Dar es Salaam. Maafisa uhamiaji katika jiji la Kuala Lumpur, Malaysia, zinamshikilia mwanamke mmoja wa Kitanzania, ambaye jina lake limehifadhiwa, baada ya kubainika akiwatumia wanawake wenzake wa Kitanzania kuendesha biashara ya ukahaba katika jiji hilo maarufu kwa kuwa na maghorofa makubwa ya vioo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Malaysia, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 32 ni sehemu ya mtandao mpana wa kihalifu unaosafirisha wanawake kwa njia za haramu kutoka Tanzania kwenda Malaysia na kuwaingiza kwenye biashara ya ukahaba.
Taarifa zinadai kwamba mtandao huo huwalaghai akina dada hao wa Kitanzania kwamba watawapatia fursa za kazi wakifika huko Malaysia, nchi inayojulikana kwa kuwa na wafanyakazi wengi wahamiaji, lakini baada ya kufika tu hulazimishwa kujiingiza kwenye biashara hiyo ya ukahaba bila ya ridhaa yao.
Akinukuliwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo, Ruslin Jusoh, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uhamiaji ya Malaysia, alisema kwamba akina dada hao hulazimika kujiingiza kwenye biashara hiyo baada ya ‘bosi’ wao kuwanyang’anya hati zao za kusafiria.
SOMA ZAIDI: Kumi na Tatu Wakamatwa Kwa Udhalilishaji wa Watoto Wa Kiume Zanzibar
Mtandao huo uligundulika baada ya maafisa uhamiaji kufanya operesheni maalumu katika jiji la Kuala Lumpur ambayo pia ilifanikiwa kumuokoa binti mmoja mwenye umri wa miaka 29, ambaye jina lake pia limehifadhiwa, aliyekuwa akitumikishwa kingono na mwanamke huyo jijini humo.
“Msichana huyu alikuwa akidhibitiwa na mwana mtandao ambaye pia ni Mtanzania na kutumikishwa kingono,” Jusoh aliviambia vyombo vya habari vya Malaysia. “Hati yake ya kusafiria alinyang’anywa bila ridhaa yake. Kwa sasa binti huyu yupo sehemu salama amehifadhiwa kwa muda.”
Binti huyo aliokolewa katika operesheni hiyo maalumu kufuatia uchunguzi wa maafisa uhamiaji wa Malaysia na taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Malaysia iliyofanyika majira ya saa kumi na nusu mchana.
Jusoh alisema kesi hiyo kwa sasa inachunguzwa chini ya sheria za Malaysia zinazopinga usafirishaji haramu wa binadamu na endapo mwanamke huyo mwana mtandao akipatikana na hatia anaweza kufungwa kifungo cha miaka 30 jela au maisha pamoja na viboko.
SOMA ZAIDI: Vijana Zanzibar Watoweka Katika Mazingira Tatanishi. Wazazi, Polisi Watoa Kauli Kinzani
Hii siyo mara ya kwanza kwa operesheni maalumu kuwanasa Watanzania wanaofanya biashara ya ukahaba katika jiji la Kuala Lumpur.
Mnamo mwaka 2022, mamlaka katika jiji hilo liliendesha operesheni kama hii na kuwanasa wanawake sita wa Kiafrika wakijihusisha na biashara hii, wanne kati yao wakiwa ni Watanzania.
Malaysia ni moja tu kati ya sehemu nyingi ambazo wanawake wa Kitanzania wanaripotiwa kupelekwa kwa ajili ya kazi mbalimbali, ikiwemo ukahaba na utumishi majumbani.
Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ya mwaka 2023, sehemu nyingine ni kama vile Oman, UAE, Yemen na Qatar.
Usafirishaji haramu wa binadamu ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi na Serikali, kwa kushirikiana na wadau wengine, imekuwa mstari wa mbele kwenye kukomesha aina hiyo ya uhalifu nchini.