The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kumi na Tatu Wakamatwa Kwa Udhalilishaji wa Watoto Wa Kiume Zanzibar

Polisi wasema hakuna mtandao wa kihalifu Zanzibar, yalaumu mmomonyoko wa maadili visiwani humo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi wa Mjini Magharibi, Richard Thadei Mchomvu ametangaza leo kukamatwa kwa watu 13 wakituhumiwa kuhusika na matukio ya udhalilishaji kwa vijana wa kiume Zanzibar kama ilivyoripotiwa na The Chanzo wiki iliyopita.

Katika ripoti yake, The Chanzo ilifichua wahalifu ambao hutumia mbinu mbalimbali kuwarubuni vijana wa kiume, hasa wale wanaoishi mazingira hatarishi. Wahusika katika mtandao huo huwabaka vijana wa kiume, kuwarekodi video na kisha kutumia video hizo kuwatumikisha kwa kuwauza kwa wanaume wengine.

Ripoti hiyo iliyoibua mjadala mpana katika pande mbalimbali za nchi ilionesha kuwa kuna wahusika mbalimbali wenye vitendo hivyo, wakiwemo madalali, wanunuaji na wauzaji.

Wahalifu hao huwavizia vijana wanaoshinda maeneo ya Forodhani Zanzibar, hasa vijana wale waliotoroka majumbani kwao kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kutoelewana na wazazi, na kuwarubuni na kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji.

Akiongea na waandishi wa habari, Mchovu alieleza kuwa Polisi walizifanyia kazi taarifa ya The Chanzo punde tu baada ya kutoka, wakifanya uchunguzi maeneo ya Rahaleo, Kisauni, Fuoni, Bububu, Malindi na Magomeni.

SOMA ZAIDI: ‘Nimeamua Kuacha Kesi, Nibaki na Binti Yangu’: Masaibu ya Waathirika wa Udhalilishaji Walemavu Zanzibar

Operesheni hiyo iliyofanyika kwa siku kadhaa iliweza kufanikisha kukamatwa kwa watu 13 ambao wameonekana kuhusika kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo.

Waliokamatwa ni pamoja na Ibrahim Saleh (29), Ibrahim Saleh Rashid (22), Ali Abdallah Mohammed (27), Yassin Abdallah Mohammed (17), Twalib Salum Mohammed (25), Suleiman Juma Omar (22), Othman Mohammed Salum (49), Ali Haji Hamisi (25), Mudathir Jacob Simon (27), Ali Salim Abdallah (53), na Mohammed Fuad Mohammed (21).

“Majalada manne tumeshapeleka kwa Mkurugenzi wa Mashataka kwa hatua zaidi,” alieleza Mchomvu. “Lakini tuna majalada matano ambayo bado tunayapeleleza.”

Ameeleza kuwa tayari watu watatu wameshafikishwa Mahakamani, leo Novemba 22, 2023, ambapo watashitakiwa kwa kufanya mapenzi kinyume na maumbile, kitendo ambacho ni cha kinyume na sheria kwa mujibu wa sheria za Zanzibar.

Edwin Mugambila, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Relief Initiative (TRI), shirika lisilo la kiserikali linalofanya shughuli ya kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu, alipendekeza wahusika washitakiwe kwa makosa ya usafirishaji haramu wa binadamu kutokana na uzito na namna walivyotekeleza uhalifu huo.

SOMA ZAIDI: Ofisi ya Mufti Zanzibar: Vitendo vya Udhalilishaji Watoto Vinahuzunisha

Hata hivyo, Mchomvu amewaeleza waandishi wa habari kuwa uchunguzi wa Polisi Zanzibar umeonesha kuwa matukio hayo hayahusiani moja kwa moja na mtandao wa kihalifu.

Mchomvu alisema sehemu kubwa ya matukio yaliochunguzwa yalihusiana moja kwa moja na changamoto za kifamilia, ikiwemo kutengana kwa wazazi na pia wazazi kutokuwa na muda wa kutosha katika kuwaangalia watoto wao.

“Wazazi wanajifanya wana majukumu mengi wanashindwa kutoa malezi kwa watoto,” alifafanua Mchomvu. 

“Kwa hiyo, tukio hili limetokea kwa sababu ya mmonyoko wa maadili kwenye jamii yetu,” afisa huyo, akisisitiza umuhimu wa wazazi kuwaangalia kwa karibu watoto wao, hasa kwa kuwapa mafundisho ya dini.

“Hakuna mtandao hapa Zanzibar unaoendesha mambo haya,” alisisitiza. “Wahusika walitelekeza matukio hayo wakiwa sehemu mbalimbali. Serikali iko makini na imejidhatiti kupinga udhalilishaji kwa watoto Zanzibar.”

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *