikali za mitaa, madiwani wabunge na Rais.”
Barua hiyo imeendelea kueleza, “chama kipya cha siasa kina hatua mbalimbali ili kiweze kushiriki katika chaguzi. Mpaka sasa hatujapata cheti cha usajili wa awali ili tuweze kuruhusiwa kutafuta wanachama. Uchaguzi ukuu unaanza mwakani kwa hiyo tunaomba utoe idhini ili muda uliobaki nasi tuweze kutafuta wanachama na hatimaye tuweze kujua kiasi gani mawazo yetu yanakubalika kwa Watanzania.”
Kusajili chama ni haki siyo fadhila
Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 2019 Mtanzania yeyote aliyekidhi vigezo anahaki ya kuanzisha chama cha siasa. Kitendo cha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuchelewesha mchakato huo kimeelezwa kuwa kinafanya kama usajili wa chama kuwa ni kitendo cha fadhila jambo ambalo halitakiwi kuwa hivyo.
“Kusajili chama cha siasa ni haki ya kikatiba, ni haki ya kiraia, siyo suala la fadhila,” Gregory Urima wa chama cha IPP ameiambia The Chanzo.
“Hili ni suala la watu wanaotambua wajibu wao kwa ajili ya ustawi wa nchi yao wanaweza wakaamua wakasajili chama, wakafanya shughuli za siasa kwa ajili ya ustawi wa nchi yao. Sasa halipaswi kuwa jambo la kama vile unamuomba mtu ndiyo afanye fadhila, hapana.”
“Ipo ofisi ile ya msajili ile ndiyo kazi yake na kama tunavyojua ni zaidi ya miaka 10 sasa ile ofisi haijasajili chama chochote cha siasa. Sasa kidogo tunashindwa kuelewa shida ni nini?
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com