The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Nimeamua Kuacha Kesi, Nibaki na Binti Yangu’: Masaibu ya Waathirika wa Udhalilishaji Walemavu Zanzibar

Wazazi wenye watoto walemavu ambao ni waathirika wa udhalilishaji wanadhani hali za watoto wao zinawafanya wakose haki.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Miaka minne iliyopita, Zahor Issa* alifiwa na mke wake aliyebahatika kupata naye watoto wawili wa kike. Binti yake wa kwanza ni mlemavu wa afya ya akili. Pia, mtoto huyo hupoteza fahamu pale akiwa amelala, hali inayomfanya asikumbuke chochote.

Issa, mfanyabiashara wa nguo za mitumba, aliona sehemu anayoishi si salama kwa watoto wake kwa sababu ya kazi yake hiyo. Hivyo, aliamua kuwapeleka watoto wake hao kwa ndugu zake aliko hisi kwamba watapatiwa uangalizi sahihi. 

Huyu anayepoteza kumbukumbu, ambaye kiumri ana miaka sita, alimpeleka kwa dada yake, huku akiendelea na masomo. Hata hivyo, binamu yake wa kiume, mwenye umri wa miaka 19, alikuwa anafahamu tatizo la msichana yule, na hivyo kumbaka kila giza liingiapo.

“Nilipokuwa naenda kumuona nilianza kuona hali yake ya  furaha inapotea,” Issa aliieleza The Chanzo kwenye mahojiano maalum. “Amesawijika hivi na alionekana kuwa na hofu. Nikauliza, nikaambiwa hakuna kitu. Nikamuuliza [binti yangu] lakini alisema hakuna kitu pia.”

Ni mpaka baada ya miezi mitatu tangu Issa ahitaji majibu kuhusiana na hali ya binti yake ndipo alipoweza kuyapata pale binti yake huyo alipomuambia kuhusu maumivu anayoyapata kwenye sehemu zake za siri.

SOMA ZAIDI: Watoto 1,173, Wanawake 185, Wanaume 3 Wafanyiwa Ukatili Zanzibar 2022

“[Binti yangu] ni mlemavu wa akili lakini ana uwezo wa kuzungumza na anafahamu. Lakini ni lazima uwe umetulia kumsikiliza,” Issa anasema. “Aliponiambia kuwa ana maumivu sehemu zake za siri, nilimchukua mpaka hospitali. Na kweli, [ikabainika kwamba] ni muda mrefu alikuwa akiingiliwa.”

Issa, aliyekuwa akiongea huku machozi yakimlenga machoni mwake, aliiambia The Chanzo kwamba haikuwa rahisi kwake kupigania haki ya mtoto wake kwa sababu aliyefanya hivyo ni mtoto wa dada yake. 

Hata hivyo, alijikaza ili vyombo vya dola vimchukulie hatua aliyemdhalisha binti yake huyo. Issa alimshtaki mtoto wa dada yake, kesi ikafika mahakamani, lakini hali ile ile iliyompelekea binti yake kubakwa ilimpelekea pia akose haki yake.

“Mtoto wangu ndiye aliyetakiwa kusema nini kimetokea,” Issa anasimulia. “Alisema ila katikati ya mazungumzo alikwama, na hapo ndipo changamoto ilipoanza. Ilienda hivyo kwa muda mrefu, nikaamua kuacha kuendelea na kesi, nikabaki na binti yangu.”

Siyo kisa pekee

Kisa cha Issa si kisa pekee kinachohusisha waathirika wa vitendo vya udhalilishaji ambao ni walemavu kukosa haki zao pale kesi hizo zinapofikishwa mbele ya vyombo vya haki.

Saumu Ridhiwani analea mtoto mwenye ulemavu wa miguu ambaye amekuwa akitembelea kiti cha mwendo kwa takriban miaka saba sasa.

SOMA ZAIDI: Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni

Saumu, mfanyakazi wa kiwanda cha mafuta, huamka kila siku asubuhi kwenda kazini na kumuacha binti yake, mwenye umri wa miaka 14, na msichana wake wa kazi.

Mnamo Novemba 24, 2022, Saumu, mama wa mtoto mmoja, alitoka kwenda kazini na kumpigia simu fundi wa bomba la maji aje atengeneze.

“Msichana wangu wa kazi alimpeleka mwanangu pale ukumbuni kwenye TV na fundi akaja kuanza kutengeneza,” Saumu aliihadithia The Chanzo. “Ubaya dada akatoka kwenda dukani kununua kitu, akamucha msichana na fundi. Anarudi, anamkuta fundi ameshamtoa [mtoto] kwenye kiti, ameshamuweka chini na kumvua nguo.”

Fundi huyo alikamatwa na kushtakiwa. Mashahidi ni msichana wa kazi na binti aliyefanyiwa udhalilishaji. Saumu alidhani ingechukua muda mfupi tu mpaka mdhalilishaji wa binti yake ahukumiwe. Hali ikawa tofauti. 

“Imechukua zaidi ya miezi saba, na hakuna hukumu,” Saumu anasema kwa uchungu. “Naacha kazi, naenda na kurudi mahakamani, [lakini] hakuna kinachoendelea. Mwisho wa siku, nikaacha.”

SOMA ZAIDI: Ofisi ya Mufti Zanzibar: Vitendo vya Udhalilishaji Watoto Vinahuzunisha

Malalamiko ya Issa na Saumu ni sehemu ya malalamiko mengi ya jamii ya watu wenye ulemavu visiwani hapa wanaohisi kwamba watu wa jamii hiyo wanakosa haki zao kwa sababu tu ya kuwa ni walemavu.

Jumuiya za walemavu zinaamini kwamba waathirika wa vitendo vya udhalilishaji walemavu wanakosa haki zao kwa sababu Mahakama imeshindwa kuzitumia jumuiya hizo katika uendeshaji wa kesi, hususan kwenye huduma za kutoa ukalimani.

Inatia aibu

Kheri Mohamed Simai, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wakalimani wa Lugha ya Alama Zanzibar (JUWALAZA), ameiambia The Chanzo kwamba suala la watu wenye ulemavu kukosa haki zao kwa kisingizio cha kutokuwepo kwa watoa msaada ni jambo linalotia aibu.

“Upatakanaji wa haki kwa waathirika wa udhalilishaji walemavu ni mdogo kwa sababu ni jambo ambalo halijawekewa mkazo,” Simai aliimbia The Chanzo. “Mara nyingi Mahakama inalalamikia suala la gharama kwenye kesi hizi. Lakini sisi tunahitaji gharama kiasi gani mpaka tuweze kutoa msaada kwenye kesi hizo?”

Zanzibar inaruhusu huduma hizo kutolewa kwenye uendeshaji wa kesi zinazohusu waathirika wa vitendo vya udhalilishaji walemavu lakini licha ya miongozo hiyo kuwepo Mahakama haizitumii huduma hizo, hali inayowakwaza walemavu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussy Khamis Debe, amesema kwamba ipo haja ya kuongeza uelewa wa watendaji wa Mahakama kuona mchango wa huduma za ukalimani kwenye mchakato wa kuhakikisha haki inatendeka kwa waathirika wa vitendo vya udhalilishaji walemavu.

SOMA ZAIDI: Ukatili Kwenye Ndoa Watajwa Kuchochea Talaka Zanzibar

Debe alisema kwa mwaka 2020/2021 kesi 10 zilizohusisha waathirika wa udhalilishaji walemavu ziliripotiwa kwenye Mahakama na mwaka 2021/2022 kesi saba ziliripotiwa, hali aliyoihusisha na kuongezeka kwa mwamko wa kuripoti kesi hizo mahakamani.

“Kundi ambalo linashambuliwa zaidi ni kundi la watu wenye ulemavu wa akili; ni kundi ambalo limekuwa linashambuliwa zaidi,” alibainisha Debe kwenye mahojiano hayo. “Kwa hiyo, hatuwezi kusema moja kwa moja kwamba wako salama.”

Sara Omar Hafidh, Hakimu wa Mahakama ya Mkoa wa Vuga anayeshughulikia kesi za udhalilishaji, amesema kwa sasa Mahakama inawatumia wataalamu wa lugha kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar kwenye kutoa msaada wa kesi za watu wenye ulemavu.

“Mahakama ndiyo inalipa hao wataalamu, japo bado kuna changamoto,” Sara aliiambia The Chanzo. “Unaweza ukakuta siku ratiba zimeingiliana, kuna kesi na hakuna mtaalamu. Ndiyo inabidi isogezwe mbele. Ila tunajitahidi kwa sasa.”

*Siyo jina lake halisi.

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar.Kwa maoni unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *