The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Waamuzi Zanzibar Wametia Doa Kombe la Mapinduzi

Ni muhimu kwa ZFF kufanyia kazi eneo hilo kwa ajili ya si tu kunufaisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi, bali mpira wa miguu kwa ujumla katika visiwa vya Zanzibar.

subscribe to our newsletter!

Kwa muda mrefu, hayati Hafidh Ali alikuwa akichukuliwa kama taswira ya waamuzi bora kutoka Zanzibar, akiaminiwa na Idara ya Football Zanzibar (IFOZA) wakati huo na baadaye ZFA na sasa shirikisho (ZFF), Bara na hadi Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na lile la dunia, FIFA.

Hafidh Ali hakuishia kuchezesha mechi uwanjani tu, bali alipewa majukumu ya kuratibu mechi baada ya kustaafu na alikuwemo kwenye kamati za CAF akichangia uzoefu wake katika uendeshaji mchezo huo maarufu duniani.

Alikuwa taswira ya uamuzi bora kwa sababu Zanzibar ilizalisha waamuzi wengine wengi baada yake ambao pia waliaminiwa na CAF na FIFA na hivyo kupewa mechi nje ya nchi.
Lakini uamuzi makini na wenye weledi visiwani Zanzibar sasa unaelekea kupotea na mashindano ya Kombe la Mapinduzi ya mwaka huu yameonyesha kiwango cha fani hiyo cha sasa.

Kumekuwepo na makosa mengi ya dhahiri ambayo yamezigharimu timu kama Singida Fountain Gate na Armee Patriotique Rwandese (APR), ambayo kocha wake alidiriki kusema hawatashiriki tena mashindano hayo.

Picha nyingine za video zinaonyesha kiongozi wa Singida akiwatia moyo wachezaji wake baada ya timu hiyo kutolewa na Simba kwa mikwaju ya penati, akisema walikosa ushindi kwa sababu ya mambo ya nje ya uwanja na si uwanjani.

SOMA ZAIDI: Kamati ya Hamasa Bila ya Mkakati wa TFF

Imekuwa ajabu kwamba timu zilizonufaika na makosa ya waamuzi, yaani Simba na Mlandege, ndizo zimefuzu kucheza fainali, jambo linalopoteza ladha ya mashindano.

Wakati kamati ya waamuzi ya ZFF imekiri kuwa kona iliyozalisha bao la kusawazisha la Simba katika muda wa majeruhi haikuwa halali kwa sababu mpira ulishatoka, bao ambalo lingekuwa la ushindi la APR dhidi ya Mlandege, halijatolewa maelezo.

Mfungaji wa bao hilo hakuwa eneo la kuotea, lakini mwamuzi msaidizi akanyoosha kibendera kuashiria kuotea baada ya kuona wachezaji wengine wawili wa APR wakiwa eneo hilo. Wachezaji hao hawakugusa mpira licha ya kuruka juu kujaribu kuugusa. 

Kwa sasa kitendo chao cha kujaribu kuucheza mpira hakihesabiwi kuwa na kuotea na hivyo APR walinyimwa bao halali ambalo lingewapeleka fanali.

Haikuwa sahihi kwa kocha wa APR kutangaza kuwa timu hiyo haitakubali tena mwaliko kushiriki Kombe la Mapinduzi kwa kuwa ni suala la uongozi kuweka msimamo huo si kocha ambaye inawezekana asiwe na timu hiyo wakati mashindano hayo yatakapofanyika mwakani, 2025.

SOMA ZAIDI: Simba Iongeze Muda wa Maoni Marekebisho ya Katiba

Lakini kauli yake na taswira yake wakati akizungumzia uamuzi huo unaakisi kile kilichokuiwemo ndani ya timu hiyo baada ya kunyimwa bao ambalo lingewapeleka mbele mashindanoni. 

Kibaya zaidi ni kwamba kauli yake haiishii visiwani Zanzibar tu, bali inakwenda mbali zaidi kuchafua mashindano hayo ambayo yamekuwa burudani na yenye umuhimu wa aina yake wakati wa mapumziko mafupi ya msimu.

ZFF haina budi kuchukulia kwa umuhimu mzito makosa yaliyofanyika mwaka huu na kuyafanyia kazi ili thamani ya mashindano hayo iendelee na pengine iongezeke na klabu za ndani na nje ya nchi zione umuhimu na ziwe na hamu ya kushiriki.

Pengine makosa yanaweza kuonekana kuwa ni yale yaliyozinufaisha Mlandege na Simba tu, lakini yapo mengi yaliyoonekana katika mechi nyingine ambazo hazikuamua timu kuendelea kuwa mashindanoni au kutolewa na ndiyo maana yahakuzungumzwa sana.

Mara kadhaa waamuzi wasaidizi walinyoosha kibendera kuashiria kuotea wakati hali halisi ilikuwa tofauti. Kama ilivyo kwa Ligi Kuu ya Bara, na pengine ilitokea kwa bahati mbaya, tukio la muda wa majeruhi ulioongezwa lakini mchezo ukavuka muda huo, lilitokea katika mechi za vigogo wa Dar es Salaam, Simba na Yanga.

SOMA ZAIDI: Kila la Heri Maandalizi ya Stars AFCON 2023

Wakati Yanga haikunufaika na muda huo, Simba ilinufaika kwa kupata bao la kusawazisha. Mara nyingi tukio kama hilo linapotokea kwa vigogo hao wawili, hufuta lawama kwa waamuzi. Sijui hufanyika kwa makusudi au bahati mbaya, lakini haya si mambo ya kuyalea kabisa.

Uamuzi ni kitu muhimu sana katika mashindano yoyote kwa sababu ndiyo unaamua mshindi wa haki katika mechi na hatimaye bingwa wa haki. Pale uamuzi unapolegalega, ndipo mashindano huchukuliwa kama yameandaliwa kwa ajili ya kuipa ubingwa timu fulani na hivyo kupoteza ladha na thamani yake.

Ni muhimu kwa ZFF kufanyia kazi eneo hilo kwa ajili ya si tu kunufaisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi, bali mpira wa miguu kwa ujumla katika visiwa hivyo na kurejesha ile taswira ambayo hayati Hafidh Ali aliijenga barani Afrika kuwa Zanzibar huzalisha waamuzi makini na wenye weledi ambao si tu wanastahili kuchezesha ligi, bali hata fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

 1. Lugha nyepesi nni kusema kuwa kuna haja katika Maindzui Cup kuajiriwa Waamuzi wa Kimataifa, ili kuondosha kazoro zilizojitokeza aidha kuhakikishwe Video Assist Referee ”VAR” zinafungwa.

  Mpira siku hizi kasi yake nikubwa sana na kwa kuchezwa pattern tafauti Waamuzi wanapata tabu sana kuja na maamuzi saa nyengine wanakuwa hawalaumiki. Nalisoma utafiti mmoja ambao uliangalia nani uwanjani mapigo yake ya moyo yanapiga kwa nguvu na anayekimbia zaidi, Khitimisho imeonekana ni muaamuzi.

  Muamuzi anakuwa na wasiwasi humfanya kuwa na wasi wasi kisha ni yeye anayekimbia zaidi ukijumuisha kutokana na yeye lazima afwate mpira, saa nyengine utakuta ukichanganya wachezaji wakati na mabek kukimbia kwao na Refa utakuta Refa amewazidi.

  Makosa yametendeka ila Kocha wa APR hakuwa Mwanaspoti kwa mahojiano alioyatoa. Imekuwa Mlandege kubeba hili Kombe kwa wengine kama hawakuwa wanastahiki kwa kusahau na wao wamejiandaa. Siku hizi kila timu inajipanga.

  AFVON 2024 Misri katiwa Kabari na Msumbiji, Cape Verde kamhenyesha Ghana, Algeria na Angola suluhu, hakuna yale ya kizamani kuwa baadhi ya timu zikicheza na timu kama za visiwa au za Kusini mwa Jangwa la Sahara nikwenda kujichukulia Points hayo hayapo sasa.

  Kutumia Video kujifunza sasa ni kwa wote, wachezaji mmoja mmoja siku hizi wanajiendeleza wenyewe kupitia youtube n.k.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *