The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ukatili Kwenye Ndoa Watajwa Kuchochea Talaka Zanzibar

Wadau wanasema juhudi za kuokoa ndoa zisivunjike Zanzibar lazima ziendane na juhudi za kupinga ukatili katika ndoa. 

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Maryam Said ni mama wa watoto wawili kila mmoja akiwa na baba tofauti. Akiwa na umri wa miaka 30 tu, tayari Maryam alishaolewa mara mbili. Mtoto wake wa kwanza ana miaka miwili na miezi mitano na wapili ana mwaka mmoja sasa. Ndoa yake ya kwanza ambayo ilifanyika 2017 akiwa mke wa pili kwa mume wake huyo , ilidumu kwa kipindi cha mwaka mmoja tu na kisha kupewa talaka. 

Maryam anadai mpaka sasa hajui sababu ya kuachika katika ndoa hio. Maryam aliolewa tena mwaka 2019 na mume ambaye alishaoa wake wanne na kuwaacha. Maryam anasema kwamba aliamini kuwa huko atapata amani na kulea binti yake. Ila mambo hayakuwa kama alivyotarajia. Baada ya ndoa kuzoeleka kwenye maisha hayo mapya ndipo mume wake alipombaka binti yake wa miaka miwili, jambo ambalo lilimfanya Maryam adai talaka na kuondoka kwa mume na kurudi nyumbani kwao. 

“Siku moja nikamka usiku nikaenda kumuasha mtoto aende chooni nakuta damu kwenye shuka la kitanda. Nikashanga na kumuuliza mtoto wangu kuna nini kwa sababu ni mdogo. Binti yangu akawa hasemi kitu badala ya kusema tu, ‘Baba,’” anasema Maryam wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo yaliyofanyika nje ya Ofisi ya Khadhi Zanzibar,Agosti 24,2021. 

“Nikamuangalia [binti yangu] sehemu zake za siri nikaona hali mbaya,” anaendelea kusimumulia. “Kwa kweli nilichanganyikiwa. Nikaweka maji ya moto na kumkanda. Sikujua kwamba kufanya hivyo nilikuwa napoteza ushahidi. Kwa hiyo, kesi yangu haikufika mbali na hakuna mashtaka. Kwa hiyo siwezi kuwa sehemu mmoja na mtu aliyetugeuza kuwa wake sote mimi na mwanangu.”

Licha ya udhalilishaji huu ambao Maryam anadai binti yake kufanyiwa na baba yake wa kufikia, Maryam alilazimika kumrudishia aliyekuwa mume wake mahari aliyopokea ambayo ni kitanda cha futi tano kwa sita na godoro lake ili aweze kupata talaka yake.

Maryam siyo mwanamke pekee visiwani hapa aliyelazimika kudai talaka kutokana na tabia za udhalilishaji zinazofanywa na waume zao. Huko Nyamazi, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, mwanamke mmoja mwenye mtoto wa miaka minne wa kiume alilazimika kudai talaka baada ya aliyekuwa mume wake kumlawiti mtoto huyo. 

“Yeye ni baba yake mzazi na sikuwa na shida kuona nikienda safari kumuacha nae amsimamie,” anaeleza mama huyo ambaye hakutaka jina lake liwekwe mitandaoni kwa sababu binafsi. 

Akiongea na The Chanzo wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake Nyamazi, Agosti 26,2021, mama huyo anasimulia: “Lakini sikuweza kulala kwa siku nne baada ya kuona mtoto wangu anapitwa na haja kubwa kwenye nguo zake za ndani. Hapo nikaanza kufuatilia ndipo nilipokuja kujua kwamba ni baba yake ndio anamuharibu. 

“Sikuweza kubaki [na kuendelea kuishi na mume wangu]. Niliomuomba talaka na kuoandoka. Mimi sitaki kesi ila Mungu atanilipia. Nililazimika kuhama kwetu na kwake. Nimekuja kuishi mbali na wanaonifahamu ili nimlinde mtoto wangu na aibu na unyonge uliosababishwa baba yake. Sijuwi kwa nini mambo kama haya hutokea kwenye jamii.” 

Gumzo la talaka Zanzibar

Kwamba idadi ya watu wanaoomba kuachana Zanzibar ni kubwa ni jambo ambalo si siri. Ofisi ya Kadhi ya Zanzibar, asasi za kiraia, vyombo vya habari, na wadau wengine mbalimbali wamekuwa wakipiga kelele kuhusiana na hali hiyo ambayo kwenye macho ya wachambuzi wa masuala ya kijamii inaonekana kuwa ni hali isiyokuwa ya kawaida. 

Mnamo Mei 2020, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma aliitaka Ofisi ya Mufti Zanzibar inaanzisha ofisi maalumu katika wilaya zote za Zanzibar ambayo itakuwa inasimamia “mafunzo ya ndoa” ili kukabiliana na ongezeko la talaka visiwani humo. 

Jumla ya malamiko 1600 ya talaka yaliwasilishwa katika Ofisi ya Kadhi Zanzibar mnamo mwaka 2018 huku mashauri 48 yalipokelewa na Ofisi ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) kati ya Januari na Juni 2021. ZAFELA taasisi isiyo ya kiserikali inayojikita katika kuwasaidia wanawake kupata haki zao kupitia usaidizi wa kisheria

Serikali pamoja na wadau wengine wamekuwa wakiwasihi wanandoa kujitahidi kumaliza tofauti zao bila kufikia hatua ya kupeana talaka, wakisema kwamba talaka si tu zinaongeza idadi ya wajane na wategemezi nchini bali pia huwanyima watoto malezi ya baba na mama, kitu ambacho ni muhimu katika ukuwaji na ustawi wao kwa ujumla.

Hata hivyo, haijulikani ni kwa namna gani ushauri huu unaweza kutekelezeka kwa kuzingatia kesi kama za akina Maryam na wengine ambao watoto wao wamekutana na vitendo vya kikatili na udhalilishaji kutoka kwa watu ambao ungedhani wangekuwa kwenye mikono salama kwao. 

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), jumla ya kesi 230 za ukatili dhidi ya wanawake na utoto ziliripotiwa ofisini hapo kati ya kipindi cha Januari hadi Julai, 2021. Kati ya kesi hizo, 115 ni za ubakaji; 65 ni za ulawiti; na nane ni za kujaribu kubaka. 

Ndoa ni mapenzi kama hayapo si ndoa

“Ndoa ni sehemu ya amani na mapenzi, ikiwa hakuna hayo hakuna haja ya kukaa kwa kuogopa aibu ya [kuachika],” anasema Clara Thomas, mkazi wa Mbweni, Zanzibar. “Udhalilishaji hauwezi kuwa sehemu moja na ndoa. Hapo hakuna ndoa. Ni mateso na maumivu tu. Binafsi nitachagua kuondoka, nipate talaka au nisipate.”

Mwamvua Issa ni mama wa watoto watano ni mfanyabiashara wa barafu katika kituo cha daladala Mwanakwerekwe, Zanzibar: “Mtoto amekaa tumboni kwa mama miezi tisa na mume nimekutana nae ukubwani. Siwezi kuchangua mume dhidi ya mtoto wangu. Lazima nihakikishe anafungwa [mume kama atabainika kumdhalilisha mwanangu kingono]. Hapo ndoa ndiyo basi na maisha yanendelee.”

Salma Lusangi ni Mratibu wa Mradi wa Wanawake na Uongozi kutoka TAMWA – Zanzibar. Wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo yaliyofanyika Kwa Njia Ya Simu, Salma anasema kwamba licha ya kwamba ongezeko la talaka katika jamii si jambo linaloleta picha nzuri, hakuna haja ya kubaki kwenye ndoa yenye matukio ya udhalilishaji kwa wenza au kwa watoto wao.

“Hakuna sababu ya kubaki kwenye ndoa iliyo na matukio ya udhalilishaji,” anabainisha Salma. “Ikiwa mwanaume amemdhalilishaji mwanao hakuna haja ya kubaki. Kudai Talaka ni haki ili jamii ijue uonevu huo na sheria zichukuliwe dhidi yake. Kuona aibu na kuficha [udhalilishaji] ni kumpa nafasi mhusika aendelee na tabia hizo.”

Tume maalum ya rais

The Chanzo ilimtafuta Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia Wazee na Watoto wa Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui kutaka kufahamu Serikali ina mtazamo gani kuhusiana na maoni haya ya akina mama na wadau wengine kuhusiana na mtanziko uliopo kati ya kudumisha ndoa kuepuka ongezeko la talaka na harakati za kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji visiwani humo. 

Kwa mujibu wa Mazrui, talaka na udhalilishaji kila moja lina athari zake katika jamii huku akibainisha kwamba utu wa mtu hupimwa kwa matendo na endapo hayo matendo yatakosekana kwenye muunganiko wa ndoa basi hakuna budi kuvunjika.

“Kwa sasa, Rais [Hussein] Mwinyi yupo kwenye hatua za mwisho za kuunda tume maalum ya kupambana na udhalilishaji,” alisema Mazrui wakati wa mahojiano hayo yaliyofanyika ofisini kwake Mnazi Mmoja, Zanzibar, Agosti 30, 2021. Rais Mwinyi alitangaza nia ya kuunda tume hiyo mwanzoni mwa mwaka 2021 ikiwa ni sehemu ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji visiwani humo.

“[Baada ya tume hii kuundwa] kutakuwa na wataaalam ambao watapewa nguvu kwenye masuala ya kifedha, elimu, na nguvu kazi,” aliongeza Mazrui. “Hivyo, wahusika wote watapewa adhabu kali kulingana na sheria za nchi.”

Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najjatomar@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na makala haya, unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *